KUWEPO KWA MOLA MTAKATIFU

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

 KUWEPO KWA MOLA MTAKATIFU

Sisi tunaamini kuwa Mwenyeezi Mungu ndiye muumbaji wa vitu vyote, na athari ya utukufu na elimu yake inaonekana kwa uwazi kabisa katika kila kiumbe ulimwenguni, katika umbile la mwanaadamu, wanyama, mimea, katika nyota ziliopo mbinguni, na katika kila kitu ulimwenguni.

Sisi tuna itikadi ya kuwa; kila tukifikiri na kutafakuri zaidi kuhusiana na siri ya viumbe vyote duniani, tutafahamu utukufu wa elimu na qudra ya dhati ya Mola Mtakatifu, na kwa kuonekana maendeleo ya elimu na taaluma ya wanaadamu ya kila siku kunapatikana na kufunguka elimu mpya kutokana na elimu na hekima zake Allah (s.w), na tafakuri za wanaadamu zinazidi kukua na kuenea kwa wingi zaidi, na tafakuri hizo ndio chanzo cha kuwa karibu naye Mola mtakatifu na kunufaika na upeo wa nuru ya utukufu wake. Qur-ani takatifu inasema:-

وَفِى الاَرْضِ آيَاتٌ لِّلْمُوقِنِينَ. وَفِى اَنفُسِكُمْ اَفَلاَ تُبْصِرُونَ[1]

Na katika ardhi zipo Ishara kwa wenye yakini. Na pia katika nafsi zenu - Je! Hamwoni?.

إِنَّ فِى خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالاَرْضِ وَاخْتِلاَفِ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ لآيَاتٍ لِّاُوْلِى الالْبَابِ. الَّذِينَ يَذْكُرُونَ اللّهَ قِيَاماً وَقُعُوداً وَعَلـٰيَ جُنُوبِهِمْ وَيَتَفَكَّرُونَ فِى خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالاَرْضِ رَبَّنَا مَا خَلَقْتَ هَذا بَاطِلاً سُبْحَانَكَ فَقِنَا عَذَابَ النَّارِ[2]

Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi na kukhitalifiana usiku na mchana ziko Ishara kwa wenye akili.

Ambao humkumbuka Mwenyezi Mungu wakiwa wima na wakikaa kitako na wakilala, na hufikiri kuumbwa mbingu na ardhi, wakisema: Mola wetu Mlezi! Hukuviumba hivi bure. Subhanaka,Umetakasika! Basi tukinge na adhabu ya Moto.

 SIFA TUKUFU ZA KIJALALI NA KIJAMALA ZA ALLAH (S.W).

Sisi tuna itikadi ya kuwa; Mwenyeezi Mungu (s.w) ametakasika na kila aibu, Mwenyeezi Mungu ni mkamilifu wa kila kitu, kwa maelezo mengine, kila jema, na kila kamilifu liliopo katika ulimwengu huu linatokana na dhati iliyotakasika yake Yeye Allah (s.w).

هُوَ اللهُ الَّذِى لاَ إِلَهَ إِلاَّ هُوَ الْمَلِكُ الْقُدُّوسُ السَّلاَمُ الْمُؤْمِنُ الْمُهَيْمِنُ الْعَزِيزُ الْجَبَّارُ الْمُتَكَبِّرُ سُبْحَانَ اللهِ عَمَّا يُشْرِكُونَ. هُوَ اللهُ الْخَالِقُ الْبَارِئُ الْمُصَوِّرُ لَهُ الاَسْمَاء الْحُسْنَي يُسَبِّحُ لَهُ مَا فِى السَّمَاوَاتِ وَالاَرْضِ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ[3]

Yeye ndiye Mwenyezi Mungu ambaye hapana mungu isipo kuwa Yeye tu. Mfalme, Mtakatifu, Mwenye salama, Mtoaji wa amani, Mwenye kuyaendesha Mwenyewe mambo yake, Mwenye nguvu, Anaye fanya analo litaka, Mkubwa, Ametakasika Mwenyezi Mungu na hayo wanayo mshirikisha nayo.

Yeye ndiye Mwenyezi Mungu, Muumbaji, Mtengenezaji, Mtia sura, Mwenye majina mazuri kabisa. Kila kilioko katika mbingu na ardhi kinamtakasa, naye ni Mwenye kushinda, Mwenye hekima.

Maelezo kuhusiana na Aya:

Aya hizo zinataja sifa nyingi za Mwenyeezi Mungu, sifa ambazo zimeelezewa fadhila zake katika hadithi nyingi za Mtume Muhammad (s.a. w.w). katika makala ifuatayo tutaelezea sifa za kijalali na kijamala za Mola Mtakatifu.

 

[1] Surat Adh-Dhariyat Aya ya 20-21

[2] Surat al-Imrani Aya ya 190-191

[3] Surat Al-Hashr Aya ya 23-24

MWISHO