MCHANGO WA MAZINGIRA SAFI KATIKA MALEZI

MCHANGO WA MAZINGIRA SAFI KATIKA MLEZI
Mazingira yana mchango mkubwa katika malezi ya mwanadamu, humfanya awe mwema au humharibu. Mazingira tunayokusudia hapa ni wale watu wanaomzunguka mwanadamu ambao mwanadamu huyu hupokea kutoka kwao misingi ya maarifa yake na lugha yake. Wanadamu ambao kupitia kwao hujifunza elimu na maarifa mbalimbali na huongoka kupitia kwao, kwani huathirika kulingana na wanadamu wanaomzunguka, hivyo yeye huwaathiri na wao humwathiri.
Familia ndio mazingira ya mwanzo ambayo wanadamu hukulia ndani yake wakiwemo manabii na walinganiaji wa tawhidi ambao walisi-mama kidete kupiga vita shirki, maadili machafu na mila potovu. Hakika Mwenyezi Mungu aliwaumba na kuwalea katika familia za tauhidi zenye kujisalimisha kwa Mwenyezi Mungu.
Baba wa manabii Adam (a.s.) ndiye aliyefundishwa majina yote na Mwenyezi Mungu kabla hajaletwa aridhini. Na yeye ndiye wa kwanza kumtakasa Mwenyezi Mungu na ndiye wa kwanza aliyeumbwa na Mwenyezi Mungu katika tauhidi. Hivyo kwa mwenendo huo wakafuata manabii wote, manabii ambao wamehitimishwa na Muhammad (s.a.w.w.).
MAZINGIRA YA MTUME (S.A.W.W.) KWA MUJIBU WA MAELEZO YA AHLUL-BAYT
Imam Ali (a.s.) ameelezea mazingira ya tauhidi ambayo Mtume (s.a.w.w.) alitokana nayo akasema: “Akamteua kutokana na mti wa manabii, shubaka yenye mwanga, nywele za utosi wa watukufu na kitovu cha Makka”1 “….Mahala pake alipoishi (Mfuko wa uzazi) ndiyo mahala bora, na chimbuko lake ndio chimbuko bora katika machimbuko ya madini ya utukufu na busati la amani.”2
“Hivyo akamleta toka ndani ya madini yenye chimbuko bora na asili tukufu, toka ndani ya mti ambao alikusudia kuwatoa ndani yake manabii na kuteua waaminifu wake kutoka humo.”3
“Kila Mwenyezi Mungu alipokiongeza kizazi kwa kugawa makundi mawili basi alikiweka kizazi chake katika kundi bora, kundi ambalo mzinifu hakuchangia chochote wala hakupata fungu lolote.”4
Pindi Qur’ani ilipotaja kuteuliwa kwa ajili ya ulimwengu wote Adam, Nuh, kizazi cha Ibrahim na kizazi cha Imran Mwenyezi Mungu aliendelea kwa kusema:
ذُرِّيَّةً بَعْضُهَا مِنْ بَعْضٍ ۗ وَاللَّهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ {34}
“Kizazi cha wao kwa wao na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua” (Al Imrani: 34).
Akamtaja kipekee mtume wake wa mwisho kwa kusema:
وَتَوَكَّلْ عَلَى الْعَزِيزِ الرَّحِيمِ {217}
الَّذِي يَرَاكَ حِينَ تَقُومُ {218}
وَتَقَلُّبَكَ فِي السَّاجِدِينَ {219}
“Na umtegemee Mwenye nguvu, Mwenye rehema. Ambaye anakuona unaposimama.
Na mageuko yako katika wale wanao- sujudu (Shu’araa: 217-219).”
Hivyo wote waliomtangulia Muhammad walikuwa wakisujudu na kunyenyekea kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na wala hawajamshirikisha na chochote hata sekunde moja.
Imam Jafar As-Swadiq (a.s.) amefafanua geuko hili kwa kusema: “Ndani ya mifupa ya migongo ya manabii kulikuwa na nabii baada ya nabii mpaka akamleta toka mifupa ya mgongo wa baba yake kutokana na ndoa na wala si kwa uzinzi, hali hii ni tokea kwa Adam.”5
Nabii mwenyewe (s.a.w.w.) kaelezea hali hiyo waziwazi kwa kusema: “Nilihamishwa toka ndani ya mifupa ya migongo mitakasifu mpaka kwenye kizazi kitakasifu katika hali ya ndoa wala si hali ya uzinzi.”6
Pia akasema: “Hakika Mwenyezi Mungu alimteua Ibrahim toka kizazi cha Adam akamfanya kipenzi. Akamteua Isma’il toka kizazi cha Ibrahim. Kisha akamteua Nazari toka kizazi cha Isma’il. Kisha akamteua Mudhira toka kizazi cha Nazari. Kisha akamteua Kinana toka kizazi cha Mudhar.
Kisha akamteua Qurayshi toka kizazi cha Kinana. Kisha akateua kizazi cha Hashim toka kizazi cha Qurayshi. Kisha akateua kizazi cha Abdul Muttalib toka kizazi cha Hashim. Kisha akaniteua mimi toka kizazi cha Abdul Muttalib.”7
MAZINGIRA YA MTUME (S.A.W.W.) KWA MUJIBU WA MAELEZO YA WANAHISTORIA
Wanahistoria wameeleza wazi kuwa Abdul Muttalib alikataa kuabudu masanamu. Akampwekesha Mwenyezi Mungu, akatekeleza nadhiri. Akaanzisha mienendo ambayo mingi kati ya hiyo imetajwa na Qur’ani huku ikiridhiwa na Mtume (s.a.w.w.) kupitia sunna yake.
Kati ya mienendo hiyo ni kutimiza nadhiri, fidia ya ngamia mia moja, kutooa maharimu na kutoyaendea majumba kwa nyuma. Pia kukata mkono wa mwizi, kukataza kuwauwa watoto wa kike, maapizano, kuharamisha pombe, kuharamisha zinaa na kutoa adhabu kwa mzinifu. Kuteua kwa bahati, kukataza kutufu uchi, kumkirimu mgeni, kutokutoa kitu wanapohiji isipokuwa toka kwenye mali waipendayo na kutukuza miezi mitukufu.
Walipokuja watu wa tembo maquraishi waliikimbia Haram, Abdul Muttalib akawaambia: “Naapa kwa Mwenyezi Mungu sitoki haramu natafuta ushindi kupitia njia nyingine.”
Maquraishi wakawa wakisema: “Abdul Muttalib ni Ibrahim wa pili. Al-Masuudiy amesema: “Abdul Muttalib alikuwa akiwausia wanawe kuunga undugu, kulisha chakula na akiwatamanisha na kuwahofisha kufanya na kuaacha kitendo cha mtu anayetaraji siku ya Kiyama na ufufuo.”8
Al-Shahrastaniy amesema: “Alikuwa akiwaamrisha wanawe waache dhuluma na ujeuri. Akiwahimiza juu ya maadili mema. Akiwakataza mambo duni. Katika usia wake alikuwa akisema: Hakika dhalimu hatotoka ndani ya dunia hii isipokuwa baada ya malipo ya kisasi na kufikiwa na adhabu.”
Hivyo alipofariki mtu mmoja dhalimu ambaye hakufikiwa na adhabu, watu wakaanza kumuuliza Abdul Muttalib kuhusu hilo. Akafikiri na kusema: Naapa kwa Mwenyezi Mungu hakika nyuma ya nyumba hii kuna nyumba nyingine ambayo ndani ya nyumba hiyo mwema hulipwa wema wake na muovu ataadhibiwa kwa uovu wake.”9
MTOTO WA VICHINJWA VIWILI
Imam Ali Ridha (a.s.) aliulizwa kuhusu maana ya kauli ya Mtume : “Mimi ni mtoto wa vichinjwa viwili.” Akajibu: “Hakika Abdul Muttalib alijining’iniza katika mlango wa Kaaba akamuomba Mwenyezi Mungu amruzuku watoto kumi. Akaweka nadhiri kwa Mwenyezi Mungu kuwa atamchinja mmoja kati ya hao iwapo tu Mwenyezi Mungu atajibu dua yake.
Hivyo walipofika watoto kumi akasema: Hakika Mwenyezi Mungu kanitekelezea ombi langu, basi ni lazima nitekeleze nadhiri kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Akawaingiza wanawe Kaaba na kuanza mchakato kati yao, na hatimaye mchakato huo ukaangukia kwa Abdullah baba wa Mtume (s.a.w.w.) na ndiye aliyekuwa kipenzi chake sana.
Akarudia mara ya pili mchakato huo ukaangukia tena kwa Abdullah. Akarudia kwa mara ya tatu mchakato ukaangukia kwa Abdullah. Ndipo alipomchukua na kuazimia kumchinja. Wakakusanyika maquraishi na kumkataza asifanye hivyo.”10
Imam Al-Baqir (a.s.) amesema: “Mchakato ukaangukia kwa Abdullah. Akazidisha majina kumi lakini bado mchakato ukamwan- gukia Abdullah. Akaendelea kuzidisha majina kumi kumi mpaka yakafika mia moja ndipo mchakato ulipoangukia kwa ngamia.
Hapo Abdul-Muttalib akasema: ‘Sikumtendea haki Mola wangu,’ hivyo akarudia mara tatu na mara zote ukaangukia kwa ngamia. Akasema: ‘Sasa nimejua kuwa Mola Wangu kaniridhia.’ Ndipo alipochinja ngamia.”11
AMINA BINTI WAHAB
Baada ya miaka kumi tangu kuchimbwa Zamzamu na baada ya mwaka mmoja12 tangu Abdullah kufidiwa kwa ngamia Abdul Muttalib alitoka na mwanae Abdullah na kuenda nae katika nyumba ya Wahab bin Abdul Manafi bin Zahrat (wakati huo alikuwa ndio bwana wa kizazi cha Zahrah kinasaba na kisharaf). Hapo akamposa binti wa Wahabi, Amina kwa ajili ya Abdullah.
Amina alikuwa ndiye mwanamke bora kinasaba na kimaadili kwa maquraishi, hivyo Abdul Muttalib akamuozesha na kummilikisha Abdullah, Amina. Ndani ya nyumba ya Abdul Muttalib ndimo Abdullah alimomuingilia Amina na kupata ujauzito wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.).13
Imam Ali (a.s.) amesema: “Amina binti Wahabi aliona usingizini kuwa anaambiwa: Hakika aliyomo tumboni mwako ni bwana, hivyo ukimzaa mwite Muhammad.” Kisha Ali (a.s.) akasema: “Hivyo Mwenyezi Mungu alimpa jina kutoka ndani ya jina lake, kwani hakika Mwenyezi Mungu ni Mahmudu na huyu ni Muhammad.”14
Hakika Abdullah alipata umashuhuri mkubwa akawa ni mtu muhimu kwa watu, akawa ndiyo mazungumzo yao na kipenzi chao. Baada ya tukio la kisa cha fidia yake, kisa ambacho kilifanana na kisa cha babu yake Isma’il…… Mwenyezi Mungu akamjalia kukutana na binti bora kati ya mabinti wa kiquraishi……lakini hakumjalia kuishi nae muda mrefu. Kwani utafutaji ulimpeleka Sham akiwa na maquraishi kwa ajili ya biashara.
Alielekea Gaza huku akiwa amemuacha mke wake mja mzito, na alipokuwa akirudi alielekea Madina kwa lengo la kuwazuru wajomba zake na kuzidisha undugu, lakini mipango ya Mwenyezi Mungu haikumpa muda, hivyo akaugua huko na rafiki zake kulazimika kumwacha na kurudi huku wakiwa wamebeba habari za ugonjwa wake na kufikisha kwa baba yake Abdul Muttalib.
Abdul Muttalib akamtuma Al-Harithi ambaye ni mwanae mkubwa ili akamuuguze ndugu yake mpaka apone kisha arudi nae Makka. Isipokuwa mipango ya Mwenyezi Mungu ilikuwa ikimuharakisha Abdullah, hivyo Al-Harithi hakufika Madina isipokuwa baada ya siku nyingi tangu kufariki kwa ndugu yake.15
Hivyo akarudi kwa baba yake akiwa na moyo wa huzuni, mwenye kutetemeka huku akibeba habari za kifo cha mtoto kipenzi kati ya watoto wa baba yake. Hakika ni habari nzito kwa Abdul Muttalib lakini hazikuteteresha subira yake wala hazikudhoofisha uvumilivu wake.
MUHTASARI
Hakika Mwenyezi Mungu aliweka umuhimu maalumu kwa manabii wake, hivyo akawezesha wazaliwe toka ndani ya familia takasifu ili wawe na uwezo wa kuwasafisha watu dhidi ya shirki. Hivyo ndivyo alivyomteua nabii Muhammad (s.a.w.w.). Hakika alihama toka mifupa ya migongo mitakasifu yenye imani na toka mapaja ya utawa mpaka dunia ilipopata sharafu kwa kuzaliwa kwake.
Familia ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.) ilikuwa ni familia na damu yenye kuheshimika, kwani yeye ametokana na nabii Ibrahim (a.s.). Pia ilikuwa ikijihusisha na kulinda Haram ya Makka na kuitetea dhidi ya maadui.
Babu wa Mtume Abdul Muttalib aliishi zama ambazo ujumbe wa Mwenyezi Mungu ulikuwa umetoweka huku nguvu za shirki zikiwa zimedhihiri na ufisadi na dhuluma vikishamiri, lakini pamoja na hayo yote alikuwa ni mwenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu huku akilingania maadili mema, na njia hiyo ndiyo waliyopita watoto wake.
Abdul Muttalib alimjali sana mwanae Abdullah, hivyo akamwozesha mwanamke bora toka familia na damu yenye heshima. Lakini matak- wa ya Mwenyezi Mungu yalitaka Abdullah afariki kabla ya kuzaliwa mwanae Muhammad (s.a.w.w.).
MASWALI
1.    Elezea nafasi ya mazingira katika malezi ya mwanadamu?
2. Taja dalili inayothibitisha imani ya utohara wa wazazi wawili wa manabii?
3.Taja mifano halisi ya imani na tauhidi ya Abdul Muttalib babu wa Mtume Muhammad (s.a.w.w.)?
4. Inamaanisha nini kauli ya Mtume (s.a.w.w.): “Mimi ni mtoto wa vichinjwa viwili”?
5. Kwa nini Mwenyezi Mungu huwateua manabii wake toka kwenye vizazi vitakasifu?
6. Kwa nini Abdul Muttalib aliazimia kumchinja mwanae Abdullah?
7. Elezea jinsi Abdullah alivyosalimika kuchinjwa?
REJEA
•    1. Nahjul-Balaghah, hotuba ya 161.
•    2. Nahjul-Balaghah hotuba ya 98.
•    3. Nahjul-Balaghah hotuba ya 94.
•    4. Nahjul-Balaghah hotuba ya 214.
•    5. Fadhailul-Khamsa mina Sahihi Sita, Juz. 1, uk. 9.
•    6. Fadhailul-khamsa mina Sahihi sita, Juz. 1, uk. 9.
•    7. Dhakhairul-U’quba, uk. 10, na Sahih Muslim, Juz. 4, uk. 461.
•    8. Muruju Dhahabi, Juz. 2 uk. 103-108.
•    9. Mausuatu Ta’rikh Al-Islamiyi Juz. 1, uk., 244.
•    10. Uyunu Akhbari Ridha Juz. 1, uk. 212.
•    11. Al-Khisal, uk. 156.
•    12. Tarikh Yaaqubiy: Juz. 2 Uk. 9.
•    13. Siratun-Nabawiyyah ya Ibnu Hisham, Juz. 1, uk. 165.
•    14. Al-Ihtijaj, Juz. 1, uk. 321.
•    15. Biharul-Anwar, Juz. 15 uk. 124. Tazama tafsiri ya Surat Dhuha kwenye kitabu Majma’ul-Bayan na Al-Mizan Fidhilalil-Qur’ani.

MWISHO