Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

SHARTI ZA KUKAMILIKA KWA MWANAADAMU

0 Voti 00.0 / 5

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

SHARTI ZA KUFIKIA MJA KATIKA UKAMILIFU NO.3

Tukiendelea na mada yetu inayohusiana na masharti na vizuizi vinavyompelekea mwanaadamu asiweze kufikia katika ukamilifu, katika makala hii tutaelezea masharti sharti jengine linalomfanya mwanaadamu asifikie katika ukamilifu. Sharti hilo ni:-

Kunufaika na muongozo wa Mitume na Maimamu (a.s).Ili tumfahamu Mwenyeezi Mungu zaidi ni lazima tujiepushe na yale aliyotukataza, ili tunufaike na uongofu na uwalii wa Mitume na Maimamu (a.s), kwa sababu Mtume Muhammad (s.a.w.w) ndio kiumbe bora aliye karibu na Mwenyeezi Mungu, na ni m-bora zaidi kuliko hata Malaika, kama anavyosema katika Qur-ani:-

ثُمَّ دَنَا فَتَدَلَّي  .  فَكَانَ قَابَ قَوْسَيْنِ اَوْ اَدْنَي

Kisha akakaribia na akateremka.

Akawa ni kama baina ya mipinde miwili, au karibu zaidi.

Kwa hiyo Mtume Muhammad (s.a.w.w), ambaye ndiye mpokeaji wa wahyi kutoka kwa Mwenyeezi Mungu, ndiye m-bora kuliko wengine, ambaye anaweza kuwaongoza wanaadamu kufikia katika njia yake Allah (s.w).

Na anaweza kuwafahamisha wanaadamu yale ambayo hawawezi kuyafahamu kiakili. Kama anavyosema Allah (s.w):-

كَمَا اَرْسَلْنَا فِيكُمْ رَسُولاً مِّنكُمْ يَتْلُو عَلَيْكُمْ آيَاتِنَا وَيُزَكِّيكُمْ وَيُعَلِّمُكُمُ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ وَيُعَلِّمُكُم مَّا لَمْ تَكُونُواْ تَعْلَمُونَ[1]

Kama tulivyo mtuma Mtume kwenu anaye tokana na nyinyi, anakusomeeni Aya zetu na kukutakaseni na kukufundisheni Kitabu na hikima na kukufundisheni mliyo kuwa hamyajui.

Vile vile watu wa nyumba ya Mtume (Ahlulbayt (a.s) ambao wapo karibu na Mwenyeezi Mungu na Mtume Muhamad (s.w), na wana elimu ya kutosha ya kuwaelimisha wanaadamu, wanaweza kuwa kilengo bora cha kuwafuata, katika dua ya kumail ambayo ni ya Imamu aliy (a.s), na dua ya arafah, ambayo ni ya Imamu Husseyn (a.s) inaonyesha nuru ya elimu waliyonayo watu hao watukufu, Imamu Aliy (a.s) anasema:-

ما شککت فی الحق مذ رایته[2]

Yaani: sijaingiwa na shaka  tangu pale nilipoishuhudia haki . kwa hiyo shetani au bilisi hawezi kuwaghilibu na kuwapotoa watu hao, kama anavyosema Allah (s.w):-

قَالَ رَبِّ بِمَا اَغْوَيْتَنِى لاُزَيِّنَنَّ لَهُمْ فِى الاَرْضِ وَلاُغْوِيَنَّهُمْ اَجْمَعِينَ  .  إِلاَّ عِبَادَكَ مِنْهُمُ الْمُخْلَصِينَ[3]

Akasema: Mola wangu Mlezi! Ilivyo kuwa umenitia makosani, basi nahakikisha nitawazaini hapa duniani na nitawapoteza wote,Ila waja wako walio safika.

Kwa hiyo natija ya somo hilo ni kwamba ili tumfahamu Mwenyeezi Mungu na kuutambua uhakika wake, majina na sifa za Mwenyeezi Mungu , Mitume na watu wa nyumba ya Mtume ndio nyenzo bora zitakazotuwezesha kumfahamu Mwenyeezi Mungu.

Maelezo kwa ufupi kuhusiana na somo lililopita.

*wanaadamu ni lazima wazifahamu sifa za Mwenyeezi Mungu ili kujiepusha na kumshabihisha Mwenyeezi Mungu.

*Miongoni mwa masharti yatakayomsaidia mwanaadamu kumfahamu Mwenyeezi Mungu, ni kuwa mcha Mungu, kuishi katika mazingira ambayo viongozi wake ni watu waaminifu katika kutii amri za Mola wao, kutokuwa na chuki au kuiga mambo bila ya kuwa na elimu nayo au kuiga yaliyofanywa na wengine, na kuwa karibu na Mwenyeezi Mungu kwa kumtakasa na kumsabihi kila wakati.

Masuala.

1.Kwa nini Imamu Aliy (a.s) amepambanua baina ya sifa za Mwenyeezi Mungu, na kukamilika kiilhlasi yaani wanaadamu hawawezi kumfahamu Mwenyeezi Mungu kwa sifa zake tu – kwa sababu Utukufu wa Mwenyeezi Mungu ni wa juu kabisa kiasi ya kwamba wanaadamu hawawezi wakaudiriki utukufu huo.

2. Kumcha Mwenyeezi Mungu kunaleta athari gani katika kumfahamu Mwenyeezi Mungu?.

3. Mitume ya Mwenyeezi Mungu, na watu wa nyumba ya Mtume, vipi wanaweza kuwasaidia wanaadamu katika kumfahamu Mwenyeezi Mungu?.

4.Kwa kuzingatia mtizamo wa Qur-ani Elezea vipi tunakatazwa kuiga matendo ya wengine?.

 

[1] Suratul-Baqarah Aya ya 151

[2] Nahjulbalagha, hutuba ya 4

[3] Suratul-Hijr Aya ya 39-40

MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini