UONGOZI WA IMAMU MUOKOZI NO.2

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

UONGOZI WA IMAMU MUOKOZI NO.2

Moja katika matatizo yaliyowakuta wafuasi wa Imam Mahdi ni kutomuona Imamu wao wakati alipotoweka, na kutokuwa na mawasiliano naye uso kwa uso, lakini inaeleweka wazi kwamba katika kipindi alichotoweka Imam kulikuwa na Naibu ambao walikuwa na mawasiliano naye , na kwa kupitia naibu hao wafuasi wengine wa Imam walikuwa wakituma barua kwa Imamu kuuliza masuala yao na kutatua matatizo yao kupitia Naibu hao, na Imam alikuwa akiwajibu kwa barua kupitia Naibu hao, na wao walikuwa wakiwapelekea wenzao jawabu. Lakini kuna baadhi ya Maulamaa wana akida ya kwamba katika zama hizi tulizonazo pia kuna watu wana mawasiliano na Imam Mahdiy, katika sehemu hii natutupilie macho baadhi ya Maulamaa ambao wana akida hiyo, na wanathibitisha kauli zao kwa kutoa kisa kifuatacho:-

Ama kabla ya kuelezea kisa hicho ni vizuri tukaangalia maelezo yafuatayo:-

1.Baadhi ya wakati mtu anaweza kumuona Imam lakini akaingiwa na hofu.

2. Mtu anaweza kumuona Imam akiwa katika hali ya kawaida na asiwe na hofu.

Kwa ufafanuzi zaidi ni kwamba inatokea wakati mtu anakutwa na matatizo na asiweze kuyatatua matatizo hayo, mfano baadhi ya watu wanakuwa wanapotea njia wakati wanapohiji Makka, na Imam huwaendea watu hao na kuwaonyesha njia, bila ya watu hao kufahamu kuwa mtu aliyewasaidia ni Imam Mahdi, Ama kuhusu kumuona Imam katika hali ya kawaida hii inategemea na hali ya mtu alivyo, watu ambao ni wacha Mungu sana mara nyingi hupata fursa ya kumuona Imam , watu hao huwa katika hali ya kawaida hawana hofu yoyote na wanakuwa wanamjua kuwa mtu aliyemjia ni Imam. Na baadhi ya watu wanafikiria kwamba kumuona Imam ni jambo rahisi sana, na kila mtu anaweza kumuona Imam. Lakini ni lazima tuzingatie kwamba sio kila mtu anayedai kuwa amemuona Imam ni kweli, kwani katika zama hizi tulizonazo watu wengi huhadithia kuwa wamemuona Imam, hali ya kuwa sio kweli.

Katika kipindi hiki ambacho Imam ametoweka watu wengi wana akida ya kuwa kama utasoma dua fulani utamuona Imam, au kama utakusanya watu na kuwapa chakula unaweza kumuona Imam,ambapo hali hii imepelekea watu kuyatia dosari madhehebu ya kishia, na kusema kuwa mashia wana akida za uongo zisizofahamika wala kukubalika, basi ni lazima ifahamike kwamba Imam ametoweka kwa idhini ya Mola wake, na anapoonana na watu anapata idhini kwa Mola wake, na anaonana na watu ambao wamezitakasa nafsi zao, wacha Mungu na ni wenye kufanya mema.

Imam huonana na wacha Mungu na wakati anapoona nao huwa kuna maslahi kwa watu hao, kuna baadhi ya watu hufanya jitihada sana ili wapate fursa ya kumuona Imam, lakini kwa sababu hakuna maslahi hawamuoni, na baadae watu hao hutokwa na matumaini, na husema kwamba sisi ni wenye kumuasi Mola kwa sababu hii hatumuoni Imam, na baadhi ya watu hupata fursa ya kumuona Imam huingiwa na ghururi na kujisifu kuwa ni wacha Mungu.Kuonana na Imam na kuzungumza nae ni neema iliyo kubwa, ama Maimamu akiwemo Imam Mahdi aliwataka wafuasi wake wasiende kuonana nae, na Maimamu wamewataka wafuasi wao waombe dua na kufanya mambo mema ili Imam adhihiri, na wawe na matumaini ya kwamba iwapo Imam atadhihiri atapambana na watu madhalimu walioleta dhulma katika dunia na ataleta uadilifu.

Imam Mahdiy anasema:-

"Ili nidhihiri haraka ombeni dua kwa wingi".

Katika sehemu hii natuangalie kisa cha bwana Mar-huwm Haaj Aliy Bagh-dadiy kinachohusiana na kuonana na Imam Mahdiy (a.s).Bwana Mar-huwm Haaj Aliy ni mcha Mungu sana katika zama zake, kila siku alikuwa akienda katika jengo ambalo amezikwa Imam Mussa bin Jaafar, na Imam Hadiy (a.s),kwa ajili ya kuyazuru makaburi hayo, kuna siku wakati alipokuwa akienda kwa ajili ya kuyazuru makaburi hayo alikuwa na mali pamoja na humsi ambazo ilim-bidi azipeleke kwa wenyewe ambao walikuwa wakiishi Najaf, moja kati ya watu hao ni bwana An-swary alimpa shilingi 20.000, bwana Muhammad Husein Kaadhiymi, 20.000, na bwana muhammad Hassan shuruwqiy 20.000, alikusudia shilingi 20.000 nyengine atakaporejea Bagh-dad ampelekee bwana Al-yaasin, akarejea Bagh-dad siku ya jumatano, ama kwanza alienda katika jengo ambalo amezikwa Imam Mussa bin Jaafar na Imam Hadiy ili kuzuru makaburi yao, baada ya hapo alienda kwa bwana Al-yaasin na kupeleka pesa hizo, na alimuomba kuwa zilizobakia atazipeleka au atampa mtu ambaye ana uhakika naye azipeleke,alipotaka kumuaga bwana Al-yaasin akamuomba abakie pale siku ile, lakini alimuomba radhi arudi nyumbani kwa sababu alikuwa na kazi siku hiyo, akamuaga na kuelekea Bagh-dad, wakati alipokuwa akitembea, karibu ya mail tatu akaonana na mtu ambaye alikuwa amevaa kilemba cheusi kilichochanganyika na rangi ya kijani, na alikuwa akielekea katika jengo ambalo amezikwa Imam Mussa bi Jaafar na Imam Hadiy ili kuzuru makaburi yao, wakasalimiana na kupeana mikono, baadaye akamuuliza unaenda wapi?, bwana Haaj Aliy Baghdad akamwambia nnatoka kuzuru makaburi na sasa nnarejea Bagh-dad, akamwambia leo ni usiku wa Ijumaa ni bora zaidi kama utarejea ulikotoka na usiku waleo ubakie huko huko, bwana Haj-Aliy akamwabia siwezi kwa sababu nna kazi nyumbani, mtu huyo akamwambia unaweza Bwana Haj Aliy anasema "alimuomba bwana Al-yaasin mtu huyo akamjibu nisikujue vipi na wewe ni mwenye kupeleka haki za watu bila ya kufanya hiyana katika haki hizo?. Bwana Haj- Aliy akamuuliza haki gani? akamwambia haki ambazo umewapa wakili wangu, akamuuliza Wakili wako ni nani? akamwambia Sheikh Muhammad Hassan, akasema hivi bwana Hassan ni wakili wako?, akamjibu ndiyo.

Bwana Haaj-Aliy akastaajabishwa na maneno ya mtu huyo, akafikiria kwamba ni miongoni mwa rafiki zake lakini amemsahau, kwa sababu walipoonana alimwita kwa jina lake, na alikuwa ana shaka kwamba mtu huyo anamaanisha pesa za humsi ambazo zimebakia nizipeleke kwa sababu ni katika mali za Mtume Muhammad (s.a.w.w), akamwambia mimi nna pesa hizo lakini nimeomba ruhusa kubakia na pesa hizo kwa sababu nnazihitajia katika kipindi hiki, mtu huyo alitabasamu na kusema ndio baadhi ya pesa umezipeleka kwa Wakili wangu Najaf, bwana Haj- Aliy akamuuliza hivi Allah anaridhia mimi kukopa pesa ambazo ni humsi za Mtume Muhammad (s.a.w.w)?, mtu huyo akasema ndio hapana shaka. Haaj- aliy alishangaa kwa nini mtu huyo anasema kwamba Maulamaa hao ni wakili wake, lakini akaona ni bora awachilie mbali mazungumzo hayo, na akaanza kuzungumzia mambo mengine akamuuliza ewe bwana wangu hivi ni kweli mtu anayesoma ziyara ya Imam Hussein siku ya Ijumaa Mwenyeezi Mungu humuondoshea adhabu mtu huyo, akamjibu ndiyo, na akamuona bwana huyo analia, baada ya muda mfupi akaona tayari wameshafika mahali ambapo walikuwa wanakwenda, wakasimama mbele ya jengo hilo na kumwambia soma ziyara (dua) ya Imam hussein akamjibu kuwa hawezi kusoma vizuri, akamwambia basi mimi nasoma, akaanza kusoma kwa kumtolea salam Mtume na Maimamu wote, alipofikia kumtolea salam Imam Askariy akamuuliza hivi wewe unamjua Imam wako wa mwisho akamwambia ndiyo, akamwambia basi mtolee salamu, akamsalimia kwa kusema asalamu alaykum ya Hujjatu llahi, ya Saahibu Zamani, ya ibnil-Hassan, bwana huyo alitabasam na kusema waalaykum salam warahmatu llahi wabarakatuhu. Baadaye wakaingia ndani ya jengo hilo na akamwambia soma ziyara akamjibu ewe bwana wangu siwezi kusoma vizuri, akasoma yeye ziyara ya Amiynu-llah, akamuuliza unasoma ziyara ya babu yangu bwana Hussein, akamjibu ndio leo ni usiku wa Ijumaa ni siku ya kusoma ziyara ya Imam Hussein, akasoma ziyara hiyo, na kwa sababu ulikuwa umefika wakati wa sala wa Magharibi, wakasali sala ya magharibi lakini alipomaliza hakumuona tena mtu huyo,na alimtafuta sana lakini hakumuona, akaanza kujiuliza kwa nini alimwita kwa jina lake?, na kwanini alimtaka arudie alikotoka, na kwa nini aliwataja Maulamaa wakubwa kuwa ni wakili wake?,na baadae baada ya muda mchache mtu huyo alitoweka na asimuone tena, akahakikisha kwamba mtu huyo ni Imam Zamani lakini alishindwa kumuelewa kwa mara moja[1].


[1]Rejea kitabu Buharul-an-war, juzuu ya 53, ukurasa wa 315, wannajmu-thaqib, historia ya 31.
MWISHO