Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

VITUO VYA KIAMA KWA WAUMINI NA WAOVU

0 Voti 00.0 / 5

BISMILAHI RAHMANI RAHIMI
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
VITUO VYA KIAMA BAINA YA WAUMINI NA WAOVU
Katika makala iliyopita tulielezea kuhusu visimamo vya siku ya Kiama, ama katika  makala hii tutaelezea namna ya uingiaji wa vituo hivyo vya Kiyama baina ya Waumini na waovu, kumeashiriwa tofauti tatu za uingiaji wa vituo vya Kiyama baina ya Waumini na Waovu.

1. a.)Hofu, woga, na taharuki.

Walimwengu ambao watahudhuria katika uwanja wa siku ya Kiayama wakiwa na hofu na taharuki kubwa, hofu hiyo ni kutokana na yale waliyoyatenda, kiitikadi na kiamali, kiwango cha hofu ya wanaadamu katika siku hiyo ni kutokana na kupinga maamrisho yake Allah (s.w), kama tunavyosoma ndani ya Qur-ani:-

وَمَا اَدْرَاكَ مَا الْعَقَبَةُ . فَكُّ رَقَبَةٍ. اَوْ إِطْعَامٌ فِى يَوْمٍ ذِى مَسْغَبَةٍ. يَتِيماً ذَا مَقْرَبَةٍ. اَوْ مِسْكِيناً ذَا مَتْرَبَةٍ[1]

Na nini kitakujuvya ni nini njia ya vikwazo vya milimani?. Kumkomboa mtumwa; Au kumlisha siku ya njaa . Yatima aliye jamaa, Au masikini aliye vumbini.

Maelezo kuhusiana na Aya ya 13 ya Suratul-Balad

Watu watiao aibu Dini ya Kiislamu kwa utumwa nawatafadhali wainue macho yao watazame Aya hii, na nyingi mfano wake katika qur-ani zinazopigania uhuru, na atafahamu kuwa utumwa haupendelezi aslan abadan katika Dini hii takatifu.

1.b.) Amani na salama.

Walimwengu Waumini kutokana na amali zao njema, kwa kutekeleza yale waliyoamrishwa na Mola wao na  kuacha yale aliyowakataza watakuwa katika amani na salama, wala hawatakuwa na hofu yoyote. Kama anavyosema Allah (s.w):-

مَن جَاء بِالْحَسَنَةِ فَلَهُ خَيْرٌ مِّنْهَا وَهُم مِّن فَزَعٍ يَوْمَئِذٍ آمِنُونَ[2]

Watakao kuja na mema, watapata bora kuliko hayo. Nao watasalimika na mahangaiko ya Siku hiyo. Na katika Aya nyengine tunasoma:-

لاَ يَحْزُنُهُمُ الْفَزَعُ الاَكْبَرُ وَتَتَلَقَّاهُمُ الْمَلاَئِكَةُ هَذَا يَوْمُكُمُ الَّذِى كُنتُمْ تُوعَدُونَ[3]

Hicho Kitisho Kikubwa hakito wahuzunisha. Na Malaika watawapokea (kwa kuwaambia): Hii ndiyo Siku yenu mliyo kuwa mkiahidiwa!

Ama makafiri na waovu watahudhuria katika uwanja wa Kiyama wakiwa na hofu kubwa, kama tunavyosoma ndani ya qur-ani:-

قُلُوبٌ يَوْمَئِذٍ وَاجِفَةٌ . اَبْصَارُهَا خَاشِعَةٌ[4]

Siku hiyo nyoyo zitapiga piga, Macho yatainama chini.

Watu waovu watasailiwa na kuulizwa masuala magumu katika uwanja wa
 hesabu.

[وَقِفُوهُمْ إِنَّهُم مَّسْئُولُونَ[5

Na wasimamisheni. Hakika hao watasailiwa.

2. kutokuwa na ruhusa ya kuzungumza.

Miongoni mwa utukufu wa Mwenyeezi Mungu katika siku ya Kiyama, ni kuwa; siku hiyo hakutakuwa na mtu yoyote atakayeweza kuzungumza bila ya idhini yake Allah (s.w).

يَوْمَ يَاْتِ لاَ تَكَلَّمُ نَفْسٌ إِلاَّ بِإِذْنِهِ فَمِنْهُمْ شَقِيٌّ وَسَعِيد[6]

Siku hiyo itakapo fika, hatosema hata mtu mmoja ila kwa idhini yake Mwenyezi Mungu. Kati yao watakuwamo waliomo mashakani na wenye furaha.

Na miongoni mwa hekima za Mwenyeezi Mungu katika siku hiyo ya Kiyama ni kuwa siku hiyo ni siku ya kuhudhuria watu wote katika hukumu zake Mola Mtakatifu, basi waovu watadhalilika na Waumini watakuwa katika rehema na baraka zake Allah (s.w).

Na ni kwa sababu hiyo basi, waovu hawatapewa idhini ya kuzungumza katika baadhi ya vituo ili udhalili wao uonekane na wapate jazaa na malipo yao watakayolipwa kutokana na yale maovu waliyoyatenda. kama anavyosema Allah (s.w):-

الْيَوْمَ نَخْتِمُ عَلـٰي اَفْوَاهِهِمْ وَتُكَلِّمُنَا اَيْدِيهِمْ وَتَشْهَدُ اَرْجُلُهُمْ بِمَا كَانُوا يَكْسِبُونَ[7]

 Leo tunaviziba vinywa vyao, na iseme nasi mikono yao, na itoe ushahidi miguu yao kwa waliyo kuwa wakiyachuma.

Muhuri wa kuwekwa kimya peke yake ni adhabu tosha kwa waovu hao, kama anavyosema Mwenyeezi Mungu Mtukufu kuwaambia watu hao wa Jahannamu:-

قَالَ اخْسَؤُوا فِيهَا وَلاَ تُكَلِّمُونِ[8]

Atasema Mwenyezi Mungu: Tokomeeni humo, wala msinisemeze.

Na ikiwa watu waovu watapewa ruhusa ya kuzungumza katika baadhi ya vituo, ni kwa sababu ya kuthibitisha uhalifu wao walioufanya:-

يَوْمَ تَشْهَدُ عَلَيْهِمْ اَلْسِنَتُهُمْ وَاَيْدِيهِمْ وَاَرْجُلُهُم بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ[9]

Siku ambayo zitawashuhudia ndimi zao na mikono yao na miguu yao kwa waliyo kuwa wakiyatenda.

Au watapewa idhini ya kuzungumza kwa ajili ya kuthibitisha uhasama na uadui wao, kama anavyosema Allah (s.w):-

ثُمَّ إِنَّكُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ عِندَ رَبِّكُمْ تَخْتَصِمُونَ[10]

Kisha bila ya shaka mtashitakiana siku ya Kiyama mbele ya Mola wenu.

Au kwa ajili ya kuuonyesha uma kuwa mazungumzo yao ni alama tosha inayoonesha majuto na hasara waliyoipata watu hao.

يَوْمَ يَقُولُ الْمُنَافِقُونَ وَالْمُنَافِقَاتُ لِلَّذِينَ آمَنُوا انظُرُونَا نَقْتَبِسْ مِن نُّورِكُمْ قِيلَ ارْجِعُوا وَرَاءكُمْ فَالْتَمِسُوا نُوراً فَضُرِبَ بَيْنَهُم بِسُورٍ لَّهُ بَابٌ بَاطِنُهُ فِيهِ الرَّحْمَةُ وَظَاهِرُهُ مِن قِبَلِهِ الْعَذَابُ[11]

Siku wanaafiki wanaume na wanaafiki wanawake watapo waambia walio amini: Tungojeni ili tupate mwangaza katika nuru yenu. Waambiwe: Rejeeni nyuma yenu mkaitafute nuru! Utiwe baina yao ukuta wenye mlango - ndani yake mna rehema, na nje upande wake wa mbele kuna adhabu.

ama mazungumzo ya watu Waumini na wacha Mungu ni alama inayoonyesha utukufu wa watu hao mbele ya Mola wao, kama tunavyosoma kuhusianana waislamu na Mtume Muhammad (s.a.w.w):

وَكَذٰلِكَ جَعَلْنَاكُمْ اُمَّةً وَسَطاً لِّتَكُونُواْ شُهَدَاء عَلـٰي النَّاسِ وَيَكُونَ الرَّسُولُ عَلَيْكُمْ شَهِيداً وَمَا جَعَلْنَا الْقِبْلَةَ الَّتِى كُنتَ عَلَيْهَا إِلاَّ لِنَعْلَمَ مَن يَتَّبِعُ الرَّسُولَ مِمَّن يَنقَلِبُ عَلـٰي عَقِبَيْهِ وَإِن كَانَتْ لَكَبِيرَةً إِلاَّ عَلـٰي الَّذِينَ هَدَي اللّهُ وَمَا كَانَ اللّهُ لِيُضِيعَ إِيمَانَكُمْ إِنَّ اللّهَ بِالنَّاسِ لَرَؤُوفٌ رَّحِيمٌ[12]

Na vivyo hivyo tumekufanyeni muwe Umma wa wasitani, ili muwe mashahidi juu ya watu, na Mtume awe ni shahidi juu yenu. Na hatukukifanya kibla ulicho kuwa nacho ila tupate kumjua yule anaye mfuata Mtume na yule anaye geuka akarejea nyuma. Na kwa yakini hilo lilikuwa jambo gumu isipo kuwa kwa wale alio waongoa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu hakuwa mwenye kuipoteza Imani yenu. Kwani Mwenyezi Mungu ni Mpole kwa watu na Mwenye kuwarehemu.

Maelezo kuhusiana na aya ya 143 ya Suratul Baqarah.

Wameambiwa kuwa “Mwenyeezi Mungu hakuwa mwenye kuipoteza imani yenu” ili kuwapa habari kuwa hizo sala zao walizozisali mwaka unusu kwa kuelekea Baytil-Muqadas hazikupotea bure- watapewa thawabu zake kwani hayo yalikuwa vile vile kwa amri ya Mwenyeezi Mungu. Imebainishwa hapa kuwa umma wetu huu, uma wa nabii Muhammad (s.a.w.w) ndio uma bora kuliko uma zote zilizopita, kwa sababu nyingi, na moja kubwa ya sababu hizo ni kuwa- kama ilivyobainishwa katika Aya ya 110 ya Surat aali Imrani- kuwa wanaamrishana mema na kukatazana mabaya, na sura nyengine nyingi zimeamrisha haya pia, basi natukamatane sana sana na sifa hii au tutakosa ukubwa huu, isitufike laana iliyowafika uma zilizotangulia kwa kuwa hazikuwa zikiamrishana mema wala kukatazana mabaya, kila mmoja alikuwa anashughulika na yake tu hana haja na mwenzake.

[1] Suratul-Balad Aya ya 12-16.

[2] Surat Namli Aya ya 89

[3] Surat Al-Anbiyaa Aya ya 103

[4] Surat Naziati Aya 8-9

[5] Surat As-Saffat Aya ya 24

[6] Surat Hud aya ya 105

[7] Surat yasiyn aya ya 65.

[8] Suratul-Muuminuun aya ya 108

[9] Surat Nuur Aya ya 24

[10] Surat Zumar Aya ya 31.

[11] Surat Al-Hadiyd Aya ya 13

[12] SuratulBaqarah Aya ya 143

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini