MWONEKANO WA UTU WA IMAM ALI BIN ABU TALIB (A.S.)

MWONEKANO WA UTU WA IMAM ALI BIN ABU TALIB (A.S.)
Sifa za ukamilifu zilikusanyika kwa Imam Ali bin Abu Talib. Alikuwa na sifa nzuri za kusifika, mahsusi za kupendeza, nasaba bora na sharafu tukufu, asili takatifu na nafasi yenye kuridhiwa. Sifa ambazo hakubahatika kuzipata mtu yeyote mwingine, kwani yeye ni jemedari wa waumini, mbora wa mawasii na khalifa wa kwanza wa Mtume (s.a.w.w.) kati ya makhalifa waongozao kwa amri ya Mwenyezi Mungu.
Maelezo ya Mtume (s.a.w.w.) na Qur’ani tukufu vimeeleza wazi kuhusu umaasumu wake dhidi ya kila uchafu.1 Mtume (s.a.w.w.) akaapizana na wakristo wa Najran kupitia yeye, mkewe, na wanawe wawili.2
Pia alimfanya ni kati ya ndugu zake wa karibu ambao tumewajibishwa kuwapenda3 huku mara kwa mara Mtume (s.a.w.w.) akitueleza wazi kuwa wao ni sawa na Kitabu kitukufu,4 hivyo huokoka yule atakayevishika viwili hivyo na huangamia yule atakayeviacha.
Imam Ali bin Abu Talib (a.s.) aliishi zama za Mtume (s.a.w.w.) na utume, kuanzia pale ufunuo ulipoanza kushuka mpaka ulipokatika kwa kufariki Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) huku akiwa na nafasi ya juu ambayo hutamaniwa. Nayo ni katika kumhami Mtume (s.a.w.w.) na utume muda wote wa miaka ishirini na tatu, ikiwa ni jihadi yenye kuendelea na mapambano endelevu ya kuhami Uislamu na tukufu zake. Hivyo misimamo yake, utendaji wake na sifa zake vimejiakisi katika Aya za Kitabu kitukufu na maelezo ya hadithi za Mtukufu Mtume (s.a.w.w.).
Ibnu Abbas amesema: “Ziliteremka Aya mia tatu kuhusu fadhila za Ali (a.s.),5 hakuna Aya iliyoteremka na ibara ya: “Enyi mlioamini” isipokuwa Ali (a.s.) ndio kiongozi na mlengwa wa mwanzo katika Aya hiyo.6 Hakika Mwenyezi Mungu amewalaumu wafuasi wa Muhammad katika baadhi ya Aya za Qur’ani lakini hakumtaja Ali (a.s.) isipokuwa kwa heri.”7
Kutokana na kukithiri Aya zilizoteremka kuhusu fadhila za Ali (a.s.) baadhi ya wasomi wa zamani wameandika vitabu mahsusi ambavyo vimekusanya Aya zilizoteremshwa kwa ajili yake. Hivyo hapa tutaashiria baadhi ya Aya ambazo wanahadithi wameeleza wazi kuwa ziliteremshwa kwa ajili yake.
Imepokewa kutoka kwa Ibnu Abbas kuwa: “Ali (a.s.) alikuwa na dirhamu nne tu huku akiwa hana nyingine, hivyo usiku akatoa sadaka dirhamu moja, mchana dirhamu moja, na dirhamu nyingine akaitoa sadaka kwa siri na nyingine kwa dhahiri, hapo Mwenyezi Mungu akateremsha Aya isemayo: “Wale watoao mali zao usiku na mchana, kwa siri na dhahiri, basi wana malipo yao kwa Mola wao, wala haitakuwa khofu juu yao wala hawatahuzunika.”8
Ibnu Abbas amesema: “Ali (a.s.) alitoa sadaka pete yake huku akiwa katika hali ya rukuu. Mtume (s.a.w.w.) akamuuliza mwombaji: “Ni nani aliyekupa pete hii?” Akajibu: “Ni yule aliye katika hali ya rukuu, hapo Mwenyezi Mungu akateremsha Aya isemayo: “Hakika kiongozi wenu khasa ni Mwenyezi Mungu na Mtume wake na walioamini ambao husimamisha Swala na hutoa Zaka na hali ya kuwa wamerukuu.”9
Aya ya utakaso10 imemfanya Ali (a.s.) kuwa kati ya Ahlul-Bayt wa Mtume (s.a.w.w.) ambao wametakaswa dhidi ya kila uchafu, huku Aya ya maapizano11 ikimfanya kuwa nafsi ya Mtume (s.a.w.w.).
Ama Sura Insan imeashiria ukunjufu wa moyo aliyonao Ali (a.s.) na watu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.w.) na jinsi wanavyomwogopa Mwenyezi Mungu. Pia imebeba ushahidi wa Mwenyezi Mungu kuthibitisha kuwa wao ni watu wa peponi.12
Waandishi wa vitabu Sahihi sita na wengineo miongoni mwa wanazuoni wa hadithi wametenga milango mahsusi ndani ya vitabu vyao inayoelezea fadhila za Imam Ali (a.s.) kupitia hadithi za Mtume wa Mwenyezi Mungu.
Wanadamu ndani ya historia yao ya muda mrefu hawajamwona mtu bora kuliko Ali (a.s.) baada ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.). Wala hakuna mtu ambaye fadhila zake zimeandikwa kama zilivyoandikwa fadhila za Imam Ali (a.s.).
Japokuwa muda wote wa utawala wa kizazi cha Umayya maadui na wanafiki walimwelekezea matusi na kashfa juu ya mimbari zao wakiwa na lengo la kumtia dosari, lakini hawakupata sehemu yoyote kwake yenye dosari na aibu.
Kati ya kauli za Umar bin Al-Khatab ni: “Mtume wa Mwenyezi Mungu alisema: ‘Hakuchuma mchumaji mfano wa fadhila za Ali, kwani yeye humwongoza mfuasi wake kwenye uongofu na humzuwia dhidi ya maangamio.”13
Imam Ali (a.s.) aliulizwa: “Kwa nini wewe una Hadithi nyingi kuliko maswahaba wengine wa Mtume (s.a.w.w.)?” Akajibu: Hakika mimi nilikuwa nimuulizapo ananijibu, na ninyamazapo hunianza”.14
Imepokewa kutoka kwa Ibnu Umar kuwa: Siku Mtume (s.a.w.w.) ali- pounga undugu kati ya maswahaba zake, Ali alikuja huku macho yake yakidondoka machozi, hapo Mtume (s.a.w.w.) akamwambia Ali (a.s.): “Wewe ni ndugu yangu hapa duniani na kesho Akhera.”15
Imepokewa kutoka kwa Abu Layla Al-Ghaffariy kuwa alisema: “Nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) akisema: “Baada yangu itatokea fitina, basi ikitokea hali hiyo shikamaneni na Ali bin Abu Talib, hakika yeye ndiye wa kwanza kuniamini, na ndiye wa kwanza atakayenipa mkono siku ya Kiyama, yeye ni mkweli mno, na yeye ndiye atakayefarakisha kati ya haki na batili ya umma huu, yeye ndiye jemedari wa waumini na mali ndio jemedali wa wanafiki.”16
Makhalifa wote wamekiri kuwa Ali (a.s.) ndiye mjuzi zaidi kuliko maswahaba wote na ndiye anayefahamu sheria zaidi kuliko maswahaba wote, na kuwa laiti si Ali (a.s.) basi wangeangamia, mpaka ikafikia kauli ya Umar kuwa mfano halisi, nayo ni: “Laiti kama si Ali Umar angeangamia.”17
Imepokewa kutoka kwa Jabir bin Abdullah Al-Answar kuwa alisema: “Tulikuwa hatuwatambui wanafiki isipokuwa kwa kumchukia Ali bin Abu Talib (a.s.).”
Zilipomfikia Muawiya habari za kuuwawa Ali (a.s.) alisema: “Sheria na elimu yote imeondoka kwa kifo cha mwana wa Abu Talib.”18
As-Shaabiy amesema: “Ali bin Abu Talib ndani ya umma huu ni sawa na Masihi mwana wa Mariam kwa wana wa Israel: Kuna kundi lililompenda mpaka likakufuru ndani ya mapenzi yake, na kundi lingine likamchukia hivyo likakufuru kwa kumchukia.”19 Alikuwa mkarimu sana. Alikuwa na maadili ayapendayo Mwenyezi Mungu katika ukarimu, katu hakuwahi kumjibu mwombaji hapana sina.20
Swaa’swaa’ bin Swawhan alimwambia Ali bin Abu Talib siku aliy- opewa kiapo cha utii kuwa: “Naapa kwa Mwenyezi Mungu ewe kion- gozi wa waumini! Hakika umeupamba ukhalifa lakini wenyewe haujakupamba, umeuinua lakini wenyewe haujakuinua, na wenyewe unakuhitajia sana kuliko wewe unavyouhitajia.”
Ibnu Shabramat amesema: “Hakuna mtu yeyote asiyekuwa Ali bin Abu Talib mwenye uwezo wa kusema juu ya mimbari: ‘Niulizeni.”21
Qaaqaa bin Zararat alisimama kaburini kwa Imam Ali (a.s.) kasha akasema: “Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yako ewe kiongozi wa waumini, naapa kwa Mwenyezi Mungu kuwa hakika uhai wako ulikuwa ni ufunguo wa kheri, na laiti watu wangekukubali basi wangekula toka juu yao na toka chini ya miguu yao, lakini wao wameidharau neema na wakaijali sana dunia.”22
MUHTASARI
Imam Ali (a.s.) alijitenga kwa kuwa na sifa mahsusi ambazo zilimtofautisha na maswahaba wengine, zikamwajibisha awashinde wote waliotaka kulingana nae miongoni mwa maswahaba na wasiokuwa maswahaba. Aya za Qur’ani zimejaa fadhila hizi za pekee huku maelezo ya Mtume (s.a.w.w.) yakiashiria sifa hizi zilizomtofautisha Ali (a.s.) na wengine.
Ushahidi wa maswahaba na waliokuja baada ya maswahaba unaashiria undani wa fadhila za Ali (a.s.) ndani ya umma huu japokuwa watu wengi hawakufuata uimamu wa mtu huyu mtukufu.
MASWALI
1. Taja alama za utu wa Imam Ali (a.s.) katika nyanja za: Elimu, sheria, imani, ushujaa, ujasiri, ukaribu wake na Mtume (s.a.w.w.), haiba, unyenyekevu na kutoipenda dunia kama alivyoonekana na wenzake?
2. Je unaweza kutoa sura halisi kuhusu jinsi utu wa Imam Ali (a.s.) ulivyoathiri katika safari ya tablighi ya Mwenyezi Mungu kwa mujibu wa mtazamo wa wenzake?
3. Ikiwa fikira na rai zote zinamsifu Imam Ali (a.s.), basi ni kwa nini hakupewa haki yake?
4. Taja Aya tatu za Qur’ani zinazoashiria muhtasari wa fadhila na sifa mahsusi za Imam Ali (a.s.)?
5. Taja hadithi tatu mashuhuri za Mtume (s.a.w.w.) zinazomwinua Ali bin Abu Talib (a.s.)?
•    1. Al-Ahzab: 33
•    2. Al Imran: 61.
•    3. Shuraa: 23.
•    4. Tazama hadithi ya vizito viwili katika somo la nane.
•    5. Al-Futuhatl-Islamiyyah, Juz. 2, Uk. 516. Tarikh Baghdad, Juz. 6, Uk. 221. Sawaiqul-Muhriqah, Uk. 76. Pia tazama kitabu Shawahidut-Tanzil na Nurul-Abswar, Uk. 87 – 90.
•    6. Kashful-Ghummah, Uk. 93.
•    7. Yanabiul-Mawadda, Uk. 93.
•    8. Al-Baqarah: 274. Rejea kitabu Yanabiul-Mawadda, Uk. 93.
•    9. Al-Maidah: 55. Rejea kitabu Tafsir Tabari, Juz. 6, Uk 156. Na Tafsir Al-Baydhawiy.
•    10. Al-Ahzab: 33. Rejea Sahihi Muslim, fadhila za maswahaba.
•    11. Al Imran: 61. Sahihi Tirmidhiy, Juz. 2, Uk. 300.
•    12. Al-Kashafu cha Az-Zamakhshar. Ar-Riyadh an-Nadhrah cha Tabariy, Juz. 2, Uk. 207.
•    13. Ar-Riyadh an-Nadhrah cha Tabariy, Juz. 1, Uk. 166.
•    14. Tabaqat cha Ibnu Saad, Juz. 2 Uk. 338. Hilyatul-Awliyai, Juz. 1, Uk. 68.
•    15. Sunan Tirmidhiy, Juz. 5 Uk 595, hadithi ya 3720.
•    16. Al-Isabat cha Ibnu Hajar, Juz. 4, Uk. 171, namba 994. Majmauz-Zawaid, Juz. 1, Uk 102.
•    17. Sharhu Nahjul-Balagha, Juz. 1, Uk. 6. Tadhkiratul-Khuwas, Uk. 87.
•    18. Al-Istiab pambizoni mwa Al-Isabat, Juz. 3, Uk. 45.
•    19. Al-Aqdu Al-Farid, Juz. 2, Uk. 216.
•    20. Sharhu Nahjul-Balaghah, Juz. 1, Uk. 7.
•    21. Aayanus-Shia, Juz. 3, kifungu cha 1 Uk. 103
•    22. Tarikh Yaaqubiy, Juz. 2, Uk. 213

MWISHO