Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

UBORA WA NIDHAMU YA AKHERA KULIKO DUNIA

0 Voti 00.0 / 5

 BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

UBORA WA NIDHAMU YA AKHERA KULIKO DUNIA

* Ni nidhamu gani iliyo bora? nidhamu ya duniani au nidhamu ya Akhera?

* Ni dalili gani zilizo bora zinazoonesha maendeleo ya ubora huo wa nidhamu?.

Dunia ni madrasa na shule ya mpito, dunia ni sehemu inayomkuza mwanaadamu na kumzidishia kiwango chake cha fikra, dunia ni sehemu inayompeleka mwanaadamu katika ukamilifu na kumfanya awe mcha Mungu, dunia ni sehemu ya biashara ya kuitakasa nafsi na maovu kwa wale Mawalii wa Mwenyeezi Mungu, kama tunavyosoma ndani ya Qur-ani takatifu:-

وَمِنَ النَّاسِ مَن يَشْرِى نَفْسَهُ ابْتِغَاء مَرْضَاتِ اللهِ وَاللّهُ رَؤُوفٌ بِالْعِبَادِ[1]

Na katika watu yupo ambaye huiuza nafsi yake kwa kutaka radhi za Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu ni Mpole kwa waja wake.

Maelezo kuhusiana na Aya.

Watu wauzao nafsi zao… ni wanaotoa mali yao, na wakazikalifu nafsi zao, kufanya mambo anayoyataka Mwenyeezi Mungu.

Dunia ni kama shamba au konde iliyo na mapato kwa ajili ya siku ya Kiama.

مَّثَلُ الَّذِينَ يُنفِقُونَ اَمْوَالَهُمْ فِى سَبِيلِ اللهِ كَمَثَلِ حَبَّةٍ اَنبَتَتْ سَبْعَ سَنَابِلَ فِى كُلِّ سُنبُلَةٍ مِّئَةُ حَبَّةٍ وَاللّهُ يُضَاعِفُ لِمَن يَشَاءُ وَاللّهُ وَاسِعٌ عَلِيمٌ[2]

Mfano wa wanao tumia mali zao katika Njia ya Mwenyezi Mungu ni kama mfano wa punje moja iliyo chipuza mashuke saba. Katika kila shuke zimo punje mia. Na Mwenyezi Mungu humzidishia amtakaye, na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa na Mwenye kujua.

Maelezo kuhusiana na aya.

Aya hii inahimiza kutoa katika njia za kheri, na za kuonyesha fadhila anazowapa Mwenyeezi Mungu kwa kufanya hayo, lakini kwa sharti wafanye:

a) Kwa ajili ya Mwenyeezi Mungu, (isiwe kutoa kwa kuwaonyesha watu tu).

b)Vilivyo vizuri, (wakitoa visivyo vizuri hawatopata thawabu kubwa namna hiyo).

c) Isiwe kuwaudhi hao wanaowapa.

d) Isiwe kuwasumbulia hao wanaowapa, ikiwa si hivyo basi hapana thawabu ila khasara tu, na maneno mazuri yatakuwa bora kuliko sadaka hizo.

e) Hicho kinachotolewa kiwe ni halali yake mwenyewe mtu anayekitoa.

Ama, kwa sababu nidhamu ya dunia ni nidhamu ya ulimwengu wa kimada, basi ulimwengu huo una mwisho wake, basi dunia hii ni ya muda mfupi tu, basi baadae itatoweka, kama anavyosema Mola Mtakatifu:-

وَلاَ تَدْعُ مَعَ اللهِ إِلَهاً آخَرَ لاَ إِلَهَ إِلاَّ هُوَ كُلُّ شَيْءٍ هَالِكٌ إِلاَّ وَجْهَهُ لَهُ الْحُكْمُ وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ[3]

Wala usimwombe pamoja na Mwenyezi Mungu mungu mwenginewe. Hapana mungu ila Yeye. Kila kitu kitaangamia isipo kuwa Yeye. Hukumu iko kwake, na kwake mtarejezwa.

