Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

UMUHIMU WA DINI KATIKA JAMII

0 Voti 00.0 / 5

 BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.

UMUHIMU WA DINI KATIKA JAMII

Neno “dini” ni neno lililozoeleka katika jamii. Na kila mmoja kidhahiri anafahamu maana yake, lakini maana hasa ya dini sio ile maana ambayo kila mmoja wetu amezoea kuisikia, kwani watu hulitumia neno hilo  kwa maana tofauti, na kila dini, madhehebu, au kundi hulitumia neno hilo kwa manufaa ya dini yake au madhehebu yake, jambo ambalo ni lazima kila mmoja kulitambua ni kwamba neno hilo kwa mtazamo wa kitaalamu (kiistilaha) lina maana pana zaidi. Maana sahihi ya neno dini tunalokusudia ni dini ya Kiislamu, kwa hiyo kuna tofauti baina ya neno dini (linalotumiwa likiwa na maana ya dini) ya Kiislamu, na neno dini linalotumiwa likiwa na maana ya dini zilizopotoshwa.

Kimsingi dini iliyopotoka sio dini, kwa hiyo sio sahihi na ni jambo lisilowezekana kulitumia neno dini, (lenye maana ya dini iliyopotoka) dhidi ya dini ya haki.

Dini ya haki ni ile dini ambayo kila taaluma yake kwa mfano; maamrisho yake, hukumu na makatazo yake,n.k yote yawe yanahusiana na Mola Mtukufu. Dini ya haki ni ile dini inayotoa muongozo na inayowapa wanaadamu saada na neema ya duniani na Akhera. Kwa hiyo ikiwa dini haitakuwa na sifa au vigezo kama hivyo, au ikiwa imepotoshwa na wanaadamu, au ikiwa kama ni maonyesho na mapendekezo ya watu katika mwenendo na matendo kwa madai ya kuwa mwenendo au matendo hayo yanakubaliwa na Mola muumba, basi hiyo sio dini isipokuwa njia tu waliyoishikilia watu katika kuziridhisha nafsi zao kwa yale wanayoyataka. Ndio, hiyo sio dini ya haki ya Mwenyeezi Mungu, bali ni dini iliyopotoka.

Katika dunia ya leo, neno dini linatumiwa vibaya, na liko chini ya milki ya maadui wa kiislamu, maadui ambao wana madai ya kuwaonyesha watu njia ya haki na iliyo halali, lakini kwa himaya ya waislamu wote maadui hao hawataona mafanikio yoyote katika propaganda zao za kutaka kuiharifu na kuipotoa dini ya Kiislamu, kwa sababu dini ya Kiislamu ni dini ya haki iliyoteremshwa na Mwenyeezi Mungu na Yeye ndiye atakayeihifadhi. Kwa hiyo kusudio la dini katika maudhui ya falsafa ya dini, ni dini ya Kiislamu pekee, (na Waislamu wa haki ni wale ambao wanaifuata dini hiyo kutokana na maamrisho ya Mola wao, humtii Mwenyeezi Mungu na Mitume yake, pamoja na Ahlulbayt (a.s)) ndio dini ya kiislamu ndio dini ya haki inayobainisha mambo ya uhakika na ya haki.

Zingatio: Kuifafanua dini kuwa ni mfumo wa mwanaadamu unaomuweka yeye katika mipaka maalumu sio sahihi, kwa sababu mipaka huwekwa katika mambo ambayo yanawezekana kuachwa maslahi yake, kwa hiyo ikiwa dini itafafanuliwa kuwa ni mipaka inayomfunga na kumuweka mwanaadamu katika hali fulani, basi mipaka hiyo haitomletea mwanaadamu huyo maslahi yoyote, isipokuwa itamletea hatari katika maisha yake, kwa hiyo dini sio mipaka, kwa sababu dini kuwa mipaka hakutoiletea dini hiyo manufaa wala maslahi yoyote, yale yanayobainishwa na dini ni haki na yenye ukweli ndani yake, dini imewapa ahadi wanaadamu ya kuwatekelezea mahitajio yao, na dini ina majukumu ya kuwaongoza wanaadamu katika neema, kwa hiyo ikiwa watu watajitetea na kutoa udhuru kuwa dini ni mipaka, na sababu hiyo ndiyo iliyowafanya kuikana na kuikataa dini, kwa hakika hawajafahamu maana ya mipaka hiyo iliyodaiwa kuwa ni mipaka ya dini, watu hao wamefuata njia iliyo na hatari, na wako katika hilaki hali ya kuwa wenyewe hawajitambui, wamejiweka mbali na dini na wenye dini kwa udhuru wa kuwa eti wao ni watu huru, watu hao wanadai kuwa wanakimbia mipaka hiyo ya dini, kwa hakika huko sio kukimbia, huko ni kujitia katika hatari na majanga hali ya kuwa wenyewe wanatambua kuwa wanapotea, au kwa pengine hawajitambui kua wako katika njia iliyopotoka. Allah anawaambia watu hao kwa kusema:-

بَلْ يُرِيدُ الإِنسَانُ لِيَفْجُرَ اَمَامَهُ  . يَسْاَلُ اَيَّانَ يَوْمُ الْقِيَامَةِ[1]

Lakini mtu anataka tu kuendelea na maasi kwa siku zilioko mbele yake. Anauliza: Lini itakuwa hiyo Siku ya Kiyama?.

Zingatio: Kwa ufafanuzi huo wa dini, kumeonekana kwa uwazi, sababu zinazompelekea mwanaadamu kujiepusha na dini, kwa hiyo ikiwa mwanaadamu atadai kuwa hana mahitajio yoyote yale anayoyahitajia katika maisha yake, (mahitajio yaliyomo ndani au nje ya nafsi yake), kwa upande mwengine, akiwa anayahitajia, basi ili kuyafikia mafanikio yake, akitaka asitake ni lazima aanze harakati kuelekea katika dini, (ingawaje mwanaadamu huyo anaweza kuelekea katika njia isiyo sahihi). kwa sababu ni dini pekee ndiyo itakayomtatulia na kumtimizia mahitajio hayo, kwa hiyo, kwa wale ambao wameikubali na kuifuata dini ya haki, kwa hakika watatimiziwa matakwa yao na watapata mahitajio na manufaa yao ya duniani na Akhera.vile vile kwa upande mwengine, kwa wale ambao wamepinga dini ya haki na kutoikubali dini hiyo, na wakatafuta njia walizounda wenyewe kwa fikra zao na kuzifanya njia hizo kuwa ndio maficho yao, wakadhani kuwa maficho hayo ndiyo marejeo yao yanayoweza kuwatimizia mahitajio yao, hali ya kwamba wanajua hawafuati njia iliyo sawa, basi hayo maficho yao ni alama bora inayoonyesha kuwa watu hao wanahitajia dini, basi kwa hakika watu hao hawatapata chochote duniani na Akhera isipokuwa wataambukia majuto na ni hasara ilioje hiyo watakayoipata katika maisha yao ya duniani na Akhera.

 

[1] Surat qiyamah Aya ya 5-6

 

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini