Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

MAISHA YA NABII WA MWISHO

0 Voti 00.0 / 5

MAISHA YA NABII WA MWISHO
Hakika Mwenyezi Mungu alipenda asimamie malezi ya Muhammad (s.a.w.w.) amtoe mikononi mwa familia yake ili awe chini ya ulinzi wake ikiwa ni maandalizi ya kupata familia kubwa ambayo kiongozi wake atakuwa ni Muhammad.
Familia ambayo haitopendelea taifa wala lugha au rangi bali mbora wao ndani ya familia hiyo ni yule tu mwenye uchamungu. Hivyo Qur’ani imeelekeza maana hii kwa kusema: “Je hakukukuta ni yatima akakuhifadhi?” (Dhuha: 6). Mtume akaelezea kwa kusema: “Hakika Mola wangu alinilea akaboresha maadili yangu.”1
Hakika busara za Mwenyezi Mungu zilimnyima Muhammad (s.a.w.w.) mapenzi na huruma ya muda mfupi huku Mwenyezi Mungu akimpangia huruma na mapenzi ya muda mrefu usio na kikomo, kwani alimuhifadhi kwa babu yake kisha kwa ami yake, hivyo hao wawili wakawa wakimpendelea zaidi ya nafsi zao na zaidi ya watoto wao wa kuzaa.
Katika njia hiyo ya malezi wakatoa kila aina ya mapenzi na huruma kwa kiwango ambacho wazazi hawawezi kujitolea kwa watoto wao wa kuzaa.
Hilo ni miongoni mwa fadhila za Mwenyezi Mungu kwa Mtume (s.a.w.w.) bali hakika alimfanyia umuhimu maalumu pindi alipojitolea mwenyewe kumlinda na kumuhami kwa huruma yake, na hakika hakuna neema kubwa kama hii ambayo kaielezea Mwenyezi Mungu kwa kusema: “Na hakika fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yako ni kubwa.”2
KUZALIWA KWAKE: ZAMA, SEHEMU NA NAMNA
Alizaliwa (s.a.w.w.) katika mji wa Makka ndani ya mwaka wa ndovu (tembo) mwezi wa mfungo sita. Kwa Shia Imamiya ni mashuhuri kuwa alizaliwa alfajiri ya siku ya ijumaa ya terehe kumi na saba. Kwa wengine mashuhuri ni kuwa alizaliwa siku ya jumatatu terehe kumi na mbili wakati wa kuchomoza alfajiri au jua au wakati wa kukengeuka jua.
Lililo mashuhuri toka kwa Amina binti Wahabi kama alivyoelezea Ibnu Is’haqa ni kuwa: “Wakati Amina alipokuwa akielezea siku za mimba ya Mtume (s.a.w.w.) alisema: Hakika Amina aliona nuru iki- toka mpaka akaona makasiri ya Basra kutokea ardhi ya Sham. Akaambiwa hakika wewe umembeba bwana wa umma huu, hivyo atakapotua aridhini sema: Namkinga kwa Mwenyezi Mungu mmoja dhidi ya shari ya kila hasidi, kisha mwite Muhammad.”3
Halima binti Dhuaybu As-Saadiyyah ameongeza kuwa: “Amina alise- ma: ‘Kisha naapa kwa Mwenyezi Mungu hakuna mimba niliyoona ni nyepesi kwangu na rahisi kama yake.’”4
Al-Yaaqubiy amesema: “Alipozaliwa Muhammad (s.a.w.w.) mashetani yalilaaniwa na nyota ziliporomoka, watu wakasema: Hakika hii ni alama ya Kiyama, watu wakapatwa na tetemeko la ardhi ambalo lilienea dunia nzima mpaka makanisa na mahekalu yakabomoka, na kikatoka sehemu yake kila kilichokuwa kikiabudiwa kinyume na Mwenyezi Mumgu.
Mambo ya kichawi yakaharibika na mashetani wao wakafungwa, kasri la Kisra likatetemeka hivyo yakaporomoka masharafu kumi na tatu na moto wa Farsi ukazimika.
