DHAHIRI NA BATINI YA QUR_ANI NO.1

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

DHAHIRI NA BATINI YA QUR_ANI NO.1

Taawili (tafsiri ya dhahiri shahiri) ni tafsiri yenye kumurika maneno kupitia darubini ya udhahiri wa mambo, na maana dhahiri za maneno zilivyo.

Taawili ni kufasiri na kutafuta maana za maneno kupitia darubini ya nguvu za kiakili zenye uwezo wa kujua maana dhahiri na kuilenga ile maana halisi iliyojificha ndani ya maneno. Kwa hiyo kwa msingi huo tunaweza kusema kuwa tafsiri ya dhahiri shahiri ni tafsiri ya wazi yenye kuonekana dhahiri shahiri bila ya mashaka yoyote.

Taawili ni tafsiri mficho ambayo maana yake ni lazima itafutwe huko mafichoni iliko, tafsiri mficho ni yenye kuyasaka na kuyatafuta maneno yaliyo mafichoni, (yaani maneno yaliyo batini, yaani maneno yaliyojificha ndani ya ibara, au sentensi). Kwa mfano:-

Mwenye kufasiri Qur-ani kwa njia ya dhahiri anatumia akili yake kwa kiwango kidogo tu, wala hatakiwi kutafakari kwa kiwango kikubwa, ama kwa yule mfasiri ambaye anaifasiri Qur-ani kwa ubatini wake, basi mfasiri huyo atakuwa anatumia akili na kiwango kikubwa cha kutafakari. Natuzingatie mfano huu wa Aya unaoonyesha tafsiri ya dhahiri na tafsiri ya batini, Allah (s.w) anasema:-

إِنَّ الَّذِينَ يُبَايِعُونَكَ إِنَّمَا يُبَايِعُونَ اللهَ يَدُ اللهِ فَوْقَ اَيْدِيهِمْ فَمَن نَّكَثَ فَإِنَّمَا يَنكُثُ عَلـٰي نَفْسِهِ وَمَنْ اَوْفَي بِمَا عَاهَدَ عَلَيْهُ اللهَ فَسَيُؤْتِيهِ اَجْراً عَظِيماً[1]

Bila ya shaka wanao fungamana nawe, kwa hakika wanafungamana na Mwenyezi Mungu. Mkono wa Mwenyezi Mungu uko juu ya mikono yao. Basi avunjaye ahadi hizi anavunja kwa kuidhuru nafsi yake; na anaye tekeleza aliyo muahadi Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu atamlipa ujira mkubwa.

Na katika Aya nyenginea anasema:-

وَقَالَتِ الْيَهُودُ يَدُ اللهِ مَغْلُولَةٌ غُلَّتْ اَيْدِيهِمْ وَلُعِنُواْ بِمَا قَالُواْ بَلْ يَدَاهُ مَبْسُوطَتَانِ يُنفِقُ كَيْفَ يَشَاءُ وَلَيَزِيدَنَّ كَثِيراً مِّنْهُم مَّا اُنزِلَ إِلَيْكَ مِن رَّبِّكَ طُغْيَاناً وَكُفْراً وَاَلْقَيْنَا بَيْنَهُمُ الْعَدَاوَةَ وَالْبَغْضَاء إِلَي يَوْمِ الْقِيَامَةِ كُلَّمَا اَوْقَدُواْ نَاراً لِّلْحَرْبِ اَطْفَاَهَا اللّهُ وَيَسْعَوْنَ فِى الاَرْضِ فَسَاداً وَاللّهُ لاَ يُحِبُّ الْمُفْسِدِينَ[2]

Na Mayahudi walisema: Mkono wa Mwenyezi Mungu umefumba. Mikono yao ndiyo iliyo fumba, na wamelaaniwa kwa sababu ya waliyo yasema. Bali mikono yake iwazi. Hutoa apendavyo.

Kwa yakini yaliyo teremshwa kwako kutoka kwa Mola wako Mlezi yatawazidisha wengi katika wao uasi na kufuru. Na Sisi tumewatilia uadui na chuki baina yao mpaka Siku ya Kiyama. Kila mara wanapo washa moto wa vita, Mwenyezi Mungu anauzima. Na wanajitahidi kuleta uharibifu katika ardhi. Na Mwenyezi Mungu hawapendi waharibifu.

Maelezo kuhusiana na Aya:

Katika Aya hiyo unaonekana moto wa Mayahudi unavyowaka na kuzimika mara kwa mara, na mwisho utazimika kabisa, Mwenyeezi Mungu kasema Mayahudi hawatapata ukubwa ulimwenguni ila kwa sharti mbili:-

a) Washikamane na mwenendo mzuri aliyouweka Mwenyeezi Mungu, au

b) Wawe wanapata msaada kwa dola nyenginezo; kama tunavyoona hivi sasa lakini wenyewe Mayahudi tu peke yao hawataweza kuwa chochote maishani mwao.

c) Mayahudi eti wanamtia mori Mwenyeezi Mungu azidi kuwapa kwa kusema:-

“Siku hizi mkono wa Mwenyeezi Mungu hautoi sana”.

Mwenye kufasiri aya hizo kutokana na udhahiri wake atafasiri kuwa Mwenyeezi Mungu ana mikono, kutokana na neno “yad” lililokuja katika Aya hizo, likiwa na maana ya mkono, basi inawezekana kwa mfasiri atakayefasiri kwa udhahiri wake akasema kuwa mkono wa Mwenyeezi Mungu uko juu ya mikono yao, hali ya kwamba katika Qur-ani takatifu kuna Aya zinazopinga kuwa Allah (s.w) ana mkono, kwa sababu Yeye Allah (s.w) anasema kuwa Yeye hajafanana na kitu chochote pale aliposema:-

فَاطِرُ السَّمَاوَاتِ وَالاَرْضِ جَعَلَ لَكُم مِّنْ اَنفُسِكُمْ اَزْوَاجاً وَمِنَ الاَنْعَامِ اَزْوَاجاً يَذْرَؤُكُمْ فِيهِ لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ وَهُوَ السَّمِيعُ البَصِيرُ[3]

Yeye ndiye Muumba mbingu na ardhi, amekujaalieni mke na mume katika nafsi zenu, na katika nyama hoa dume na jike, anakuzidishieni namna hii. Hapana kitu kama mfano wake. Naye ni Mwenye kusikia Mwenye kuona.

[1] Surat Al-Fat-h Aya ya 10.

[2] Surat Al-Maidah Aya ya 64.

[3] Surat Ash-Shuura Aya ya 11

 

MWISHO