Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

PEPO ( JANNAT ) YA SHADDAD

0 Voti 00.0 / 5

PEPO ( JANNAT ) YA SHADDAD
JE SHADDAD NI NANI …
Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alipokwenda katika Mi’raj alikutana na Malakul Mauti. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alimwuliza :
“Je ni wakatigani ambapo wewe kwa hakika ulisikitika katika kutoa roho ya wanaadamu ?”
Kwa hayo Malakul Maut akajibu :
“Ewe Mtume wa Allah swt !
Zipo nyakati mbili tu ambapo mimi kwa hakika nilisikitika mno wakati wa kutoa Roho nazo ni, kwanza kulikuwa na jahazi moja iliyokuwa baharini ikiwa na wasafiri walikuwamo humo, na Allah swt aliniamrisha kuipindua jahazi hiyo na kuzitoa roho zote za wasafiri waliokuwamo isipokuwa mwanamke mmoja aliyekuwa ana mimba. Nami nikafanya hivyo hivyo nilivyoamrishwa.
Mwanamke huyo aliweza kuelea kwa msaada wa ubao alioupata wakati wa kuzama. Wakati mwanamke huyo anaelea, alimzaa mtoto, ndiye aliyeitwa Shaddad. Alipomzaa mtoto huyo, mama huyo akafa( hapa niliposikitika wakati wa kuitoa roho ya mama huyu) na mtoto akabakia peke yake majini juu ya ubao, ambapo kwa amri za Allah swt aliweza kufika salama u salimini hadi nchi kavu (kisiwa kilichokuwapo karibu).Hapo Allah swt alimwamrisha Swala mmoja kumnyonyehsa maziwa mtoto huyo kwa muda usipungua miaka miwili.
Ulifika wakati ambapo kulitokezea wasafiri kisiwani hapo na walipomwona mtoto huyo na alivyokuwa mzuri, walishauriana kumpelekea mfalme kwani alikuwa hana mtoto. Na walifanya hivyo, na Mfalme alimpenda mtoto huyo na kumchukua kama mtoto wake …..
Mtume Adam a.s. tangu aje duniani humu ilipofika miaka 2647 ndipo Mtume Hud a.s. alipozaliwa na kulipofika miaka 2700 ndipo Shaddad bin ‘Aad alipokuwa Mfalme na ni Mfalme huyu ambaye ametengeneza mfano wa Jannat (Peponi) yenye bustani za kupendeza humu duniani. Humu yeye alijenga majumba ya kuvutia na kupendeza, na aliweka wajakazi warembo:wasichana kwa wavulana kutoka sehemu mbalimbali humu duniani ambao kwa hakika waliifanya pepo yake ipendeze na kuvutia.
JE KUNA MTU ALIYEBAHATIKA KUIONA PEPO HIYO?
Katika zama za Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. kuna mtu mmoja aitwaye ‘Bwana ‘Abdullah bin Kalaba ndiye aliyebahatika kuiona. Na hapa tunaelezea vile inavyopatikana katika vitabu vya historia.
WASEMAVYO WANAHISTORIA
“Katika Bara la Uarabuni kulikuwa na Shakhsiyyah moja aliyekuwa akiitwa ‘Bwana ‘Abdullah bin Kalaba ambaye alikuwa na Ngamia wake aliyekuwa ametoroka na kupotelea katika majangwa ya ‘Aden na katika kumtafuta huyo ngamia wake alifika katika majangwa ambapo aliuona mji mmoja ukivutia. Mji huo ulikuwa umezungukwa na ngome. Ndani ya mji huo kulikuwa na majumba ya kupendeza na yenye kuvutia sana. Na juu ya kila jengo kulikuwa na bendera zilizokuwa zikipepea. Yeye anasema kuwa alifanikiwa kuingia ndani ya mji huo.
‘BWANA ‘ABDULLAH ANAELEZEA ALIVYIONA PEPO YA SAHADDAD
“Mimi niliteremka chini kutokea ngamia wangu na nikamfunga katika nguzo mojawapo. Nikauchukua upanga wangu nikawa ndani ya ngome hiyo. Milango yake ilikuwa ni madhubuti na ya kupendeza sana kiasi kwamba kamwe nilikuwa sijawahi kuona kabla ya hapo. Milango ilikuwa imetengenezwa kwa ubao mzuri sana na manukato mazuri sana na ufundi uliotumika ulikuwa ni wa utalaamu wa hali ya juu sana na juu ya mbao zake kulikuwa kumepachikwa Yaqut za rangi mbalimbali. Ukiangalia chumba kimoja utakisahau chumba cha pili katika ngome hiyo. Madirisha yake yalikuwa yametengenezwa kwa dhahabu na shaba, ukiona milango , kuta na sakafu yake ilivyokuwa iking’ara na kwa hakika kila kitu humo utakachokiona utastaajabika mno.”
‘Bwana ‘Abdullah alipoyaangalia majengo hayo yaliyokuwa mazuri na yenye kuvutia alishangazwa kuona kuwa hapakuwapo na mtu yeyote, na alijaribu kusonga mbele akaona miti ambayo imejaa maua ikiwa inapeperushwa na upepo mzuri sana. Na chini mwake kulikuwa na mito iliyokuwa ikitiririsha maji.
Kwa hakika hii ndiyo ile Jannat ambayo Allah swt ametupa habari zake. Basi mimi kwa hayo nilimshukuru Allah swt kwa kunijaalia bahati hiyo. Mimi niliokota vipande vidogo vidogo vyenye harufu nzuri mno ya Mishk na Ambar. Na hapo nikawaza kuwa sasa itabidi nitoke zangu nje kwa haraka. Nilipofika katika mji wa Yemen huko niliwasimulia watu kuhusu Jannat hii. Kwa hakika nilishangazwa kuona kuwa habari zangu hizi zilienea kila mahali kama upepo.
Mu’awiya alimtuma mjumbe kwenda kwa Hakim San’aan ili kumwita ‘Bwana ‘Abdullah na kutaka kujua kwa undani zaidi kuhusu swala hili. Huyo ‘Bwana ‘Abdullah alielezea yote yale kwa uhakika vile alivyokua ameyaona. Na hapo Mu’awiya alimwita Ka’bul Ahbar na kumuuliza
“Je yanayozungumzwa na ‘Bwana ‘Abdullah yanapatikana katika vitabu vya historia vyovyote vile unavyovijua wewe ? Je kuna mji wowote humu duniani ambao umetengenezwa na kurembeshwa kwa fedha Ambamo kuna aina mbalimbali za miti na mimea zinazoota ? Na ardhi ambayo inanukia kwa manukato mazuri sana, na badala ya mchanga kumetandazwa vito mbalimbali vya thamani ?”
Ka’bul akamjibu kuwa mji huu kama ulivyo wa Jannat umetengenezwa na mtoto wa ‘Aad aliyekuwa akiitwa Shaddad kama vile ambavyo Allah swt anaizungumzia ka tika Qur'an Tukufu.: Sura Al-Fajr, 89, ayah 6-8.
Kwani hakuona jinsi Allah swt Mlezi alivyo wafanya kina A’adi ?
Wa Iram, wenye majumba marefu ?
Kwa kuyasikia hayo yote Mu’awiya alimwambia Ka’bul kuwa
“Mimi ninataka habari kamili za kihistoria kuhusu watu wa Makabila hayo ya ‘Aad.
Ka’bul alimwambia
“Kabla ya ‘Aad kulikuwapo na ‘Aad mmoja katika Kabila la Mtume Hud a.s. Naye alikuwa ana watoto wawili. Mmoja alikuwa akiitwa Shadiid na mwingine akiitwa Shaddad na baada ya ‘Aad kufa basi watoto wote wawili wakawa Wafalme ambao walikuwa wanatawala dunia nzima na hivyo watu wa mashariki hadi magharibi kwa kila upande walikuwa wakiwafuata kama ndio watawala wao. Na Shadiid pia baada ya muda si mwingi alikufa, na hivyo akabakia Shaddad ambaye akawa ndiye mfalme pekee wa dunia nzima.
Shaddad alikuwa na tabia ya kusoma sana na alikuwa amesoma mambo mengi sana na katika kusoma kwake huku mara nyingi alikuwa akisoma kuhusu habari na sifa na mandhari za Jannat ambayo Allah swt ameitengeneza kwa ajili ya muumin na waja wake wema.
Shaddad naye pia akasema kuwa yeye angeweza kutengeneza Jannat kama vile alivyoitengeneza Allah swt . Na azma yake hiyo alitaka kuitekeleza haraka iwezekanavyo.
Mtume aliyekuwapo wakati wa zama zake alipokuwa akifanya kazi ya Tabligh, Shaddad alikuwa akimwuliza ‘je kwa kuwa mja mwema Allah swt atakulipa nini ?’ Basi Mtume wa zama zake hizo alimjibu kuwa, ‘Allah swt atakulipa Jannat.’
Na kwa hayo Shaddad aliuliza ‘Je Jannat ni nini na humo kuna nini.’ Huyo Mtume aliyekuwepo katika zama za Shaddad alimjibu na kumwelezea ‘mazuri yote yalivyokuwa katika Jannat ya Allah swt .’
Shaddad kwa kuyasikia hayo alimwambia Mtume huyo kuwa yeye pia alikuwa na uwezo kamili wa kuweza kutengeneza Jannat kama hiyo na hapo ndipo alipojitangaza kuwa yeye ni mungu. Hivyo watu wote wamwabudu yeye. Ili kutaka kutimiza azma yake hiyo yeye aliwakusanya wataalamu mia moja wa fani mbalimbali na kila mmoja wao aliwapa watu elfu moja wafanye kazi nao haraka iwezekanavyo kwa kutafuta kwanza kabisa mahali yeye anapotaka kujenga mji mmoja wa kiajabu kabisa ambao haujawahi kutokea. Mji ambao utakuwa na majumba ya kushangaza na kuvutia mno ambayo yatakuwa yamejengwa kwa dhahabu na fedha na watandaze Yaqut na lulu na almasi chini na kuwe na manukato ya kila aina yaliyo bora kabisa kiasi kwamba hata hewa inapovuma inavuma iwe ya manukato. Mtengeneze mito inayotiririka maji humo vizuri.
Kwa kuyasikia hayo hao walistushwa kwa maagizo hayo na wakamwuliza Shaddad : ‘Ewe Mfalme wetu! Je kiasi chote hiki cha dhahabu, fedha, almasi na lulu tutatoa wapi ?’
Kwa kuyasikia hayo Mfalme mwenye kiburi alianza kupiga makelele kama inavyo unguruma radi na akasema :
‘Je dunia nzima haipo mikononi mwangu ? Machimbo yote ya ulimwenguni ya fedha na dhahabu na vito vingine vya thamani vyote vichukuliwe mikononi mwetu na si hayo tu bali raia wote wanyang’anywe fedha na dhahabu na vito vya thamani walivyonavyo na ujenzi wa mji huu wa ajabu kabisa uanze mara moja bila ya uchelewesho wa aina yoyote ile. Muwaandikieni barua magavana mia nne kuwa wao nao washiriki nami katika kutekeleza swala hili.”
Kwa kutokana na amri hii au mwito huu uliotolewa na Shaddad Magavana wote walimwitikia na kushirikiana naye katika kulitimiza azma aliyokuwa anayo yeye.
Kwa hivyo wafanya kazi wote walikuwa wakifanya kazi ngumu sana kwa usiku na mchana na hatimaye baada ya miaka mia tatu kupita (wengine wanasema miaka mia moja) mji huu wa ajabu na wa aina yake ulikuwa tayari. Shaddad aliwatafuta wasichana na wavulana warembo kabisa kutoka sehemu mbalimbali za duniani kuja kubakia katika Jannat hiyo ambayo yeye aliipa jina la babu yake Iram na humo aliwaleta matajiri kabisa waje kuishi humo.
Shaddad alitoa amri kuwa raia wote wajiandae kwa ajili ya sherehe kubwa ambayo ataitangaza kuhusiana na kuwa tayari kwa Jannat yake hiyo. Inasemekana kuwa kulichukua muda wa miaka kumi kufanya matayarisho ya kwenda katika Jannat yake hiyo. Shaddad pamoja na jeshi lake na watu wengi mno kupita kiasi waliandamana kwenda katika Jannat hiyo.
Wakati anaendelea na safari yake ya kwenda katika Jannat yake hiyo, kulipobakia safari ya kama masaa ishirini na manne alisikia sauti moja ambayo ilimtia hofu mno na alipoinua macho yake akaona uso wenye kuchukiza na kutisha mno. Na hakusita kuuliza,
“Je ni nani wewe ?”
Akajibiwa kuwa
“Mimi ni Malakul Mauti yaani mimi ni yule malaika ambaye natoa roho za watu humu duniani. Na mimi nimetumwa na Allah swt kuja kuitoa roho yako.”
Shaddad alimwambia :
“Ninaomba unipe muhula kiasi cha kwamba mimi niweze kwenda kuangalia Jannat na mabustani niliyoyatengeneza !!!”
Malaika huyo mtoa roho akamwambia kuwa
“Wewe hauna ruhusa hiyo.”
Na imepatikana katika riwaya kwamba mguu wake mmoja ulikuwa ndani ya Jannat na mguu wa pili ulikuwa nje ndipo hapo roho yake ilipotolewa na pepo hiyo na mabustani yake ikapotea katika macho ya watu. Na watu waliokuwamo humo wote wakateketea kwa pamoja.
Kwa kusema hayo Ka’bul Ahbar akasema kuwa katika zama hizi kutatokezea mtu mmoja ambaye atakuwa ametoka kwenda kumtafuta ngamia wake huko porini na atabahatika kuangalia mabustani haya. Mtu huyo uso wake na nywele zake zitakuwa za rangi nyekundu, atakuwa ni mtu mfupi, na upande wa shingo utakuwa na madoa mawili meusi.
Wakati mazungumzo haya yalipokuwa yakifanyika
Bwana ‘Abdullah Kalaba alikuwa ameketi hapo. Na wakati Ka’bul anazungumza alimwona huyo mtu na mara kwa ghafla akasema kwa sauti ya juu:
“Bwana ‘Abdullah mwenyewe aliyeiona Jannat ya Shaddad ndiye huyo aliyeketi hapo.”

MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini