Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

HATUA YA MWANZO KUELEKEA KWENYE MASOMO YA SERA NA HISTORIA YA UISLAMU

0 Voti 00.0 / 5

HATUA YA MWANZO KUELEKEA KWENYE MASOMO YA SERA NA HISTORIA YA UISLAMU
KWANZA: SERA NA LENGO LA KUISOMA
1- Sera Kiistilahi
Sera ya mwanadamu ni njia yake na mwenendo wake katika maisha, hivyo sera ya Mtume na kizazi chake ni njia na mwenendo wao katika maisha. Sera hii inaonekana katika kauli zao, matendo yao na misimamo yao dhidi ya matukio na mambo mbalimbali ambayo yalitokea katika zama zao na wakaishi nayo kipindi cha karne tatu na miongo minne.
Yaani tangu uanze utume wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) mpaka mwisho wa ghaiba ndogo ya Imam wa kumi na mbili Muhammad bin Hasan Al-Askariy, Al-Mahdi hoja mwenye kungojewa.
2- Jinsi Qur’ani Ilivyotilia Umuhimu Sera
Hakika Qur’ani imetilia umuhimu sera kwa kubainisha sera ya man- abii na watu wema. Ikataka tufuate sera yao na kujifunza kupitia sera ya wale waliopita huku tukiwaidhika na sera yao. Pia imetuhimiza kujali sera ya hitimisho la manabii na bwana wa mitume, Muhammad bin Abdullah (s.a.w.w.) ikataka tumuige1 baada ya kumwambia: “Na kwa hakika wewe unaongoza kwenye njia iliyonyooka.”2
Kisha akawaamrisha waislamu wote kukazania yote yanayotoka kwa yule asiyetamka la matamanio yake akasema: “Na anachokupeni Mtume basi kipokeeni, na anachokukatazeni basi jiepusheni.”3
Kisha akatuelekeza kwa kizazi cha Mtume, ambao Mwenyezi Mungu kawaondolea uchafu na kuwatakasa kabisa4. Akahimiza kushikamana na wakweli na kufuata mwenendo wao, hivyo Mwenyezi Mungu akasema: “Enyi mlioamini, mcheni Mwenyezi Mungu na kuweni pamoja na wakweli.”5
3 - Lengo La Kusoma Sera
Hakika kumfuata Mtume wa Mwenyezi Mungu na kizazi chake kitakasifu ni kufuata njia iliyonyooka inayofikisha kwenye wema na ushindi kwa sababu ni njia inayokuepusha na upotovu na ghadhabu za Mwenyezi Mungu. Na ndio njia ya manabii ambao Mwenyezi Mungu aliwaneemesha kwa neema ya uongofu wake unaowapeleka kwenye haki6. Ndiyo maana akaamrisha kuwafuata, Mwenyezi Mungu akasema: “Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu amewaongoza, basi fuata mwongozo wao.”7
Pia kwa ajili hiyo ndiyo maana sera ya yule hitimisho la manabii na sera ya mawasii wake watakasifu imekuwa ni chanzo kati ya vyanzo vya sheria ya kiislamu, na ni chemchemu ya maarifa na elimu ya kiis- lamu na ni sawa na Kitabu cha Mwenyezi Mungu cha milele, kama ilivyoelezea kuhusu hilo Hadithi ya vizito viwili iliyo mutawatir.8
Zaidi ya hapo ni kuwa sera yao - Amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao wote kwa ujumlaina faida kubwa katika kufahamu makusudio ya Kitabu kitakatifu na tafsiri ya Aya zake tukufu.
Pia sera yao hutubainishia jinsi ya kutekeleza mafunzo ya juu ya kiislamu katika maisha ya mwanadamu anayeishi katika maisha haya. Kwa hiyo tunafahamu kuwa kusoma sera yao kwa namna sahihi kutatupa silabasi muhimu katika malezi ya kiislamu na njia sahihi ya kujifunza mwenendo sahihi katika maisha.
PILI: MAHUSIANO KATI YA HISTORIA YA UISLAMU NA SERA
HISTORIA
Historia ni mkusanyiko wa matukio na uzoefu wa wanadamu waliopita ukilinganisha na zama tunazoishi hivi sasa.
HISTORIA YA UISLAMU
Hakika historia ya Uislamu ni historia ya dini ya milele ya kiislamu, tangu ulipodhihiri, kuenea kwake na harakati zake katika maisha. Pia inakusanya historia ya walioibeba dini na kuihami ambao walikesha wakihudumia na kulinda dini dhidi ya vitimbi vya maadui wake.
