DESTURI NA MAADILI YA DINI

 BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

DESTURI NA MAADILI YA DINI NO.1

Dini ni njia maalumu anayoifuata mwanaadamu, njia ambayo ndani yake imekusanya desturi na maadili mbali mbali ambayo yanamuongoza mwanaadamu Katika uongofu.

Ufafanuzi huo hautoshi kufafanua haki na uhakika wa dini, kwa sababu sio desturi na maadili mbali mbali tu yanayoweza kuifafanua dini, au kumuongoza mwanaadamu katika uongofu. Kwa hiyo, maelezo na mabainisho aliyoyatoa ustadh Sayyid Qutub kuhusiana na dini hayawezi kutosheleza wala hayakubaliki katika kuifafanua dini. Sayyid Qutub anasema:-

“Dini ni njia na mfumo maalumu, dini ni haki, dini ni uongofu, dini ni njia asili ya kimaumbile iliyomo ndani ya nafsi ya mwanaadamu, dini ni fitra ya kila mwanaadamu, kwa hiyo kila mwanaadamu ana fitra maalumu ya dini iliyomo katika nafsi yake, fitra ambayo inamfanya yeye kuwa na shauku ya kutafuta dini, kuwa na imani na dini; yaani kufuata mwenendo wa dini kimatendo, dini ni mkusanyiko wa mitazamo ya kilimwengu, na itikadi maalumu”.[1]

Ufafanuzi huo sio ufafanuzi kamili unaoweza kubainisha uhakika wa dini, kwa sababu:-

Moja: Ufafanuzi kamili wa dini ni ule ufafanuzi unaoiarifisha dini kwa kuzingatia hali halisi ya uhakika wake, na kwa kuzingatia nyanja na pande zote za dini, kwa hiyo kuifafanua dini kuwa ni njia iliyo na mfumo maalumu, mfumo ambao umekusanya ndani yake haki na mambo mengine haukubaliki, kwa sababu njia na mfumo huo ni miongoni mwa sehemu ya haki na uhakika wa dini, na kuna tofauti nyingi baina ya vitu hivyo viwili, (haki na uhakika, (ukweli)) hivyo hatuwezi kuifafanua dini kutokana na sifa zake za nje tu.

Mbili: Katika jamii kuna njia nyingi, njia ambazo kila moja inawezekana ikawa na mfumo wake maalumu, na baadhi ya njia pia zinawezekana zikawa zimekusanya fitra maalumu katika nafsi ya mwanaadamu, kwa upande mwengine, kila njia kwa namna fulani inawezekana ikawa imekusanya desturi na amri mbali mbali, kwa hiyo kuifafanua dini kuwa ni njia iliyo na mfumo, mfumo ambao umekusanya mambo mbali mbali kijumla jamala, kwa hakika ni kuiarifisha dini bila ya kuzingatia sifa zake maalumu. Basi ufafanuzi huo haukubaliki.

Tatu: Dini sio mwenendo tu, mwenendo ambao ndani yake mna matendo yanayotakiwa kufanyiwa amali zake, yaani kuyafanyia amali matendo yaliyoamrishwa peke yake sio dini, kwa maelezo mengine, ili mtu awe ni mwenye dini ni lazima kwanza awe na itikadi, itikadi ambayo inatakiwa iwe katika dhati ya nafsi yake, baada ya kuwa na itikadi, atakuwa na hisia, hisia ambazo zinatokana na itikadi yake aliyonayo, wakati huo mtu huyo anaweza kuikubali dini kwa dhati ya nafsi yake na kwa hisia zake zote. Ndio, hiyo ndio maana ya mtu kuwa na dini, na mtu kama huyo huitwa mtu mwenye dini.

Nne: Kuifafanua dini kuwa ni fikra na mitazamo ya kiulimwengu, au itikadi maalumu hakukubaliki, na ufafanuzi huo una utata ndani yake, kwa sababu kila fikra za kiulimwengu sio dini, na kuwa na itikadi maalumu pia hakumaanishi mtu kuwa na dini, vile vile kila kundi lililo na itikadi au fikra za kilimwengu halimaanishi kuwa lina dini, tukiachana na hayo, mabainisho hayo hayaonyeshi uhakika wala haki ya dini.

Tutaendelea na mada hiyo katika makala inayofuata.


[1] Sifa za itikadi za Kiislamu. Sayyid Qutub, tarjama ya Sayyid Muhammad Khomenei, uk 11-19