YESU (A.S)

YESU (A.S)

YESU - NABII ALIYETOKA NAZARETI MTUMISHI WA MUNGU

Masih hataona uvunjifu kuwa mtumwa wa Mwenyezi Mungu.(Qur'ani) An Nisaa 4.172
Biblia inahakikisha ukweli huu wa Qur'ani. Mara nyingi tunaona Yesu anatafakhari kujitangaza kuwa yeye ametumwa na Mungu, na mara nyingi anaitwa "mtumishi wa Mungu". Katika Injili ya Yohana mathalan tunasoma: Na uzima wa milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma. Mimi nimekutukuza duniani, hali nimeimaliza kazi ile uliyonipa niifanye. Yohana 17.3-4

Kwa unyenyekevu wa safi ya niya Yesu anamkhatibu Mola wake, "Mungu wa pekee wa kweli", siye mungu wa uwongo miongoni wa miungu ya uwongo uwongo iliyokuwa ikiabudiwa na makafiri. Ajuulikane Mwenyezi Mungu na kadhaalika ajuulikane yeye Yesu Kristo, Mtume na mtumishi wa Mwenyezi Mungu. Katika kitabu cha Matendo ya Mitume kiliomo katika Agano Jipya la Biblia tunasoma: Mungu, akiisha kumfufua mtumishi wake Yesu, alimtuma kwenu ninyi kwanza, ili kuwabarikia kwa kumwepusha kila mmoja wenu na maovu yake. Matendo 3.26

Mungu wa Ibrahimu na wa Isaka na wa Yakobo, Mungu wa baba zetu, amemtukuza mtumishi wake Yesu, ambaye ninyi mlimsaliti na kumkana mbele ya Pilato, alipokuwa ametoa hukumu yake afunguliwe.
Matendo 3.13

Basi sasa, Bwana, yaangalie matisho yao; ukawajalie watumwa wako kunena neno lako kwa ujasiri wote, ukinyosha mkono wako kuponya; ishara na maajabu vifanyike kwa jina la Mtumishi wako mtakatifu Yesu.
Matendo 4.29-30

Wagonjwa wanaponyeshwa, ishara zinaonyeshwa, na maajabu yanatendeka. Nani afanyae yote haya? Ni kudra na uwezo wa Mwenyezi Mungu. Jina la Yesu huenda likatumiwa, lakini ni kama chombo tu, wasila, mwombezi, kwani kama atavyokuwa yeye ni "mtumishi mtakatifu wa Mungu." Katika Matendo 3.26 na 3.13 hapo juu Paulo aliwaandikia Mayahudi ambao walimkataa mtumishi wa Mungu, Yesu Kristo, alipowajia na utumishi kutoka kwa Mungu wa babu zao Mayahudi, Mungu wa Ibrahimu na wa Isaka na Yakobo. Mwenyezi Mungu ni yule yule mmoja, Mitume ni mbali mbali, lakini utumishi wao ni mmoja. Mayahudi wakawakubali wote waliotangulia wakamkataa Yesu. Mwenyewe Yesu anawasimanga Mayahudi kama inavyotueleza Injili ya Yohana: Mimi mnanijua, na huko nitokako mnakujua; wala sikuja kwa nafsi yangu; ila yeye aliyenipeleka ni wa kweli, msiyemjua ninyi. Mimi namjua, kwa kuwa nimetoka kwake, naye ndiye aliyenituma.
Yohana 7.28-29

Katika Injili ya Marko Yesu anasimuliwa alimchukua mtoto akasema: Mtu akimpokea mtoto mmoja wa namna hii kwa jina langu, anipokea mimi: na mtu akinipokea mimi, humpokea, si mimi, bali yeye aliyenituma.
Marko 9.37

Kama hayo aliambiwa Mtume Muhammad s.a.w. na Mwenyezi Mungu katika Qur'ani: Sema: Ikiwa ninyi mnampenda Mwenyezi Mungu, basi nifuateni mimi, Mwenyezi Mungu atakupendeni na atakusameheni madhambi yenu, kwani Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
(Qur'ani) Al Imran 3.31

Yesu amesema: Chakula changu ndicho hiki, niyatende mapenzi yake aliyenipeleka, nikaimalize kazi yake. Yohana 4.34

Haya khasa ndio maana ya neno Uislamu. Uislamu ni kujisalimisha nafsi yako kwenye mapenzi ya Mwenyezi Mungu, kutenda apendavyo Mola wako Mlezi. Na hicho ndicho chakula chake Yesu, kama asemavyo, yaani kama anavyohitaji kula kila siku ili aishi, kama wanavyohitaji wanaadamu wote, basi hali kadhaalika kuwa daima anajisalimu mbele ya matakwa ya Mwenyezi Mungu aliyemtuma duniani kuwa ni Mtume. Tena Yesu amesema: Mafunzo yangu si yangu mimi, ila ni yake yeye aliyenipeleka. Mtu akipenda kuyatenda mapenzi yake, atajua habari ya yale mafunzo, kwamba yatoka kwa Mungu, au kwamba mimi nanena kwa nafsi yangu tu. Yeye anenaye kwa nafsi yake tu hutafuta utukufu wake mwenyewe; bali anayetafuta utukufu wake aliyempeleka, huyo ni wa kweli, wala ndani yake hamna udhalimu.Yohana 7.16-18

Tunaona basi kwa ushahidi wake mwenyewe Yesu kuwa fakhari yake ni kunyenyekea kwa Mwenyezi Mungu wake aliyemuumba na akamtuma kwa Wana wa Israili waliopotea kama kondoo. Kwa uthibitisho wake mwenyewe yeye ni mtumishi wa haki aliyepewa Unabii na kufanywa Mtume. Hataki utukufu wake yeye, bali utukufu wa Mungu wake aliyemtuma na kumpeleka awaongoe watu wafwate njia iliyo nyooka. Katika Injili ya Mathayo anazidi kufafanua nini wadhifa wake na nini cheo chake mbele ya Mwenyezi Mungu na mbele ya wanaadamu wenziwe. Alipowateua wanafunzi wake kumi na mbili kuwapeleka kuwahubiria Mayahudi alisema: Awapokeaye ninyi, anipokea mimi; naye anipokeaye mimi, ampokea yeye aliyenituma. Ampokeaye nabii kwa kuwa ni nabii, atapata thawabu ya nabii; naye ampokeaye mwenye haki kwa kuwa ni mwenye haki, atapata thawabu ya mwenye haki.
Mathayo 10.40-41

Yeye mwenyewe Yesu amesema kuwa yeye ni Mtume, yeye ni Mtumishi, yeye ni Nabii. Je, nini mawazo ya wale wafwasi wake waliomuamini na wakamwona na wakaishi naye? Injili zinatwambia: Basi watu wale, walipoiona ishara aliyoifanya, walisema, Hakika huyu ni nabii yule ajaye ulimwenguni .Yohana 6.14

Nao walipotafuta kumkamata, waliwaogopa makutano, kwa maana wao walimwona kuwa nabii. Mathayo 21.46

Hata alipoingia Yerusalemu, mji wote ukataharuki, watu wakisema, Ni nani huyu? Makutano wakasema, Huyu ni yule nabii, Yesu, wa Nazareti ya Galilaya.
Mathayo 21.10-11

Na tazama, siku ile ile watu wawili miongoni mwao walikuwa wakienda kijiji kimoja, jina lake Emau, kilichokuwa mbali na Yerusalemu kama mwendo wa saa mbili. Nao walikuwa wakizungumza wao kwa wao habari za mambo hayo yote yaliyotukia. Ikawa katika kuzungumza na kuulizana kwao, Yesu mwenyewe alikaribia, akaandamana nao. Macho yao yakafumbwa wasimtambue. Akawaambia, ni Maneno gani haya mnayosemezana hivi mnapotembea? Wakasimama wamekunja nyuso zao. Akajibu mmoja wao, jina lake Kleopa, akamwambia, Je! wewe peke yako u mgeni katika Yerusalemu, hata huyajui yaliyotukia humo siku hizi? Akawauliza, Mambo gani? Wakamwambia, Mambo ya Yesu wa Nazareti, aliyekuwa mtu nabii, mwenye uwezo katika kutenda mbele za Mungu na watu wote. Luka 24.13-19

