Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

MAKUNDI YA WANAADAMU SIKU YA KIAMA NO.2

0 Voti 00.0 / 5

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
MAKUNDI YA WANAADAMU SIKU YA KIAMA NO.2


* wanaadamu watagawika makundi mangapi katika siku ya malipo na jazaa?
Katika makala iliyopita inayohusiana na makundi ya wanaadamu siku ya Kiama, tulilielezea kundi la mwanzo, na ama katika makala hii tutaendelea kuelezea makundi mengine.
Siku ya Kiama walimwengu watagawiwa katika makundi totfauti kwa mujibu wa itikadi na amali zao walizozifanya duniani.
*Kundi la watu watakaoelekea upande wa kulia. Neno یمین ndani ya Qur-ani limekuja likiwa na maana ya upande wa kulia, na watu watakaoelekea upande wa kulia ni wale ambao siku ya Kiyama watapewa daftari ya amali zao walizozitenda kwa mkono wa kulia, basi hiyo ni alama inayoonyesha saada njema ya watu hao, kama tunavyosoma ndani ya qur-ani kuhusiana na watu hao.

فَاَمَّا مَنْ اُوتِيَ كِتَابَهُ بِيَمِينِهِ. فَسَوْفَ يُحَاسَبُ حِسَاباً يَسِيرا. وَيَنقَلِبُ إِلَي اَهْلِهِ مَسْرُوراً[1]  

Ama atakaye pewa daftari lake kwa mkono wa kulia, Basi huyo atahisabiwa hisabu nyepesi, Na arudi kwa ahali zake na furaha.
Watu hao watabakia Peponi milele na kunufaika na neema zake Allah (s.w), wengi wao wa kundi hilo watakaofaidika na neema hiyo ni kutoka katika uma wa Hadharati Muhammad (s.a.w.w) kama tunavyosoma ndani ya qur-ani:-

لِّاَصْحَابِ الْيَمِينِ. ثُلَّةٌ مِّنَ الاَوَّلِينَ. وَثُلَّةٌ مِّنَ الآخِرِينَ[2]

Kwa ajili ya watu wa kuliani. Fungu kubwa katika wa mwanzo, Na fungu kubwa katika wa mwisho.
Watu hao ni waumini, na waliishi duniani kwa kutekeleza maamrisho ya Mol wao, na walipokuwa wakikutwa na tabu au mashaka hunasihiana na kuhimizana kuwa na subra, na walikuwa wakifanya jitihada zao zote ili kuwaondolea matatizo yao wale waliokuwa wakihitajia misaada kutoka kwao, basi waliwasaidia na kuwapa himaya mafakiri, mayatima, na masikini, Mwenyeezi Mungu anawaarifisha watu hao kwa kusema:-

ثُمَّ كَانَ مِنَ الَّذِينَ آمَنُوا وَتَوَاصَوْا بِالصَّبْرِ وَتَوَاصَوْا بِالْمَرْحَمَةِ. اُوْلَئِكَ اَصْحَابُ الْمَيْمَنَةِ[3]

Tena awe miongoni mwa walio amini na wakausiana kusubiri na wakausiana kuhurumiana. Hao ndio watu wa kheri wa kuliani.
*Kundi la watu wanaosonga mbele katika mambo ya kheri. Kundi litakalosonga kuelekea mbele ni lile kundi la watu ambao, baada ya kuwadhihirikia haki hawakupinga wala kufanya uvivu, bali walimuamini Mwenyeezi Mungu na waliyaamini yale waliyokuja nayo Mitume, na walivuka hatua ya kufanya amali njema nzuri na kutii maamrisho na desturi za Mola wao, katika qur-ani tunasoma:-

اُوْلَئِكَ يُسَارِعُونَ فِى الْخَيْرَاتِ وَهُمْ لَهَا سَابِقُونَ[4]

Basi wote hao ndio wanao kimbilia katika mambo ya kheri, na ndio watakao tangulia kuyafikia.
Watu hao waliotangulia katika kufanya yale ambayo wameamrishwa na Mola wao, na wakamtii Mwenyeezi Mungu na Mitume yake, na walipokutwa na tabu walivuta subira, na wakapigana jihadi katika njia ya Mwenyeezi Mungu, hapana shaka kuwa watu hao ndio watu bora ukilinganisha na watu wengine


وَمَا لَكُمْ اَلاَّ تُنفِقُوا فِى سَبِيلِ اللهِ وَلِلَّهِ مِيرَاثُ السَّمَاوَاتِ وَالاَرْضِ لاَ يَسْتَوِى مِنكُم مَّنْ اَنفَقَ مِن قَبْلِ الْفَتْحِ وَقَاتَلَ اُوْلَئِكَ اَعْظَمُ دَرَجَةً مِّنَ الَّذِينَ اَنفَقُوا مِن بَعْدُ وَقَاتَلُوا وَكُلّاً وَعَدَ اللهُ الْحُسْنَي وَاللهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ[5]
Na mna nini hata hamtoi katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na hali urithi wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu? Hawawi sawa miongoni mwenu wenye kutoa kabla ya Ushindi na wakapigana vita.
Hao wana daraja kubwa zaidi kuliko wale ambao walio toa baadae na wakapigana. Na wote hao Mwenyezi Mungu amewaahidia wema. Na Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda.
Watu waliotangulia katika mambo ya kheri ni wale walio karibu na Mola wao, kama anavyosema Allah (s.w):

وَالسَّابِقُونَ السَّابِقُونَ. اُوْلَئِكَ الْمُقَرَّبُونَ[6]

Na wa mbele watakuwa mbele. Hao ndio watakao karibishwa.
Watu hao watapata jazaa na malipo mema, hata utakapofika muda wao wa kuitika wito wa Mola wao (yatakapowafikia mauti) hawatakuwa na hofu wala woga wowote, na watanufaika na kila neema ya Mwenyeezi Mungu katika makazi yao huko Peponi. kama tunavyosoma ndani ya Qur-ani:-

فَرَوْحٌ وَرَيْحَانٌ وَجَنَّةُ نَعِيمٍ. وَاَمَّا إِن كَانَ مِنَ اَصْحَابِ الْيَمِينِ . فَسَلاَمٌ لَّكَ مِنْ اَصْحَابِ الْيَمِينِ وَاَمَّا إِن كَانَ مِنَ الْمُكَذِّبِينَ الضَّالِّينَ [7]
Basi akiwa miongoni mwa walio karibishwa, Basi ni raha, na manukato, na Bustani zenye neema. Na akiwa katika watu wa upande wa kulia, Basi ni Salamu kwako uliye miongoni mwa watu wa upande wa kulia.
*Kundi la watu wenye (Ikhlasi) waliozitakasa na kuzisafisha nafsi zao na maovu.
Kundi hilo ni kundi la waja wema na watiifu wa Mwenyeezi Mungu (s.w), watu wa kundi hilo mbali ya kumuamini Mwenyeezi Mungu, na kutangulia katika kufanya mambo mema, vile vile wana utukufu maalumu mbele ya Allah (s.w), utukufu ambao hauwezi kuonekana katika viumbe wengine, Mwenyeezi Mungu huwaepusha waja wake hao na kila maovu na machafu, kama tunavyosoma kuhusiana na Nabii Yussuf (a.s):-


وَلَقَدْ هَمَّتْ بِهِ وَهَمَّ بِهَا لَوْلا اَن رَّاَي بُرْهَانَ رَبِّهِ كَذٰلِكَ لِنَصْرِفَ عَنْهُ السُّوءَ وَالْفَحْشَاء إِنَّهُ مِنْ عِبَادِنَا الْمُخْلَصِينَ[8]


Na hakika yule mwanamke alimtamani, na Yusuf angeli mtamani lau kuwa hakuona ishara ya Mola wake Mlezi. Hayo hivyo ni kwa ajili tumuepushe na uovu na uchafu. Hakika yeye alikuwa katika waja wetu waliosafishwa.
Watu hao wema watukufu walio na Ikhlasi wametukuka na wako katika daraja ya juu kabisa, kiasi ya kwamba hawawezi kufanya maasi hata kwa kukosea au kusahau, wako katika amani,  na wamesalimika na wasi wasi wa shetani na iblisi. Mwenyeezi Mungu Mtukufu kuhusiana na watu hao anasema hivi:-

قَالَ فَبِعِزَّتِكَ لاَغْوِيَنَّهُمْ اَجْمَعِينَ. إِلاَّ عِبَادَكَ مِنْهُمُ الْمُخْلَصِينَ[9]

Akasema (Iblisi): Naapa kwa utukufu wako, bila ya shaka nitawapoteza wote,Isipo kuwa wale waja wako miongoni mwao walio khitariwa.

[1] Surat Inshiqaaq Aya ya 7-9.

[2] Suratul-Waqiah Aya ya 38-40.

[3] Suratul Balad Aya ya 17-18.

[4] Surat Al-Muuminuun aya ya 61

[5] Suratul-Al-Hadiyd Aya ya 10.

[6] Surat-Al-Waqiah Aya ya 10-11

[7] Surat Al-Waqiah aya ya 88-91

[8] Surat Yussuf Aya ya 24

[9] Surat sad Aya ya 82-83.

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini