MAKHALIFA WATAKAOENDELEZA NJIA ZA MITUME

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

* Hivi kweli ni lazima Mitume iwe na Makhalifa baada ya wao?.

* Ni watu wa aina gani wanaostahiki kuwa ni Makhalifa wa Mitume?.

MAKHALIFA WANAOENDELEZA NJIA ZA MITUME.

Malengo na madhumuni waliyokuja nayo Mitume ni kuwaongoza watu katika njia ya Mwenyeezi Mungu, Mitume huwaongowa watu na kuwaongoza katika njia ya saada iliyo kamilifu.

Kwa sababu hiyo basi ili kufikia katika malengo yao hayo, hawakuegemea na mawaidha au ujumbe waliopewa na Mola wao tu, bali walistahamili tabu na mashaka za makafiri na wale waliowapinga. Vile vile walifanya jitihada na kuwa viongozi wema na walio bora ili kuondoa serikali za za kitaghuti,na kupinga suna za kijahilia.

Vile vile walifanya jitihada katika kupitisha hukumu za Mwenyeezi Mungu na kujenga Serikali ya Kiislamu iliyohukumu kwa uadilifu, na mategemeo yao makubwa ni kuendeleza na kudumisha ujumbe wa Mwenyeezi Mungu, ili kuwaongoza wanaadamu na kudumisha uongofu utakaowasaidia wanaadamu hao katika maisha yao ya kila siku. Basi na tutupilie macho kauli ya Nabii Ibrahimu (a.s) pale alipoomba dua kwa Mola wake kwa kusema:-

رَبَّنَا وَابْعَثْ فِيهِمْ رَسُولاً مِّنْهُمْ يَتْلُو عَلَيْهِمْ آيَاتِكَ وَيُعَلِّمُهُمُ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ وَيُزَكِّيهِمْ إِنَّكَ اَنتَ العَزِيزُ الحَكِيمُ[1]

Ewe Mola Mlezi wetu! Waletee Mtume anaye tokana na wao, awasomee Aya zako, na awafundishe Kitabu na hikima na awatakase. Hakika Wewe ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima.

Baada ya jitihada na stahamala walizozifanya Mitume hiyo, wasiwasi mkubwa waliokuwa nao ni kusita au kusimama kwa mapinduzi yaliyokuwa na baraka ya Kiislamu, na kuhofia watu kurudi katika ukafiri na ujahili. Na kwa sababu hiyo basi wadhifa muhimu waliokuwa nao Mitume ni kwamba, pindi walipokuwa wakienda safari kutoka mji kwenda  mji mwengine, au baada ya kufariki kwao, walichagua na kuwaarifisha watu Mtume atakayekuja baada ya wao. Au waliwachagua viongozi na Makhalifa wanaostahiki kuwa na ukhalifa huo baada ya Mtume huyo aliyekuwepo kuondoka au kufariki.

Kwa mfano, Nabii Mussa (a.s) wakati ilipotimia miadi ya Mola wake alimteua kaka yake kuwa khalifa badala yake, na akamwambia:-

وَوَاعَدْنَا مُوسَي ثَلاَثِينَ لَيْلَةً وَاَتْمَمْنَاهَا بِعَشْرٍ فَتَمَّ مِيقَاتُ رَبِّهِ اَرْبَعِينَ لَيْلَةً وَقَالَ مُوسَي لاَخِيهِ هَارُونَ اخْلُفْنِى فِى قَوْمِى وَاَصْلِحْ وَلاَ تَتَّبِعْ سَبِيلَ الْمُفْسِدِينَ[2]

Tulimuahidi Musa masiku thalathini na tukayatimiza kwa kumi; ikatimia miadi ya Mola wake Mlezi masiku arubaini. Na Musa akamwambia nduguye Haarun: Shika mahala pangu kwa watu wangu na utengeneze wala usifuate njia ya waharibifu.

* Nabii Mussa (a.s) ndiye aliyekuwa mkubwa kwa utume kuliko Nabii Haruni, ingawa Nabii Haruni ni mkubwa kuliko nabii Musa kwa umri.

Mitume mingi ilikuwa ikipendelea kizazi chao au watoto wao wanufaike na saada hiyo tukufu ya kupewa cheo cha utume au Uimamu. Kama pale Hadharati Ibrahimu (a.s) alipopewa cheo cha Uimamu alimuuliza Mola wake:-

وَإِذِ ابْتَلَي إِبْرَاهِيمَ رَبُّهُ بِكَلِمَاتٍ فَاَتَمَّهُنَّ قَالَ إِنِّى جَاعِلُكَ لِلنَّاسِ إِمَاماً قَالَ وَمِن ذُرِّيَّتِى قَالَ لاَ يَنَالُ عَهْدِى الظَّالِمِينَ[3]

Na Mola wake Mlezi alipo mjaribu Ibrahim kwa kumpa amri fulani, naye akazitimiza, akamwambia: Hakika Mimi nitakufanya uwe mwongozi wa watu. Akasema: Je, na katika vizazi vyangu pia? Akasema: Ahadi yangu haitawafikia wenye kudhulumu.

* Nabii Ibrahimu alipofanyiwa mitihani yote ya amri za Mwenyeezi Mungu na makatazo yake na ya mambo mengine, na akafuzu, Mwenyeezi Mungu alimwambia kuwa kampa daraja ya Uimamu juu ya viumbe. Nabii Ibrahimu alifurahi akashukuru na akamuomba kuwa na katika kizazi chake wapewe Uimamu pia, Mwenyeezi Mungu akamwambia kuwa Nasaba tupu ya kunasibika naye (Nabii Ibrahimu) haitakuwa sababu ya kuwapatia Uimamu – sharti wafanye amali nzuri - .
Na yote haya ni kufundishwa na sisi pia kuwa tusitegemee nasabu zetu, siyo nguzo ya kuegemea, nguzo ya kuegemea ni amali njema zinazofanywa kwa nia njema.

 

[1] Surat- Albaqarah Aya ya 129

[2] Surat Al-Aaraf Aya ya 142

[3] Surat Albaqarah Aya ya 124

MWISHO