TABIA NA MWONEKANO WA HITIMISHO LA MANABII 3

TABIA NA MWONEKANO WA HITIMISHO LA MANABII 3
UKARIMU
Ibnu Abbas amesema: “Mtume (s.a.w.w.) alikuwa mkarimu sana kati- ka mambo ya kheri, ukarimu wake ulikuwa ukiongezeka zaidi ndani ya mwezi wa Ramadhani……Alikuwa akikutana na Jibril ndani ya kila mwezi wa Ramadhani kila mwaka, hivyo akikutana na Jibril huwa mkarimu sana kuliko upepo uvumao.”1
Jaabir amesema: “Mtume (s.a.w.w.) hakuombwa chochote akajibu hapana.”2
Imepokewa kuwa Mtume (s.a.w.w.) alikwenda kwa muuza nguo aka- nunua kanzu kwa dirhamu nne akatoka huku kaivaa. Ghafla akatokea mtu kati ya answari na kusema: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, nivishe kanzu, hakika Mwenyezi Mungu atakuvisha nguo kati ya nguo za Peponi.”
Hapo Mtume (s.a.w.w.) akavua kanzu na kumvisha. Kisha Mtume (s.a.w.w.) akarudi dukani na kununua tena kanzu kwa dirhamu nne huku akibakiwa na dirhamu mbili. Ghafla akatokea kijakazi njiani huku akilia. Mtume akamuuliza: “Kitu gani kinakuliza?” Akjajibu: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu mabwana zangu wamenipa dirhamu mbili nikanunulie unga lakini zimepotea.” Basi hapo Mtume (s.a.w.w. ) akatoa dirhamu mbili na kumpa.
Kijakazi yule akasema: “Nahofia watanipiga.”
Mtume (s.a.w.w.) akaenda naye kwa mabwana zake, kisha Mtume (s.a.w.w.) akawatolea salamu. Wakaijua sauti yake, kisha akatoa mara ya pili, kisha mara ya tatu. Ndipo walipomjibu salamu yake. Mtume akasema: “Je mlisikia salamu yangu ya mwanzo?” Wakajibu: “Ndio, lakini tulipenda utusalimie zaidi, je ni jambo gani lililokusumbua?”
Mtume (s.a.w.w.) akajibu: “Nilimuonea huruma kijakazi huyu msije mkampiga.” Hapo bwana wake akasema: “Yeye yuko huru katika njia ya Mwenyezi Mungu, hivyo utaondoka naye.”
Hapo Mtume wa Mwenyezi Mungu akawabashiria heri na pepo kwa kusema: “Hakika Mwenyezi Mungu ametia baraka katika dirhamu kumi, kamvisha kanzu Mtume wake na mtu kati ya answari, na akam- pa uhuru mtumwa, ninamhimidi Mwenyezi Mungu, hakika Yeye ndiye aliyeturuzuku haya kwa uwezo Wake.”3
Alikuwa akiwaachia watumwa wote huru uingiapo mwezi wa Ramadhani huku akimpa kila mwombaji.4
UPOLE NA USAMEHEVU
Zaid bin Aslam amesema: “Tulipata habari kuwa Abdullah bin Salama alikuwa akisema: “Hakika sifa za Mtume wa Mwenyezi Mungu ndani ya Taurati ni: Ewe nabii hakika tumekutuma uwe shahidi, mbashiri, mwonyaji na kinga kwa wasiojua kusoma na kuandika. Wewe ni mja Wangu na Mtume Wangu, nimekuita jina la Al- Mutawakkil (Mwenye kunitegemea).
Si mkali wala si mshupavu wa moyo. Si mpiga kelele masokoni wala halipi ubaya kwa ubaya lakini husamehe. Sitomfisha mpaka ninyooshe dini iliyopinda na watu waseme: Hapana Mola wa haki isipokuwa Allah, hivyo kupitia yeye Mwenyezi Mungu afungue macho yasiyoona, masikio yasiyosikia na nyoyo zilizoziba.” Maneno hayo yalipomfikia Kaaby akasema: “Amesema kweli Abdullah bin Salama.”
Imepokewa toka kwa Aisha kuwa: “Hakika Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) hakulipiza kisasi dhidi ya jambo lolote alilotendewa binafsi isipokuwa linapovunja utukufu wa Mwenyezi Mungu. Hivyo hakukipiga kitu chochote kwa mkono wake isipokuwa akipige katika njia ya Mwenyezi Mungu. Hakuna chochote alichoombwa akanyima isipokuwa aombwe jambo la dhambi. Hakika alikuwa mbali na jambo lolote la dhambi.”5
Ubaydu bin Umayr amesema: “Hakuna jambo lolote alilofanyiwa Mtume (s.a.w.w.) lisilolazimu adhabu kisheria isipokuwa alisamehe.”6
Anas amesema: “Nilimhudumia Mtume wa Mwenyezi Mungu muda wa miaka kumi, ndani ya muda wote huo hakuwahi kunifyonza na nilipofanya jambo lolote hakuniambia: Kwa nini umefanya hivi? Na nilipoacha jambo lolote hakuwahi kuniuliza: Kwa nini umeacha?”7
Alikuja bedui na kuvuta nguo ya Mtume (s.a.w.w.) kwa nguvu mpaka upinde wa nguo ukamuumiza Mtume shingoni, kisha bedui yule akasema: “Ewe Muhammad amrisha nipewe sehemu ya mali ya Mwenyezi Mungu iliyopo kwako.”
Mtume (s.a.w.w.) akamgeukia huku akitabasamu, kisha akaamrisha apewe.
Hakika Mtume alifahamika kwa usamehevu na upole muda wote wa maisha yake…….Hivyo alimsamehe Wahshiyu muuaji wa ami yake Hamza……Alimsamehe mwanamke wa kiyahudi aliyempa nyama ya mbuzi yenye sumu. Pia alimsamehe Abu Suf’yani huku akifanya kitendo cha kuingia nyumbani mwa Abu Suf’yani ni usalama dhidi ya kuuawa. Aliwasamehe maquraishi ambao walimpiga vita kwa kila aina ya nyenzo waliyokuwa nayo……huku akiwa katika kilele cha uwezo na nguvu lakini anawaombea heri kwa kusema: “Ewe Mola Wangu! waongoze jamaa zangu, hakika wao hawajui…….Nendeni hakika nyinyi ni watu mlioachiwa huru.”
Qur’ani imeweka bayana usamehevu wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) ikaelezea hilo kwa kusema:
“Basi kwa sababu ya rehema ya Mwenyezi Mungu umekuwa mpole kwao na kama ungekuwa mkali mshupavu wa moyo wangekukimbia. Basi wasamehe na uwaombee msamaha na ushauriane nao katika mambo.”8
Na ikasema tena: “Bila shaka amekufikieni Mtume kutoka miongoni mwenu, yanamuhuzunisha yanayokutaabisheni, anakuhangaikieni, kwa waumini ni mpole, mwenye kurehemu.”9
Kwa usamehevu huu mkubwa Mtume (s.a.w.w.) aliweza kukonga nyoyo ngumu kakamavu na kuzifanya zimzunguke na kuamini utume wake wa kudumu.
HAYA:
Imepokewa kutoka kwa Abu Saad Al-Khidriy kuwa: “Mtume (s.a.w.w.) alikuwa na haya sana kuliko mtawa katika utawa wake, hivyo iwapo akichukizwa na jambo hufahamika kupitia uso wake.”10
Imepokewa kutoka kwa Ali (a.s.) kuwa: “Iwapo Mtume (s.a.w.w.) kaombwa kutenda jambo na akataka kulitenda basi husema: Ndio. Na iwapo hataki kulitenda hunyamaza kimya, wala hakuwa anasema hapana akataapo kutenda jambo.”11
UNYENYEKEVU
Imepokewa kutoka kwa Yahya bin Abi Kathiri kuwa Mtume (s.a.w.w) alisema: “Ninakula kama alavyo mtumwa, nakaa kama akaavyo mtumwa, hakika mimi ni mtumwa.”12
Siku moja Mtume (s.a.w.w.) alimsemesha mtu, basi mtu huyo akatetemeka, hapo Mtume (s.a.w.w.) akasema: “Tulia, hakika mimi si malaika isipokuwa mimi ni mtoto wa mwanamke wa kikurayshi ambaye alikuwa akila nyama kavu tu.”13
Imepokewa kutoka kwa Abu Amamah kuwa: “Mtume alitujia huku anatembelea fimbo basi tukasimama, hapo Mtume (s.a.w.w.) akasema: Msisimame kama wanavyosimama waajemi kwani baadhi yao huwatukuza wengine.”14Alikuwa akiwatania maswahaba zake isipokuwa hatamki ila la kweli.15
Pia alikuwa akiwatolea watoto salamu.16 Alishirikiana na swahaba zake katika kujenga msikiti.17
Akachimba handaki,18na mara nyingi alikuwa akiomba ushauri toka kwa maswahaba zake, japokuwa yeye ndiye aliyekuwa na akili bora kuliko watu wote.19
Mara nyingi alikuwa akisema: “Ewe Mola Wangu nipe uhai katika hali ya umaskini na unifishe nikiwa masikini. Hakika muovu wa kutupa ni yule anayekusanyikiwa na ufakiri wa dunia na adhabu ya Akhera.”20
Hii ni sura fupi sana kuhusu sifa za shakhsia ya Mtume (s.a.w.w.), na hizi ni baadhi tu ya tabia zake binafsi na za kijamii.
Pia kuna sura nyingi nzuri kuhusu mwenendo wake na sera yake kiutawala, kisiasa, kijeshi, kiuchumi na kifamilia, mwenendo ambao unahitaji masomo ya ndani zaidi ili kufuata na kuuiga, hivyo masomo hayo tunayaacha kwa ajili ya muhula ujao.
Hivyo ndivyo zilivyotubainikia sifa za pekee za Mtume Muhammad (s.a.w.w.) ambazo tunaweza kuzifupisha katika maneno yafuatayo:
Usafi wa familia, ulinzi wa Mwenyezi Mungu daima, tabia za hali ya juu, nafasi ya juu ya kijamii, maadili mema, ufasaha wa lugha, maisha mepesi, kujiepusha na kila aina ya shirki na kila aina ya mila potovu, kufikia kilele katika ibada ya Mwenyezi Mungu na unyenyekevu kwa ajili ya haki katika hali yoyote ile.
MUHTASARI
Hakika Mtume (s.a.w.w.) alikuwa mkarimu sana, hivyo alikuwa akieneza upendo, ukarimu, wema na mali kwa watu wote, huku akitoa msamaha, huruma na ulaini kwao. Ili awaokoe toka kwenye ujinga wao na apate kuwaunganisha pamoja wawe kitu kimoja.
Mtume (s.a.w.w.) alikuwa anaishi na waislam kama mmoja wao huku haya zikimtukuza kwa kumpa haiba na heshima, huku unyenyekevu ukimzidishia heshima na utukufu. Hivyo alikuwa akiwahurumia wadogo na kuwaheshimu wakubwa. Alikuwa akisikia ushauri wa mnasihi ilihali yeye ni mwenye akili zitokazo mbinguni kwa njia ya ufunuo.
MASWALI
1. Elezea jinsi Mtume (s.a.w.w.) alivyoshirikiana na ombaomba?
2. Thibitisha ukarimu wa Mtume (s.a.w.w.) kwa makafiri kwa kuonyesha matukio mbalimbali?
3. Ni sehemu gani Mtume (s.a.w.w.) alikuwa akipiga au akiacha?
4. Ni wakati gani Mtume (s.a.w.w.) alikuwa akiwasamehe wanaomkosea. Thibitisha hilo
kwa kutoa visa viwili?
5. Elezea tunavyoweza kufaidika na sifa ya kutoa msamaha tunapolingania katika njia ya
Mwenyezi Mungu?
6. Kwa nini Mwenyezi Mungu alimwamuru Mtume wake atoe msamaha na kuwaombea
maghfira watu wake?
7. Elezea jinsi Mtume (s.a.w.w.) alivyopambana na yule aliyesimama kidete kuzuia dini ya Mwenyezi
Mungu baada ya kuenea?

REJEA
•    1. Sahih Muslim, Juz. 4, Uk. 481, hadithi ya 3308. Musnadi Ahmad, Juz. 1, Uk. 598, hadithi ya 3415.
•    2. Sunanud-Daramii, Juz. 1, Uk. 34.
•    3. Al-Mu’ujam Al-Kabir cha Tabaraniy, Juz. 12 Uk. 337, hadithi ya 13607.
•    4. Hayatun-Nabii wa Siratuhu, Juz. 3 Uk. 311 na 303 na 306 na 307.
•    5. Hayatun-Nabii wa Siratuhu, Juz. 3, Uk. 311 na 303 na 306 na 307.
•    6. Sahihi Bukhari, Juz. 5 Uk. 2260, hadithi ya 5738.
•    7. Tazama: Muhammad fil-Qur’ani, Uk. 60-65.
•    8. Al Imrani: 159.
•    9. At-Tawba:128.
•    10. Sahihi Bukhari, Juz. 3 Uk. 1306, hadithi ya 23369.
•    11. Majmauz-Zawaid, Juz. 9, Uk. 13.
•    12. Tabaqat ya Ibnu Saadi, Juz. 1, Uk. 37. Majmauz-Zawaid, Juz. 9, Uk. 19.
•    13. Sunanu Ibnu Majah, Juz. 2, Uk. 1101, hadithi ya 3312.
•    14. Sunanu Abi Daudi, Juz. 4, Uk. 358, hadithi ya 5330.
•    15. Sunanut-Tirmidhiy, Juz. 4, Uk. 304, hadithi ya 1990.
•    16. Hayatun-Nabii wasiratuhu, Juz. 3, Uk. 313, kutoka kwa Ibnu Saad.
•    17. Musnad Ahmad, Juz. 3, Uk. 80.
•    18. Tabaqat cha Ibnu Saad, Juz. 1, Uk. 240.
•    19. Durul-Manthur, Juz. 2, Uk. 359. Al-Mawahibu Ad-Daniyyah, Juz. 2, Uk. 331.
•    20. Sunanut-Tirmidhiy, Juz. 4, Uk. 499, hadithi ya 2352.

MWISHO