KIAMA NA WATENDAO MATENDO YA KHERI

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

KIAMA NA WATENDAO MATENDO YA KHERI

Kauli muhimu za Mitume ya Mwenyeezi Mungu ni kuwalingania watu kuamini Mola mmoja na kuwakumbusha maisha baada ya mauti. Jitihada kubwa walizozifanya Mitume baada ya kuwalingania watu kuabudu Mola mmoja ni kuihuisha Siku ya Kiama katika nyoyo za watu.

Katika makala iliyopita tulimalizia kwa mada ya faida za kuikumbuka siku ya Kiama. katika makala hii tutazungumzia kuhusiana na na matendo ya kheri wanayoyatenda wale walio na imani na siku hiyo.

A. Kuwapa msaada watu wanyonge.

Waumini kwa sababu wana imani ya kuwepo siku ya Qiyamah, husamehe hata chakula wanachokihitaji na kuwapa wanyonge, kama tunavyosoma kuhusiana na watu wa nyumba ya Mtume Muhammad (s.a.w.w).

وَيُطْعِمُونَ الطَّعَامَ عَلـٰي حُبِّهِ مِسْكِيناً وَيَتِيماً وَاَسِيراً. إِنَّمَا نُطْعِمُكُمْ لِوَجْهِ اللهِ لاَ نُرِيدُ مِنكُمْ جَزَاء وَلاَ شُكُوراً. إِنَّا نَخَافُ مِن رَّبِّنَا يَوْماً عَبُوساً قَمْطَرِيراً[1]

Na huwalisha chakula, juu ya kukipenda kwake, masikini, na yatima, na wafungwa.

Hakika sisi tunakulisheni kwa wajihi wa Mwenyezi Mungu. Hatutaki kwenu malipo wala shukrani.

Hakika sisi tunaiogopa kwa Mola wetu Mlezi hiyo siku yenye shida na taabu.

B. Kuwapa wanyonge wanavyo hitaji kwa siri.

Watu ambao wanapenda anasa za dunia, na wana sehemu fulani katika jamii huwasaidia wanyonge na kuwapa mali zao au vile wanavyovihitaji  kwa ria, Na wakati wanapotoa mali zao, hutoa kwa kujifakharisha na kujionesha.

Ama wale watu ambao wana imani ya kuwepo siku ya Qiyama hutoa walivyonavyo na kuwapa wanyonge

kwa siri au kwa dhahiri bila ya riya, kwa sababu wana imani kuwa kila walichonacho ni kutoka kwake Allah (s.w). kama tunavyosoma ndani ya qur-ani:-

إِنَّ الَّذِينَ يَتْلُونَ كِتَابَ اللهِ وَاَقَامُوا الصَّلاَةَ وَاَنفَقُوا مِمَّا رَزَقْنَاهُمْ سِرّاً وَعَلاَنِيَةً يَرْجُونَ تِجَارَةً لَّن تَبُورَ. لِيُوَفِّيَهُمْ اُجُورَهُمْ وَيَزِيدَهُم مِّن فَضْلِهِ إِنَّهُ غَفُورٌ شَكُورٌ[2]

Hakika wale wanao soma Kitabu cha Mwenyezi Mungu, na wakashika Sala, na wakatoa kwa siri na kwa dhaahiri katika tulivyo waruzuku, hao hutaraji biashara isiyo bwaga.

Ili Yeye awalipe ujira wao kwa ukamilifu, na awazidishie kutokana na fadhila zake. Hakika Yeye ni Mwenye kusamehe Mwenye shukrani.

c. Kuwa na nia nzuri katika muamala.

Kuikumbuka siku ya Qiyamah kunamfanya mwanaadamu ajiepushe  na kufanya hiana katika amana. Na vile vile kuwa na imani na siku ya Qiyamah humsaidia mwanaadamu awe hadhari na kila maovu katika maisha yake ya kila siku. Na kwa sababu hiyo basi Allah (s.w) anawaambia wale wanaouza vitu huku wakiwapunja watu na kuwadhulumu.

اَلاَ يَظُنُّ اُولَئِكَ اَنَّهُم مَّبْعُوثُونَ . لِيَوْمٍ عَظِيمٍ[3]

Kwani hawadhani hao kwamba watafufuliwa .

Katika Siku iliyo kuu. Kutokana na maelezo hayo yaliyoelezewa katika somo hili imeeleweka kuwa mwanaadamu anapokumbuka siku ya Qiyamah huingiwa na hamu ya kufanya amali na matendo mema, na hujiepusha kumuabudu asiye kuwa Mola wake.Kwa hiyo kuikumbuka siku ya Qiyamah kunamfanya mwanaadamu awe na shauku ya kukutana na Mola wake. Kama tunavyosoma ndani ya Qur-ani:-

قُلْ إِنَّمَا أَنَا بَشَرٌ مِثْلُكُمْ يُوحَى إِلَيَّ أَنَّمَا إِلَهُكُمْ إِلَهٌ وَاحِدٌ فَمَنْ كَانَ يَرْجُو لِقَاءَ رَبِّهِ فَلْيَعْمَلْ عَمَلا صَالِحًا وَلا يُشْرِكْ بِعِبَادَةِ رَبِّهِ أَحَدًا[4]

Sema: Mimi ni mwanaadamu kama nyinyi. Ninaletewa Wahyi kwamba Mungu wenu ni Mungu Mmoja. Mwenye kutaraji kukutana na Mola wake Mlezi basi naatende vitendo vyema, wala asimshirikishe yeyote katika ibada ya Mola wake Mlezi

* Maelezo kwa ufupi ya makala zilizopita

* Kuwa huru kitabia na kimatendo, kutakasika kwa nafsi, kuwa na ukarimu na kuwa na upeo wa hali ya juu katika kutafakari mambo, ni miongoni mwa faida za kuwa na itikadi ya siku ya Qiyamah.

* kuikumbuka siku ya Qiyamah humfanya mwanaadamu aweze kustahamili  tabu na mashaka, kuwa thabiti katika itikadi yake, na kufanya jitihada zake zote ili abakie katika njia ya Mwenyeezi Mungu.

* Kuwa na itikadi ya siku ya Qiyamah, na kuukumbuka ulimwengu wa Akhera kunamfanya mwanaadamu awe na shauku ya kufanya ibada na matendo mema, ili apate ridhaa ya Mola wake.

  Maswali:

1.Kuikumbuka siku ya Qiyamah kunaleta athari gani katika maisha ya mwanaadamu?.

2. Kukumbuka ulimwengu baada ya mauti kunaleta athari kitabia na kimatendo?.

3. Kwa nini kuikumbuka siku ya Qiyamah kunamfanya mwanaadamu awe huru na kuitakasa nafsi yake ?.

4. Kuikumbuka siku ya Qiyamah kunachukua nafasi gani katika kukabiliana na Taluti na Maadui wa Mwenyeezi Mungu?.

5. Kuikumbuka siku ya Qiyamah kunaleta athari gani katika kufanya ibada na mambo ya kheri?.

[1] Surat-dahr Aya ya 8-10.

[2] Surat Faatir Aya ya 29-30

[3] Surat Muttafifiyn, Aya ya 4-5.

[4] Surat Al-Kahfi Aya ya 110.

 

MWISHO