Na watu wote waliopo ulimwenguni pia watatoweka.

كُلُّ مَنْ عَلَيْهَا فَانٍ[4]

Kila kilioko juu yake kitatoweka.

Lakini kwa sababu nyenzo nyingi zinazomtambulisha mwanaadamu ni hisia zake, kwa maana hiyo mwanaadamu hawezi kufahamu uhakika wa mambo, kwa sababu nguvu za uoni, na usikivu, ambazo ndio nguvu muhimu zinazomfanya mwanaadamu adiriki na kufahamu taaluma mbali mbali zina mipaka maalumu, na baadhi ya wakati zinaweza kumpeleka mwanaadamu katika makosa, kama tunavyosoma kuhusiana na wachawi wa firauna.

قَالَ اَلْقُوْاْ فَلَمَّا اَلْقَوْاْ سَحَرُواْ اَعْيُنَ النَّاسِ وَاسْتَرْهَبُوهُمْ وَجَاءوا بِسِحْرٍ عَظِيمٍ[5]

Akasema: Tupeni! Basi walipo tupa waliyazuga macho ya watu na wakawatia khofu, na wakaleta uchawi mkubwa.

Na hata shughuli za ulimwengu wa kimada zinazomfanya mwanaadamu aghafilike na Akhera humpelekea mwanaadamu kutodiriki baadhi ya elimu na taaluma:-

وَلَقَدْ ذَرَاْنَا لِجَهَنَّمَ كَثِيراً مِّنَ الْجِنِّ وَالإِنسِ لَهُمْ قُلُوبٌ لاَّ يَفْقَهُونَ بِهَا وَلَهُمْ اَعْيُنٌ لاَّ يُبْصِرُونَ بِهَا وَلَهُمْ آذَانٌ لاَّ يَسْمَعُونَ بِهَا اُوْلَـئِكَ كَالاَنْعَامِ بَلْ هُمْ اَضَلُّ اُوْلَـئِكَ هُمُ الْغَافِلُونَ[6]

Na tumeiumbia Jahannamu majini wengi na watu. Wana nyoyo, lakini hawafahamu kwazo. Na wana macho, lakini hawaoni kwayo. Na wana masikio, lakini hawasikii kwayo. Hao ni kama nyama howa, bali wao ni wapotofu zaidi. Hao ndio walio ghafilika.

Maelezo kuhusiana na Aya

Hapa wanatajwa watu wa motoni, na sababu ya kutiwa kwao motoni, ni hiyo iliyotajwa, sio wameonewa na Mwenyeezi Mungu, sababu yake ni hiyo, kuwa wamepewa ala (vitu) za kutambua haki - waifuate- na kuitambua batili, waiepuke, nao hawataki, basi hii ndiyo sababu ya kutiwa motoni, Mwenyeezi Mungu hawaonei viumbe vyake, anawapitishia uadilifu wote.

kwa hiyo kudiriki uhakika katika nidhamu ya dunia ni tabu sana, na kudiriki uhakika wa amali ni tabu inayoonekana na wengi miongoni mwa wanaadamu. lakini katika nidhamu ya Akhera uhakika wa kila kitu utadhihirika, na viumbe vyote vitakuwa na uhai, mbali ya hayo, katika nidhamu ya akhera pia kutakuwa na ujira na malipo mema kwa wale waliofanya mema na malipo mabaya kwa wale waliotenda mabaya.

Katika somo hili tutaashiria baadhi ya masadikisho yanayothibitisha ubora wa nidhamu ya Akhera kuliko nidhamu ya dunia.

 

[1] Suratul-Baqarah Aya ya 207.

[2] Suratul Baqarah Aya ya 261.

[3] Suratul-Qasas Aya ya 88.

[4] Surat Arrahman Aya ya 26.

[5] Surat Al-aaraf Aya ya 116

[6] Surat Al-Aaraf Aya ya 179

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini