URITHI WA IMAM ALI (A.S.)

URITHI WA IMAM ALI (A.S.)
Baada ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.) hatupati hazina kubwa yenye rutuba iliyokamilika na iliyo maarufu kama hazina aliyoiacha Imam Ali bin Abu Talib (a.s.). Na ya kwanza ni hazina inayojulikana kwa jina la kilele cha fasaha, yaani Nahjul-balaghah. Ya pili ni ijulikanayo kwa jina la hekima bora na makusudio ya maneno, yaani Ghurarul- Hikam wa Durarul-Kalim.
Kamusi za maudhui ya vitabu hivi viwili vya thamani zimetupa sura ya wazi na halisi kuhusu ukubwa na upana wa hazina hii. Kuanzia ujazo wake, kina chake hadi mjumuisho wake uliojumuisha sekta mbalimbali za maisha ya mwanadamu, kuanzia kijamii hadi mtu mmoja mmoja.
Sisi hapa tumechagua toka kwenye hazina hii kubwa maudhui mbili muhimu zenye uhusiano wa karibu na mtu mmoja mmoja hadi jamii nzima.
HALI HALISI YA WEMA NA UOVU
Akhera ndio kufaulu kwa watu wema.
Tutakaposimama mbele ya Mwenyezi Mungu ndipo wema na uovu utabainika.
Utamu wa Akhera huondoa makali ya uchungu wa mateso ya dunia.
MTU MWEMA
Mwema ni yule anapoogopa adhabu hujisalimisha, na anapotarajia thawabu hutenda mema. Inatosha mtu kuwa mwema kwa kuaminiwa katika mambo ya dini na dunia.
Ni mwema wa hali ya juu sana yule ambaye moyo wake umekutanishwa na ubaridi wa yakini. Hawi mwema ambaye ndugu zake ni waovu. Mwema ni yule anayedharau asichokipata.
VINAVYOPELEKEA MTU KUWA MWEMA
AKILI NA MAARIFA
Atakayeuwa ujinga wake kwa kutumia elimu yake basi amefaulu kwa kupata hadhi ya juu ya wema. Atakayemfahamu vizuri Mwenyezi Mungu basi daima hatokuwa muovu.
IKHLASI NA UTIIFU KWA MWENYEZI MUNGU
Atakayemtii Mwenyezi Mungu milele hatokuwa muovu. Mtu huwa hawi mwema isipokuwa kwa kumtii Mwenyezi Mungu. Mwema ni yule ambaye utiifu wake una ikhlasi.
Harakisha kutii utakuwa mwema. Mtu yeyote hawi mwema isipokuwa kwa kusimamisha sheria za Mmwenyezi Mungu.
Kukesha usiku katika hali ya kumtii Mwenyezi Mungu ni mavuno ya mawalii na ni bustani ya watu wema. Mkesho wa macho kwa kumtaja Mwenyezi Mungu ni fursa ya watu wema na utakaso wa mawalii.
BIDII KATIKA KUITENGENEZA NAFSI
Atakayepiga vita nafsi yake katika kutafuta wema wake basi atakuwa mwema.Hakika nafsi ambayo inajitahidi kung’oa mabaki ya matakwa itapata inalolitafuta na itapata wema katika marejeo yake.
JIHADI KATIKA NJIA YA MWENYEZI MUNGU
Jihadi ni nguzo ya dini na njia ya watu wema.
UTAWA DHIDI YA DUNIA ISIYODUMU
Hakika dunia hutolewa na hukataliwa, hivyo watu wema huachana nayo, huku waovu huitamani. Jiepushe na dunia utapata wema katika marejeo yako na yatakuwa mema mafikio yako.
Watakaopata wema wa dunia kesho ni wale wanaoikimbia leo.
Ikiwa kweli mnatafuta neema basi ziacheni huru nafsi zenu toka nyumba ya uovu.
UZURI WA KUJIANDAA NA KIFO
Jitahadhari na mauti, yaandalie maandalizi mazuri utapata wema kati- ka marejeo yako.
Kifo kina raha kwa watu wema.
KUITATHMINI NAFSI
Atakayeitathmini nafsi yake atakuwa mwema.
KUKITAFUTA KILICHOKUPOTEA
Kutafuta mwishoni mwa umri wako kile ulichokipoteza mwanzoni mwa umri wako hukufanya uwe mwema katika marejeo yako.
KUKAA NA WANAVYUONI
Kaa na wanavyuoni uwe mwema.
KUTOA KATIKA NJIA YA MWENYEZI MUNGU
Mkarimu husifiwa hapa duniani na hupata mema huko Akhera. Ukitoa mali yako kwa ajili ya Akhera yako kisha ukamwachia Mwenyezi Mungu yule aliyekuja baada yako, utakuwa umepata wema kwa yale uliyotoa na umeutendea wema urithi wako kwa yule uliyemwachia.
ALIYE MWEMA KULIKO WENGINE
Ukitamani kuwa mwema kuliko wengine basi yafanyie kazi yale uliyoyajua.
Mwema zaidi kwenye kheri ni yule anayetenda kheri.
Mwema zaidi kuliko watu wengine ni yule muumini mwenye akili. Mwema kuliko watu wengine ni yule mwenye kujihukumu mwenyewe kwa kumtii Mwenyezi Mungu.
Mwema zaidi kuliko watu wote duniani ni yule mwenye kuiacha dunia, na mwema zaidi huko Akhera ni mwenye kutenda kwa ajili ya Akhera.
Mwema zaidi kuliko watu wote ni yule atakayejua fadhila zetu na akajikurubisha kwa Mwenyezi Mungu kupitia sisi. Akawa na mapenzi ya dhati kwetu, akatenda yale tuliyohimiza na kuamrisha, akaacha yale tuliyokataza, basi mtu kama huyo ni katika sisi na yeye atakuwa pamoja nasi katika nyumba ya kudumu.
MTU MWOVU
Atakayetegemea dunia ndio mwovu asiye na kitu.
ALAMA ZA MWOVU
Miongoni mwa uovu ni mtu kuzuia dini yake kupitia dunia yake. Miongoni mwa alama za uovu ni kuwatendea ubaya watu wema. Miongoni mwa alama za uovu ni kumlaghai rafiki.
VINAVYOSABABISHA UOVU
Upumbavu ni uovu. Nia mbaya ni uovu. Kulimbikiza haramu ni uovu.
Mtu hawi mwovu isipokuwa kwa kumwasi Mwenyezi Mungu. Miongoni mwa uovu wa mtu ni shaka kuharibu yakini yake. Sababu ya uovu ni kuipenda mno dunia.
Yule ambaye lengo lake ni dunia basi Siku ya Kiyama uovu wake utarefuka.
Matokeo ya husda ni uovu wa dunia na Akhera. Kupenda mali na shari husababisha uovu na udhalili.
Kitendo cha mtu kudhulumu hapa duniani ni anwani ya uovu wake huko Akhera.1
MUHTSARI
Qur’ani imetilia umuhimu mambo yote yanayohusu maisha na mus- takabali wa mwanadamu, hivyo Mtume (s.a.w.w.) na kizazi chake nao wakafuata njia hiyo ya Qur’ani, wakisimama imara kutafsiri makusudio ya Qur’ani na kubainisha ishara na alama zake.
Suala la wema na uovu ni suala la mwanzo kabisa walilotilia umuhimu na kuliashiria, hivyo wakafafanua kipimo cha wema na uovu huku wakifafanua alama na mwonekano wa mtu mwema na mtu mwovu. Waligusia vinavyosababisha wema na uovu, hivyo kwa maelezo hayo wakatoa mfumo kamili wa ukamilifu wa mwanadamu katika maisha.
MASWALI
1. Kutokana na maneno ya Imam Ali (a.s.) ni kipi kipimo cha wema?
2. Kwa mtazamo wa Imam Ali (a.s.) ni yupi aliye mwema?
3. Elezea jinsi wema unavyopatikana?
4. Ni nani aliye mwema kuliko watu wote?
5. Ni vitu gani vinavyompelekea mtu kuwa mwovu, na ni zipi alama za uovu?
•    1. Tazama Ghurarul-Hikam Wadurarul-Kalim cha Al-Amidiy.

MWISHO