Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

WATU WA TEMBO ( AS-HAB-I-FIIL )

0 Voti 00.0 / 5

WATU WA TEMBO ( AS-HAB-I-FIIL )
Allah swt anatuambia katika Qur'an Tukufu, Sura Al Fiil, 105, Ayah ya 1-5 :
Kwani hukuona jinsi Allah swt, Mlezi wako alivyo watendEa wale wenye tembo ?
Kwani hakujaalia vitimbi vyao kuharibika ?
Na akawapelekea ndege makundi kwa makundi,
Wakiwatupia mawe ya udongo wa Motoni,
Akawafanya kama majani yaliyoliwa !
Najjashi (Negus), alikuwa ni Mfalme wa Abisynnia ambaye alijichukulia jukumu la kueneza Ukristo na alifanya kila jitihada alizoziweza ili aweze kuirudisha vile ilivyo kuwa miongoni mwa watu wake na ikafuatwa na wingi wa raia zake.
Alipopata habari kuwa watu kutoka sehemu mbalimbali za Ulimwenguni walikuwa wakienda Makka kuhiji huko Al Ka’abah Tukufu, basi naye aliamua kuvumbua jambo ambalo litawavutia watu kutokwenda Makkah kuizuru Al Ka’abah Tukufu na badala yake waende nchini mwake.
Hivyo, basi yeye alijenga Kanisa moja kubwa katika Sana’, mji uliopo Yemen na kuipamba vizuri kwa kila kitu cha kuvutia zikiwemo mazulia, mapazia n.k. Kwa hakika lilikuwa ni jambo la kuvutia sana kwa mtu yeyote aliye angalia kwa kuona ufundi wa kistadi uliotumika katika ujenzi wake. Najjashi alifikiria kuwa baada ya kuona maajabu ya ujenzi huo wa Kanisa watu hawatakwenda tena Makkah kuzuru Al-Ka’abah Tukufu na badala yake watakwenda Sana’ kuzuru hilo Kanisa, na vile vile watu wa Makkah pia watakuja kuhiji hapo Sana’, Yemen. Pamoja na hayo yote watu wa Makkah hawakujali chochote. Vile vile sio kwamba ni watu wa Yemen na Abisynnia tu walioisahau Makkah, laa, wao kama kawaida yao waliendelea na safari zao za kwenda mji mtukufu wa Makkah na kuzuru Al Ka’abah Tukufu.
Kwa kuona haya kulimwia jambo la kusikitisha na likawa ndilo tatizo kubwa kwake. Na kwa hakika likawa ni jambo gumu kabisa kuwalazimsha watu wenye imani zao kwenda kinyume na imani na itikadi zao.
Ikatokezea kwamba kukawa na msafara wa wafanya biashara kutoka Makkah waliofika Sana’. Wao wote wakawa ni Waarabu na wakawa wamekuja huko katika safari ya kibiashara. Baadhi yao walipumzika hapo Kanisani usiku katika safari yao na usiku huo ulikuwa ni wa baridi na ili kutaka kupata ujoto kidogo wao walikoka moto ili kupunguza ubaridi uliokuwa humo chumbani na kwa bahati mbaya wakati wa kuondoka wao walisahau kuuzima huo moto, na ikatokezea kwamba Kanisa hilo likashika moto na likachomwa na kuwaka moto. Najjashi alipopata habari kuwa Kanisa hilo limechomwa moto, hakusita kufikiria kuwa Waarabu wale waliokuwapo usiku huo ndio walioichoma moto kwa makusudi. Na katika ghadhabu hii yeye aliamua kwenda kuiteketeza na kuibomoa Al Ka’abah Tukufu huko Makka.
Ili kutimiza azma yake hii, yeye alimtuma Kamanda Amir Jeshi wake Abraha kutangulia Makka pamoja na jeshi moja kubwa wenye farasi, waliopanda tembo na vikosi mbalimbali.
Abraha alielekea Makka akiwa pamoja na jeshi lenye nguvu sana na wakiwa njiani, miji yote walipopita waliiteketeza na kuiharibu na walikuwa wakishika wanyama waliokumbana nao humo njiani. Katika jangwa la Arabia yeye alikutana na mtu mmoja mwenye ngamia wasio pungua mia mbili. Ngamia hao walikuwa ni mali ya Bwana ‘Abdul Muttalib. Abraha aliwachukuwa hao ngamia wa Bwana ‘Abdul Muttalib. Yeye aliendelea kuelekea Makkah. Alipoukaribia mji wa Makka alipiga kambi katika vitongoji vya kukaribia Makka. Abraha alikuwa amekaa katika kiti chake na maaskari walikuwa wakimlinda. Punde akaja askari na kusema,
“Ewe Mheshimiwa ! Mheshimiwa wa Makka na Chifu wa kabila la Quraishi, ambaye jina lake ni Bwana ‘Abdul Muttalib, yuko nje ya kambi yetu na anataka kuonana nawe.”
Abraha alimwambia askari wake amruhusu Bwana ‘Abdul Muttalib aje mbele yake. Na punde si punde Bwana ‘Abdul Muttalib aliingia ndani ya hema lake. Heshima pamoja utukufu na nuru yalikuwa yakionyesha usoni mwa Bwana Bwana ‘Abdul Muttalib.
Abraha alipo mwona tu Bwana Bwana ‘Abdul Muttalib, aliinuka na kutoa heshima na kumwambia akae karibu naye. Na kwa kupitia Mkalimani Abraha alimwuliza sababu ya Bwana ‘Abdul Muttalib kutaka kumwona yeye.
Bwana ‘Abdul Muttalib alijibu,
“Mimi nimepata habari kuwa majeshi yako wamewachukua ngamia zangu. Na nimekuja hapa kukuomba unirudishie ngamia zangu hizo.”
Abraha akasema :
“Jambo gani hili la kushangaza ? Mimi nimekuja hapa kuiteketeza na kuiharibu kabisa Al Ka’abah na kuuondoa kabisa utukufu wake. Lakini mtu huyu naona hayajali hayo na badala yake naona anawajali ngamia zake. Lau kama Bwana ‘Abdul Muttalib angekuja kuniomba mimi nisiivunje na kubomoa Al Ka'abah Tukufu, basi kwa hakika kwa heshima zote nisingebomoa na badala yake ningerudi bila kutenda vurugu yoyote.”
Kwa kumjibu Abraha, Bwana ‘Abdul Muttalib alijibu,
“Mimi ni mmiliki wa ngamia zangu na hiyo Nyumba Tukufu (Al Ka'abah Tukufu) inayo mmiliki wake, vile vile. Mimi inanibidi nijali mali yangu na mwenye Nyumba hiyo Tukufu atajua mwenyewe namna ya kuiokoa na kuinusuru.”
Abraha kwa kusikia hayo alishangazwa mno na alitoa amri kuwa ngamia wa Bwana ‘Abdul Muttalib zirejeshwe kwake. Na baadae aliendelea na safari yake ya azma yake ya kuibomoa na kuiteketeza Al Ka'abah Tukufu.
JESHI ZIMA KUTEKETEZWA
Alikuwa bado hajafika mbali katika kuukaribia Makka mara akakuta kundi kubwa la ndege wadogo wadogo waliokuwa wameitwa Ababil walionekana katika anga za Makkah na wakakuta wote wapo wanaruka juu ya vichwa vya majeshi ya Abraha. Kwa hakika ndege hawa walikuwa ni kama ndege za kivita kwani wao walikuwa wanavyo vijiwe vidogo vidogo mdomoni mwao na walikuwa wakiyadondosha juu ya vichwa vya wanajeshi hao wa Abraha. Na kila jiwe lililodondoshwa juu ya kichwa cha mwanajeshi kiligonga kichwa na kukipasua na wakawa wanajeshi hao wanaanguka juu ya ardhi na kufa papo hapo.
MMOJA APONEA CHUPUCHUPU
Katika muda mchache kabisa wanajeshi wote wa Abraha waliuawa na ndege hao isipokuwa mmoja tu ambaye alinusurika na akakimbia hadi Abisynnia kwenda kuripoti hali hii ya maajabu yaliyotokea, kwa mfalme Najjashi. Baada ya kufika hapo alielezea habari zote za jeshi kubwa la Abraha lilivyoangamizwa na kuteketezwa na viumbe vidogo kabisa visivyo na nguvu ya aina yoyote. Najjashi alimwomba huyo mtu ampe habari zaidi kuhusu aina ya ndege aliokuwa amewaona yeye. Na ikatokezea kwamba ndege mmoja kama hao waliokuwa huko Makka alitokezea mbele yao na mtu huyo alimwelezea Najjashi kwa kumnyooshea ndege huyo kidole akisema :
“Ewe Mtukufu ! Huyu ndege ni hatari kabisa kwani hawa ndio wameweza kuliteketeza jeshi lote zima la maaskari.”
Punde alipomaliza tu kuyazungumza hayo na kutoa taarifa kamili ndege huyo alimpiga na kijiwe kidogo kutoka mdomo wake, jiwe ambalo likaenda kumpiga kichwani na hatima yake akafa papo hapo mbele ya Najjashi.
Tukio hili limetokea katika mwaka huo huo ambao Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. aliokuwa amezaliwa Makka.
MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini