Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

NJIA ZA UHAKIKI WA DINI

0 Voti 00.0 / 5


 BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

 NJIA ZA UHAKIKI WA DINI
VIGEZO NA NJIA ZA UHAKIKI WA DINI:

Uhakiki wa dini unapatiwa ufumbuzi kwa kuzingatia mikondo (mambo) mitatu. Taaluma ya ndani ya dini, taaluma ya nje ya dini, na utendaji wa amali.

6.  Wahakiki wanaotaka kutambua uhakika na haki ya dini wanaweza kuitafiti dini na kuipatia ufumbuzi wake kupitia vigezo hivi vifuatavyo:-

- Kupitia elimu na taaluma ya nje ya dini, yaani kupitia misingi mikuu ya dini, (umbile la nje la dini).

- Kupitia elimu na taaluma ya ndani ya dini, yaani kuzingatia maamrisho, makatazo, hukumu mbali mbali n.k. (umbile la ndani la dini).

- Kuwa na elimu na taaluma katika kuyafanyia amali yote yaliyoamrishwa na Mwenyeezi Mungu kwa kuyafanyia amali kimwenendo na kimatendo, na kujiepusha na yale aliyoyakataza Mola Mtakatifu.

Basi wahakiki wote wanaotaka kuitambua dini inawalazimu kuitafuta dini kupitia mambo hayo matatu yaliyobainishwa hapo juu, mbali ya mambo hayo vile vile inawalazimu kuzingatia na kukuza fikra kiakili katika mambo yaliyomo ndani ya nafsi ya mwanaadamu, kwa sababu baadhi ya mambo ni ya kimaumbile na yanakuwa katika kila nafsi ya mwanaadamu. Kwa upande mwengine wahakiki wanatakiwa kuwa na elimu inayowapa taaluma katika utambuzi wa mambo, inayowapa utambuzi katika kumtambua mwanaadamu, na inayowapa utambuzi katika kutambua viumbe na mambo mbali mbali yanayohusiana na maisha yao, baada ya kupata taaluma hizo muhakiki anaweza kutalii mambo mbali mbali yanayohusiana na taaluma ya dini na elimu kwa ujumla.

7. Miongoni mwa mambo mengine ambayo wahakiki wa dini wanatakiwa kuyafanya, ni lazima kuuliza masuala mbali mbali yanayowajia akilini mwao wakati wanapofanya uhakiki wao, kila muhakiki anatakiwa kutafakari na kukubali au kupinga mambo kwa mujibu elimu aliyonayo na yale aliyoyatambua kupitia elimu hiyo, hivyo muhakiki anaweza kutoa fikra na mtazamo wake katika Nyanja mbali mbali na sio katika taaluma ya dini tu, muhakiki katika upingaji wa mambo ambayo ana elimu nayo anaweza kutoa fikra au nadharia mpya ambazo zinaweza kuiamsha jamii kifikra na kiakili.

8. Muhakiki ni lazima awe na hadafu maalumu katika shughuli zake za uhakiki, miongoni mwa hadafu hizo ni kutambua haki na ukweli wa mambo, ingawaje kuna umuhimu mkubwa utakaozingatiwa kutokana na nadharia za wahakiki.

9. kutokana na ukuwaji wa maendeleo katika dunia na jamii kwa ujumla, na kutokana na masuala au tata mbali mbali zinazotokea kwa sababu tofauti, kumeifanya jamii na watu wote kwa ujumla kutafakari na kukuza fikra zao ili kutambua mambo tofauti yanayowahusu wanaadamu au mambo mengine yoyote, hii imepelekea uwanja wa uhakiki kuenea na kusambazika siku hadi siku, na wahakiki wamekuwa wakifanya jitihada zao ili kupata jawabu ya masuala yao.

Ama ni lazima tuzingatie kuwa sio kila muhakiki anayeingia katika uwanja wa tahakiki ana malengo na hadafu njema katika uhakiki wake, hivyo sio vibaya kubainisha baadhi ya malengo au hadafu za wahakiki.

 Jitihada za wahakiki zinaweza zikawa kwa ajili ya malengo na hadafu tofauti: -

-Baadhi ya wahakiki hufanya uhakiki wao kwa ajili ya kueneza na kusambaza ukoloni mambo leo, unaotoka katika mataifa makubwa wenye nia ya kutaka kuutawala ulimwengu kifikra na kiutamaduni.

-Baadhi ya wahakiki hufanya uhakiki wao kuhusiana na dini wakiwa na malengo ya kutaka kutambua ukweli na uhakika wa dini hiyo.

- Baadhi ya wahakiki huingia katika uwanja wa uhakiki wakiwa na malengo ya kuhujumu au kufosi fikra za watu na jamii kwa ujumla, wahakiki kama hao huwa na nia ya kuharibu fikra za watu na jamii kwa ujumla.

- Baadhi ya wahakika huingia katika uwanja wa tahakiki kutokana na udadisi walionao wa kutaka kutambua na kujua mambo tofauti yanayohusiana na dini au mambo mbali mbali.

-Baadhi ya wahakiki huingia katika uwanja wa uhakiki wakiwa na malengo ya kutaka kufahamu uhakika wa mambo na kujua jamii inataka mahitajio gani katika maisha yao, basi wahakiki hao hufanya jitihada zao zote ili kudhamini mahitajio yanayohitajiwa na wanaadamu.

-Baadhi ya wahakiki huingia katika uwanja wa tahakiki kwa ajili ya kuharibu na kuhujumu fikra za watu wenye dini, au walio na itikadi au imani ya dini fulani.

Hayo yalikuwa ni baadhi ya malengo tu ya wahakiki, hivyo ni wadhifa wa kila mtu mwenye fikra salama kuwa makini katika kutambua hadafu na malengo ya uhakiki wake, na wanadini wote mahasusi Waislamu inawawajibikia kukabiliana na vile vitengo vya wahakiki ambavyo malengo yao ni kuiharibu dini au kuitawala jamii.

Kwa upande mwengine Waislamu ni lazima wawe na elimu ya kutosha katika kuwapatia wahakiki majibu ya masula yao, majibu ambayo yatamtoa muhakiki katika shaka na kumridhisha kiakili na kiakida, hatimae kuelewa na kutambua haki na uhakika wa dini.

Ni wadhifa wa kila Muislamu kupokea suala, tata, au mapingaji yoyote yale yanayotolewa na wahakiki bila ya kudharau nadharia au mitazamo ya wanahakiki, kutafiti tata na masuala ambayo yanatolewa na wahakiki na kuyapatia ufumbuzi wake.

Ni wadhifa wa Waislamu kupokea tata za wahakiki kwa nia moja, na malengo mamoja ya kuzitafutia ufumbuzi wa kielimu tata hizo, na sio kuzitoa maana tata au masuala mbali mbali yanayoulizwa na wahakiki, kwa sababu kufanya hivyo hakutapelekea faida yoyote katika jamii na dini ya Kiislamu, kwani malengo makuu ya dini ya Kiislamu na Waislamu kwa ujumla ni kuitangaza dini hiyo tukufu ili kuenea katika pande zote za dunia, kwani dini hiyo ndio dini ya haki inayohitajiwa na kila mwanaadamu katika kuendeleza na kupata saada njema ya maisha yake ya duniani na Akhera.

10. Wahakiki wa dini katika hatua ya mwanzo ni lazima kufahamu na kutambua uhakika wa dini kupitia udhahiri wa matini za kidini, na katika hatua ya pili baada ya kufahamu kwa uzuri dhahiri ya dini basi anaweza akafanya jitihada katika kufahamu batini ya dini, lakini ni lazima azingatie kuwa analazimika kutumia dhahiri ya dini kwa ajili ya kufahamu batini ya dini, na sio kutoka nje ya dini, kwa sababu kile anachokifahamu katika undani wa dini ni ule ufahamu wa yale aliyoyakubali katika udhahiri wa dini. Kwa hiyo uhakiki wa kweli hauwezi kukubalika kwa kuhakiki katika njia za logical Politivism, kutafsiri kwa kutumia njia yaTaawiyl ( kutafsiri kwa njia ya dhahiri shahiri), au kuhakiki kwa njia ya Hermenutics. Katika paragrafu hii tutazielezea njia hizo kwa undani zaidi, kwani inawezekana baadhi ya watu wasielewe makusudio ya njia hizo ni nini.

 a) Logical Politivism: Ni kitu ambacho kinaweza kufanyiwa majaribio na tajriba. Kwa maana nyengine tunaweza kusema hivi:-

Ni sentensi, mada,au tungo yoyote ile ya sheria ya kidini, jamii, serikali, ni lazima iwe na uwezo wa kuiingiza katika maabara na kutafutiwa utafiti na majaribio ambayo yataweza kuonyesha kwa kina uhakika wake, kwa mfano kama inadaiwa kuwa siku ya kiama kuna Pepo kwa watu wema, na kuna jahanamu (moto) kwa watu wabaya, basi ni lazima pafanyiwe utafiti utakaoonyesha ukweli wa Pepo na Jahanamu hiyo, na ikiwa kutokana na uhakiki au utafiti utakaofanywa hakukupatikana uhakika wala ufumbuzi wowote utakaothibitisha kuwepo kwa vitu hivyo, basi madai hayo ya kuwa kuna Pepo na moto hayatakubalika.

b)Taawili (tafsiri ya dhahiri shahiri) ni tafsiri yenye kumurika maneno kupitia darubini ya udhahiri wa mambo, na maana dhahiri za maneno zilivyo.

Taawili ni kufasiri na kutafuta maana za maneno kupitia darubini ya nguvu za kiakili zenye uwezo wa kujua maana dhahiri na kuilenga ile maana halisi iliyojificha ndani ya maneno. Kwa hiyo kwa msingi huo tunaweza kusema kuwa tafsiri ya dhahiri shahiri ni tafsiri ya wazi yenye kuonekana dhahiri shahiri bila ya mashaka yoyote.

Taawili ni tafsiri mficho ambayo maana yake ni lazima itafutwe huko mafichoni iliko, tafsiri mficho ni yenye kuyasaka na kuyatafuta maneno yaliyo mafichoni, (yaani maneno yaliyo batini, yaani maneno yaliyojificha ndani ya ibara, au sentensi). Kwa mfano:-

Mwenye kufasiri Qur-ani kwa njia ya dhahiri anatumia akili yake kwa kiwango kidogo tu, wala hatakiwi kutafakari kwa kiwango kikubwa, ama kwa yule mfasiri ambaye anaifasiri Qur-ani kwa ubatini wake, basi mfasiri huyo atakuwa anatumia akili na kiwango kikubwa cha kutafakari. Natuzingatie mfano huu wa Aya unaoonyesha tafsiri ya dhahiri na tafsiri ya batini, Allah (s.w) anasema:-

إِنَّ الَّذِينَ يُبَايِعُونَكَ إِنَّمَا يُبَايِعُونَ اللهَ يَدُ اللهِ فَوْقَ اَيْدِيهِمْ فَمَن نَّكَثَ فَإِنَّمَا يَنكُثُ عَلـٰي نَفْسِهِ وَمَنْ اَوْفَي بِمَا عَاهَدَ عَلَيْهُ اللهَ فَسَيُؤْتِيهِ اَجْراً عَظِيماً[1]

Bila ya shaka wanao fungamana nawe, kwa hakika wanafungamana na Mwenyezi Mungu. Mkono wa Mwenyezi Mungu uko juu ya mikono yao. Basi avunjaye ahadi hizi anavunja kwa kuidhuru nafsi yake; na anaye tekeleza aliyo muahadi Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu atamlipa ujira mkubwa.

[1] Surat Al-Fat-h Aya ya 10.

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini