Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

MAPINDUZI YA IMAM MAHDI (AS)

0 Voti 00.0 / 5

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
MAPINDUZI YA IMAM MAHDI (A.S)

ALAMA ZA KUDHIHIRI

Mapinduzi ya Imam Mahdi yana alama maalum, kupatikana kwa alama hizi kutakuwa kuna athari kubwa, kwa kutokana na kwamba alama hizi ni zenye kubashiria faraja ya Imam, basi kila inapotokea moja kati ya alama hizo husababisha kuzidi nuru ya matamanio kupatikana katika nyoyo za wenye kumsubri, na kwa wale wapinzani na wasongomanishaji huwa ni changamoto na ukumbusho ili waweze kuwacha maovu yao, na huwasababisha wale wenye kusubiri waweze kudiriki kudhihiri kwake na kutafuta matayarisho muhimu ili waweze kuwa naye hapo atakapodhihiri, na vile vile alama hizi zitakuwa ni zenye kutupa habari kwa matokeo yatakayokuja baadaye na kutufanya tuwe tayari katika kupanga mipango ya kukabiliana naye, na vile vile alama hizi ni kipimo bora cha kuweza kuwatambua wale waongo wenye kudai kuwa wao ndio Imam Mahdi anayesubiriwa, kwa hiyo basi iwapo mtu atadai kuwa yeye ni Mahdi lakini akawa yeye kuja kwake hakuna alama maalum zilizotajwa itakuwa ni rahisi kutambua uongo wa mtu huyo.

Katika riwaya za maimamu kumetajwa alama tofauti za kudhihiri ambazo baadhi yake ni alama zitakazotokea katika dunia na nyengine ni miujiza, sisi tutataja baadhi ya alama zilizotajwa katika hadithi zenye kuaminika na baadae tutaja alama nyengine kwa ufupi.

Imam sadiq (a.s) amesema:-

"Kusimama kwa Mahdi (a.s) kuna alama tano:-

Kudhihiri kwa Sufiani, Yamaniy, sauti kutoka mbinguni, kuteketezwa kwa nafsi zilizo takatifu, kudidimia kwa ardhi ya Baydaa[1]".

Kwa kuzitupia macho riwaya alama tano hizi zilizotajwa zimekaririwa katika riwaya tofauti, kwa hiyo acha sisi tuzielezee ingawaje kipengele kimoja kimoja katika alama hizi hakijaweza kuthibitika mbele yetu.

A) KUJA KWA SUFIANI

Kuja kwa Sufiani ni moja kati ya alama zilizotajwa katika hadithi tofauti, Sufiani ni mtu anayetokana na kizazi cha Abu Sufiani ambaye atadhihiri katika ardhi ya Shamu, yeye ni mtu muasi ambaye katika mauaji hakuna mtu anayefanana naye, na atapambana na wale wanaokwenda kinyume naye katika hali mbaya kabisa.

Imam Sadiq (a.s) akimsifia mtu huyo anasema:-

"Ikiwa mtu atamuona Sufiani basi atakuwa amemuona mtu mbaya alioje[2]".

Kusimama kwa Sufiani kutaanza katika mwezi wa Rajab, na baada ya kuitawala Sham na pembezoni mwake itaivamia Iraq na atafanya

mauaji makubwa, katika riwaya imepokelewa kuwa kuja kwake hadi kuuliwa kwake kutachukua kipindi cha miezi kumi na tano[3].

B) KUDIDIMIA KWA ARDHI YA BAYDAA

Baydaa ni sehemu ya ardhi baina ya Makka na Madina, Sufiani ataongoza jeshi lake ili kuelekea Makka kwenda kupambana na Imam, na atakapofika Baydaa utatokea muujiza wa kudidimia kipande hicho cha ardhi.

Imam Baqir (a.s) akizungumzia suala hili anasema:-

"Habari itamfikia kiongozi wa jeshi la Sufiani kwamba , Mahdi (a.s) ameelekea Makka, naye ataliamrisha jeshi kuelekea huko, lakini hawatompata Imam kwani jeshi la Sufiani litakapofika Baydaa itatoka sauti kutoka mbinguni ikisema:-

"Ewe ardhi ya Baydaa wahilikishe hao na ardhi hiyo itawameza watu hao[4]".

C) KUSIMAMA KWA YAMANIY

Kusimama kwa kiongozi katika ardhi ya Yemen ni moja katika alama ambapo suala hili litatokea katika kipindi kichache kabla ya kudhihiri Imam, Yamaniy ni mtu mwema aliye muumini atakayesimama na kupambana na uovu, lakini ufafanuzi juu ya mapambano yake mpaka hivi sasa hatunao.

Imam Baqiri (a.s) anasema:-

"Kabla ya kuja kwa Imam atasimama Yamaniy na hakutakuwa na bendera ya haki iliyo juu zaidi kuliko bendera yake yeye, kwani yeye atakuwa anaita watu kuelekea kwa Imamu[5]".

D) SAUTI KUTOKA MBINGUNI

Moja kati ya alama za kudhihiri Imam ni sauti kutoka mbinguni, na sauti hii kama ilivyokuja katika baadhi ya riwaya ni sauti ya Jibrail (a.s) itakayosikika katika mwezi wa Ramadhani[6].

Na kutokana kwamba kusimama kwa, mtengenezaji pekee atakayeleta Mapinduzi ya kilimwengu, na watu wote watakuwa wanasubiri tokeo hilo, basi moja kati ya jambo litakalowagutua watu kutokana na tokeo hili la kilimwengu ni sauti itokayo mbinguni.

Imam Baqiri (a.s) anasema:-

"kuja kwa Imam Mahdi (a.s) hakutatokea mpaka pale sauti ya mnadiaji kutoka mbingni itakaponadi, na kusikika na watu wote wa Mashariki na Magharibi[7]".

Ukenja huo kama vile itakavyokuwa ni furaha kwa waumini basi itakuwa ni adhabu vile vile kwa watu waasi, ili waweze kuwacha maasi yao na wajiunge na kikosi cha wafuasi wa Imamu.

Kuhusiana na ufafanuzi wa sauti hii kuna riwaya tofauti zilizozungumzia suala hili, moja kati ya hizo ni riwaya ya Imam Sadiq isemayo:-

"Mnadiaji kutoka mbinguni atanadi kwa jina la Imamu na la baba yake[8]".

E) KUULIWA KWA NAFSI TAKATIFU

Nafsi takatifu ina maana ya mtu aliyebobea katika ukamilifu au mtu aliyetakasika na asie na maasi, ambaye hajawahi kuuwa, na kuuliwa kwa nafsi takatifu inakusudiwa kuwa kabla ya kudhihiri kwa Imam kwa muda kidogo watauliwa watu walio watakatifu wasio na makosa kwa mikono ya waovu, wenye kwenda kinyume na Imam.

Kumepokelewa katika baadhi ya riwaya kuwa tokeo hili litatokea katika mausiku kumi na tano ya kabla ya kudhihiri.

Imam Sadiq (a.s) anasema:-

"Baina ya kudhihiri kwa Imam na kuuliwa kwa nafsi takatifu kuna tofauti ya mausiku kumi na tano[9].

Kuna alama nyengine tofauti ambazo zimetajwa katika riwaya, ambazo baadhi yake ni kuja kwa Jadal, (Jadal ni kiumbe mwenye hila na muovu atakayewapotosha watu wengi, kupatwa kwa jua na mwezi ndani ya mwezi wa Ramadhani, kudhihirika kwa fitna xza aina tofauti na kusimama kwa mtu mmoja katika mji wa Khurasani. Jambo muhimu la kuelezea ni kwamba ufafanuzi na uchambuzi wa alama hizi kumezungumziwa kwa uzuri zaidi katika vitabu vikubwa[10].

 


[1] Rejea ghaybati Nuumani, mlango wa 14, juzuu ya 9, ukurasa wa 261.

[2] Rejea kamalu-din, juzuu yz 2, mlango wa 57, ukurasa wa 557.

[3]Rejea Ghaybati-Nuumani, mlango wa 18, ukurasa wa 310.

[4] Rejea kitabu kilichopita mlango wa 14, ukurasa wa 286.

[5] (Rejea kitabu kilichopita ukursa wa 264).

[6] Rejea kitabu kilichopita ukurasa wa 262.

[7] Rejea kitabu kilichopita ukurasa wa 265.

[8] Rejea kitabu kilichopita mlango wa 10, ukurasa wa 137.

[9] Rejea Kamalu-din, juzuu ya 2, mlango wa 57, ukurasa wa 554.

[10] Rejea Buharul-an-war, juzuu ya 52, ukurasa wa 181 hadi 278.

 

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini