DHATI YAKE ALLAH (S.W)

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

SIFA ZAKE MOLA MTAKATIFU

DHATI YAKE ALLAH (S.W)

 DHATI YA ALLAH (S.W) IMETAKASIKA NA ISIYOKUWA NA MWISHO.
Sisi tunaamini kuwa dhati  ya Mwenyeezi Mungu imeenea sehemu zote, naye hana mwanzo wala mwisho, dhati hiyo inaonekana katika elimu yake, qudra ya utukufu wake, kubakia kwake milele katika sehemu zote na zama zote, na kwa sababu hiyo basi ndio tukasema kuwa Mwenyeezi Mungu hana sehemu maalumu wala kipindi maalumu, kwa sababu sehemu au nafasi na zama zina kiwango maalumu, ijapokuwa Mwenyeezi Mungu hana sehemu maalumu wala zama maalumu lakini Yeye yuko katika sehemu na zama zote, kwa sababu dhati ya utukufu wake iko juu zaidi kuliko sehemu na zama, kama tunavyosoma ndani ya Qur-ani:-

وَهُوَ الَّذِى فِى السَّمَاء إِلَهٌ وَفِى الاَرْضِ إِلَهٌ وَهُوَ الْحَكِيمُ الْعَلِيمُ[1]

Na Yeye ndiye Mungu mbinguni, na ndiye Mungu katika ardhi. Naye ndiye Mwenye hikima, Mwenye ujuzi.
هُوَ الَّذِى خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالاَرْضَ فِى سِتَّةِ اَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَي عَلـٰي الْعَرْشِ يَعْلَمُ مَا يَلِجُ فِى الاَرْضِ وَمَا يَخْرُجُ مِنْهَا وَمَا يَنزِلُ مِنَ السَّمَاء وَمَا يَعْرُجُ فِيهَا وَهُوَ مَعَكُمْ اَيْنَ مَا كُنتُمْ وَاللهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ[2]

Yeye ndiye aliye ziumba mbingu na ardhi katika siku sita; kisha akakaa vyema juu ya enzi. Anayajua yanayo ingia katika ardhi na yanayo toka humo, na yanayo teremka kutoka mbinguni, na yanayo panda humo. Naye yu pamoja nanyi popote mlipo. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona mnayo yatenda.

Ndio, Mwenyeezi Mungu yuko karibu na wanaadamu, na Mwenyeezi Mungu yuko ndani ya nafsi za wanaadamu, Naye yuko katika sehemu zote, hali ya kwamba hana sehemu, makani, wala zama maalumu.

وَلَقَدْ خَلَقْنَا الإِنسَانَ وَنَعْلَمُ مَا تُوَسْوِسُ بِهِ نَفْسُهُ وَنَحْنُ اَقْرَبُ إِلَيْهِ مِنْ حَبْلِ الْوَرِيدِ[3]

Na hakika tumemuumba mtu, nasi tunayajua yanayo mpitikia katika nafsi yake. Na Sisi tuko karibu naye kuliko mshipa wa shingoni mwake.

Maelezo yanayopatikana katika Aya hiyo.

Aya hiyo inataja ujuzi wa Mwenyeezi Mungu na uweza wake.

هُوَ الاَوَّلُ وَالآخِرُ وَالظَّاهِرُ وَالْبَاطِنُ وَهُوَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ[4]

Yeye ndiye wa Mwanzo na ndiye wa Mwisho, naye ndiye wa Dhaahiri na wa Siri, naye ndiye Mjuzi wa kila kitu.

Kwa hiyo, ikiwa katika Qur-ani tunasoma:-

ذُو الْعَرْشِ الْمَجِيدُ[5]

Mwenye Kiti cha Enzi, Mtukufu, Neno “ARSHI” lililokuja katika Aya hiyo halimaanishi kiti cha ufalme, bali linamaanisha utukufu na mamlaka yake Allah (s.w).

Aya hiyo haina maana ya kuwa; Mwenyeezi Mungu ana sehemu au zama maalumu, bali inathibitisha utukufu wa utawala wake katika ulimwengu mzima wa kimada na ule usiokuwa wa kimada,kwa sababu kama tukijaalia kuwa Mwenyeezi Mungu sehemu au zama maalumu, tutakuwa tumemuweka Mwenyeezi Mungu katika mipaka maalumu, na tumempa sifa ya viumbe, na tukamfahamu Mwenyeezi Mungu kama tunavyovifahamu vitu vyengine vya kikawaida hali ya kwamba Yeye Mwenyewe Mola Mtakatifu anasema:-
فَاطِرُ السَّمَاوَاتِ وَالاَرْضِ جَعَلَ لَكُم مِّنْ اَنفُسِكُمْ اَزْوَاجاً وَمِنَ الاَنْعَامِ اَزْوَاجاً يَذْرَؤُكُمْ فِيهِ لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ وَهُوَ السَّمِيعُ البَصِيرُ[7]

Yeye ndiye Muumba mbingu na ardhi, amekujaalieni mke na mume katika nafsi zenu, na katika nyama hoa dume na jike, anakuzidishieni namna hii. Hapana kitu kama mfano wake. Naye ni Mwenye kusikia Mwenye kuona.

Na katika Aya nyengine anasema:-

وَلَمْ يَكُن لَّهُ كُفُواً اَحَدٌ[8]

Wala hana anaye fanana naye hata mmoja.
Baadhi ya Aya za qur-ani, zinathibitisha kuwa, kiti cha ufalme wa Mwenyeezi Mungu kimeenea mbinguni na ardhini, kwa hiyo, ufalme na mamlaka ya Mwenyeezi Mungu yameenea ulimwengu mzima, kama tunayosoma  katika Suratul-Baqarah Aya ya 255.


اللّهُ لاَ إِلَـهَ إِلاَّ هُوَ الْحَيُّ الْقَيُّومُ لاَ تَاْخُذُهُ سِنَةٌ وَلاَ نَوْمٌ لَّهُ مَا فِى السَّمَاوَاتِ وَمَا فِى الاَرْضِ مَن ذَا الَّذِى يَشْفَعُ عِنْدَهُ إِلاَّ بِإِذْنِهِ يَعْلَمُ مَا بَيْنَ اَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ وَلاَ يُحِيطُونَ بِشَيْءٍ مِّنْ عِلْمِهِ إِلاَّ بِمَا شَاء وَسِعَ كُرْسِيُّهُ السَّمَاوَاتِ وَالاَرْضَ وَلاَ يَؤُودُهُ حِفْظُهُمَا وَهُوَ الْعَلِيُّ الْعَظِيمُ

Mwenyezi Mungu - hapana mungu ila Yeye Aliye hai, Msimamia mambo yote milele. Hashikwi na usingizi wala kulala. Ni vyake pekee vyote viliomo mbinguni na duniani. Ni nani huyo awezaye kuombea mbele yake bila ya idhini yake? Anayajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao; wala wao hawajui chochote katika vilio katika ujuzi wake, ila kwa atakalo mwenyewe. Enzi yake imetanda mbinguni na duniani; na wala haemewi na kuvilinda hivyo. Na Yeye ndiye aliye juu, na ndiye Mkuu.

Maelezo kuhusiana na Aya ya 255 ya Suratul-Baqarah

Aya hii huitwa Ayatul-Kursiyyu, aya tukufu kabisa, anahimizwa kila Muislamu kuyaweka maana ya Aya hii mbele ya macho yke daima, ili asimuone muqaddim wala muakhkhir, ila Mwenyewe tu Mwenyeezi Mungu Subhanahu Wataala, na mahala pengi katika hadithi za Mtume amehimizwa mtu kuisoma, kama
a) Baada ya kutoa salamu katika sala, b) kabla ya kulala, c) anapotoka nje, d) anapoingia ndani,
e) anapokuwa na hofu ya kuogopa vinavyoonekana na visivyoonekana.

[1] Surat Az-Zukhruf Aya ya 84

[2] Surat Al-Hadiyd Aya ya 4

[3] Surat Qaf Aya ya 16

[4] Surat Al-Hadiyd Aya ya 3.

[5] Suratul-Buruj Aya ya 15

[6] Suratul Baqarah Aya ya 255.   

[7] Surat Ash-Shuura Aya ya 11

[8] Surat At-Tawhiyd Aya ya 4

MWISHO