DINI NA SEREKALI

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

DINI NA SEREKALI

Kuna kauli za wale wanaosema kuwa:-

“Ama jambo lisilokubalika katika serikali ya dini ni kule kutoendana sambamba baina ya serikali ya dini na elimu ya dini ambayo ndio ushahidi unaotumiwa na wanaserikali wa dini hiyo katika kuendeleza malengo ya serikali yao, na kwa sababu serikali ya dini siku zote ina mtizamo na mfumo maalumu ambao unaotokana na itikadi za dini, basi ni jambo lisilowezekana kwa serikali hiyo kuwa na mitazamo (mifumo) tofauti ambayo inaendana kinyume na elimu ya dini (au uhakiki wa dini ) wa serikali hiyo. Basi vipi inakubalika kwa serikali ya dini kuwa na mtazamo (mfumo) huo maalumu, na kuwa na mitazamo (mifumo) mengine isiyoendana sambamba na serikali ya dini kwa wakati mmoja”? na watu wengine wamedai kuwa:-

Suala lenye kukataliwa katika Nyanja za utafiti wa kidini na wale wanaohakiki suala la uongozi wa kidini, ni kwamba haiwezekani kwa siasa ya kidini kuwa ishike mtazamo mmoja tu wa kidini, bali kinachotakiwa ni kwamba siasa za kidini ziitupilie macho mitazamo yote ya kidini kutoka kwa watafiti mbali mbali, na kutokana na kwamba siasa ya kidini haiwezi kuitupia macho mitazamo yote na kuifanyia kazi yote kwa pamoja, hivyo basi siasa za kidini zinatakiwa kuzisoma fikra hizo kisha kupitia ile fikra iliyobobea zaidi katika kuleta mafanikio ya uongozi wa kidini na manufaa ya jamii. Na hilo ndilo lililo na maana kwamba siasa ya kidini kushikamana na mfumo mmoja na fikra moja. Kwa msingi huo tuliouzungumza hapo; kuwa siasa ya dini inatakiwa kuisoma misimamo na fikra zote, jambo hilo limesababisha baadhi ya wanasiasa na viongozi kuitumia mifumo ya dini na kuichanganya na mifumo ya nchi za kimagharibi huku wakitilia mkazo katika kushikamana nayo. Kupitia mifumo ya kiakili na kimantiki haiwezekani mtu au serikali kuchanganya mifumo tofauti kisha akaifanya kuwa ni mfumo mmoja, ule mfumo ambao unakwenda na upepo wa jamii zilivyo, hauwezi kuwa mfumo bora wa siasa. (Serikali ni lazima iwe na kanuni na sheria maalumu zitakazoweza kuleta maslahi ya wanajamii). Hivyo ikiwa tutatafuta mifumo ambayo inakwenda sambamba na mifumo tofauti hatuwezi kupata mfumo ambao ndani yake utakuwa na mifumo tofauti, kwa upande mwengine, huku mfumo huo ukawa unakwenda sambamba na mifumo mengine. Kama siasa itajengwa katika mfumo kama huo, basi hapana shaka haiwezi kuyafikia malengo ya kisiasa, na mfumo huo utatoka nje ya siasa.

kwa hakika kauli hiyo haikubaliki kwa sababu:-

Moja: Ingelikuwa serikali ya dini ni yenye mitazamo na mifumo mbali mbali bila shaka tungelikuwa tuna aina mbali mbali za dini, lakini kama tulivyokwisha elezea hapo mwanzo kuwa malengo ya dini ni yenye kwenda sambamba na elimu ya dini, kwa hiyo kwa sababu malengo ya dini ni mamoja, uongozi wa kisiasa wa dini nao ni lazima uwe mmoja, hii ni kutokana na kwamba uongozi huo hujengeka kupitia misingi ya dini, na lengo la kujengwa mfumo huo wa siasa ya uongozi wa dini ni kuyadhamini yale malengo yote ambayo yamesajiliwa na dini kwa ajili ya kuboresha maisha ya wanaadamu ya duniani na Akhera.

Mbili: Ikiwa Serikali ya dini iko chini ya uongozi wa muokozi wa mwisho, Hadharati Mahdi Ajjala Llahu Taala Sharifu (r.a) hivi inawezekana au kukubalika kuwepo mifumo mengine yasiyoendana na serikali ya dini hiyo, au isiyoendana na elimu ya serikali ya dini hiyo?. Yaani msimamizi wa serikali hiyo atakubali au hatakubali mfumo wa Serikali kama hiyo?

Ikiwa Imamu (a.s) atakubali mfumo wa serikali hiyo, basi maelezo hayo yatakuwa yanapinga Uimamu wa Hadharati Mahdi (a.s), na ikiwa Imamu (a.s) anaupinga mfumo wa Serikali hiyo basi katika serikali ya dini hakuna malengo wala mifumo tofauti isiyoendana na nidhamu ya serikali ya dini, au isiyoendana na maadili ya dini kijumla, na katika Serikali hiyo ya dini hakutakuwa na athari zozote mbaya zinazopinga mfumo huo wa Serikali ya dini.

Tatu: Hivi Mtume Muhammad (s.a.w.w) alikuwa na mfumo au malengo yasiyoendana sambamba na serikali ya dini yake? Au hakuwa na mfumo kama huo? Kama alikuwa na mfumo kama huo basi ni kwa sababu gani Serikali ya siasa ya dini yake ilikuwa na mafanikio na yenye kukubalika? Na ikiwa hakuwa na mfumo kama huo basi natija inayopatika ni kuwa katika serikali ya siasa ya Mtume (s.a.w.w) hakukuwa na mfumo kama huo.

Nne: Kimsingi, malengo na mifumo inayotakiwa kuwa katika serikali ya siasa ya dini huwekwa mwanzo pale tu inapoanzishwa serikali hiyo, na sio kwanza serikali ianzishwe na baada ya kupita muda mrefu kufikiriwe malengo na mfumo unaotakiwa kutekelezwa katika serikali hiyo, hivi serikali ya siasa ya dini ni lazima iwe katika mfumo unaoendeshwa na Mtume Muhammad (s.a.w.w), au iwe katika mfumo wa Abuhurayra? Na hivi serikali ya siasa ya dini ni lazima iwe katika mfumo wa Imamu Ali (a.s) au iwe katika mfumo wa Ibni Khatab?

Ikiwa uendaji sambamba wa malengo (mifumo) ya Serikali ya dini na elimu ya dini inamaanisha kuwa Serikali hiyo ina upungufu basi ni mfumo wa malengo gani ni haki na mfumo wa malengo gani sio haki? Hapana shaka mfumo alioutumia Mtume Muhammad (s.a.w.w.) katika kuendesha serikali ya dini ni mfumo bora na ndio mfumo wa haki, na mfumo huo basi ndio utakaoendelezwa na khalifa wake Hadharati Mahdi Ajjala Llahu Taala Sharifu (r.a).

Kutokana na maelezo hayo tuliyoyaelezea itakuwa imefahamika kuwa serikali ya siasa ya dini inaendeshwa kwa mujibu wa misingi (mifumo) ya elimu ya dini. Na vitu viwili hivyo vinaendana sambamba katika malengo na mifumo ya uendeshwaji wa serikali hiyo ya siasa ya dini.

Inawezekana msemaji wa kauli hiyo hakuweza kupambanua baina dini ya Kikiristo na dini ya Kiislamu, na amezitizama dini hizo kwa mtazamo mmoja, basi kakosea katika kutafautisha baina ya Imamu Ali (a.s) na watu wa Hawariyuna. Na amemuweka Imamu Ali (a.s) na Hawariyuna katika nafasi moja, hali ya kwamba wanatofautiana katika kila kitu, daraja ya utukufu aliyonayo Imamu Ali (a.s) haiwezi kufananishwa na watu hao kwa mtazamo wowote ule, natuangalie kauli ya Mwenyeezi Mungu juu ya Hawariyuna:-

فَلَمَّا اَحَسَّ عِيسَي مِنْهُمُ الْكُفْرَ قَالَ مَنْ اَنصَارِى إِلَي اللهِ قَالَ الْحَوَارِيُّونَ نَحْنُ اَنصَارُ اللهِ آمَنَّا بِاللهِ وَاشْهَدْ بِاَنَّا مُسْلِمُونَ[1]

Isa alipo hisi kuwa kati yao pana ukafiri alisema: Nani wasaidizi wangu kwa Mwenyezi Mungu? Wanafunzi wake wakasema: Sisi ni wasaidizi wa Mwenyezi Mungu. Tumemuamini Mwenyezi Mungu, na shuhudia kwamba sisi hakika ni Waislamu

Na katika aya nyengine Allah (s.w) anasema:-

وَإِذْ اَوْحَيْتُ إِلَي الْحَوَارِيِّينَ اَنْ آمِنُواْ بِى وَبِرَسُولِى قَالُوَاْ آمَنَّا وَاشْهَدْ بِاَنَّنَا مُسْلِمُونَ[2]

Na nilipo wafunulia Wanafunzi kwamba waniamini Mimi na Mtume wangu, wakasema: Tumeamini na shuhudia kuwa sisi ni Waislamu.

Hawariyuna ijapokuwa walidai kuwa wana imani, lakini hatima ya watu hao walihalifu amri za Mola wao na Mjumbe wao. Kwa upande mwengine sifa za Imamu Ali (a.s) na utukufu wake unashuhudiwa na kila mmoja wetu, Imamu Ali (a.s) tangu alipozaliwa hadi kufa kwake alikuwa ndiye Muumini bora aliyetii amri za Mola wake na Mtume wake Muhamaad (s.a.w.w), na aliiendesha serikali ya dini katika mfumo ule ule aliouacha Mtume Muhammad (s.a.w.w.), na kwa sababu ya utukufu wake mtu huyo Mwenyeezi Mungu Mtukufu alimchagua kuwa ni khalifa na kiongozi wa kuiongoza dini yake baada ya Mtume Muhammad (s.a.w.w). pale Allah (s.w) aliposema:-

يَا اَيُّهَا الرَّسُولُ بَلِّغْ مَا اُنزِلَ إِلَيْكَ مِن رَّبِّكَ وَإِن لَّمْ تَفْعَلْ فَمَا بَلَّغْتَ رِسَالَتَهُ وَاللّهُ يَعْصِمُكَ مِنَ النَّاسِ إِنَّ اللّهَ لاَ يَهْدِى الْقَوْمَ الْكَافِرِينَ[3]

Ewe Mtume! Fikisha uliyo teremshiwa kutoka kwa Mola wako Mlezi. Na ikiwa hukufanya hayo basi hukufikisha ujumbe wake. Na Mwenyezi Mungu atakulinda na watu. Hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi watu makafiri.

 

[1] Surat Al-Imrani Aya ya 52

[2] Surat Al-Maidah Aya ya 111.

[3] Surat Al-Maidah Aya ya 67