TABIA NA MWONEKANO WA HITIMISHO LA MANABII 2

TABIA NA MWONEKANO WA HITIMISHO LA MANABII 2
MSOMI ASIYEWAHI KUSOMA WALA KUANDIKA
Kati ya sifa za kipekee alizonazo Mtume wa mwisho (s.a.w.w.) ni kuwa yeye hakujifunza kusoma wala kuandika kutoka kwa mwalimu yeyote yule wa kibinadamu,1 wala hakukulia katika mazingira ya kielimu bali alikuwa ndani ya jamii ya wajinga.
Hakuna yeyote aliyepinga ukweli huu uliyoelezwa na Qur’ani tukufu, bali alikuwa ndani ya jamii ambayo watu wake walikuwa ni wajinga sana kuliko watu wa jamii nyingine yoyote ile, lakini pamoja na hali hiyo alileta Kitabu kinacholingania elimu na maarifa, kikiamsha fikra na akili huku kikiwa kimekusanya aina zote za maarifa.
Hakika Mtume (s.a.w.w.) alianza kuwafunza watu Kitabu na hekima2 kwa silabasi nzuri sana mpaka akaibua ustaarabu wa kipekee ambao ulizamisha Magharibi na Mashariki kupitia elimu na maarifa yake, na bado mpaka leo nuru yake inang’aa, hivyo yeye Mtume (s.a.w.w.) ni mtu asiyewahi kusoma wala kuandika lakini alikuwa aking’oa ujinga, ujahili na ibada za masanamu huku akiwa amewaletea wanadamu dini ya hadhi ya juu na sheria ya kimataifa ambayo itawafaa wanadamu muda wote wa maisha yao.
Hivyo kupitia elimu, maarifa yake, maneno yake timilifu, ubora wa akili yake, mafunzo yake na silabasi yake ya malezi yeye mwenyewe huwa ni muujiza, kwa sababu hiyo Mwenyezi Mungu akasema:
“Basi mwaminini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake nabii asiyewahi kuandika wala kusoma, ambaye anamwamini Mwenyezi Mungu na maneno yake, na mfuateni ili mpate kuongoka.”3
Hakika Mwenyezi Mungu alimfundisha yale aliyokuwa hayajui na akamfunza kitabu na hekima mpaka akawa nuru, taa yenye kuangaza, dalili, shahidi, mtume wa wazi, mshauri nasaha mwaminifu, mkum- bushaji, mwenye kutoa habari njema na mwenye kuonya.4
Yeye ndiye aliyemkunjua kifua kwa ajili yake, akamwandaa kupokea ufun- uo na kutekeleza jukumu la kuongoza katika jamii ambayo ilikuwa imetawaliwa na ubaguzi, chuki na majivuno ya kijahiliya. Hivyo akawa ni kiongozi bora wa hali ya juu aliyetambuliwa na wanadamu katika uhubiri, malezi na mafunzo.
MWISLAMU WA KWANZA NA MBORA WA WANAIBADA
Hakika kilele cha mwanzo ambacho ni lazima kwa kila mwanadamu akifikie ili ajiandae kuteuliwa na kuchaguliwa na Mwenyezi Mungu ni unyenyekevu kamili kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Muumba wa ulimwengu. Pia kujisalimisha kiukamilifu mbele ya nguvu Zake tuku- fu na hekima zake kamilifu. Pia utumwa wa hiari uliotimia mbele ya Mwenyezi Mungu mmoja wa pekee aliye tegemeo.
Hakika Qur’ani tukufu imemtolea ushahidi nabii huyu aliyewapita manabii wote katika kila kitu, ikasema: “Na mimi ni wa kwanza wa waliojisalimisha.”5
Hakika hicho ni kilele cha ukamilifu ambacho alikifikia mja huyu mkweli katika ibada zake, na akawa kawapita watu wote kwa ujumla. Hakika unyenyekevu wake wa kweli ulidhihirika katika matendo na kauli zake, hivyo akasema: “Kitulizo cha macho yangu ni Swala.”6
Hakika Swala ilipendezeshwa kwake kama yalivyopendezeshwa maji kwa mtu mwenye kiu, hivyo anywapo maji hukata kiu, lakini Mtume (s.a.w.w.) hakukatwa kiu na Swala, kwani daima aliusubiri kwa hamu muda wa Swala huku shauku ya kusimama mbele ya Mola wake ikiongezeka. Alikuwa akimwambia mwadhini wake: “Tupe raha ewe Bilal”.7
Imepokewa kuwa alikuwa akizungumza na familia yake na wao wakimzungumzisha lakini unapoingia wakati wa Swala huwa kama vile hawajui na hawamjui.8 Kipindi anaposali kifua chake hutoa sauti ya kutetemeka kama sauti ya mchemko wa chungu huku akilia kutokana na kumwogopa Mwenyezi Mungu mtukufu hadi msala wake unalowana.9
Hivyo alikuwa akisali mpaka nyayo zake zinatoa harufu. Watu humwambia unafanya hivyo ilihali Mwenyezi Mungu ame- shakusamehe madhambi yako yaliyotangulia na yaliyofuatia. Hujibu: “Hivi haifai nikawa mja mwenye kushukuru?”10
Alikuwa akifunga mwezi wa Shabani na Ranadhani na siku tatu ndani ya kila mwezi,11 huku akibadilika rangi uingiapo mwezi wa Ramadhani, Swala zake huongezeka huku akinyenyekea katika dua.12
Linapoingia kumi la mwisho la Ramadhani hujitenga na kuwahama wakeze huku akiupitisha usiku akiwa faragha kwa ajili ya ibada.13
Alikuwa akisema: “Dua ndiyo roho ya ibada, silaha ya muumini, nguzo ya dini na nuru ya mbingu na ardhi.”14
Daima alikuwa katika mawasiliano na Mwenyezi Mungu, akijifunga kwake kwa unyenyekevu na dua katika kazi yoyote ile kubwa au ndogo, bali alikuwa akimwomba Mwenyezi Mungu msamaha na kutubu kila siku mara sabini bila ya kuwa na dhambi yoyote.15
Hakuamka usingizini ila ni mnyenyekevu mwenye kusujudu.16
Alikuwa akimhimidi Mwenyezi Mungu kila siku mara mia tatu sitini akisema: “Kila sifa njema ni ya Mwenyezi Mungu Mola wa ulimwen- gu wote, na ni nyingi katika kila hali.”17
Daima alikuwa akisoma Qur’ani huku akiwa ni mwenye kushughulishwa sana na usomaji huo. Imani isiyo na mipaka kwa Mwenyezi Mungu:
Mwenyezi Mungu amemhimiza Mtume Wake (s.a.w.w.) awe na imani isiyo na mipaka na Mola Wake kwa kusema: “Je, Mwenyezi Mungu hamtoshei mja wake?”18
Pia alisema: “Na umtegemee Mwenye nguvu, Mwenye rehema.* Ambaye anakuona unaposimama.* Na mageuko yako katika wale wanaosujudu.”19
Imepokewa kutoka kwa Jabir (r.a.) kuwa: “Tulikuwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) tukafika kwenye mti wenye kivuli tukamwachia mti huo. Ghafla akatokea mtu kati ya mushrikina huku upanga wa Mtume (s.a.w.w.) ukiwa umetungikwa kwenye mti, ndipo mushrik yule alipouchukua upanga ule na kumwambia Mtume (s.a.w.w.): “Je unaniogopa? “ Mtume akajibu: “Hapana.” Mushriku akasema: “Nani atakuzuwia dhidi yangu?” Mtume akajibu: “Mwenyezi Mungu.” Hapo upanga ukadondoka toka mikononi mwa mushriku.
Ndipo Mtume wa Mwenyezi Mungu alipouchukua na kusema: “Na wewe ni nani atakayekuzuwia dhidi yangu?” Akajibu: ‘Mbora wa wachukuaji.” Mtume akasema: “Je unakiri kuwa hapana mola wa haki isipokuwa Allah na kwamba hakika mimi ni Mtume wa Allah?” Mushriku akajibu: “Hapana, isipokuwa ninakuahidi kuwa sitokupiga vita, wala sitokuwa pamoja na watu wanaokupiga vita.
Hapo Mtume akamwachia, na mushriku akaenda kwa jamaa zake na kuwaambia: “Nimewajia toka kwa mbora wa watu.”20
USHUJAA WA HALI YA JUU
Mwenyezi Mungu ameeleza sifa za Mtume Wake (s.a.w.w.) kwa kusema: “Wale wanaofikisha ujumbe wa Mwenyezi Mungu na kumwogopa Yeye wala hawamwogopi yeyote isipokuwa Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ndiye atoshaye kuh- esabu.”21
Imam Ali (a.s.) ambaye mashujaa wa kiarabu waliinamisha vichwa mbele yake ametupa wasifu makini kuhusu ushujaa wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) akasema: “Pindi vita vinapokuwa vikali na kundi moja likalizidi kundi lingine basi tulikuwa tukijikinga kwa Mtume, hivyo hakuna yeyote anayekuwa karibu sana na maadui kuliko yeye.”22
Mikidad ameelezea msimamo wa Mtume (s.a.w.w.) siku ya Uhud baada ya watu kutawanyika huku wakimwacha Mtume (s.a.w.w.) peke yake, Mikidad amesema: “Naapa kwa yule aliyemtuma kwa haki, ukimwona Mtume (s.a.w.w.) kainua mguu wake shibri moja basi ujue yuko mbele ya adui huku kundi la jamaa wa adui likiwa limemvamia na muda huo huo likitawanyika kwa kumkimbia, utamwona kasimama akirusha upinde au akirusha jiwe mpaka mawe yawaenee.”23
UTAWA USIYOKUWA NA MFANO
Mwenyezi Mungu amesema kumwambia Mtume Wake (s.a.w.w.) kuwa: “Wala usivikodolee macho yako tulivyowastarehesha watu wengi miongoni mwao, ni mapambo ya maisha ya dunia, ili tuwajaribu kwa hayo, na riziki ya Mola Wako ni bora mno na iendeleayo.”24
Hakika Mtume wa Mwenyezi Mungu alikuwa mkweli katika kuiacha dunia na mapambo yake. Aliiacha dunia mpaka ikapokewa toka kwa Abu Umamah toka kwa Mtume (s.a.w.w.) kuwa alisema: “Mola Wangu alinitunukia akataka aifanye Makka yote iwe dhahabu kwa ajili yangu, nikasema: Hapana Mola Wangu! lakini napenda niwe nashiba siku moja na kushinda na njaa siku nyingine……..Kwani nitakapokuwa na njaa nitakunyenyekea na kukukumbuka, na nitakaposhiba nitakushukuru na kukuhimidi”.25
Akalala juu ya changarawe na alipoamka zilikuwa zimeathiri ubavu wake. Akaambiwa: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu tungekuwekea kizuwizi.” Akajibu: “Mimi nina nini na hii dunia, kwani mimi si chochote ndani ya dunia hii isipokuwa ni kama msafiri aliyejipumzisha chini ya mti wa kivuli na baada ya mapumziko ataon- doka na kuuacha ule mti.”
Ibnu Abbas amesema: “Mtume (s.a.w.w.) alikuwa akilala njaa siku zenye kufuatana, huku familia yake ikiwa haipati chakula cha usiku. Mara nyingi mkate wao ulikuwa ni mkate wa shairi.”
Aisha amesema: “Familia ya Muhammad haikula milo miwili ndani ya siku moja isipokuwa mlo mmoja ulikuwa ni tende tu.”26
Akamwambia mtoto wa dada yake Urwah: “Hakika sisi tulikuwa tukiutazama mwezi mwandamo, kisha mwezi mwandamo mwingine hadi miezi miandamo mitatu katika miezi miwili huku ndani ya muda wote huo haujawashwa moto katika nyumba za Mtume (s.a.w.w.).”
Urwah akamuuliza: “Ewe mama mdogo; alikuwa akiwalisha nini usiku?” Akajibu: “Vyeusi viwili: Tende na maji. Isipokuwa Mtume alikuwa na jirani yake wa kianswari aliyekuwa na mifugo, hivyo alikuwa akimpa Mtume wa Mwenyezi Mungu maziwa yake na Mtume anatupa sisi.”27
Pia amesema: “Mtume (s.a.w.w.) alifariki huku ngao yake ikiwa imewekwa rehani kwa yahudi kwa thamani ya vibaba thelathini vya shairi.”28
Imepokewa toka kwa Anas bin Malik kuwa: “Fatima (a.s.) alimpelekea Mtume (s.a.w.w.) kipande cha mkate. Mtume akasema: “Ewe Fatima, kipande hiki cha nini? “Akajibu: “Ni kipande cha mkate kwani roho yangu haijaridhika mpaka nikuletee kipande hiki.” Mtume akasema: “Hakika hiki ni chakula cha kwanza kilichoingia ndani ya kinywa cha baba yako tangu siku tatu zilizopita.”29
Hii ni sura fupi na halisi ya utawa wa Mtume (s.a.w.w.) na jinsi alivyoipa mgongo dunia mpaka akafariki.
Muhtasari
Mtume wa Mwenyezi Mungu Muhammad bin Abdullah hakujifunza mikononi mwa mwanadamu yeyote, lakini alikuja na Kitabu cha kie- limu na kimaarifa cha kimataifa ambacho kimewataka wanadamu wote katika zama zote walete mfano wake.
Kupitia Kitabu hicho Mtume (s.a.w.w.) aliweza kumtoa mwanadamu toka jamii ya kijinga mpaka jamii ya kielimu iliyokamilika yenye kustaarabika, huku akihimiza usiku na mchana juu ya utafutaji wa elimu na maarifa mbalimbali.
Hivyo kupitia Kitabu hicho aliasisi dola kubwa na kujenga ustaarabu wa pekee ambao mfano wake hau- jashuhudiwa na mwanadamu.
Mtume (s.a.w.w.) alibeba maana kamili ya ibada kwa Mwenyezi Mungu Muumba, hivyo alikuwa na mahusiano ya karibu sana na Mola Wake Mtukufu, mahusiano ambayo yalitokana na ujuzi, mapenzi, utashi, na moyo mkunjufu, hivyo akawa ni kiigizo chema katika swala yake, funga, dua na uombaji msamaha, kiigizo ambacho kinamchorea mwanadamu njia ya ukamilifu kuelekea kwa Muumba, Mjuzi.
Mtume (s.a.w.w.) alianza harakati akiwa amebeba jukumu kubwa huku akimtegemea Mwenyezi Mungu katika kila harakati na kila jambo, hivyo akawa ni shujaa, jasiri na mkakamavu katika kulingania njia ya Mwenyezi Mungu.
Mtume (s.a.w.w.) aliishi mbali na ladha za dunia na starehe zake, hivyo alikuwa ni sehemu ya mafakiri na masikini, akishirikiana nao katika taabu zao huku akitarajia rehema za Mola Wake, mnyenyekevu Kwake, mwenye kujitenga na kila ujeuri utokanao na starehe za dunia na furaha za mapambo yake.
Maswali
1. Ni nani nabii mwarabu asiyewahi kusoma wala kuandika. Na nini makusudio ya kutowahi kusoma
wala kuandika?
2. Je, Qur’ani ni kitabu cha elimu na maarifa? Kwa nini?
3. Elezea ibada ya Mtume (s.a.w.w.) na jinsi alivyojielekeza kwa Mwenyezi Mumgu?
4. Toa sura halisi ya utegemezi na imani kubwa ya Mtume kwa Mwenyezi Mungu?
5. Elezea jinsi Mikidad alivyoelezea msimamo wa Mtume wa Mwenyezi Mungu na ushujaa
wake siku ya Uhudi?
6. Elezea utawa wa Mtume wa Mwenyezi Mungu?

REJEA
•    1. Al-Ankabuti: 48. Na An-Nahli: 103.
•    2. Al-Jum’ah: 2.
•    3. Al-A’araf: 158.
•    4. Al-Maidah: 15. Al-Ahzab: 46. An-Nisai: 174. Al-Fat’hu: 8. Az-Zukhruf: 29. Al-Aaraf: 68. Al-Ghashiyah: 21. Al-Israi: 105. Al-Maidah: 19.
•    5. Al-An’am: 163.
•    6. Amali Twusiy, Juz. 2, Uk. 141.
•    7. Biharul-An’war, Juz. 83 Uk. 16.
•    8. Akhlaqin-Nabiyyi Waadabihi, Uk. 251 na 201.
•    9. Akhlaqin-Nabiyyi Waadabihi, Uk. 251 na 201.
•    10. Sunan-Nabiyyi, Uk. 32.
•    11. Akhlaqin-Nabiyyi, Uk. 199. Sahih Bukhar, Juz. 1, Uk. 381, hadithi ya 1078.
•    12. Wasailus-Shia, Juz. 4 Uk. 309.
•    13. Sunan-Nabiyyi, Uk. 300.
•    14. Al-Kafiy, Juz. 4 Uk. 155.
•    15. Al-Mahijjatul-Baydhau, Juz. 2, Uk. 281 – 284.
•    16. Biharul-An’war, Juz. 16, Uk. 217 na 253.
•    17. Biharul-An’war, Juz. 16, Uk. 217 na 253.
•    18. Az-Zumar: 36.
•    19. Shuaraa: 217 – 219.
•    20. Riyadhu As-Swalihina ya An-Nawawiy Uk. 5. Sahihi Muslim, Juz . 4, Uk. 465.
•    21. Al-Ahzab:39.
•    22. Fadhailul-khamsa mina Sahihi sitta, Juz. 1, Uk. 138.
•    23. Al-Maghaziy Al-Waqidiy, Juz. 1, Uk. 239-240.
•    24. Taha:131.
•    25. Sunani Tirmidhiy, Juz. 4 Uk. 1518 na 508, hadithi ya 2377 na 2360.
•    26. Sahih Bukhari Juz. 5 Uk. 2371, hadithi ya 6090.
•    27. Sahih Bukhari Juz. 2 Uk. 907, hadithi ya 2428.
•    28. Sahih Bukhari Juz. 3 Uk. 1068, hadithi ya 2759.
•    29. Tabaqati ya Ibnu Saad, Juz. 1, Uk. 400.

MWISHO