HIJJATUL_WIDAA

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
HIJJATUL_WIDAA
Allah (s.w) katika kitabu chake kitukufu anasema:-

يَا اَيُّهَا الرَّسُولُ بَلِّغْ مَا اُنزِلَ إِلَيْكَ مِن رَّبِّكَ وَإِن لَّمْ تَفْعَلْ فَمَا بَلَّغْتَ رِسَالَتَهُ وَاللّهُ يَعْصِمُكَ مِنَ النَّاسِ إِنَّ اللّهَ لاَ يَهْدِى الْقَوْمَ الْكَافِرِينَ[1]

Ewe Mtume! Fikisha uliyo teremshiwa kutoka kwa Mola wako Mlezi. Na ikiwa hukufanya hayo basi hukufikisha ujumbe wake. Na Mwenyezi Mungu atakulinda na watu. Hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi watu makafiri.

Maelezo kuhusiana na Aya.

Tarehe kumi na nane mwaka wa kumi hijiria, majira ya asubuhi, Mtume Muhammad (s.a.w.w) alipokuwa akirejea kutoka Makka baada ya kufanya ibada ya Hijja, akiandamana na Waislamu zaidi ya laki moja. Mtume (s.a.w.w) pamoja na Waislamu walipofika njia panda, njia ziendazo Madina, Misri na Iraqi, katika bonde la khom, ndipo Mwenyeezi Mungu alipoteremsha aya :-

“Ewe Mtume! Fikisha uliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wako, na kama hutafanya basi hukufikisha ujumbe wake.

“Mtume Muhammad (s.a.w.w) akashika mkono wa Imamu Ali (a.s) akasema:

Ambaye mimi natawalia mambo yake, basi ali ni mtawala wake. Ee Mwenyeezi Mungu! Muunge atakayemuunga (Ali) na mtenge atakayemtenga (Ali) na mnusuru atakayemnusuru, mtupe atakayemtupa (Ali)”. Kisha baada ya hapo masahaba walianza kutoa kiapo cha utiifu kwa Imamu Ali (a.s), na akapewa hongera na masahaba ya kuwa yeye amekuwa kiongozi wa waislamu wote.

Pale pale Mwenyeezi Mungu akateremsha Aya:-

الْيَوْمَ اَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَاَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِى وَرَضِيتُ لَكُمُ الإِسْلاَمَ دِيناً[2]

Leo nimekukamiliishieni Dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni UISLAMU uwe ndiyo Dini.

Katika maelezo hayo tuliyoyaelezea kuhusiana na Aya hiyo ya 3 na Aya ya 67 ya Suratul Maidah inathibitisha kuwa Mwenyeezi Mungu alimuhimiza Mtume Muhammad (s.a.w.w) afikishe kila aliloambiwa asibanie hata chembe wala asiogope lolote kumfika, hakuna awezaye kupitisha lake pasi na Mwenyeezi Mungu kutaka, Aya hiyo ilishuka wakati Mtume Muhammad (s.a.w.w.) alipokuwa akirudi hija, (hija ambayo inajulikanwa kwa jina la hijjatul-widaa), yaani hijja ya muago, na hiyo ilikuwa ndio hija yake ya mwisho kabla ya kufa kwake, basi Mwenyeezi Mungu alimuamrisha Mtume wake kumchagua kiongozi atakayeongoza uma wa Kiislamu baada yake, basi Mtume Muhammad (s.a.w.w) aliwaita na aliwakusanya wafuasi wake wote akawabainishia kuwa Imamu Ali (a.s) ndiye atakayekuwa walii na kiongozi wao baada yake.

Jambo jengine wanalokumbushwa waislamu kupitia Aya hiyo ni kuwa; kila mwenye kujua jambo anatakiwa awabainishie wengine bila ya kuficha hata chembe au kuogopa hata kidogo.

Wakikushituwa Wewe usishituke   Yupi awezaye kupitisha lake.

Wakiwa na lao Mungu ana Yake    wakikushituwa wewe usishituke.

Ibara maarufu ambayo inajulikana na kila mmoja wetu inayohusiana na siku hiyo inasema hivi:-

"من کنت مولاه فهذا علی (علیه السلام ) مولاه ..."

Tukiendelea na mada yetu inayohusiana na madai yaliyotolewa na baadhi ya watu kuwa serikali ya dini haiendani na mifumo ya kidini, tunasema hivi:-

Aliyesema kauli hiyo hakuzingatia utukufu wa serikali ya dini ya Mtume Muhammad (s.a.w.w), na hakuweza kuitambua thamani na daraja aliyonayo Mtukufu huyo, kwa mtazamo wa mtu huyo, thamani ya mfumo wa malengo ya serikali ya dini ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) ni sawa na thamani ya mfumo na malengo ya Serikali ya Abuhurayra na Ibni Khatab.

Hivi mfumo wa Serikali ya dini ya Hadharati Muhammad (s.a.w.w) ndio mfumo bora kulinganisha na mifumo ya serikali nyengine, au mifumo ya serikali nyengine ndio mifumo bora? Ikiwa mifumo mengine ndio mifumo bora basi utume wa Hadharati Muhammad (s.a.w.w) na Uimamu wa Imamu Ali (a.s) utakuwaje? Na ikiwa mfumo wa serikali ya dini ya Hadharati Muhammad (s.a.w.w.) ndio mfumo bora basi kwa mujibu wa madai hayo yaliyotolewa haiwezekani kuwepo mfumo mwengine ulio bora isipo kuwa mfumo wa Serikali ya dini ya Mtukufu huyo, (Nabii Muhammad (s.a.w.w.). Na kwa nini Mtume Muhammad (s.a.w.w) na Imamu Ali (a.s) walikuwa na kauli moja na mwenendo mmoja katika kuiendesha serikali ya dini?. Na kwa nini Ahlulbayt (a.s) walifanya jitihada zao zote katika kuendesha na kuendeleza mfumo mmoja tu wa serikali ya siasa ya dini?. (ambao ni mfumo ule ule alioutumia Hadharati Muhammad (s.a.w.w)).

Mwisho kabisa tunaifunga mada hiyo kwa kumpa ushauri bwana au bibi mheshimiwa aliyetoa madai hayo, kuwa ni vyema kama utafanya uhakiki na utafiti kuhusu serikali ya dini na taaluma za dini, kwa sababu kama utasoma qur-ani takatifu na tarekhe ya Kiislamu utakuta kwamba: Uislamu ni dini na dola, kwa hiyo siasa imekuwa na fungamano kubwa na dini, na tunasema kwamba:

Mwanasiasa, kazi yake ni kuisaidia serikali katika kuweka sheria na uongozi mzuri, na kuisaidia jamii katika kufahamiana na Serikali, na wala si kuwasaidia madhalimu katika kudhuru umma, kwa sababu katika uislamu hakuna baya ambalo huwa ni zuri kwa ajili ya siasa, wala hakuna haramu ambayo huwa halali katika siasa.

[1] Surat Al-Maidah Aya ya 67


[2] Surat Al-Maidah Aya ya 3

 


MWISHO