Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

MALAIKA: HARUT NA MARUT

0 Voti 00.0 / 5

MALAIKA: HARUT NA MARUT
Imepokelewa riwaya kutoka kwa Imam Muhammad al-Baquir a.s. kuwa:
Baada ya kifo cha Mtume Sulayman bin Daud a.s., Ibilisi alitengeneza uchawi na kuuviringa na nyuma yake aliandika kuwa mzigo huu umetengenezwa na Asif bin Barkhiyyah kwa ajili ya ufalme wa Mtume Suleyman, na kwamba imetolewa kutoka hazina ya ilimu. Na kwa nguvu zake kila jambo linawezekana. Na baada ya hapo aliifukia chini ya kiti cha Mtume Sulayman a.s. Na baadaye aliifukua chini ya kiti hicho na kuidhihirisha mbele ya watu wa zama hizo. Kwa kuyaona hayo, wale waliokuwa Makafiri walianza kusema kuwa Mtume Suleyman a.s. aliweza kuwatawala kwa uchawi lakini wale waliokuwa Mumin walikuwa wakisema kuwa Mtume Sulayman a.s. alikuwa ni Mtume wa Allah swt na mwenye taqwa. Allah swt anatuambia kuwa ni Sheitani ndiye asemaye kuwa Mtume Suleyman a.s. alikuwa ni mchawi. Na jambo hilo ndilo walilolifuata na kuliamini Mayahudi. Lakini Mtume Suleyman a.s. kamwe hakufanya tendo lolote la kukufuru au la ushirikina hivyo kamwe hawezi kuwa mchawi. Wale wanaohalalisha uchawi ni makafiri kwa sababu Masheitani walikuwa wakifanya uchawi na kuwafundisha watu uchawi na ushirikina.
Baada ya kupita zama za Mtune Nuh a.s., kulikuja zama moja ambamo wakazi wake walikuwa wakijishughulisha mno na mambo ya uchawi na ushirikina, kwa sababu ya kufuata imani hizo zilizopotofu, kulikuwa kukitendeka matendo maovu kabisa. Hivyo wakazi walikuwa wameupuuzia Uislamu, na kwa hayo Allah swt aliwatuma malaika wawili waliokuwa wakiitwa Harut na Marut, ambao walitumwa katika mji uitwao Babul, katika maumbile ya mwanadamu ili waweze kuwazuia wanadamu wasiendelee na uchawi na ushirikina uliokuwa umepindukia kiasi.
Malaika hao walitii amri ya Allah swt na walimwelezea Mtume wa zama hizo kuwa uwafundishe mambo fulani fulani wakazi wako ili waweze kujiepusha na uchawi na ushirikina huo uliokuwa umewapotosha kabisa. Basi Mtume huyo aliwaambia watu wake kuwa wajifunze mafunzo hayo makhsusi ili waweze kujiepushe na uchawi na kamwe wasiwatendee chochote wenzao. Allah swt anatuambia kuwa katika mji huo wa Babul kulikuwapo na Mayahudi ambao wao kwa hakika walikuwa wakitenda kinyume na kile walichokuwa wakiambiwa na Mtume huyo, yaani wao badala ya kuutokomeza uchawi, wao ndio wakawa waabudu wa uchawi na wakawa wakifanya uchawi. Malaika wakawaambia sisi tunawafundisheni haya kwa ajili ya kutaka kuwajaribu na kuwajua wale waliona imani ya kurudi kwa Allah swt na hivyo kujiepusha na uchawi. Na kutaka kuwatambua wale walioasi na kutumia ilimu hii kwa ajili ya kuwadhuru wengine.
Hapo ndipo watu walikuwa wakijifunza uchawi za aina zote mbili yaani watu hao walikuwa wakijifunza uchawi uliokuwa umezuliwa na Shaytani kwa jina la Asif bin Barkhiyyah na ilimu waliofundishwa na Mtume Suleyman a.s. kwa ajili ya kujikinga na uchawi wa aina yoyote. Wao walikuwa wakijifunza uchawi hata wa kuwatenganisha mume na mke wake na walikuwa wakiwapatia hasara kubwa sana watu. Kwa hakika sote tunaelewa kuwa Allah swt kamwe hapendezewi na matendo kama haya na hivyo huwaadhibu wale wote wanaojishughulisha na matendo maovu kama haya ya Sihri. Katika Ayah hapa panazungumziwa neno idhn ingawaje kunamaanisha bila ya ruhusa ya Allah swt, lakini wanazuoni wanasema kuwa kuna maana nyingi na kwa neno idhn hapa kunamaanishwa ilimu yaani kujua, hivyo Allah swt anayajua yote yanayotendeka. Iwapo sisi tutachukulia maana ya idhn kuwa ni idhini basi kumwua Mtume na kumdhulumu haki zake ni kwa idhini yake Allah swt. Na kwa hakika Allah swt si dhalimu na hivyo hawezi kamwe kuwafanyisha watu mambo yoyote yaliyo batili.