Hivyo hakika sera ya bwana wa mitume na sera ya kizazi chake kitakasifu ambacho kilipewa jukumu la kufikisha dini, kutekeleza na kuilinda, inakuwa ni sehemu isiyogawika ndani ya historia yenyewe ya Uislamu (yaani ndio historia yenyewe ya Uislamu).
Kwa sababu wao walizama ndani ya Uislamu na wakaihami sheria, wakatoa nafsi zao na maisha yao kwa ajili ya Uislamu. Hivyo misimamo yao ya kidini ndio Uislamu wenyewe na harakati zao ndio harakati za Uislamu wenyewe. Wao hudhihirisha kimatendo mafunzo halisi ya Uislamu na huyaelezea maelezo halisi. Hivyo historia yao ndio historia ya Uislamu katika hatua zake zote na mambo yake yote, wala siyo historia ya mtu fulani kati ya waislamu.
VYANZO VYA HISTORIA YA UISLAMU NA SERA YA MTUME (S.A.W.W.)
Hakika chanzo muhimu cha historia ya Uislamu na historia na sera ya manabii hasa historia na sera ya nabii wa mwisho (s.a.w.w.) ni Kitabu cha milele cha Mwenyezi Mungu, Qur’ani yake ya muujiza ambayo: “Hautakifikia upotovu mbele yake wala nyuma yake, kimeteremshwa na Mwenye hekima, Mwenye kuhimidiwa.”9
Ama vitabu vya sera, historia, tafsiri na Hadithi ambavyo viliandikwa baada ya kupita karne moja au zaidi tangu kufariki kwa Mtume (s.a.w.w.) vyenyewe ni vyanzo vya daraja la pili.
Hakika vyanzo hivi vilivyokuja nyuma vimejumuisha ukweli huku pembeni yake vikiwa vimejaza visa vya uongo, Hadithi na habari za uzushi zilizowekwa kupitia ndimi za maswahaba au wanafunzi wa maswahaba.
Kwa ajili hiyo vyanzo hivi vinahitajia kipimo makini ili kupembua habari sahihi na kuzitenganisha na habari zilizochomekwa. Pia inatakiwa kuzipima na Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna sahihi ya Mtume na akili salama ili ziwe ni mwongozo kwa watafuta ukweli.
ZAMA ZA HISTORIA YA UISLAMU
Historia ya Uislamu inaanzia pale alipopewa utume Mtukufu Mtume, tarehe ishirini na saba mfungo kumi (Rajabu) miaka kumi na tatu kabla ya hijra ya Mtume (s.a.w.w.), muda ambao maisha ya Uislamu wa kudumu yalianza na yakaendelea kuchanja mbuga ndani ya jamii ya kiarabu na mwanadamu chini ya mkono wa Mtukufu Mtume Muhammad bin Abdullah.
Uislamu ulikuwa ni mapinduzi ya Mwenyezi Mungu yenye mabadi- liko katika kila kitu, hivyo yalianzia Makka tukufu na kuishia kwenye kuasisi dola ya kiislamu iliyobarikiwa huko Madina na Bara la Arabu. Baada ya jihadi kubwa chini ya uongozi wa Mwenyezi Mungu Mwenye busara matunda yake yalionekana ndani ya muda mfupi, kinyume na historia nyingi za wito wa mabadiliko.
Zama hizi ambazo Mtume Muhammad (s.a.w.w.) alianzisha mapinduzi haya yaliyobarikiwa tunaweza kuziita ni zama za Mtume Muhammad (s.a.w.w.), nazo ni zama za kufikisha Uislamu.
Ama zama zilizofuatia zenyewe ni zama za mawasii waliousiwa mapinduzi na dola ya Mtume. Hizi tunaweza kuziita zama za Maimam maasumina au zama za Maimam viongozi wema. Zama zote mbili zinagawanyika katika vipindi na nyakati mbili.
A) ZAMA ZA MTUME (S.A.W.W.)
Zama za Nabii zina vipindi viwili tofauti navyo ni: Kipindi cha Makka na kipindi cha Madina. Kipindi cha kwanza kinaanzia pale ali- poruhusiwa kutangaza utume huko Makka na kinakomea pale alipohama toka Makka kuelekea Madina (Yathirib) katika usiku wa mwanzo wa mfunguo sita mwaka wa kumi na tatu tangu kupewa utume.
Kipindi cha pili kinaanzia pale alipofika Madina tarehe kumi na mbili ya mfungo sita ndani ya mwaka huo huo, na kinakomea pale alipofariki Mtume (s.a.w.w.) tarehe ishirini na nane mfunguo tano mwaka wa kumi na moja tangu kuhamia Madina.
Katika kipindi cha Makka Mtume alitengeneza nguvu kali, alijenga Uislamu kiimani na kisheria kwa ajili ya maisha, hivyo ni kipindi cha kutengeneza umma wa kiislamu na kuanzisha kundi la waumini wenye kuamini Uislamu.
Ama kipindi cha Madina kinajitofautisha kwa kuasisiwa dola ya kiislamu, nayo ndiyo jengo la kwanza la kisiasa lenye sura ya dola ya kiislamu iliyojengeka katika kutekeleza sheria ya kiislamu ndani ya maisha. Katika vipindi vyote viwili wahyi wa Mwenyezi Mungu ndiyo uliokuwa ukimuelekeza yeye Mtume kama kiongozi wa umma wa kiislamu kupitia Aya za Qur’ani ambayo iliteremka ndani ya muda wa miaka ishirina na tatu.
Qur’ani imetuhifadhia matukio ya vipindi vyote viwili kupitia Aya zake. Hivyo tunaweza kuijua historia ya zama hizi iwapo tu tutajua kwa usahihi utaratibu wa kushuka Aya za Qur’ani tukufu. Hivyo tunaweza kugawa kipindi cha Makka katika vipindi viwili vifuatavyo:
Kipindi cha kuwalingania watu mahsusi na kuandaa mbegu za mwanzo za kundi la waumini. Muda wa kipindi hiki unakadiriwa ni miaka mitatu mpaka mitano.
Kipindi cha kuwalingania watu wote au kipindi cha kutangaza na kuanza mapambano dhidi ya shirki na ukafiri. Muda wa kipindi hiki unakadiriwa ni miaka mitatu mpaka minne.
Kipindi cha uhamishoni, nacho ni kipindi cha kuendeleza mkondo wa Uislamu. Kipindi hiki kimekusanya hijra tatu zenye kufuatana nazo ni: Kuhama kuelekea Uhabeshi (Ethiopia ya sasa), kisha kuelekea Taif na kisha kuelekea Madina.
Pia tunaweza kugawa kipindi cha Madina katika vipindi viwili tofauti navyo ni: Kipindi cha kuasisiwa dola ya kiislamu na kuihami ndani ya nusu ya kwanza ya kipindi cha Madina kuanzia hijra na kumalizikia vita vya Handaki au Ahzab.
Kipindi cha ufunguzi na kuendeleza mapinduzi ya kiislamu na kupan- ua wigo wa dola ya kiislamu. Hii ni kuanzia suluhu ya Hudaybiya mpaka mwaka wa Hijja ya mwisho ya kuaga, nayo ni nusu ya pili ya kipindi cha Madina.
B) ZAMA ZA MAIMAM WEMA
Hakika harakati za mageuzi ziliienea jamii ya kijahiliya hivyo kutokana na zilivyokuwa fikra, mafunzo, mila, na desturi za kijahiliya ni kuwa mapinduzi ya kiislamu na dola mpya ya Mtume (s.a.w.w.) vilikuwa vinahitajia usia wa kiitikadi. Hiyo ni kwa sababu njia mbele ya harakati ilikuwa bado ndefu huku ikiendela kipindi chote cha vita nzito vya kiroho kati ya Uislamu na ujahiliya.
Kipindi kilichochukuliwa na mapinduzi, kisha dola ya Mtume hakikuwa kinatosha kung’oa mizizi yote ya ujahiliya na athari zake. Na hilo ni kama ilivyothibitisha historia ya matukio ambayo yalitokea baada tu ya kifo cha Mtume (s.a.w.w.).
Kwani baada ya Mtume (s.a.w.w.) utawala wa kiislamu ulibakia ni mpira unaochezewa na watoto wa kizazi cha Umayya ambao kabla ya hapo walikuwa wamesimama kidete dhidi ya Uislamu kuanzia mwanzo mpaka sekunde ya mwisho.10
Kuanzia hapo Mtume kiongozi aliainisha Maimam kumi na wawili maasumina kwa amri toka kwa Mwenyezi Mungu. Ambao ni mawasii wenye uwezo watakaoshika nafasi yake ili kulinda mapinduzi yake, ujumbe wake, umma wake, na dola yake baada yake. Hivyo baada yake walisimamia jukumu la kutetea sheria ya Mwenyezi Mungu na dola ya bwana wa mitume na umma wa hitimisho la manabii.
Zama zao zimegawanyika katika vipindi viwili tofauti navyo ni: Kipindi cha kuonekana na kipindi cha ghaibu. Kipindi cha kuonekana kinaanzia pale alipofariki Mtume (s.a.w.w.) na kinakomea mwaka 260 A.H. Pale alipofariki Imam wa kumi na moja kati yao naye ni Hasan Al-Askariy.
Ama kipindi cha ghaibu ni kipindi cha kutoonekana Imam wa kumi na mbili kati yao naye ni maasumu wa kumi na wane. Hujja bin Al- Hasan Al-Mahdi (a.s.) mwenye kungojewa. Ambaye uimamu wake umefungana na ghaibu yake.
Kipindi cha Ghaibu nacho kina vipindi viwili:
Cha kwanza: Kipindi cha ghaibu fupi ambacho kilifikia muda wa miongo saba. Yaani kuanzia mwaka 260 mpaka 329 A.H.
Cha pili: Kipindi cha ghaibu ndefu ambacho kilifuata baada ya fupi ikiwa ni mwishoni mwa muongo wa tatu karne ya nne baada ya kufariki balozi wake wa nne mwaka 329 A.H. Nacho kinaendelea mpaka leo.
MUHTASARI
Sera ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na sera ya kizazi chake kitakasifu ni chanzo muhimu kati ya vyanzo vya maarifa na sheria ya kiislamu. Huzingatiwa pia kuwa ni nyenzo kati ya nyenzo za kufikia wema na mafanikio, kwa sababu kuwafuata wao ni mfano halisi wa kufuata njia ya Mwenyezi Mungu iliyonyooka.
Historia ya kiislamu ndio historia ya Uislamu na ndio historia ya watetezi ambao walizama ndani na kujitoa muhanga kila dakika ya maisha yao katika njia ya Uislamu. Nao ni Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na kizazi chake kitakasifu kilichotakasika dhidi ya kila aina ya uchafu na kila aina ya dosari.
Qur’ani ndio chanzo muhimu cha historia na sera ya Mtume (s.a.w.w.) na historia ya kiislamu. Kwa ajili hiyo vyanzo vyote vingine vya sera na historia vinapimwa kwa Qur’ani, kwa sababu vyanzo vingine vimekosa sifa ya “kumdiriki Mtume (s.a.w.w.)”, “kudiriki yote, umakini, na kutoegemea” kwenye maslahi ya makundi na madhehebu ambayo yalizuka baada ya zama za Mtume (s.a.w.w.).
Zama za Mtume wa mwisho (s.a.w.w.) huchukuliwa kama mwanzo wa zama za historia ya kiislamu kisha hufuatiwa na zama za Maimam wema (a.s.).
Maswali
1. Elezea maana ya sera ya Mtume na sera ya kizazi chake kitakasifu.
2. Bainisha msimamo wa Qur’ani kuhusu sera na kujifunza kwake.
3. Elezea malengo na faida itokanayo na kujifunza sera ya Mtume (s.a.w.w.) na kizazi chake.
4. Ni upi uhusiano uliyopo kati ya sera ya Mtume (s.a.w.w.) na histo- ria ya kiislamu?
5 . Ni vipi vyanzo vya sera na historia ya kiislamu?
6. Ni zipi sifa za kipekee za Qur’ani zinazoifanya iwe ni chanzo cha sera na historia ya Uislamu?
7: Orodhesha zama za historia ya kiislamu?
•    1. Al-Ahzab: 21.
•    2. As-Shura: 52.
•    3. Al-Hashri: 7.
•    4. Al-Ahzab: 33.
•    5. At-Tawba: 119.
•    6. Al-Fatiha: 5 – 7.
•    7. Al-An’aam: 90.
•    8. Rejea Hadithi hiyo kwenye somo la saba.
•    9. Fusilat: 42
•    10. Kwa ufafanuzi zaidi rejea kitabu Nash’atutashayyu wa Shia cha Shahid Sayyid Muhammad Baqir As-Sadri, uhakiki wa Dr. Abdul-Jabar Shararah, Uk. 51 – 57 na 58 – 61.

MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini