Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

WALIOWAHALIFU MITUME NO.2

0 Voti 00.0 / 5

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

WALIOWAKHALIFU MITUME NO.2

* Kwa nini baadhi ya watu walisimama kidete kuwakhalifu Mitume?

* Waliowakhalifu Mitume walitumia njia gani katika kupingana na Mitume?.

Katika makala iliyopita tulielezea sababu zilizowafanya baadhi ya watu kuwakhalifu Mitume, katika makala hii tutaendelea kuelezea sababu na dalili nyengine.

DALILI ZILIZOWAFANYA WAWAKHALIFU MITUME.

Tangu hapo mwanzo, baada tu ya Mitume kupewa utume walikumbana na watu ambao waliwakhalifu kutokana na malinganio waliyokuja nayo Mitume hiyo. Kwa sababu malinganio hayo yalikuwa hayawiani na itikadi zao au manufaa yao ambayo walikuwa wakiyahitajia, hivyo watu hao walisimama kedete kuupinga ujumbe wa Mwenyeezi Mungu waliokuja nao Mitume hiyo.

Qur-ani Karym imeelezea kwa uwazi dalili zilizowafanya watu hao wawakhalifu Mitume, njia walizotumia katika kupingana nao na hatima ya watu hao, katika somo hili tutaelezea njia hizo, kwa sababu kuzifahamu njia hizo kutawapelekea wafuasi wa Mitume kuzifahamu hila za maadui wao, na kuwafanyia wepesi katika kustahamili tabu na matatizo watakayoweza kuyapata.

4. Kudidimia na kuzama katika upotofu na mashaka.

Qur-ani Kariym inabainisha kauli ya watu wa Jahannam walipokuwa wakimjibu Allah (s.w) suala lake linalosema:- Hivi kweli hamkusomewa Aya zangu?

قَالُوا رَبَّنَا غَلَبَتْ عَلَيْنَا شِقْوَتُنَا وَكُنَّا قَوْماً ضَالِّينَ[1]

Mola wetu Mlezi! Tulizidiwa na uovu wetu na tukawa watu tulio potea.

NJIA WALIZOTUMIA MAADUI WA KIISLAMU KATIKA KUPINGANA NA MITUME.

Mitume siku zote walikuwa wakisumbuliwa na kuudhiwa na maadui wa kiislamu, wenye kibri, wenye mali, majahili, n.k. kila mmoja kati yao walikuwa wakiwapa mateso wafuasi wa Mitume kwa upande wake, na walikuwa wakiweka vikwazo na vizuizi ili harakati za Kiislamu zisiendelee, miongoni mwa vizuizi hivyo ni kama hivi vifuatavyo:-

1. Kuwakejeli Mitume na kuwadhihaki.

Madai ya Utume yaliyokuwa yakidaiwa na watu watukufu, ambao walikuwa na uhusiano na ulimwengu wa kighayb (yaani ulimwengu usiokuwa wa kimada) yaliwashangaza maadui wa Kiislamu,kwani kwa madai yao hayo hawakuweza kunufaika na anasa za dunia, wala hawakuweza kujipatia mali au vyeo katika jamii, hivyo iliwafanya watu hao kuleta vizuizi vile vile kutokubaliana na madai hayo. Na hata waliwadhihaki Mitume, kuwadharau, kuwakejeli, na kuwafanyia masihara, kama anavyosema Allah (s.w):-

يَا حَسْرَةً عَلـٰي الْعِبَادِ مَا يَاْتِيهِم مِّن رَّسُولٍ إِلاَّ كَانُوا بِهِ يَسْتَهْزِئُون[2]

Nawasikitikia waja wangu. Hawajii Mtume ila wao humkejeli.

Mbali ya kukejeliwa kwa Mitume, waumini na wafuasi wa Mitume pia walifanyiwa masihara na kukejeliwa. Kama navyosema Allah(s.w_:-

إِنَّ الَّذِينَ اَجْرَمُوا كَانُواْ مِنَ الَّذِينَ آمَنُوا يَضْحَكُونَ[3]

Kwa hakika wale walio kuwa wakosefu walikuwa wakiwacheka walio amini.

2.WALIWATUHUMU MITUME, KUWA WAO NI WACHAWI NA WENDAWAZIMU.

Baada ya Mitume kudai madai waliyokuja nayo, kuwa wao ni Mitume iliyokuja kwa idhini ya Mwenyeezi Mungu, na kutokuwa na nguvu zozote za kimada, hivyo walileta miujiza ili kuthibitisha madai yao, na walistahamili tabu, mashaka na mateso waliyokuwa wakifanyiwa na maadui zao, na maadui baada ya kuona kuwa hawafanikiwi na mbinu zao walitafuta mbinu nyengine zitakazoweza kuwazuia Mitume katika kuwalingania watu katika dini ya haki, hivyo wale waliowakhalifu waliwazulia na kuwatuhumu Mitume kuwa wao ni wachawi na wendawazimu. Kama tunavyosoma ndani ya Qur-ani:-

كَذٰلِكَ مَا اَتَي الَّذِينَ مِن قَبْلِهِم مِّن رَّسُولٍ إِلاَّ قَالُوا سَاحِرٌ اَوْ مَجْنُونٌ[4]

Basi ndio hivyo hivyo, hakuwajia kabla yao Mtume ila walisema: Huyu ni mchawi au mwendawazimu.

*Aya hii inaonyesha kuwa siyo Nabii Muhammad tu alipingwa, bali Mitume yote ilipingwa pia.

Na kwa upande mwengine, wafuasi wa Mitume pia walituhumiwa na kuambiwa kuwa wao ni wapumbavu.

وَإِذَا قِيلَ لَهُمْ آمِنُواْ كَمَا آمَنَ النَّاسُ قَالُواْ اَنُؤْمِنُ كَمَا آمَنَ السُّفَهَاء اَلا إِنَّهُمْ هُمُ السُّفَهَاء وَلَـكِن لاَّ يَعْلَمُونَ[5]

Na wanapo ambiwa: Aminini kama walivyo amini watu. Husema: Tuamini kama walivyo amini wapumbavu? Hakika wao ndio wapumbavu, lakini hawajui tu.

 

[1] Surat Al-Muuminuun Aya ya 106

[2] Surat Yaasin Aya ya 30

[3] Surat Mutafi-fiyna Aya ya 29

[4] Surat Adh-Dhaariyat Aya ya 52

[5] Surat Albaqarah Aya ya 13

MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini