WATU WA PANGONI (KAHF)

WATU WA PANGONI (KAHF)
Allah swt anatuambia katika Qur'an Tukufu, Sura Al Kahf, 18, ayah 9-14:
Bali unadhani ya kwamba wale watu wa Pangoni na Maandishi walikuwa ni ajabu miongoni mwa ishara zetu ?
Vijana hao walipo kimbilia kwenye pango walisema: Allah swt wetu Mlezi ! Tupe rehema itokayo kwako, na tutengenezee uwongofu katika jambo letu.
Tukayaziba masikio yao kuwalaza humo pangoni kwa muda wa miaka kadhaa wa kadhaa.
Kisha tukawazindua ili tujue ni lipi katika makundi mawili lilio hisabu sawa muda walio kaa.
Sisi tunakusimulia khabari zao kwa kweli. Hakika wao walikuwa ni vijana walio mwamini Allah swt wao Mlezi. Na Sisi tukawazidisha uwongofu.
Na tukazitia nguvu nyoyo zao walipo simama na wakasema: Allah swt wetu Mlezi ni Allah swt Mlezi wa mbingu na ardhi. Hatutamwita mwenginewe kabisa badala yake kuwa ni mungu. Hivyo itakuwa tumesema jambo la kuvuka mpaka.
DAQUIS KUJITANGAZA KUWA  MUNGU…
Katika ardhi ya Roma kulitawala Mfalme aliyekuwa mwadilifu kwa watu wake na ambaye alikuwa mkarimu pia. Yeye alitawala kwa kipindi kirefu cha kutosha na raia wake waliishi katika amani na hali nzuri.
Wakati Mfalme huyu alipokufa kulizuka tofauti miongoni mwa raia wake na ndicho kilichokuwa sababu ya kuleta maangamizo yao wenyewe. Mfalme wa nchi ya jirani, aliyekuwa akiitwa Daquis aliivamia nchi yao na kuimega katika ufalme wake.
Daquis alijenga ngome imara kwa ajili yake mwenyewe na aliipamba kwa kila kitu alichoweza kuipamba. Yeye aliwachagua watu sita wenye busara na waliokuwa na uwezo kutokana na watu wa ardhi zile alizoziteka na kuwafanya Mawaziri. Na baadae yeye aliwalazimisha watu kumwabudu yeye kama ndiye mungu. Majahili na wapumbavu miongoni mwa watu hao walimkubalia yeye kama ndiye mungu wao na walianza kumwabudu kwa kujitupa chini na kumwangukia sujuda.
SHEREHE NA HABARI ZA KUVAMIWA
Kulipita muda na kuliwadia siku ya kusherehekea sherehe yao ya maadhimisho. Katika sherehe hizi Mfalme pamoja na baraza lake na raia wote walishirikiana kwa mbwembwe na shangwe kubwa. Wakati hawa wote wanasherehekea sherehe hizi, kulikuja na mleta habari na alimpa ujumbe Mfalme. Pale aliposoma habari hizo, rangi ya uso wake ulibadilika kwa sababu ya maafa yaliyokuwa yakitaka kumpata yeye pamoja na ufalme wake. Katika ujumbe huo kulikuwa kumeandikwa kuwa majeshi ya Mfalme wa Uajemi alikuwa tayari ameishaingia katika mipaka ya Roma na walikuwa wakisonga mbele kuukaribia mji mkuu wake. Kwa kuona taabu na shida hiyo katika uso wa Mfalme, iliyotokana na kusoma habari za kuvamiwa na uvamizi kutoka nje, mmoja wa Mawaziri wake sita wa Mfalme huyo aliweza kuvumbua na kujua kutokana na sura ya Mfalme huyo na alipoangalia nyuso za wenzake watano kwa kutaka kufanya utafiti, nao pia walionyesha dalili hizo. Kwa hayo tu wao waliweza kubashiri kuwa jambo fulani kubwa la kihistoria liko litatokezea.
Baada ya sherehe kumalizika kila mmoja aliondoka kwenda nyumbani kwake na Mawaziri pia waliondoka kurudi majumbani kwao ambapo wao walizoea kuitisha vikao vyao. Wakati wote walipokuwa wamesha keti pamoja, wao walizungumzia kile walichopeana habari kwa kutazamana nyuso.
VUGUVUGU LA UASI NA KUTOROKA KWA MAWAZIRI SITA
Mmoja wao akasema,
“Je mliona uso wa kiajabu wa Mfalme ! Yeye anadai kuwa yeye mwenyewe ndiye mungu wa watu ambapo yeye anawachukulia kama ni watumwa wake. Lau kama angekuwa kweli ni mungu wa watu, basi kamwe asingekuwa ni mtu ambaye ameshtushwa kwa kupata habari zisizo mfurahisha. Hali hii ya yeye kutoweza kujisaidia imetupa sisi kiasi cha kutosha cha kufikiria, na kwa hakika imetufungua macho vya kutosha kushuku kuwa kwake mungu wa malimwengu zote.
JE NI NANI MUUMBAJI?
Enyi wenzangu ! Mimi kwa hakika ninatilia maanani sana na kuliwazia jambo muhimu sana. Je nani aliyejenga ulimwengu huu ni nani aliyezipachika hizi nyota ndani yake na kwa hukumu ya nani nyota na mwezi vinazunguka katika mizunguko yake ? Kwa nini niende mbali hadi kuzungumzia jua na mwezi ? Kwa nini nisijifikirie mimi mwenyewe ? Kwa nini nisifikirie ni nani ambaye amenileta mimi hapa nilipo akanitia katika tumbo la mama yangu, ambaye amenilea na amenipa mimi kila kitu cha kuweza kuishi na hizi nguvu nilizonazo za kimwili ?
Mimi kwa hakika sasa nimekuwa na imani kuwa mambo yote haya yanafanywa na Allah swt ambaye ni Allah swt wa Malimwengu yote na kamwe huyu hawezi kuwa mwenye Taqwa. Yeye ni mwerevu sana na wala hawezi kuzuzuliwa na kiumbe kidogo kama yeye.
Enyi marafiki zangu ! Maisha yetu yamekuwa ya kufedhehesha kwa kubakia kama watumwa wa Daquis na jambo hili haliwezi kuwa la kudumu milele. Lazima sisi tujitoe nje ya mambo ya dunia na starehe na raha ambazo zinatupeleka mbali zinatutoa mbali na ibada halisi ya Allah swt na lazima tumuombe Allah swt atusamehe kwa madhambi yetu yote.”
ATHARI ZA HOTUBA
Mtu huyo mwenye hekima alizungumza mambo haya kwa hali ya kusisitiza kiasi kwamba wenzake waliathirika sana na wote sita kwa pamoja waliamua kutoroka njia ya wenye kuabudu masanamu na wakaamua kwenda kuishi porini na jangwani huko katika maisha ya kujitenga kwa ajili ya ibada tupu na kumwabudu Allah swt .
KUTOROKA KWAO
Siku iliyofuatia hawa sita kwa pamoja walitoa majumbani mwao kisirisiri na wakaelekea jangwani. Walipofika maili fulani kutoka majumbani kwao, wao walimwaona mchungaji mmoja akichunga kondoo zake. Wao walimwomba maji kwa ajili ya kunywa. Na mchungaji aliwaambia,
“Mimi ninahisi kwenu nyie hewa ya utukufu na ucha Mungu. Je ni nani nyie na mnakwenda wapi ?”
Wao walijibu,
“Sisi tuko sita ni Mawaziri wa Mfalme, lakini tumekana nyadhifa zetu tulizopewa na mamlaka yake. Sisi tunajitenga na tunajitolea maisha kwa ajili ya ‘ibada ya Allah swt , Allah swt wa malimwengu yote kwa sababu kumwabudu Daquis ndiko kuliko tumaliza sisi kiroho na hakika nafsi zetu tunahisi vibaya mno.”
MCHUNGAJI AWA MTU WA SABA
Kwa hayo mchungaji akasema,
“Nami pia nina msimamo kama nyie, na nitapenda kuungana nanyi na kuungana nanyi pamoja katika safari yenu na kuwa nanyi katika ‘ibada ya Allah swt .”
Wao walikubaliana na ushauri na ombi alilolitoa mchungaji huyo. Mchungaji huyo aliwarudisha kondoo wote kwa mwenye mali na akarejea kuungana pamoja na hawa watu sita katika safari yao hiyo.
MBWA KUJIUNGA NAO KATIKA SAFARI YAO
Mchungaji huyo alikuwa na mbwa ambaye naye pia alijiunga nao katika safari hiyo. Kwa kuwafuata fuata. Hao sita walipinga mbwa kuja nao, kwa sababu walikuwa wana hofu kuwa iwapo mbwa angebweka basi pale walipojificha patajulikana.
Nao wakasema, “Itakuwa vyema iwapo sisi tutamwondoa huyu mbwa na kumwacha hapa na tukaendelea na safari yetu.” Kwa hivyo walifanya jitihada zao zote za kumwacha mbwa nyuma, lakini mbwa hakuacha kumfuata mmiliki wake. Basi wakawa hawana chaguo lingine isipokuwa kumkubalia mbwa awafuata na kuungana nao.
Mchungaji huyo aliwachukua hawa wenzake sita katika majabali mlimani, ambapo upande wa pili wake kulikuwa na mabonde yaliyokuwa na mashamba yamestawi vizuri na kumejaa miti ya matunda. Kulikuwa na mto pia ukipita hapo. Kulikuwa na hewa nzuri iliyokuwa ikipita katika bonde hilo. Wao walikula matunda, wakanywa maji, na wakaingia katika mapango yaliyokuwa yakiitwa Kahf. Miale ya jua ilikuwa ikipita katika sehemu ambayo palikuwa wazi katika pango hilo. Wao walipumzika kwa kipindi kidogo na wakajishughulisha katika ‘ibada ya Allah swt .
USINGIZI MREFU: JE NI NUSU SIKU AU SIKU MOJA AU MIAKA 300?
Allah swt anatwambia katika Qur'an Tukufu Sura Al Kahf, 18, ayah 19-20:
Na kwa namna hii tuliwainua usingizini wapete kuulizana wao kwa wao. Alisema msemaji katika wao: Mmekaa muda gani? Wakasema: Tumekaa siku moja au sehemu ya siku. Wakasema: Allah swt wenu Mlezi anajua zaidi muda mliokaa. Hebu mtumeni mmoja wenu na hizi fedha zenu ende mjini, akatazame chakula chake kipi kilicho bora kabisa akuleteeni cha kukila. Naye afanye mambo hayo kwa busara, wala asikutajeni kabisa kwa yeyote.
Kwani wao wakikutambueni watakupigeni mawe, au watakurudisheni katika dini yao; na hapo hamtafanikiwa kabisa !
Baada ya hawa kufanya ‘ibada walipolala pamoja na mbwa wao katika kiingilio cha pango hilo. Upepo mzuri na wa kupendeza ulikuwa ukipita juu yao pole pole na vile vile miale ya jua pia iking’ara juu yao kwa kupitia upande uliokuwa wazi wa pango lakini wao walikuwa hawana habari yoyote na hayo kwa sababu waliingia katika usingizi mrefu. Hawa As-Hab Kahf (Watu wa Pangoni) walilala zaidi ya miaka mia tatu na katika kipindi hiki cha usingizi wao mrefu wao hawakuamka kutoka usingizini mwao. Lakini baada ya kupita kipindi hicho wao waliamshwa kwa amri ya Allah swt na wakawa wakiangalia mahala palipo wazunguka. Wao walianza kuongelea kuhusu wao wenyewe. Baadhi yao walisema, “Sisi tumelala kwa siku moja”, wengine wakasema, “Tumelala nusu siku.” Lakini jambo ambalo liliwashtua na kuwastaajabisha ni kule kupotea kabisa kwa mimea na wao walikuwa wakihisi njaa pia. Wao walikuwa wakijaribu kujiuliza itawezekanaje kwa siku moja kupotea kwa mto na uoto kwa pamoja. Hatimaye wao waliamua kwenda kufuata chakula mjini kwani hawakuweza kustahimili njaa tena na zoezi hili lilikuwa lifanyike kwa mpango kabisa ili kwamba hakuna mtu yeyote atakayeweza kushuku au kujua mahala wao walipojificha, ama sivyo watu watawaua au kuwalazimisha kurudia katika kuabudu miungu.
Hivyo mmoja miongoni mwao aliyekuwa na uzoefu alivaa mavazi ya mchungaji na akaelekea mjini kwenda kutafuta chakula kwenda kutafuta mikate kwa fedha kidogo walizokuwa nazo.
Mtu huyo alipo karibia katika vitongoji vya mji, akaona imebadilika kabisa na ndani ya mji akaona mambo yote ya kustaajabisha kabisa. Mitaa, vichochoro na barabara na mistari ya milango na mistari ya majumba yalivyokuwa yamejengwa yote yalikuwa yameshabadilika kabisa. Hata mavazi ya wakazi wa mjini pia yalikuwa yamebadilika kabisa. Na hivyo alishikwa na bumbuwazi kwa kuona mabadiliko hayo kwa kiasi hicho katika mpangilio wa kila jambo katika mji huo. Na hivyo aliwaza kama yeye alikuwa katika fahamu zake sahihi au hapana au alikuwa akiota ndoto. Je ameingia katika mji mwingine kwa kupotea njia ya kwenda mji wake ? Je kwa nini ameshindwa kuwatambua watu ambao aliokuwa anawajua katika mji wake huo ?
Hatimaye alifika katika tanuru la mwoka mikate. Yeye aliagiza mikate michache kwa mategemeo ya kumlipa kwa pesa alizokuwa nazo. Mwoka mkate huyo alipoziona fedha hizo, alimwuliza,
“Ewe kijana ! Je kuna mahali umevumbua hazina?”
Mtu huyu wa Mapango alijibu,
“Laa, hizi fedha mimi nimelipwa na nimezipata baada ya kuuza tende zangu juzi. Na baada ya hapo nilikuwa nimekwenda safari nje ya mji na hivi ndipo nimerudi.”
Mwoka mikate hakuridhishwa na aliyoyasema huyo mtu, na hatimaye akamfikisha mbele ya Mfalme na kusema,
“Mtu huyu amevumbua hazina. Na uthibitisho wake ni kwamba ni kutokana na fedha alizonazo mikononi mwake.”
Mfalme akamwambia mtu huyo,
“Ewe kijana ! Usiniogope mimi. Niambie ukweli. Sisi kamwe hatutakudhuru. Mtume wetu Issa a.s. mwana wa Bi. Mariam ametuamrisha kutoza Khums (Kodi ya kidini) kutoka mtu yeyote yule anayevumbua hazina.”
Mtume huyo alimlilia Mfalme ili aweze kusikiliza kilio chake hicho. Yeye akasema,
“Mimi ni mkazi wa mji huu. Ni siku mbili tu zilizopita mimi na wenzangu tuliondoka tukaenda mapangoni kwa ajili ya kufanya ibada ya Allah swt . Wakati wetu wa kuondoka kulikuwa na Mfalme aliyekuwa akiitwa Daquis (Daqyanus), ambaye ndiye alikuwa mtawala wa mji huu na ambaye alikuwa akiwalazimisha watu wamwabudu yeye kama mungu na kujitupa mbele yake katika Sujuda. Na kwa kutokana na sisi kutokumwamini yeye kama ni mungu, ndicho sisi kilicho tusababisha kuhama mji huu na kujificha katika mapango huko jangwani. Na wenzangu wapo wanasubiri kurudi kwangu mimi kwao.”
Mfalme akasema,
“Sisi tutakwenda pamoja nawe ili tukashuhudie mambo wenyewe lau kama unasema ukweli katika habari zako hizi, kwa sababu mambo unayoyazungumza wewe ni ya kustaajabisha sana, ni mambo mapya kabisa. Ni kiasi cha miaka mia tatu iliyopita tangu Daquis alipotawala huku.”
MFALME KWENDA PANGONI
Kwa hivyo Mfalme pamoja na watu wa baraza lake waliandamana naye huyo mtu hadi katika mapango na yeyote yule aliyepata habari hizi pia alishirikiana nao wakaenda mpaka kwenye mapango hayo.
Wao walipofika katika mpitio wa mlima, mtu huyo wa pangoni akamwambia Mfalme,
“Itakuwa vyema iwapo nyie mtabaki hapa. Iwapo mtatokezea ghafla mbele ya wenzangu wataogopa na kushtushwa. Na inawezekana mshtuko huu ukawagharimu ukawa hatari kwao. Naomba mimi niende peke yangu mbele yao na niwaeleze habari zote ndipo nyie mje.”
Mtu huyo alipoingia ndani ya mapango na kuwaambia wenzake,
“Enyi wenzangu ! usingizi wenu ambao mnaufikiria kuwa ni wa siku moja haukuwa hivyo, ua haukuwa usingizi wa nusu siku, bali usingizi umechukuwa baadhi ya karne. Mimi nimekwenda mjini na nimeona kule kila kitu kimebadilika kabisa. Mfalme mdhalimu Daquis amekufa zaidi ya miaka mia tatu iliyopita, na hakuna chochote kinachoonyesha yeye au ufalme wake. Na kwa amri ya Allah swt ametumwa Mtume kwa jina la Issa a.s. mwana wa Bi. Mariam katika ardhi hiyo, na watu wa huko ndio wafuasi wake. Kwa hakika mimi nimekumbana na matatizo makubwa sana nikiwa hapo mjini. Na sarafu niliyokuwa nayo nilipowaonyesha watu, waliona maajabu kwao. Na hivyo wakadhani kuwa mimi nimevumbua hazina fulani. Wao wakanichukua kwa Mfalme wao na hapo ndipo nikaja kutambua kuwa sisi tumelala usingizi kwa amri ya Allah swt kwa zaidi ya miaka mia tatu. Mfalme na watu wa baraza lake wametusubiri hapo nje. Wao wamekuja kuthibitisha hayo niliyoyasema. Kama nyinyi mtanikubalia, mimi ninaweza kuwaleta hapa mbele yenu.”
Wale wenzake katika pango hawakumwamini huyo mwenzao. Wao walidhani kuwa mwenzao anataka kuwaponza na wakamatwe na Mfalme. Basi hapo wao walimlilia Allah swt na kumwomba kuwa yeye Allah swt awarudishe katika hali waliyokuwa nayo. Wao waliinua mikono yao juu na kuomba,
“Ewe Allah swt ! tuokoe sisi kutokana na janga hili na uturudishe katika hali yetu tuliyokuwa nayo.”
Dua yao ilikubaliwa na Allah swt aliwafanya wao tena wakarudia usingizi wao mrefu. Mfalme na watu wake waliwasubiri hao kwa muda mrefu bila kuona mtu akirejea. Nao waliingia katika pango hilo na kwa amri ya Allah swt wale waliokuwa wamelala hawakuweza kuonekana machoni mwa Mfalme na watu wake.
Kwa amri ya Mfalme, hapo kulijengwa Msikiti kwa ajili ya ‘ibada ya Allah swt .
Tukio hili ni mojawapo la ‘ishara za Allah swt yaliyoonyeshwa kwa watu ili waweze kujifunza masomo kuhusu ukuu wa Allah swt , Allah swt wa malimwengu zote.

MWISHO