Kabla ya hapo ulikuwa na muda wa miaka elfu bila kuzimika….Mtu kati ya Ahlul-kitabi alikwenda kwa maquraishi akiwemo Hisham bin Al-Mughirah, Al-Walid bin Al-Mughirah na Al-Utba bin Rabia akasema: “Usiku huu kazaliwa mtoto kwa ajili yenu5……..ndani ya usiku huu kazaliwa nabii wa umma huu naye ni Ahmad wa mwisho……Kisha akatoa alama zinazomtambulisha.”6
KUNYONYA KWAKE
Maziwa ya mwanzo aliyonyonya baada ya maziwa ya mama yake mzazi yalikuwa ni ya Thuwaybah mjakazi wa Abu Lahabi bin Abdul Muttalib. Hiyo ilikuwa ni kabla hajanyonyeshwa na Halima binti Abu Dhuaybu As-Saadiyyah,7 kwani watu wa Makka walikuwa wakiwanyonyesha watoto wao kwa wanawake wa vijijini kwa lengo la kutaka ufasaha.
Ushahidi juu ya hilo ni kauli yake mwenyewe (s.a.w.w.): “Mimi ndiye mfasaha kuliko wote wanaotamka kiarabu, zaidi ya hapo mimi ni mkurayshi na nimenyonyeshwa na watoto wa Saad.”
Alibakia (s.a.w.w.) mikononi mwa Halima muda wa miaka miwili mpaka alipoacha kunyonya, ndipo Halima akamkabidhi kwa mama yake na kumpa habari za baraka zote alizoziona, hapo Amina akam- rudisha kwa Halima kisha baadae Halima akamrudisha kwa mama yake huku Mtume (s.a.w.w.) akiwa na umri wa miaka mitano.8
MAJINA YAKE NA MAJINA YAKE YA HESHIMA
Muhammad bin Jubayri bin Mut’im amepokea toka kwa baba yake kuwa alimsikia Mtume (s.a.w.w.) akisema: “Hakika mimi nina majina kadhaa: Mimi ni Muhammad, Ahmad na mfutaji, Mwenyezi Mungu atafuta ukafiri kupitia mimi. Na mimi ni mkusanyaji, Mwenyezi Mungu atakusanya watu chini ya nyayo zangu. Na mimi ndiye niliyefuata baadae hakuna mwingine yeyote baada yangu.”9
Jina lake la heshima lililo maarufu ni: Abu Qaasim. Imepokewa kutoka kwake kuwa alisema: “Jiiteni kwa jina langu lakini msijipe heshima kwa jina langu la heshima.”10 Pia inasemekana kuwa jina lake la heshima ndani ya Taurati ni: Baba wa wajane, na jina lake ni: Swahibul-Malhama.11
Al-Halbiy amesema: “Ni wazi kuwa majina yake yote yametokana na sifa za vitendo alivyotenda ambavyo vinalazimu sifa na ukamilifu, hivyo ndani ya kila sifa ana jina.”12
VIPINDI VYA MAISHA YAKE
Maisha ya Mtume (s.a.w.w.) mwanzo yamegawanyika katika vipindi viwili tofauti:
Kipindi cha kwanza: Ni kuanzia alipozaliwa mpaka alipokabidhiwa unabii, nacho ni kipindi cha miaka arubaini.
Kipindi cha pili: Ni kuanzia alipokabidhiwa unabii mpaka alipofariki, nao ni muda wa miaka ishirini na tatu.
Katika vipindi vyote vya maisha yake, Muhammad bin Abdullah (s.a.w.w.) alijulikana kwa maadili mema, kujitenga na vitendo vya shirki, kujitenga na unywaji pombe, kutokuhudhuria vikao vya upuuzi, kamari na zaidi ya hayo ambayo vijana wa zama hizo walikuwa wakivutiwa nayo. Kutokana na maadili yake mema alijulikana kwa jina la mwaminifu, hivyo maquraishi walipozozana kuhusu mtu atakayeweka jiwe jeusi waliangukia kwenye uamuzi wa Muhammad (s.a.w.w.) huku wakikiri kuwa yeye ni mwaminifu asiyeyumba.
Wanahistoria wote wamekiri kuwa Muhammad (s.a.w.w.) hakuwahi kuabudu sanamu na alikuwa akichukizwa na masanamu hayo. Alikuwa akihamia pango la Hira kila mwaka muda wa mwezi mzima……Pia alikuwa mbali na sifa za kijahiliya ambazo walikuwa nazo vijana wa kiarabu wa zama hizo. Bali alikuwa akikataza ibada ya masanamu pale anapopata fursa ya kufanya hivyo.
Kila kipindi kati ya vipindi vya maisha yake kimegawanyika sehemu nyingi, hivyo kipindi cha kwanza unaweza kukigawa sehemu tatu:
Sehemu ya kwanza: Ni kuanzia alipozaliwa mpaka aliposafiri safari yake ya kwanza ya Sham akiwa na ami yake Abu Talib. Kipindi hicho alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili.
Sehemu ya pili: Ni kuanzia pale aliporudi kutoka Sham mpaka alipomuoa Khadija. Kipindi hicho alikuwa na umri wa miaka ishirini na tano.
Sehemu ya tatu: Ni kuanzia alipooa mpaka alipokabidhiwa unabii akiwa na umri wa miaka arubaini.
Kipindi cha pili kimegawanyika zama mbili tofauti:
Zama za kwanza: Nazo ni zama za Makka ambazo zilichukua muda wa miaka kumi na tatu.
Zama za pili: Nazo ni zama za Madina13 ambazo zilichukua muda wa miaka kumi.
MUHTSARI
Ni maarufu kuwa Mtume Muhammad (s.a.w.w.) alizaliwa yatima. Na mama yake Amina binti Wahabi aliona baadhi ya alama zilizojulisha kuwa mwanae atakuwa na jambo kubwa na cheo cha juu.
Hakukuwa na kalenda maarufu ya kuhifadhi kumbukumbu za matukio, hivyo historia ya kuzaliwa Mtume (s.a.w.w.) imehifadhiwa na tukio la kuhujumiwa kwa Kaaba, tukio ambalo hujulikana kwa jina la tukio la tembo. Qur’ani imeashiria tukio hili la kihistoria ndani ya Sura Al-Fiylu.
Ukoo wa Abdul Muttalib ulimjali sana Muhammad bin Abdullah (s.a.w.w.). Hilo lilidhihirika pale walipompeleka kunyonya kwa Bani Saad kwani baada ya maziwa ya mama yake walimpeleka kijijini ili akanyonye katika mazingira ya afya na ufasaha wa lugha.
Mtume ana majina mazuri, sifa nzuri na majina mazuri ya heshima. Maisha ya Mtume (s.a.w.w.) yalichukua miaka sitini na tatu huku yakigawanyika vipindi viwili vikuu: Cha kwanza: Kuanzia alipozaliwa mpaka alipokabidhiwa unabii. Muda wake ni miaka arubaini. Cha pili: Kuanzia alipokabidhiwa unabii mpaka alipofariki. Muda wake ni miaka ishirini na tatu.
MASWALI
1. Weka kikomo cha mwaka aliozaliwa Mtume Muhammadi (s.a.w.w.).
2. Mlezi wa kwanza wa Mtume (s.a.w.w.) ni nani?
3. Ni zipi zilizokuwa dalili za huruma ya Mwenyezi Mungu kwa Mtume (s.a.w.w.) kabla
hajazaliwa na baada ya kuzaliwa?
4. Ni mambo gani yalitokea siku ya kuzaliwa Mtume (s.a.w.w.)?
5. Wapi aliponyonya Mtume Muhammad (s.a.w.w.) na ni kwa nini?
6. Taja majina yake na majina yake ya heshima?
7. Ni upi uhusiano uliyopo kati ya majina yake na sifa zake?
KUJISOMEA
MAISHA YA MTUME NA HISTORIA YA UISLAMU NDANI YA MISTARI
I. Alizaliwa mwaka wa tembo (Ndovu) huko kwenye mji mtukufu wa Makka.
II. Alinyonyeshwa na Bani Saad.
III. Alirudishwa kwa mama yake na babu yake akiwa na umri wa miaka minne au mitano na ndani ya muda huu ilionekana karama ya kuomba mvua kupitia kwake.
IV. Mama yake alifariki Mtume (s.a.w.w.) akiwa na umri wa miaka sita.
V. Aliishi pamoja na babu yake na mama yake muda wa miaka miwili, kisha babu yake akafariki huku Mtume (s.a.w.w.) akiwa na umri wa miaka minane.
VI. Babu yake aliacha majukumu ya kumlea mikononi mwa ami yake, hivyo akabaki mikononi mwake mpaka alipooa.
VII. Alisafiri na ami yake kwenda Sham akiwa na umri wa miaka kumi na nane.
VIII. Njiani alikutana na padri Buhayra ambaye alimhadharisha ami yake Abu Talib dhidi ya vitimbi vya mayahudi.
IX. Alihudhuria kiapo cha damu baada ya miaka ishirini tangu kuzaliwa.
X. Baada ya kujengwa upya jengo la Al-Kaaba aliweka jiwe jeusi huku akishirikisha makabila yote katika hilo.
XI. Alisafiri kwenda Sham akiwa mtumishi wa mali ya Khadija.
XII. Alimuoa Khadija akiwa na umri wa miaka ishirini na tano.
XIII. Alikabidhiwa utume akiwa na umri wa miaka arobaini.
XIV. Ulinganio maalumu ulichukua muda wa miaka mitatu.
XV. Ndani ya mwaka wa nne tangu kukabidhiwa utume aliamrishwa kuwaonya jamaa zake wa karibu.
XVI. Siku aliyowaonya jamaa zake wa karibu pia alitoa maelezo ya usia wa Ali (a.s.) kwa kumteua kuwa khalifa wake baada yake.
XVII. Kisha aliamrishwa kutangaza utume wake kwa watu wote.
XVIII. Baada ya mbinyo kuzidi toka kwa maquraishi aliwapa ruhusa waislamu wahame kuelekea Ethiopia ikiwa ni mwaka wa tano tangu kuwa Mtume.
XIX. Mwaka wa saba hadi wa kumi tangu kuwa Mtume aliwekewa vikwazo yeye na Bani Hashim wote wakiwa sehemu iju- likanayo kama bonde la Abu Talib.
XX. Baada ya vikwazo kuisha Abu Talib na Khadija walifariki, hivyo akauita mwaka huo kuwa ni mwaka wa huzuni.
XXI. Israi na Miraji ilikuwa ndani ya mwaka huu au kabla ya mwaka huu au baada ya mwaka huu kulingana na kauli tofauti.
XXII. Alikuwa akitangaza utume wake kwa makabila mbalimbali ifikapo msimu wa Hijja, hiyo ni baada ya kuondolewa vikwa- zo.
XXIII. Kisha akahamia Taifa akiwa na mtoto wa ami yake Ali (a.s.).
XXIV. Kwa mara ya kwanza yeye kukutana na watu wa Madina ilikuwa mwaka wa kumi na moja kisha akaendelea kukutana nao mpaka alipofanikiwa kuhamia Madina.
XXV. Maquraishi walijikusanya kwa lengo la kumuua hivyo akamwamuru Ali (a.s.) alale kitandani kwake wakati wa kuhama kwenda Madina.
XXVI. Alifika Qubaa mfunguo sita. Na kuhama huko kukawa ndiyo mwanzo wa kalenda ya kiislamu kwa amri ya Mtume mwenyewe (s.a.w.w.).
XXVII. Ndani ya mwaka huu aliweka misingi ya mwanzo ya dola ya kiislamu kwa kuanza kujenga msikiti kisha kuunga undugu, kisha kwa kutoa waraka maalumu uliyoelekeza mpangilio wa shughuli za dola mpya, kisha akaweka mikataba na mayahudi.
