FUNGAMANO NA VIONGOZI WAOVU

 BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

FUNGAMANO NA VIONGOZI WAOVU

Duniani kuna viongozi waovu walio na nafasi kubwa katika jamii, na baadhi ya watu huwa tayari kuwafuata viongozi hao hali ya kuwa wanajua ya kwamba viongozi hao ni waovu na waliopotoka, lakini kwa sababu wanatafuta manufaa na mafanikio ya kidunia basi huwa pamoja na viongozi hao na kushirikiana nao katika uovu wao, basi watu hao nawaelewe kuwa ijapokuwa kidhahiri wana fungamano na viongozi hao, lakini kibatini hawana fungamano wala uhusiano wowote bali wako mbali mbali, kama walivyokuwa baadhi ya watu waliuokuwa na akili finyu ambao walikuwa wakiabudu masanamu ili kukidhi haja zao na mahitajio yao,na baadhi ya wengine walikuwa wakifuata na kutii amri za wakubwa wa kaumu zao au makabila yao kwa ajili ya kupata nafasi za vyeo katika jamii, na baadhi yao walikuwa ni wahudumu wanaowahudumikia mabwana na mabepari wao kwa ajili ya kupata mali. Kwa upande mwengine, baadhi ya viongozi waovu ili kuhifadhi nafasi ya vyeo walivyonavyo katika jamii au utawala, hufanya kila wawezalo ili kulinda nafasi yake hiyo iliyo bora hata kwa kuwatia tamaa au kuwatishia kutokuwa na amani na usalama katika maisha yao, viongozi hao hufanya uhabithi ili kuwaweka mbali na haki au yale waliyo na itikadi nayo ambayo yanaendana sambamba na maamrisho yake Allah (s.w), amali za viongozi hao ni sawa na amali za shetani na ibilisi ambao huwatia wanaadamu wasi wasi ili kuwapotosha na kuwatoa katika njia iliyo njema. Basi wanachopaswa kuelewa viongozi hao ni kufahamu kuwa; siku ya Kiama ni siku ya kudhihirika haki na uhakika, kwa hiyo wale wote waliofanya maovu na maasi kutokana na matamanio ya nafsi zao, au kwa ajili ya kupata manufaa na mafanikio yao, basi nawaelewe kuwa siku hiyo utadhihirika uovu wao na watalipwa adhabu kubwa na Allah (s.w) kutokana na uovu wao walioutenda.

na kila kiongozi muovu na wafuasi wake waliokuwa wakimfuata na wakishirikiana nae katika uovu na maasi yake basi siku hiyo hakutakuwa na fungamano lolote litakalokuwepo baina ya kiongozi huyo na wafuasi wake, na kila mmoja atakuwa anatapatapa kutafuta njia itakayoweza kumuokoa na adhabu za Mwenyezi Mungu bila ya kufikiria wenziwe.

Vidokezo.

1. Viongozi na wafuasi hao waovu, kwa sababu kila mmoja alikuwa ni mwenye kufanya maasi na kumkufuru Mwenyeezi Mungu, basi wana fungamano fulani lililojengeka baina yao, fungamano ambalo siku ya Kiama litawakusanya na kuwapeleka motoni, lakini kwa sababu kila mmoja atakuwa anahangaika kutafuta uokozi wa manufaa yake, fungamano hilo litabadilika na kusababisha khitilafu baina yao, basi siku ya Kiama watakuwa wanalaaniana wenyewe kwa wenyewe,

kama tunavyosoma ndani ya Qur-ani takatifu:-

قَالَ ادْخُلُواْ فِى اُمَمٍ قَدْ خَلَتْ مِن قَبْلِكُم مِّن الْجِنِّ وَالإِنسِ فِى النَّارِ كُلَّمَا دَخَلَتْ اُمَّةٌ لَّعَنَتْ اُخْتَهَا حَتَّي إِذَا ادَّارَكُواْ فِيهَا جَمِيعاً قَالَتْ اُخْرَاهُمْ لاُولاَهُمْ رَبَّنَا هَـؤُلاء اَضَلُّونَا فَآتِهِمْ عَذَاباً ضِعْفاً مِّنَ النَّارِ قَالَ لِكُلٍّ ضِعْفٌ وَلَـكِن لاَّ تَعْلَمُونَ[1]

Mwenyezi Mungu atasema: Ingieni Motoni pamoja na umma zilizo pita kabla yenu za majini na watu. Kila utakapo ingia umma utawalaani wenzake. Mpaka watakapo kusanyika wote humo, wa mwisho wao watawasema wa mwanzo wao: Mola wetu Mlezi! Hawa ndio walio tupoteza; basi wape adhabu ya Motoni marudufu. Atasema: Itakuwa kwenu nyote maradufu, lakini nyinyi hamjui tu.

2. Imani na mapenzi na takuwa yoyote ile itakayojengwa bila ya kuwa na imani na akida ya kuwepo Mwenyeezi Mungu, kwa hakika imani hiyo siyo imani ya kweli na haitodumu, basi imani ya kweli ni ile imani ya kuamini Mwenyeezi Mungu, na imani hiyo pekee ndiyo ndiyo imani madhubuti itakayobakia milele,itakayomlinda na kumuokoa mwanaadamu na adhabu ya moto wa Jahannamu, kama anavyosema Mola Mtakatifu:-

وَاعْتَصِمُواْ بِحَبْلِ اللهِ جَمِيعاً وَلاَ تَفَرَّقُواْ وَاذْكُرُواْ نِعْمَتَ اللهِ عَلَيْكُمْ إِذْ كُنتُمْ اَعْدَاء فَاَلَّفَ بَيْنَ قُلُوبِكُمْ فَاَصْبَحْتُم بِنِعْمَتِهِ إِخْوَاناً وَكُنتُمْ عَلـٰيَ شَفَا حُفْرَةٍ مِّنَ النَّارِ فَاَنقَذَكُم مِّنْهَا كَذٰلِكَ يُبَيِّنُ اللّهُ لَكُمْ آيَاتِهِ لَعَلَّكُمْ تَهْتَدُونَ[2]

Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu: vile mlivyo kuwa nyinyi kwa nyinyi maadui naye akaziunganisha nyoyo zenu; kwa neema yake mkawa ndugu. Na mlikuwa ukingoni mwa shimo la Moto, naye akakuokoeni nalo.

Namna hivi Mwenyezi Mungu anakubainishieni Ishara zake ili mpate kuongoka.

Maelezo kuhusiana na Aya.

Katika Aya hiyo wanaambiwa Waislamu washikamane wote pamoja kwa jina la dini yao ya Uislamu, wasifarikiane kwa jina la miji au kabila au vyama au mengineyo kama ilivyo sasa, kufanya hivyo ni jukumu kubwa kabisa, natuache upesi au hatari itakuwa kubwa kabisa na dhambi kubwa.

Usadikisho ulio wazi kabisa wa kuwa na imani na Mwenyeezi Mungu, imani ambayo pindi mtu akiwa nayo hatopata majuto ya aina yoyote, ni imani ya kuamini Mola mmoja na Mitume yake, na kuamini Wilaya ya Uwalii wa Mwenyeezi Mungu, kama tunavyosoma ndani ya Qur-ani takatifu:-

وَيَوْمَ يَعَضُّ الظَّالِمُ عَلـٰي يَدَيْهِ يَقُولُ يَا لَيْتَنِى اتَّخَذْتُ مَعَ الرَّسُولِ سَبِيلاً . يَا وَيْلَتَي لَيْتَنِى لَمْ اَتَّخِذْ فُلاَناً خَلِيلاً[3]

Na siku ambayo mwenye kudhulumu atajiuma mikono yake, na huku anasema: Laiti ningeli shika njia pamoja na Mtume! Ee Ole wangu! Laiti nisingeli mfanya fulani kuwa rafiki!

Maelezo kuhusiana na Aya.

Aya hii inatuthadharisha na suhuba mbovu, na mahala pengine Mwenyeezi Mungu ametwambia “ Na yule ambaye amekuwa Shetani ndiye rafiki yake, basi anarafiki mbaya kabisa:

وَالَّذِينَ يُنفِقُونَ اَمْوَالَهُمْ رِئَـاء النَّاسِ وَلاَ يُؤْمِنُونَ بِاللهِ وَلاَ بِالْيَوْمِ الآخِرِ وَمَن يَكُنِ الشَّيْطَانُ لَهُ قَرِيناً فَسَاء قِرِيناً[4]

Na ambao hutoa mali yao kwa kuonyesha watu, wala hawamuamini Mwenyezi Mungu wala Siku ya Mwisho; na yule ambaye Shet'ani amekuwa ndiye rafiki yake,basi ana rafiki mbaya mno.

Na Mtume Muhammad (s.a.w.w) ametwambia Mtu hufuata mwendo wa rafiki yake, basi jichagulieni rafiki mzuri.

Maelezo kuhusiana na aya.

Anayetaka alipwe hiyo Pepo na Mwenyeezi Mungu, basi sharti awe anafanya hayo mema kwa ajili ya Mwenyeezi Mungu, siyo kwa ajili ya kuwa watu wamuone wamsifu, atakayefanya kwa nia hiyo hatakuwa na malipo yoyote Akhera, kwani kataka aonekane duniani, na kesha kuonekana.

Maelezo kwa ufupi ya makala iliyopita.

* Mafungamano na mahusiano ya kifamilia na kiukoo, kijamii, na milki ya watu siku ya Kiama hayatakuwa na fungamano la aina yoyote, na hila zote zilizofanywa

kwa njia yoyote ile, ikiwa ya kielimu au njia nyengine yoyote zitabatilishwa na kuwekwa kando.

* Mahusiano na mafungamano yote yaliyojengwa kwa uwongo, siku ya Kiama utadhihirika uwongo huo, na uhakika utawekwa wazi kwa uwezo wake Allah (s.w).

* Siku ya Kiama Nyenzo, nguvu, uwezo, na hila zote zile zilizotumiwa na wanaadamu zitabatilishwa na kuwekwa kando, na kitu kitakachobakia ni milki na ufalme wake Mwenyeezi Mungu.

Masuali.

1. Qur-ani Kariym inaelezea nini kuhusiana na mahusiano na mafungamano ya famili, ukoo, rafiki katika siku ya Kiama?.

2. Tafakuri na fikra zisizokuwa za Mwenyeezi Mungu zina nafasi gani siku ya Kiama?.

3. Mafungamano na mahusiano ya viongozi waovu yatakuwa vipi siku ya Kiama?.

4. Kuwa na imani na itikadi ya kuwafuata viongozi na Mawalii wa Mwenyeezi Mungu kunaleta athari gani siku ya Kiama?.

 

[1] Suratul-Al-Aaraf Aya ya 38.

[2] Surat Al-Imrani Aya ya 103.

[3] Surat Al-Furqaan Aya ya 27-28

[4] Suratun-Nisaa Aya ya 38.

MWISHO