MATAWI YA TAWHIYD

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

MATAWI YA TAWHIDI NO.1

Sisi tuna itikadi ya kuwa tawhiyd ina matawi mbali mbali, na kuna manne muhimu miongoni mwa hayo, nayo ni haya yafuatayo:-

A: TAWHIYD KATIKA DHATI YAKE ALLAH (S.W).

Yaani dhati ya Allah (s.w) ni moja, naye ni mmoja tu, asiyefanana na kitu chochote ulimwenguni.

B: TAWHIYD KATIKA SIFA ZAKE ALLAH (S.W).

Tawhiyd katika sifa za Mwenyeezi Mungu, yaani sifa zote za Mwenyeezi Mungu, mfano elimu, Qudra na uwezo, ubakiaji wa milele wa Allah (s.w), na sifa nyengine nyingi zote ziko katika dhati yake Allah (s.w), sio kama sifa za viumbe, kwani sifa za viumbe haziko ndani ya udhati wa viumbe bali ziko nje ya viumbe, ama ni lazima tuzingatie kuwa; dhati hiyo ya sifa za Mwenyeezi Mungu inahitajia tafakuri na mazingatio ya kifikra.

C: TAWHIYD KATIKA MATENDO YAKE ALLAH (S.W).

Yaani athari ya kila tendo, na kila harakati inayoshuhudiwa duniani, inatokana na idhini na matakwa yake Allah  (s.w)

اللهُ خَالِقُ كُلِّ شَيْءٍ وَهُوَ عَلـٰي كُلِّ شَيْءٍ وَكِيلٌ[1]

Mwenyeezi Mungu ndiye Muumba wa kila kitu, na yeye ndiye Mlinzi juu ya kila kitu.

لَهُ مَقَالِيدُ السَّمَاوَاتِ وَالاَرْضِ يَبْسُطُ الرِّزْقَ لِمَن يَشَاءُ وَيَقْدِرُ إِنَّهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ[2]   

Yeye ndiye Mwenye funguo za mbingu na ardhi. Humkunjulia riziki amtakaye, na humpimia amtakaye. Hakika Yeye ni Mjuzi wa kila kitu. Ndio, “لا مؤثر فی الوجود الا الله”.

Lakini kauli hiyo haimaanishi kuwa sisi hatna hiyari katika matendo yetu tunayoyafanya, bali tuko huru katika maamuzi na matendo yetu tunayoyafanya.

إِنَّا هَدَيْنَاهُ السَّبِيلَ إِمَّا شَاكِراً وَإِمَّا كَفُوراً[3]

Hakika Sisi tumembainishia Njia. Ama ni mwenye kushukuru, au mwenye kukufuru.

وَاَن لَّيْسَ لِلْإِنسَانِ إِلاَّ مَا سَعَي[4]

Na ya kwamba hatapata mtu ila aliyo yafanya mwenyewe?

Aya hiyo inaonyesha kwa uwazi kabisa kuwa mwanaadamu ni mwenye uhuru na anayeweza kufanya ayatakayo, lakini kwa sababu uhuru huo alionao mwanaadamu ameupata kutokana na Qudra na nguvu zake Allah (s.w), kwa hiyo tuna majukumu na wadhifa katika amali na matendo yetu tunayoyafanya, hivyo ni lazima tuwe na mazingatio katika matendo yetu na kufanya yale ambaye Allah (s.w) ametuamrisha.

Ndio, Mwenyeezi Mungu ametuwacha huru tufanye matendo na amali zetu kwa hiyari zetu, ili kutufanyia mtihani, kwani pindi tukifanya matendo yetu kwa uhuru, kupitia njia hiyo tunaweza kufikia katika ukamilifu, kwa sababu ni uhuru peke yake ndio utakaomfanya mwanaadamu aweze kumtii Mola wake kwa hiyari yake, bila ya kulazimishwa au kufosiwa, kwani mwanaadamu kufanya amali kwa kulazimishwa sio dalili nzuri itakayomfikisha mwanaadamu katika ukamilifu.

Ikiwa mwanaadamu atalazimishwa katika kufanya amali na matendo yake basi kulikuwa hakuna umuhimu wowote wa kuteremshwa Mitume wala kuteremshwa vitabu, vitabu ambavyo Mwenyeezi Mungu ameviteremsha kwa waja wake ili kuwaongoza katika njia njema, na wala kungelikuwa hakuna maana ya malipo ya jazaa njema au adhabu kali iumizayo.

Basi kutokana na maelezo ya Maimamu na Ahlulbayt (a.s) kuwa:

لاجبر ولا تفویض ولکن امر بین امرین

 

[1] Surat-Az-Zumar Aya ya 62

[2] Surat Shuura Aya ya 12.

[3] Surat Al-Insan Aya ya 3

[4] Surat-An-Najm Aya ya 39

MWISHO