Na hapo anasema kuwa wao wanajifunza mambo ambayo yatawaletea hasara siku ya Qiyama na wala hawapati faida ndani mwake katika Dini na duniya. Kwa uhakika hao Mayahudi wana fahamu kuwa mtu yeyote aiachayo Dini ya Allah swt kwa badili ya kuchukulia uchawi, kwake hana faida ya aina yoyote huko Akhera na kamwe hawatapata uokovu kutokea adhabu za Jahannamu. Hivyo wao kwa makusudi wamejichukulia adhabu za Jahannam na kwa hayo wao kwa hakika wameziuza nafsi zao. Ni mambo maovu kabisa. Iwapo wao walitambua ubaya wa mambo hayo basi wao kamwe hawakufuata kiasi chochote walichokuwa wameelewa na hivyo watambue kuwa ni sawa na kutojua chochote.
HABARI NYINGINE ISEMAYO
Wengi wanasema kuwa Harut na Marut ni Malaika waliokuwa wametumwa na Allah swt. Wao walikusanyika katika nyumba ya mwanamke mmoja na humo walikunywa pombe, wakaua na kuabudu miungu na kwa hayo wameadhibiwa adhabu ya kuning’inizwa katika kisima kimoja kilichokuwa kikijulikana kwa jina la Babul.
Kwa hakika masimulizi kama haya hayana uhakika wowote kwa masimulizi kama haya yanapotosha na ni yenye kuzuliwa kwani ni kinyume na akili zetu. Kwa sababu Malaika ni viumbe wasio na wala hawatendi madhambi ya aina yoyote ile.
Katika ‘Uyunul Akhbar al-Ridha ni mashuhuri kuwa mtu mmoja alimwuliza Imam al-Ridha a.s. kuwa nimesikia kwamba dunia ilipojaa madhambi na maovu, basi Allah swt aliwatuma Malaika Harut na Marut kama makhalifa na kuwatuma duniani. Vile vile inasemekana kuwa wao walifanya mapenzi pamoja na mwanamke mmoja aliyejulikana kwa jina la Zehra, na pia walikunywa pombe, wakaabudu miungu, wakaua na kuzini, walizini. Ewe Mjukuu wa Mtume s.a.w.w., unasemaje kuhusu habari hizi ?
MALAIKA HAWAKUFURU
Kwa kuyasikia hayo, Imam a.s. alijibu Madhallah! Si hivyo kwani Malaika ni viumbe visivyo na makosa na wapo mbali na kufuru na maovu. Imam a.s. aliwathibitishia hao kuwa Malaika ni viumbe visivyo na kasoro zozote kwa Ayah za Qur’an na kuwaambia kuwa nyinyi ni lazima muamini kuwa Allah swt aliwatuma hao Malaika katika maumbile ya mwanadamu ili waweze kuwaonya na kuwaonyesha wanaadamu kuhusu uchawi uliokuwa ukiendelea katika zama zao. Kwa kifupi Malaika hawatendi makosa ya aina yoyote.
Kwa hayo watu waliuliza,
“Ewe Imam wetu ! Iwapo Malaika hawatendi makosa, sasa je Ibilisi Sheitani hakuwa Malaika?”
Basi Imam a.s. aliwajibu kuwa
“Yeye alikuwa ni Jinn na hayo yamesemwa katika Qur’an Tukufu”.
NASIHA
Inatubidi sisi tuisome Qur’an tukufu na kuielewa maana ya Ayah zilizomo na kujaribu kujifunza kutokana na kusoma kwetu ili tuweze kuishi vile Allah swt atutakavyo na tujiepushe pamoja na maovu ambayo ndiyo sababu kuu za maangamizo na mateketezo yetu. Vile vile tuwe na tahadhari ya masimulizi na maelezo ya mufassirina wengine ambao wanaweza kutupotosha kwani maelezo yao yanapingana pamoja na Ayah za Qur’an Tukufu pamoja na masimulizi tuliyoyapata kutoka kwa Mtume s.a.w.w. pamoja na Aimma Toharifu a.s.

MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini