MUHAMMAD BIN ABDULLAH (S.A.W.W.) NI UTABIRI WA MANABII (A.S.)

MUHAMMAD BIN ABDULLAH (S.A.W.W.) NI UTABIRI WA MANABII (A.S.)
MWENENDO WA UTABIRI
Ni mwenendo wa Mwenyezi Mungu na ni rehema na amani kutoka Kwake kuwapa habari waja Wake za kuja kwa Mtume atakayemtuma kwao muda ujao. Hivyo manabii waliotangulia walikuwa wakim- bashiri Nabii atakayekuja baada yao.
Qur’ani imeashiria jinsi Yahya alivyobashiri unabii wa Isa (Al Imran: 39). Pia imeashiria jinsi Isa alivyobashiri unabii wa Muhammad (As-Swaf: 6). Hivyo manabii wote msitari wao ni mmoja kwani aliyetangulia humbashiri atakayemfuata, na huyu aliyefuata humwamini aliyetangulia. Mwenendo huu wa kubashiri umetamkwa na Qur’ani katika Sura ya tatu Aya ya themanini na moja. Zaidi ya hapo ni ushahidi na mifano halisi utakayoiona hapa mbele:
1. Qur’ani imeelezea utabiri wa Ibrahim kipenzi juu ya utume wa Nabii wa mwisho kwa ulimi wa dua akisema:
رَبَّنَا وَابْعَثْ فِيهِمْ رَسُولًا مِنْهُمْ يَتْلُو عَلَيْهِمْ آيَاتِكَ وَيُعَلِّمُهُمُ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ وَيُزَكِّيهِمْ ۚ إِنَّكَ أَنْتَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ {129}
“Ewe Mola wetu, wapelekee mtume katika wao awasomee Aya zako na kuwafunza kitabu na hekima na kuwatakasa. Hakika wewe ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hekima.” (Al-Baqarah: 129)
Qur’ani imeeleza wazi kuwa utabiri wa Nabii Muhammad ulikuwemo ndani ya vitabu viwili: Taurati na Injili, na laiti kama utabiri huo usingekuwemo ndani ya vitabu hivyo basi watu wa vitabu hivyo wangeupinga waziwazi, Mwenyezi Mungu anasema:
الَّذِينَ يَتَّبِعُونَ الرَّسُولَ النَّبِيَّ الْأُمِّيَّ الَّذِي يَجِدُونَهُ مَكْتُوبًا عِنْدَهُمْ فِي التَّوْرَاةِ وَالْإِنْجِيلِ يَأْمُرُهُمْ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَاهُمْ عَنِ الْمُنْكَرِ وَيُحِلُّ لَهُمُ الطَّيِّبَاتِ وَيُحَرِّمُ عَلَيْهِمُ الْخَبَائِثَ وَيَضَعُ عَنْهُمْ إِصْرَهُمْ وَالْأَغْلَالَ الَّتِي كَانَتْ عَلَيْهِمْ ۚ {157}
“Ambao wanamfuata mtume, nabii aliyeko Makka ambaye wanamuona ameandikwa kwao katika Taurati na Injili, ambaye anawaamrisha mema na anawakataza yaliyo mabaya, na kuwahalalishia vizuri na kuwaharamishia maovu, na kuwaondolea mizigo yao na minyororo iliyokuwa juu yao.” (Al-A’araf: 157)
Aya ya sita ya Surat Swaffu imeelezea waziwazi kuwa Isa (a.s.) alisadikisha Taurati na akambashiri Mtume atakayekuja baada yake jina lake Ahmad. Kama inavyoashiria kauli ya Mwenyezi Mungu:
وَإِذْ قَالَ عِيسَى ابْنُ مَرْيَمَ يَا بَنِي إِسْرَائِيلَ إِنِّي رَسُولُ اللَّهِ إِلَيْكُمْ مُصَدِّقًا لِمَا بَيْنَ يَدَيَّ مِنَ التَّوْرَاةِ وَمُبَشِّرًا بِرَسُولٍ يَأْتِي مِنْ بَعْدِي اسْمُهُ أَحْمَدُ ۖ فَلَمَّا جَاءَهُمْ بِالْبَيِّنَاتِ قَالُوا هَٰذَا سِحْرٌ مُبِينٌ {6}
“Na aliposema Isa bin Mariam: Enyi wana wa Israeli, hakika mimi ni mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu. Nimethibitisha yaliyokuwa kabla yangu katika Taurati, na ni mwenye kutoa habari njema ya mtume atakayekuja baada yangu, jina lake ni Ahmad, lakini alipowaletea hoja zilizo wazi, walisema: Huu ni uchawi ulio dhahiri” (As-Swaff: 6).
AHLUL-KITAB WAMNGOJEA NABII WA MWISHO
Manabii waliyotangulia hawakuishia tu kutoa sifa kuu za nabii aliyetabiriwa, bali zaidi ya hapo walitaja baadhi ya alama ambazo wale wanaopewa utabiri wanaweza kumjua vizuri.
Alama hizo ni kama vile sehemu atakayozaliwa, atakayohamia na sifa mahsusi za wakati atakaopewa utume. Pia alama za kipekee alizonazo mwilini, tabia na sheria zake za kipekee. Bali Qur’ani imeeleza kuwa walikuwa wanamjua kama wanavyowajua watoto zao (Al-An’am: 20).
Kutokana na utabiri huo wakafuatilia kivitendo na mwisho wakagun- dua sehemu atakayohamia na kusimamisha dola yake. Hapo wakafanya makazi yao na kuanza kuiombea nusra dini yake dhidi ya makafiri (Al-Baqarah: 89), na kuomba ushindi kupitia Mtume wa Mwenyezi Mungu dhidi ya Ausi na Khazraji.
Hivyo habari hizi zikaenea kwa wengine kupitia mapadri na wasomi wao, zikazagaa Madina zikafika hadi Makka. Wakampa habari Abdul Muttalib1 na Abu Talib2 huku wakiwahadharisha na vitimbi vya mayahudi.
Hivyo baada ya Mtume kutangaza utume wake, ujumbe wa makuraishi ulikwenda kwa mayahudi wa Madina kwa lengo la kuthibitisha ukweli wa madai ya unabii waliousikia toka kwa Muhammad, wakachukua baadhi ya mambo waliyomtahini nayo Mtume,3 na hatimaye ukabainika ukweli wa madai yake.
Baadhi ya Ahlul-Kitabi na wengineo walimwamini Nabii Muhammad kwa kufuata alama hizi ambazo walizifahamu hata bila ya kumuom- ba muujiza wowote mahsusi (Al-Maidah: 83). Mpaka leo baadhi ya nakala za Taurati na Injili zimehifadhi baadhi ya utabiri huo.4
Na hivyo ndivyo ulivyofuatana utabiri wa unabii wa nabii wa mwisho Muhammad kabla ya kuzaliwa kwake. Kisha ukanukuliwa wakati wa uhai wake kabla ya kukabidhiwa unabii. Ulienea utabiri aliouelezea padri Buhayra kisha ushahidi wa Waraqa bin Nawfal juu ya utume wa Muhammad, ushahidi uliotokana na utabiri.5
Imam Ali (a.s.) ameelezea hali hiyo kwa kusema: “Mwenyezi Mungu hajawaacha viumbe wake bila ya nabii aliyetumwa au kitabu kilichoteremshwa, au hoja ya lazima, au njia ya wazi iliyonyooka. Mitume ambao uchache wa idadi yao au wingi wa wapingaji havikumzuwia aliyetangulia kumtaja atakayekuja baada yake, au aliyepita kutambulishwa na aliye kabla yake.
Kwa mwenendo huo karne zikapita…Mpaka Mwenyezi Mungu alipomleta Muhammad Mtume wa Mwenyezi Mungu ili kutekeleza utaratibu Wake na kutimiza unabii wake, huku ahadi yake ikiwa imechukuliwa kwa manabii waliyotangulia na alama zake zikiwa ni mashuhuri……..”*
SIFA ZA NABII MUHAMMAD (S.A.W.W.)
Ibnu Saad amepokea toka kwa Sahlu mtumwa wa Utayba ambaye alikuwa mkiristo wa Mar’yasi na alikuwa ni yatima aliyelelewa na mama yake mzazi na ami yake, pia alikuwa msomaji wa Injili, alisema kuwa: “Nikachukua kitabu cha ami yangu nikawa nakisoma mpaka iliponipita karatasi, hivyo nikataka kujua ni kipi kilichoandikwa katika karatasi iliyonipita. Nikaigusa kwa mkono wangu na pindi nilipoangalia nikakuta vitini vya karatasi vimeshikana hapo nikaviachanisha nikakuta ndani yake sifa za Muhammad:
“Yeye si mfupi, si mrefu, mweupe, kati ya mabega yake kuna muhuri, mara nyingi hukaa mkao wa ihtibau, hapokei sadaka, anapanda punda na ngamia, anakamua mbuzi, anavaa kanzu chakavu, na atakayefanya hivyo basi kajiepusha na kiburi na yeye hufanya hivyo, na yeye anatokana na kizazi cha Ismail na jina lake ni Ahmad.”
Sahlu akasema: “Nilipofika hapa katika kumtaja Muhammad ami yangu akaja na alipoiona karatasi alinipiga na kusema: “Kwa nini umefungua karatasi hii na kusoma?” Nikasema: Humu mna sifa za nabii Ahmad. Akasema: “Yeye bado hajakuja.”6
Muhtasari
Matukio ya kihistoria yanaonyesha kuwa mwenendo wa manabii ni wa kiukamilifu wenye lengo moja na njia moja. Pia mwenendo wa Mwenyezi Mungu ni manabii waliyopo kuwabashiri watakaochukua nafasi zao katika unabii. Ikiwa ni huruma toka kwa Mwenyezi Mungu dhidi ya mzigo walio nao wanadamu katika kuamini na kukubali na ni kumrahisishia nabii anayefuata kazi ya uhubiri na ulinganio.
Na kwa kuwa Uislamu na Mtume Muhammad vina umuhimu mkub- wa katika historia ya binadamu, na ukizingatia kuwa Uislamu ni dini inayohusu kila kitu na ndiyo dini ya mwisho huku Mtume (s.a.w.w.) akiwa ndiyo mtume wa mwisho, basi Uislamu huo ulibashiriwa tangu zamani na hilo limeelezwa na Qur’ani tukufu.
Kuna habari zilizoenea kabla ya Mtume kukabidhiwa utume ambazo zilikuwa zimebeba wasifu kamili wa Mtume Muhammadin (s.a.w.w.) na mazingira yake, zikiwataka watu wamwamini na wajiepushe na upotovu kwa kumfuata yeye.
Habari hizi zilisaidia baadhi ya Ahlul-Kitabu na wengineo kuamini dini ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.) bila ya kuomba muujiza wowote mahsusi.
Maswali
1: Ni upi umuhimu wa bishara za manabii?
2: Je, kuna utabiri mahsusi toka kwa manabii waliyotangulia unaomhusu nabii Muhammad?
3: Toa Aya kuthibitisha utabiri huo?
4: Ni kitu gani walichokifahamu Ahlul-Kitabi kuhusu Nabii (s.a.w.w.) kabla ya utume wake?
5: Ni upi ulikuwa msimamo wa Ahlul-Kitabu dhidi ya Mtume (s.a.w.w.) baada ya kupewa utume?

REJEA
•    1. Tarikh Al-Yaaqubiy, Juz. 2, uk. 12.
•    2. Siiratu Ibnu Hisham, Juz. 1, uk. 181, na Ilamul-Waraa, uk. 26.
•    3. Rejea sababu ya kuteremka Surat Kahfi.
•    4. Ashia’tul-Baytun-Nabawiyyi, Juz. 1, uk. 70, humo amenukuu kutoka kwenye Taurati. Pia rejea Siratur-Rasulu wa Ahlul-Baytihi, Juz. 1, uk. 39 humo amenukuu baadhi ya tabiri kutoka kwenye Injili ya Yohana.
•    5. Katika vitabu vikubwa vya Siira.
*Nahjul-Balagha, hotuba ya kwanza
•    6. At-Tabaqatu Al-Kubra, Juz. 1, uk. 363.

MWISHO