WAFUASI WA KWELI WA MITUME NO.1

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

WAFUASI WAKWELI WA MITUME NO.1

* Ni alama gani zinazoonesha ukweli wa wafuasi wa Mitume?.

* Kuna athari gani katika kuwakubali na kuwafuata Mitume?.

WAFUASI WAKWELI WA MITUME

Kwa hakika kuwatii Mitume ni kumtii Mwenyeezi Mungu, kama inavyosema Qur-ani takatifu:-

مَّنْ يُطِعِ الرَّسُولَ فَقَدْ اَطَاعَ اللّهَ وَمَن تَوَلَّي فَمَا اَرْسَلْنَاكَ عَلَيْهِمْ حَفِيظاً[1]

kumt'ii Mtume basi ndio amemt'ii Mwenyezi Mungu. Na anaye kengeuka, basi Sisi hatukukutuma wewe uwe ni mlinzi wao.

Mitume ndio wenye kuchukua na kubeba Wahyi wa Mwenyeezi Mungu, na vile vile ndio wenye kuufikisha ujumbe huo wa Mwenyeezi Mungu kwa watu, kama inavyosema Qur-ani:-

وَمَا يَنطِقُ عَنِ الْهَوَي . إِنْ هُوَ إِلاَّ وَحْيٌ يُوحَي[2]

Wala hatamki kwa matamanio.

Hayakuwa haya ila ni ufunuo ulio funuliwa.

Mitume, mbali ya kuwa wana wadhifa wa kufikisha ujumbe wa Mwenyeezi Mungu kwa watu, vile vile ni viongozi walioteuliwa na Mwenyeezi Mungu, na ni Mahakimu walioletwa katika jamii ili kutatua matatizo na kuwasaidia wanaadamu.

وَمَا اَرْسَلْنَا مِن رَّسُولٍ إِلاَّ لِيُطَاعَ بِإِذْنِ اللهِ وَلَوْ اَنَّهُمْ إِذ ظَّلَمُواْ اَنفُسَهُمْ جَآؤُوكَ فَاسْتَغْفَرُواْ اللّهَ وَاسْتَغْفَرَ لَهُمُ الرَّسُولُ لَوَجَدُواْ اللّهَ تَوَّاباً رَّحِيماً[3]

Na hatukumtuma Mtume yeyote ila at'iiwe kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na lau pale walipo jidhulumu nafsi zao wangeli kujia, wakamwomba Mwenyezi Mungu msamaha, na Mtume akawaombea msamaha, hapana shaka wangeli mkuta Mwenyezi Mungu ni Mwenye kupokea toba na Mwenye kurehemu.

Kwa hiyo kuwatii Mitume katika mambo ya hukumu, kwa mfano mambo ya kiserikali, kwa hakika ni kumtii Mwenyeezi Mungu.

Wafuasi wa kweli na waaminifu wa Mitume ni wale ambao wanajiweka mbali na mabaya ya matamanio ya nafsi zao, na wanajiepusha na kukhalifu amri za Mwenyeezi Mungu na Mitume yao. Na hawako tayari kughilibiwa na shetani, na humtegemea Mwenyeezi Mungu katika mfumo wa maisha yao ya kila siku, kwa upande mwengine huhifadhi dini na akida zilizo nyoyoni mwao, na kupigana na  makafiri na mataghuti ili kusimamisha dini ya Mola wao, na kwa kumtii Mwenyeezi Mungu na Mitume yake hunufaika na kuneemeka na neema zake Allah (s.w):-

وَمَن يُطِعِ اللّهَ وَالرَّسُولَ فَاُوْلَـئِكَ مَعَ الَّذِينَ اَنْعَمَ اللّهُ عَلَيْهِم مِّنَ النَّبِيِّينَ وَالصِّدِّيقِينَ وَالشُّهَدَاء وَالصَّالِحِينَ وَحَسُنَ اُولَـئِكَ رَفِيقاً[4]

Na wenye kumt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume, hao wa pamoja na wale alio waneemesha Mwenyezi Mungu miongoni mwa Manabii, na Masiddiqi, na Mashahidi, na Watu wema. Na uzuri ulioje kuwa pamoja na watu hao!

*Kila watakaofanya mema wataingia peponi, na kila watakaoingia peponi watakutana na wenzao wa peponi wachanganyike, katika baadhi za nyakati, japokuwa wako mahala mbali mbali kwa mnasaba wa daraja walizopewa kwa amali zao ambazo hazikuwa namna moja. Lakini juu ya hivi watakutana.

Miongoni mwa daraja zilizotajwa hapa ni daraja ya.

a)Unabii . b) Ussidiqi . c) Ushahidi . d)Usalih.

Mtu salih ni yule anayetekeleza haki za Mwenyeezi Mungu zilizo juu yake na kutekeleza haki za viumbe wenziwe zilizo juu yake, kwa mwisho wa uweza wake.

Na Shahidi ni anayefanya haya na akapata bahati ya kuuawa kwa ajili ya dini.

Na Saddiqi ni kama yule salih. Lakini natekeleza kwa ukamilifu zaidi kabisa.

Na Unabii ni kupindukia mipaka ya ubinaadamu kwenda umalaikani.

Katika sehemu hii tutaelezea wafuasi wa kweli na waaminifu wa Mitume, na kubainisha baadhi ya sifa za watiifu wa Mwenyeezi Mungu, na hatima ya wale wanaomtii Mwenyeezi Mungu na Mitume yake.

[1] Suratun-Nisaa Aya ya 80

[2] Suratun Najm Aya ya 3-4

[3] Suratun Nisaa Aya ya 64

[4] Suratun Nisaa Aya ya 69

MWISHO