MAIMAMU WA SHIA KATIKA UANDIKAJI NA UENEZAJI WA HADITH

MAIMAMU WA SHIA KATIKA UANDIKAJI NA UENEZAJI WA HADITH
Katika sehemu hii, twategemea kuzungumzia kwa mukhtasari msimamo wa Shia kuhusu uandikaji wa Hadith kutokea mwanzoni. Itaonekana kuwa ni kinyume na msimamo wa wengine kuhusu swala hili. Msimamo wa Kishia ulisisitiza mno juu ya uandikaji wa Hadith zikisaidia uhifadhi wake wakati ambapo Maulamaa mashuhuri wa Kisunni, hata kufikia mwanzoni mwa karne ya 3A.H./9 A.D. walikuwa wakipinga uandikaji wa Hadith. Ni baada ya uandikaji wa Hadith ulipokuwa dhahiri hao wanaopinga walipoanza kwenda kinyume na Hadith walizokuwa wamezitoa wakipinga uandishi na uenezaji wake na hapo wakaanza kuziandika.
Alba ibn al-Ahmad ananakili kuwa mara moja ‘Ali ibn Abi Talib a.s. wakati akitoa Hotuba juu ya mimbar, alibainisha: "Je, ni nani atakayeinunua elimu kwa Dirhamu moja?" Al-Harith ibn al-A’war alinunua karatasi yenye thamani ya Dirhamu moja na kumwijia Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. na kuandika kiasi cha kutosha cha elimu juu yake.1 Riwaya hii inatuonyesha vile Imam a.s. alivyokuwa akisisitiza juu ya uandikaji.
Imam Hassan ibn ‘Ali ibn Abi Talib a.s. ameripotiwa akiwashauri watoto wake kama ifuatavyo:-
"Nyinyi sasa ni watoto wa Ummah ambao katika maisha ya mbeleni mtakuwa wakubwa wao. Jielimisheni Elimu; na yeyote yule miongoni mwenu atakayeweza kuhifadhi (kukariri) elimu (yaani Hadith), basi aiandike na kuiweka nyumbani mwake."2
Imeripotiwa kuwa Hujr ibn Adi, mmoja wa Sahaba wa Mtume s.a.w.w. na Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s., aliziandika Hadith za Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. katika kitabu na kuzirejea pale alipohitaji msaada wa mwongozo katika masuala mbalimbali 3 Mifano hii inadhihirisha umuhimu aliokuwa ameuambatanisha Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s., watoto wake na Sahaba wake katika uandikaji wa Hadith. Mifano miwili ifuatayo itaonyesha dhahiri vile Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. alivyokuwa akisisitiza umuhimu wa Hadith na kuzihifadhi.
Umar ibn ‘Ali anaripoti kuwa mtu mmoja alimwuliza Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. ni vipi kuwa yeye (yaani ‘Ali) aliweza kunakili na kusimulia Hadith nyingi za Mtume s.a.w.w. kuliko Masahaba wengineo. Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. alijibu: "Hii ni kwa sababu daima nilipokuwa nikimwuliza swali Mtume s.a.w.w., alikuwa akinijibu maswali yangu. Na pale nilipokuwa nikiwa kimya, basi Mtume s.a.w.w. alianzisha mazungumzo mwenyewe." 4
‘Ali ibn Hawshab anaripoti kutoka Makhul, mwanachuo kutokea Syria, kuwa Mtume s.a.w.w. aliisoma Ayah (69:12)
لِنَجْعَلَهَا لَكُمْ تَذْكِرَةً وَتَعِيَهَا أُذُنٌ وَاعِيَةٌ
Ili tufanye hilo kuwa ni kumbusho kwenu na sikio linalosilia liyahifadhi
Na hapo alimwambia Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. "Mimi nimemwomba Allah swt kuwa masikio hayo yawe ni yako." Baadaye Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. alisema: "Mimi kamwe sikusahau Hadith yoyote au chochote kile kilichosikilizwa na sikio langu kikisemwa na Mtume s.a.w.w. 5
Umar ibn al-Harith anasema:
"Wakati mmoja ‘Ali a.s. aliuelekeza uso wake kuelekea mbinguni na kuurudisha chini akisema:"Mwenyezi Mungu na Mtume wake s.a.w.w. wamesema kweli."
"Je, kilikuwa nini?" Kikundi cha watu kiliuliza.
Imam Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. alisema: "Mimi ni mpiganaji wa vita na vita vinarithishia mtu ulaghai. Vivyo hivyo, ninaweza kukubali iwapo nitaporomoka kutokea mbinguni kwa ajili ya kunaswa na ndege kuliko kumsingizia uwongo Mtume wa Allah swt. Kwa hivyo fuateni chochote kile mukisikiacho kikitoka kwangu........" 6
Kauli juu ya uandishi wa Hadith pia zimenakiliwa kutoka Maimamu wengine.
Al-Imam al-Sadiq a.s. alisema:
"Andikeni na kuieneza elimu yenu miongoni mwa ndugu zenu, na iwapo mtafariki basi watoto wenu watarithi vitabu vyenu. Itafika siku ambapo patatokea machafuko na hapatakuwapo na mtu wa kumfanya rafiki na wala hapatakuwa na chochote cha kuweza kutegemewa isipokuwa ni vitabu tu...7
Al-Imam al-Sadiq a.s. pia amenakiliwa kwa kusema: “Hifadheni vitabu vyenu kwani mutakuja kuvihitaji hivyo siku moja." Vile vile ameripotiwa akisema kuwa nguvu za moyo na kuhifadhi akilini inategemea mno juu ya maandishi.8
Abu Basir anaripoti kuwa aliambiwa na Imam al-Sadiq a.s.: "Baadhi ya watu waliotoka Basrah walikuwa wakija na kuniuliza kuhusu Hadith na waliziandika. Je, kwa nini nawe hauziandiki?" Na aliongezea kusema, "Elewa wazi wazi kuwa wewe kamwe hautaweza kuhifadhi Hadith bila ya kuiandika."9
Idadi kubwa ya mapokezi yanaonyesha kuwa Maimamu a.s. walikuwa navyo vitabu na maandishi ambavyo walirithi kutoka vizazi vilivyowatangulia.10
Katika riwaya nyingine Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. ameripotiwa akiwa amesema: “Ikamateni elimu (kwa kuiandika),” ambavyo aliirejea mara mbili 11 Imeripotiwa kutoka Ja'bir kuwa Abu Hanifa alikuwa akimwita al-Imam al-Sadiq a.s. "Kutubi" (yaani mwenye vitabu) kwa sababu ya kutumia mno vitabu, na Imam a.s. alifurahishwa kwa jina kama hilo. 12
Vile vile imeripotiwa kuwa al-Imam Muhammad ibn ‘Ali al-Baqir a.s. ameziandika Hadith za Mtume s.a.w.w. ambazo zilikuwa zikinakiliwa na Jaabir ibn Abdullah Ansaari. 13
(Ingawaje taarifa hii inaonyesha kuwa siyo ya ukweli kwani Jaabir alikuwa ameshakwisha kufariki wakati Imam a.s. alikuwa na umri wa miaka mitano tu, labda inawezekana kuwa Hadith ziliandikwa na mjumbe).
•    1. *Tabaqat al-Kubra , j. 6, uk.168,; Taqyid al-'ilm , uk. 89,90; Kanz al-‘ummal, j. 10, uk. 156; Rabi’
al-Abrar, j.. 3 , uk. 294
•    2. Bihar al- Anwar, vol. 2 uk. 152; al- Taratib al - idariyyah vol. 2, uk. 246; Sunan al - Darimi, vol 1, uk.
130; Ilal al - Hadith, vol. 2, uk. 438; Taqiyyad al - Ilm, uk. 91; Jami’bayan al - ‘ilm, uk.99; Kanz
jumat al - Imam al - Hasan min Tarikh Dimashq, uk. 167.
•    3. Al - Tabaqat all- Kubra, vol. 6 uk.220.
•    4. Ansab al - ashraf, vol. 2 uk.98; na Hadith no. 1980 kutokea maisha ya Imam ‘Ali (a.s.) katika Tarikh
Dimashq Historia ya Damascus); Bihar al- Anwar, vol.2 uk. 230; al - Fadhail ya Ibn Hanbal, Hadith
no. 222.
•    5. Ansab al - Ashraf, vol. 1, uk. 121; Tarikh Dameshq, vol. 38, uk. 202; Hilyat al - awliya, vol. 1, uk. 67;
Shawahid al - tanzil, Hadith no. 1009.
•    6. Ansab al - Ashraf, vol. 2, uk. 145.
•    7. Bihar al - Anwar, vol. 2 uk. 50 kutoke ashf al - Mahajjah.
•    8. Bihar al - Anwar, vol. 2, uk. 152.
•    9. Bihar al - Anwar, vol. 2, uk 153.
•    10. Kwa ajili ya kutaka kuelezwa zaidi juu ya Hadith zizungumziazo swala hili urejea Makatib al –
Rasul, vol. 1, uk. 71 na 89 iliyoandikwa na ‘Ali Ahmad Miyanji.
•    11. Taqyid al - ilm, uk. 89.
•    12. Rawdhat al - Jannah, vol. 8, uk. 169.
•    13. Taqyid al - Ilm, uk. 104.

MWISHO