Ujumbe wa kwanza wa kijeshi uliongozwa na ami yake Hamza ikiwa ni mwezi wa saba tangu kuhamia Madina, hivyo kuanzia alipohama mpaka mwishoni mwa mwaka wa kwanza alituma ujumbe wa kijeshi mara tatu. Na ndani ya mwaka huo huo alianza maisha ya ndoa na Aisha baada ya kufunga naye ndoa huko Makka.
XXVIII. Ndani ya mwaka wa kwanza baada ya kuhama Aya nyingi katika Sura Baqarah ziliteremka, hivyo zikawafedhehesha wanafiki na kufichua mbinu za mayahudi huku zikileta baadhi ya hukumu.
XXIX. Mayahudi na maquraishi walikusudia kuiangusha dola changa ya Mtume (s.a.w.w.), isipokuwa Mtume (s.a.w.w.) aliweza kuzuwia harakati zao hivyo ndani ya mwaka wa pili kulitokea vita mara nane na ujumbe wa kijeshi mara mbili, vikiwemo vita vya Badr ambavyo vilikuwa ndani ya mwezi wa Ramadhani tarehe kumi na saba. Ndani ya mwaka huo huo funga ilifaradhishwa na Qibla kikabadilishwa, pia Ali (a.s.) alimuoa Fatima (a.s.).
Ndani ya mwaka huu kulishuhudiwa ushindi mbalimbali na sheria mbalimbali za kisiasa na kijamii, na ndiyo mwaka ambao maquraishi walipata pigo la kwanza la uchungu katika vita vya Badri.
Ndani ya mwaka huu liling’olewa kundi la kwanza la kiyahudi (Bani Qaynuqaa) baada ya kuvunja mkataba uliokuwepo kati yao na Mtume (s.a.w.w.), hiyo ilikuwa ni baada ya ushindi wa vita vya Badri.
XXX. Yaliendelea mashambulizi toka kwa mayahudi na maquraishi dhidi ya waislamu muda wa miaka mitatu: Mwaka wa tatu, wanne na watano. Kisha vikafuata vita vya Uhudi, kisha vya Bani Nadhiri, kisha vya Ahzab, kisha vya Bani Quraydha, kisha vya Bani Mustalaqi.
Kwa ujumla mwaka wa tano ulikuwa ndio mwaka mgumu sana kwa Mtume (s.a.w.w.) na waislam ukilinganisha na miaka mingine.
XXXI. Baada ya hapo Mwenyezi Mungu alizuwia vitimbi vya mayahudi, hivyo suluhu ya Hudaibiya ikawa ndiyo mwanzo wa ukombozi kwa waislam, kwani Mtume (s.a.w.w.) alianza kuwekeana mikataba ya ushirikiano na makabila mbalimbali, hivyo nguvu ya mayahudi na maquraishi ikaanza kudhoofika.
Kisha vikafuata vita vya Khaybar, Muuta, Ukombozi wa Makka, Hunayni na Tabuk.
XXXII. Mwaka wa tisa ulikuwa ni mwaka wa kupokea ujumbe toka sehemu mbalimbali, kisha ikafuata Hijja ya kuaga ndani ya mwaka wa kumi. Ndipo akafariki Mtume (s.a.w.w.) tarehe ishirini na nane mfunguo tano (Safar) mwaka wa kumi na moja tangu kuhamia Madina.
Ikiwa ni baada ya nguzo za dola ya kiislamu kukomaa huku akiwa kaiwekea viongozi wenye uwezo wakiwakilishwa na Imam Ali bin Abu Talib (a.s.), mtu ambaye alilelewa na mikono miwili ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kwa kumlea malezi bora kamilifu huku akimuandaa maandalizi bora chini ya msaada wa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kuongoza umati wake.
XXXIII. Matokeo ya ulinganio wa zama za Makka ni kuanzisha umma wa kiislamu kupitia mafunzo na malezi yake kiakili, kisaikolojia hadi kimantiki.
Pia kuandaa nguvu ya kijeshi ndani ya muda huo huku akifanikiwa kuweka mipango kwa amri ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya mustakbali wa Uislamu, hivyo akalea kundi la wachamungu kisha akalitangaza hatua kwa hatua, huku akijiandaa kwa uhamisho mkubwa ikiwa ni baada ya kuikomboa Madina kupitia Uislamu wa watu wema wa zama hizo.
XXXIV. Matokeo ya ulinganio wa Mtume (s.a.w.w.) zama za Madina yalionekana pale ilipoanzishwa ndani ya Bara la uarabu dola ya kwanza ya kisiasa ya kiislamu, na kuanzishwa sheria ya kijamii ambayo ilijenga heshima itokayo kwa Mwenyezi Mungu.
Na kufungua mifereji ya nguvu za kiakili katika jamii ya kibinadamu kupitia mapinduzi ya kielimu ambayo yalianzishwa na Uislamu kwa baraka za Qur’ani ambayo ilikuwa ikiwaandaa waislam kwa ajili ya kuondoa vikwazo wakati wa kueneza Uislamu nje ya Bara la uarabu kwa ajili ya kutangaza jina la Mwenyezi Mungu katika ardhi hii.
Siku ya Ghadiri baada ya hija ya kuaga Mtume (s.a.w.w.) alimtangaza rasmi kiongozi aliyestahiki kisheria kuchukua nafasi yake. Kwa ajili hiyo Mtume (s.a.w.w.) alichukua dhamana ya kuendeleza mapinduzi ya kiroho kupitia mikono ya kizazi chake ambacho Mwenyezi Mungu amekiondolea uchafu na kukitakasa kabisa.
XXXV. Hivyo matokeo ya zama za Mtume (s.a.w.w.) yalikuwa:
Kwanza, kupatikana Uislamu uliyokamilika na wa kudumu kwa ajili ya kutoa mpangilio wa maisha ya mwanadamu.
Pili: Kupatikana umma wa kiislamu uliobeba bendera ya kiislamu huku ukiamini itikadi na nidhamu za maisha kwa mujibu wa Uislamu.
Tatu: Kupatikana dola ya kiislamu ambayo inaelekeza Uislamu na kupambana na vikwazo ambavyo vinajitokeza kwa lengo la kuzuia maendeleo ya Uislamu.
Nne: Kuandaa viongozi wema wa umma wa kiislamu wenye uwezo kwa lengo la kuendeleza malezi ya kiroho ya kimapinduzi kwa misin- gi na mafunzo ya Mwenyezi Mungu, na kwa ajili ya kufungua vipaji vya wanadamu kwa lengo la kumwendeleza na kumpeleka mwanadamu katika ukamilifu.
•    1. Mizanul-Hikma, ameipokea kutoka kwenye kitabu Nuru Thaqalayni Juz. 5, Uk. 389.
•    2. An-Nisai: 133.
•    3. As-Siratu An-Nabawiyyah cha Ibnu Hisham, Juz. 1, Uk. 166.
•    4. As-Siratu An-Nabawiyyah cha Ibnu Hisham, Juz. 1, Uk. 166.
•    5. Tarikh Yaaqubiy, Juz. 2, Uk. 8 – 9.
•    6. Tabaqat ya Ibnu Saad, Juz. 1, Uk. 106. As-Siratun-Nabawiyyah, Juz. 1, Uk. 226. Al-Iswabah: 1/ 3, Uk. 181.

REJEA
•    7. Tarikh Yaaqubiy, Juz. 2, Uk. 9.
•    8. Aayanus-Shia, Juz. 1, Uk. 218.
•    9. Sahih Bukhar, Juz. 4 Uk. 225. Tabaqat Ibnu Saad, Juz. 1, Uk. 104.
•    10. Tabaqat Ibnu Saad, Juz. 1, Uk. 104.
•    11. Tabaqat Ibnu Saad, Juz. 1, Uk. 104.
•    12. As-Siratun-Nabawiyyah cha Al-Halbiy, Juz. 1, Uk. 78 – 82.
•    13. Rejea zama za Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) mwishoni mwa somo la kwanza.

MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini