SALA NA ATHARI ZAKE

SALA NA ATHARI ZAKE
17. Amesema Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w., Man la Yahdhurul Faqihi, J.1, Uk. 206:
“Mtu yeyote aichukuliaye sala pasi na uzito wake, basi hatokani nami. Hapana, Kwa kiapo cha Allah swt, mtu kama huyo hatafikia chemchemi ya Haudh Kawthar”
18. Amesema Al-Imam Ja’far as-Sadiq a.s., katika Bihar al-Anwaar, Juzuu 82, Ukurasa 236:
“Iwapo kutakuwapo na mto unaopita nyumbani mwa mtu ambamo mtu huyo anaoga mara tano kwa siku, je kutabakiapo aina yoyote ya uchafu mwilini mwake ? Kwa hivyo sala ndivyo ilivyo mfano wa mto huo. Mtu ambaye anasali sala zake basi hujiondolea madhambi yake yote isipokuwa kutabakia madhambi yale ambayo yanamtoa katika Imani yake.
19. Amesema Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w., katika Bihar-ul-Anwaar, J.99, Uk. 14:
“Sala iliyofaradhishwa kwa Allah swt ni sawa na kutimiza Hajj elfu moja na ‘Umrah elfu moja ambazo ni sahihi na zilizokubalika.”
20. Amesema Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w., katika Bihar-al-Anwaar, J.83, Uk. 14:
“Kamwe musizipoteze sala zenu, kwa hakika, mtu yeyote anayezipoteza nyakati za sala zake atainuliwa pamoja na Qarun na Hamaan na itamwia haki Allah swt awatumbukize katika moto wa Jahannam pamoja na Munafiqiin (wanafiki).
21. Amesema Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. Bihar-ul Anwaar, Juzuu 69, Uk. 408:
“Musali sala zenu kama kwamba hiyo ndiyo sala yenu ya mwisho”
22. Amesema Amir-ul-Muminiin Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. Tasnif-I-Gurar ul-Hikam, Uk.175:
“Iwapo mwenye kusali angalikuwa akifahamu kiasi alichozungukwa na rehema za Allah swt, basi kamwe asingaliinua kichwa chake kutoka hali ya kusujudu”
23. Amesema Al-Imam Al-Muhammad al-Baqir a.s., katika Bihar al-Anwaar, J.7, Uk. 267:
“Siku ya Qiyama, jambo la kwanza litakalo hisabiwa ni kuhusu sala; kwa hivyo, iwapo itakuwa imekubaliwa, basi matendo mengine pia yatakuwa yamekubaliwa (ama sivyo matendo yake mengine mema hayatamnusuru)”.
24. Amesema Al-Imam Al-Sadiq a.s. , Bihar Al-Anwaar, J.82,Uk. 236:
Katika siku za mwishoni mwa maisha yake, Imam As-Sadiq a.s. aliwaita Jama’a na wafuasi wake na kuwaambia “Kwa hakika, Uokovu wetu hautamfikia yule aichukuliaye sala kiepesi (bila ya kuichukulia kuwa ndiyo fardhi na lazima)”
25. Amesema Al-Imam Al-Muhammad al-Baqir a.s. , Al-Khisaal cha Sadduq, Uk. 432:
“Yapo mambo kumi ambayo mtu atakapokutana na Allah swt siku ya Qiyama ataingia Peponi:
1. Kuamini na kukiri kuwa hakuna Allah swt mwingine isipokuwa Allah swt,
2. Na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allah swt
3. Kukiri na kuamini kuwa kile kilichoteremshwa juu ya Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w.w.kutokea Allah swt ni Qur’an tukufu,
4. Kutimiza sala
5. Kutoa Zaka
6. Kufunga saumu mwezi wa Ramadhani,
7. Kuhiji Makkah,
8. Kuwatendea mema wale wampendao Allah swt,
9. Kujiepusha na maadui wa Allah swt,
10. Na kujiepusha mbali na ulevi wa kila aina.
26. Amesema Amir-ul-Muminiin Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s., katka Nahjul Balagha, Msemo 136:
“Kwa kila mwenye kusali, sala ndiyo sababu kubwa ya kumfanya amkaribie Allah swt,; na kwa yule aliye dhaifu, Hajj – kuhijji Makkah – ni sawa kabisa na Jihadi – kupigana katika njia ya Allah swt. Kwa kila jambo kuna zaka yake, na hivyo zaka ya mwili ni saumu. Jihadi ya mwanamke ni kuwa mwenzi mwema wa mume wake.”
27. Amesema Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. , ‘Irshad-ul-Qulub, Uk. 53:
“Hakuna usiku unaopita isipokuwa Malaika wa Mauti huwaita ‘enyi watu wa maqaburi!’ na huwauliza kile kinachowasikitisha kwa siku hiyo kwa yale waliyoyaona na maisha yajayo. Kwa hapo wafu husema ‘kwa hakika, sisi twasikitika na kuwaonea wivu muminiin wale ambao wapo misikitini mwao ambapo wao wapo wanasali wakati sisi hatusali; wao wanatoa zaka wakati sisi hatutoi; wao wanafunga mwezi wa Ramadhan wakati ambapo sisi hatufungi; wao wanatoa misaada kwa kile walichonacho ziada ya familia yao, wakati sisi hatufanyi hivyo; ….”
28. Amesema Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w., Mustadrak-ul-Wasa’il, J.3, Uk.102:
“Kwa kila wakati uliyofanywa muayyan (uliopangwa) kwa ajili ya sala , mimi huwa ninamsikia mpiga mbiu ambaye huita na kusema ‘Enyi wana wa Adam ! Dumisheni sala ili muweze kuuzima moto ambao nyinyi wenyewe muliuwasha kwa ajili yenu (kwa kutenda madhambi).”
29. Amesema Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w., Bihar-ul-Anwaar, J.82, Uk.202:
“Lazima muwe waangalifu wa Sala, kwani siku ya Qiyama Allah swt atakapomsimamisha mja wake (kwa hisabu) basi jambo la kwanza la kuulizwa litakuwa ni kuhusu Sala. Iwapo mtu atakuwa amekujanayo kamilifu, basi atakuwa miongoni mwa watu waliookoka, ama sivyo, atatupwa Motoni (Jahannam).”
30. Abu Basir Amesema kuwa Wasa’il-ush-Shiah, J.4, Uk. 26:
Yeye alimtembelea Umm-i-Hamidah (mama yake Imam Musa ibn Ja’far a.s.), kwa ajili ya kumpa pole kwa kifo cha Ja’far ibn Muhammad a.s. Yeye alilia na hivyo yeye pia alilia kwa sababu ya kilio cha mama huyo. Baadaye, mama yake al-Imam a.s. alisema,
“Ewe Aba Muhammad! Iwapo ungalikuwa umemwona Ja’far ibn Muhammad alipokuwa kitandani wakati wa kufariki, basi ungalikuwa umejionea mambo ya ajabu kabisa: Yeye alifumua macho yake na kutaka majamaa wote wakusanyw. Majamaa wote walikusanyika bila ya kubaki mtu. Hapo al-Imam a.s. alisema kwa kuwaangalia wote: “Kwa hakika, Uokovu wetu hautamfikia yule aichukuliaye Sala kiepesi (bila ya kuichukulia kuwa ndiyo fardhi na lazima)”
31. Amesema Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. , Bihar-ul-Anwaar, J.84, Uk.258:
“Ibada ya yule mtu ambaye mapato yake yanatokana na njia zilizo haramu ni sawa na kujenga nyumba juu ya mchanga."

MWISHO