FAIDA ZA KUTOWEKA IMAMU MUOKOZI NO.2

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

FAIDA ZA KUTOWEKA IMAMU MUOKOZI NO 2

Katika makala iliyopita tulielezea baadhi ya faida za kutoweka Imamu muokozi, katika makala hii tutaendelea kuelezea faida nyengine za kutoweka Imamu (a.s).

MATUMAINI.

Kuwepo kwa Imam Mahdiy kunaleta matumaini. Moja katika masuala muhimu ndani ya maisha ya mwanaadamu ni kuwa na matumaini, matumaini huleta furaha na kumfanya mwanaadamu awe na shauku ya kutafuta lile analolihitajia. Kuwepo kwa Imam kunamsababishia binaadamu awe na matumaini katika maisha yake ya baadae, katika zama zilizopita inakaribia miaka alfu moja na mia nne sasa Mashia walikuwa katika mabalaa na matatizo mbali mbali ambayo yaliletwa na maadui wa kiislamu, ama kwa kutokana na kuwa thabiti katika dini yao ,kuwa na subira na kufanya jitihada za kupigana na maadui wa kiislamu wakiwa na matumaini kuna siku watafanikiwa na wataondokewa na mabalaa yote hayo, yaani baada ya kudhuhuru Imam Mahdiy na kuondowa dhulma hizo katika dunia, kwani wao wana akida ya kuwa Imam Mahdiy yuko hai na ndie atakayepigana na kila anayeleta mabalaa duniani.

KUIMARISHA DINI.

Kila mila, nchi, kabila, dini au jamii ili kulinda na kuhifadhi nidhamu zao ni lazima pawepo kiongozi ambaye atawaongoza katika njia iliyo sahihi hadi kufikia malengo yao. Kiongozi ndie anayepanga mipango na program mbali mbali ili kuleta mafanikio mazuri kwa wafuasi wake.

Imam Mahdiy ametoweka machoni mwa watu, lakini kwa hakika yeye yupo na analinda dini ya kiislamu. Imam Mahdiy anajuwa kila mbinu ambazo maadui wa kiislamu wanazitumia ili kuuondowa uislamu, na huzivunja mbinu hizo za maadui, na huwaongoza Maulamaa vipi Waislamu waweze kuhifadhi dini yao.

Natuangalie kisa kilichotokea katika nchi ya Bahrein kinachohusiana na mashia ambao wanaishi katika nchi hiyo.

Kisa hiki kimesikika katika mazungumzo ya Alameh Majlis.

"Zama zilizopita mtawala ambaye alikuwa akiitawala Bah-raein waziri wake alikuwa ana uadui na watu wa madhehebu ya Shia, siku moja alienda kwa Raisi wake na kumpa komamanga ambalo katika gamba la komamanga hilo lilikuwa limeandikwa Lailaha illa llah Muhammada rasulu-llah, Abubakar, Omar, Othman, Aliy ni makhalifa wa Mwenyeezi Mungu. Raisi baada ya kuona maandishi hayo alistaajabu sana na akasema hii ni dalili ya kuwa madhehebu ya shia sio madhehebu ya haki. Raisi akamuuliza waziri wake una mtizamo gani kuhusu Mashia ambao wanaishi

Bahrain? Waziri akasema kwa mtizamo wangu mimi ni bora kuwakusanya Mashia wote na tuwaoneshe komamanga hilo, ikiwa watakubali kwamba maandishi haya ni miujiza basi wataacha madhehebu yao, ama kama watakataa tutawapa masharti matatu,

1.Watujibu jawabu itakayotukinaisha kuhusu muujiza huu.

2.Au walipe (jaziya), (jaziya ni pesa ambazo wanatowa watu ambao sio Waislamu lakini wanaishi katika nchi ya kiislamu ili waishi kwa amani katika nchi hiyo), na sharti la tatu ni kwamba:-

3.Tuwauwe wanaume na tuwateke nyara wanawake na watoto wao, na baadae tuwanyanganye mali zao.

Raisi aliikubali rai ya Waziri wake, siku iliyofuata akawakusanya Mashia wote wa Bahrain, na kuwaonesha komamanga hilo, baadae akawambia kama mna dalili yoyote semeni, kama hamna dalili tunawauwa na kuwateka nyara wake zenu na watoto wenu, au mtowe jaziya, watu hao waliomba fursa kwa Raisi awape siku tatu kufikiria suala hilo, baada ya watu hao kukusanyika na kulifikiria suala hilo waliamua kuchagua watu kumi ambao ni wacha Mungu, na miongoni mwa watu kumi hao wakachagua tena watu watatu, na wakamwambia mmoja katika watu watatu hao kwamba aende katika jabali na aombe dua na amuulize Imam vipi wataweza kulitatua tatizo hilo, kwa sababu yeye ndiye Imam wetu. Basi mtu huyo akafanya kama alivyoambiwa na wenziwe lakini hakufanikiwa, siku iliyofuata wakamtuma mtu wa pili na yeye akafanya kama alivyoambiwa lakini pia hakufanikiwa, siku ya tatu akenda mtu mwengine ambaye anaitwa Muhammad bin Issa akaomba dua kwa Mola wake huku akilia na kuomba msaada, baada ya muda mfupi akasikia sauti ya mtu akisema:-

"Ewe Muhammd bin Issa kwa nini uko jabalini hali unalia?, Muhammad bin Issa akamuuliza wewe ni nani? Imam akasema mimi ni Sahib Zaman (yaani Imam Mahdiy), sema unalia nini na una tatizo gani, Muhammad bin Issa akasema "kama wewe ni Imam Mahdiy basi kwa hakika unajuwa mimi nna tatizo gani na hakuna umuhimu wa mimi kukuelezea" Imam akasema,"kwa hakika wewe ni msema kweli nnajua kwamba mmetokewa na tatizo na ndilo lililokuleta hapa, bwana Muhammad akasema ndio wewe unajuwa tumetokewa na matatizo gani, na wewe ndie Imam wetu,basi Imam akasema "ewe Mhuhammad bin Issa nenda katika nyumba ya yule waziri ambaye amelaaniwa na Mola wake, katika nyumba yake kuna mti wa mkomamanga, wakati ambapo mti huo ulitowa komamanga yeye alilichukua udongo ambao aliuandika maneno hayo, na baadae aliutengeneza kwa umbo la komamanga kwa hiyo kila wakati ambapo komamanga linakuwa maandishi hayo yalikuwa yakibakia katika komamanga hilo, baada ya kuwa maandishi hayo yamebakia katika gamba la komamanga ndipo alipolichukua na kulipeleka kwa Raisi wake.

Basi kesho utakwenda kwa Raisi na utamwambia kwamba utamjibu jawabu lake katika nyumba ya waziri, wakati utakapofika nyumbani kwa waziri, nenda katika chumba fulani utakuta kifurushi cha rangi nyeupe na ndani yake mna udongo, muonyeshe Raisi kifurushi hicho, na baadae umwambie kwamba muujiza wetu sisi ni huu kama utalikata kati komamanga hilo hutashuhudia kitu chengine ila moshi na udongo.

Muhammad bin Issa baada ya kusikia maelezo hayo ya Imam aliingiwa na furaha isiyo kiasi na akarudi kwa wenziwe kuwaelezea hali ilivyo, siku iliyofuata wakaenda kwa Rais na akatekeleza kila aliloambiwa na Imam. Rais Bahrain baada ya kuona muujiza huo akawa Shia na kutoa amri ya kuuliwa waziri wake kutokana na nakshi aliyoipanga.[1]


[1] Rejea katika kitabu cha Buharul-an-war, juzuu ya 52, ukurasa wa 178

MWISHO