Injili kwa umoja wao zinathibitisha kuwa watu wake Yesu waliokuwa naye na kumuamini na wakaona miujiza yake tangu kuzaliwa kwake mpaka mwisho wake walimjua kuwa ni Nabii wa haki, naye ni mtu, mwanaadamu. "Hakika huyu ni nabii", anasema Yohana.
"waliwona kuwa nabii", anasema Mathayo.
"Huyu ni yule nabii, Yesu", anasema tena Mathayo.
"Yesu wa Nazareti, aliyekuwa mtu nabii", anasema Luka.
Jinsi ya hadhari zake asisingiziwe kuwa anazo au anadai sifa za ungu, Yesu alikataa hata kuitwa "Mwalimu mwema". Sikiliza masimulizi ya Injili ya
Marko: Hata alipokuwa akitoka kwenda njiani, mtu mmoja akaja mbio, akampigia magoti, akmwuuliza, Mwalimu mwema, nifanye nini nipate kuurithi uzima wa milele? Yesu akamwambia, Kwa nini kuniita mwema? hakuna aliye mwema ila mmoja, ndiye Mungu.
Marko 10.17-18

Tafsiri kubwa kabisa ya Biblia iitwayo The Interpreter's Bible inasema kuwa kauli hiyo ya Yesu, yaani: "Kwa nini kuniiita mwema? hakuna aliye mwema ila mmoja, ndiye Mungu", imewatatiza wataalamu wa thiolojia (ilimu ya Ungu) ya Kikristo wa baadaye. Wameona taabu kuambatisha maneno haya yalio wazi na imani yao kuwa Yesu ni mungu, na hali hapo dhaahiri yake ni kuwa anakataa ungu. Kwa hivyo basi kujitoa kimasomaso ikaandikwa katika Injili ya Mathayo (ambayo iliandikwa baada ya Marko) kwa njia nyengine. Ilivyoandikwa katika Mathayo ni hivi: Na tazama, mtu mmoja akamwendea akamwambia, Mwalimu, nitende jambo gani jema, ili nipate uzima wa milele? Akamwambia, Kwani kuniuliza habari ya wema? Aliye mwema ni mmoja.
Mathayo 19.16-17

Kila imani ilipozidi kugeuka maandiko mapya yaliandikwa na kunasibishiwa Yesu. Kitabu hicho The Interpreter's Bible kinaikataa tafsiri ya kusema kuwa makusudio ya Yesu yalikuwa ni kusema: Kama unanita mwema, basi unakusudia kuwa mimi ni Mungu. Hayo siyo. Aliyokusudia Yesu kusema ni kuwa :Sifai kupewa sifa za Mungu. Mtaalamu wa Biblia wa Kitaliana, Marcello Craveri, ameandika katika kitabu chake The Life of Jesus (Maisha ya Yesu): "Yesu kwa mara moja alimpa somo zuri kabisa la unyenyekevu, ambalo juu ya mengineyo, ni ushahidi ulio wazi ya kwamba hakupata kabisa kujiona mwenyewe ni sawa na Mungu: Kwa nini kuniita mwema? Hakuna mwema ila mmoja, ndiye Mungu." Mukhtasari wa yote tuliyokwisha yazungumza, ni kuwa tumepata uthibitisho wa kutosha kutokana na Biblia kuwa Yesu wa Nazareti ni mwanaadamu, Nabii wa Mungu, na Mtume wake. Jee, Mtume huyo katumwa kwa nani?

MWISHO