BWANA DHUL-QARNAIN

BWANA DHUL-QARNAIN
Bwana Dhulqarnain alikuwa akiitwa Ayash. Na yeye alikuwa ndiye Mfalme wa kwanza baada ya Mtume Nuh a.s., wengi wa watu wanadhani kuwa yeye ndiye Alexandria wa Kirumi lakini haya si kweli kama vile tunavyopata maelezo kutoka riwaya mbalimbali, vile vile wengi wanauliza iwapo Bwana Dhulqarnain alikuwa ni Mtume? Kwa hivyo jibu sahihi ni kwamba Bwana Dhulqarnain yeye hakuwa mtume bali alikuwa mja mwema wa Allah swt .
Allah swt anasema katika Quran, Sura Al-Kahf, 18, Ayah 83 - 98.
“Wanakuuliza khabari za Dhul-Qarnain, Waambie: Nitakusimulieni baadhi ya hadith yake.
Sisi tulimtilia nguvu katika ardhi na tukampa njia za kila kitu
Hata alipo fika machwea-jua aliliona linatua katika chemchem yenye matope mausi. Na hapo akawakuta watu. Tukasema: Ewe Dhul-Qarnaini ! Ama uwaadhibu au watwae kwa wema.
Akasema: Ama aliye dhulumu basi tutamuadhibu, na kisha atarudishwa kwa Allah swt wake Mlezi amuadhibu adhabu isiyo julikana.
Na ama aliye amini na akatenda mema basi atapata malipo mazuri. Nasi tutamwambia lilio jepesi katika amri yetu.
Kisha akaifuata njia.
Hata alipofika katikati ya milima miwili, alikuta nyuma yake watu ambao waliweza kwa shida kufahamu neno (wanaloambiwa).
Wakasema:“Ewe Dhulqarnain! Hakika Yajuj na Majuj wanafanya uharibifu katika ardhi.Basi je, tukupe ujira ili utie baina yetu na baina yao kizuizi?”
Akasema:“Yale ambayo Allah swt amenimakinishia ni bora (kuliko ujira wenu.Nitakufanyieni bure);Lakini nisaidieni kwa nguvu zenu. Nitaweka baina yenu na baina yao kizuizi chenye imara.”
Nileteeni vipande vya chuma.” Hata alipoijaza nafasi iliyo katikati ya milima miwili,alisema:“Pulizeni”mpaka alipokifanya (kile chuma) kuwa moto,alisema “Nileteeni shaba iliyoyayuka niimwage juu yake.”
Hivyo (Yajuj na Majuj) hawakuweza kuukwea wala hawakuweza kuutoboa.
Akasema:“Hili ni rehema itokayo kwa Allah swt . Na itakapofika ahadi ya Allah swt ya kufika Qayama, atauvunjavunja. Na ahadi ya Allah swt ni kweli tu.”
Je ni kwa nini akaitwa Dhulqarnain ?
Zipo sababu nyingi zinazopatikana za kuitwa kwake Dhulqarnain kwa sababu mojawapo ni kwamba yeye ncha zote za dunia Mashariki mpaka Magharibi alikuwa anaendesha hukumu yake, alikuwa ameishinda, na Allah swt alimpa uwezo juu ya Nuru na Kiza (Dhulmat) na ndio hii sababu moja kubwa ya kupata jina hili la Dhulqarnain.
Katika safari mojawapo watu walimwuliza iwapo mtu atakufuru je wewe utamwadhibu ? Naye aliwajibu kuwa yeye angewaadhibu vikali sana wale Mushiriki na Dhalimu na vile vile Allah swt atawaadhibu vikali mno, lakini yule atakayekuwa ameleta imani na anatenda matendo mema basi yeye atapata malipo yaliyo mema bora kabisa.
Bwana Dhulqarnain alikuwa na Malaika mmoja aliyekuwa anaitwa Rukail ambaye alikuwa ni rafiki yake sana na mara nyingi walisikika wakiwa wanaongea na siku moja yeye alimwuliza Malaika,
“Je ibada zinazofanywa na watu wa ulimwenguni ni sawa na zile zinazofanywa na Malaika mbinguni ?”
Malaika alimwambia,
“Kwa hakika Malaika wanazofanya ibada mbinguni ni bora kabisa kuliko zile zinazofanywa na wanaadamu humu duniani.”
Mbingu imejaa Malaika na wote kwa pamoja wapo wanafanya ibada ya Allah swt kwani humu kuna wengine maisha yao yote wako katika Rukuu, wengine wako katika hali ya Kusujudu. Kwa kuyasikia hayo Bwana Dhulqarnain alilia sana na akamwambia Malaika kuwa yeye iwapo atajaariwa umri mrefu basi atafaya ‘Ibadah za Allah swt vile itakiwavyo. Malaika Rukail kwa kusikia hayo akamwambia,
“Ewe rafiki yangu juu ya ardhi hii ya ulimwengu kuna chemchemi moja inaitwa 'Aynul Hayat (Chemchemi ya maisha ya milele) na kwamba yeyote yule atakaye kunywa maji yake basi hatakufa mpaka pale yeye mwenyewe atapoomba kufa. Hivyo Allah swt amekula kiapo kuwa yeyote yule atakaye kunywa maji ya chemchemi hiyo hatakufa na nakushauri nawe pia unywe maji ya chemchemi hiyo ili usife kama vile unavyotaka wewe.”
Kwa kuyasikia hayo Bwana Dhulqarnain alimwuliza,
“Je chemchemi hiyo ipo wapi ?”
Malaika Rukail alimjibu,
“Kwa kweli mimi siijui ilipo lakini nimesikia kuwa Allah swt ameiumba chemchemi hiyo katika Dhulmat (Kiza kali) na humo ndipo kulipoumbwa chemchemi ya maisha hiyo ambayo hadi sasa hakuna binaadamu wala majini yeyote aliyeweza kuifikia chemchemi hiyo.”
Bwana Dhulqarnain alimwuliza,
“Je hiyo (Dhulmat) iko wapi ?”
Basi Malaika Rukail akamjibu kuwa,
“Mimi sina habari nayo.”
Na kwa hayo Malaika huyo akarudi mbinguni akimwacha Bwana Dhulqarnain katika hali ya masikitiko makubwa mno kwani hakupata habari kamili alizokuwa akizitaka ili kuweza kuifikia hiyo chemchemi ya maisha marefu.
Bwana Dhulqarnain alianza kuwaita Ma’ulamaa wakubwa, Mafuqaha ambao walikuwa na ilimu ya vitabu vitukufu vya Allah swt na habari za Mitume a.s. waliotangulia,1
Basi Bwana Dhulqarnain alijaribu sana kama wao wanajua habari yoyote kuhusu chemchemi hiyo ya maisha nao wote walikuwa wakimwambia kuwa wao walikuwa hawajui chochote kuhusu swala hilo na vile vile Bwana Dhulqarnain aliwauliza iwapo wao walishawahi kusoma kuhusu Dhulmat katika vitabu vyao, nao wakajibu kuwa hawajawahi kusoma habari zake.
Kwa jitihada zake zote hizo Bwana Dhulqarnain hakufanikiwa kupata ufumbuzi wa maswala ambalo alikuwa akitaka kujua habari zake ndipo kulimfanya yeye akawa mtu mmoja mwenye hali ya uzuni kabisa na ambaye hakuwa na raha ya aina yoyote katika baraza lake na hali hii ilikuwa inadhihirika miongoni mwa raia wake. Kwa kuona hali hii ya Bwana Dhulqarnain katika baraza lake kulikuwapo na mtoto mmoja mdogo ambaye yeye alikuwa anatokana na warithi wa Mtume katika zama hizo, aliinuka na kwa heshima na taadhima akamwambia Mfalme huyo Bwana Dhulqarnain kuwa,
“Mheshimiwa yale uliyowauliza hawa watu waliokuwa na ilimu mbalimbali ambayo wao hawayajui chochote lakini mimi ninayo ilimu na habari za maswala unayotaka kuyajua ! !”
Kwa kuyasikia hayo Mfalme huyo alistaajabishwa na kushtushwa sana kwa kumwona kijana mdogo akimwambia kuwa yeye anajua habari za maswala ambayo yamemtatanisha yeye kutafuta ufumbuzi wake. Na Bwana Dhulqarnain akamwuliza kijana huyo,
“Je kweli unasema wewe kuwa unaelewa kuhusu mambo hayo ?”
Na mtoto huyo bila kusita akajibu,
“Ndio mheshimiwa !”
“Mimi nimesoma katika kitabu cha Mtume Adam a.s. (sio lazima kitabu kiwe kama vitabu vyetu siku hizi bali juu ya kitu chochote ambacho kiliandikwa juu yake wakati wa zama hizo) nimeona kuwa juu ya ardhi hii ya ulimwengu huu ipo chemchemi hiyo ya maisha katika Dhulmat. Na yeyote yule atakaye fanikiwa kunywa maji ya chemchemi hiyo hatakufa kamwe hadi pale atakapoomba yeye mwenyewe afe, na chemchemi ya maisha hiyo iliopo katika Dhulmat na pale ilipo hiyo chemchemi ya maisha katika Dhulmat hakuna binaadamu wala majini wowote waliopita”
Kwa kuyasikia haya Bwana Dhulqarnain kwa hakika roho yake ilianza kutulia sana na alijawa na furaha sana na katika siku chache zilizofuatia alianza matayarisho ya safari kuelekea Dhulmat palipo na chemchemi hiyo ya maisha, na alifunga safari akiwa amewachukua watu wenye ilimu wapatao elfu moja, Mafuqaha na Wanazuoni na aliondoka kuelekea upande wa mashariki wa dunia.
Msafara huu wa Bwana Dhulqarnain pamoja na wale waliokuwa wameambatana naye waliendea na safari kwa muda wa miaka kumi na miwili na ndipo walipokaribia Dhulmat ambapo kuna kiza kali kabisa kiasi kwamba kiza cha usiku haufai chochote mbele yake na hapo aliweka kambi akawaita wale wote aliokuwa amesafiri nao katika msafara huo na kuwaambia kuwa,
“Mimi kuanzia hapa sasa ninataka niende safari hii peke yangu na Allah swt akinijaalia nitafanikiwa katika azma yangu hiyo !”
Kwa kusikia hayo hao watu wenye ilimu na maarifa aliokuwa nao walimwambia,
“Ewe Mtukufu Mfalme wetu ! Unavyoona wewe kuwa hii Dhulmat ni kiza kali kabisa na tuna hofu kama utakwenda peke yako Mungu apishe mbali kama utapata matatizo yoyote utakuwa peke yako bila msaada wowote hivyo tunakushauri usiende peke yako.”
Kwa hayo Bwana Dhulqarnain akawajibu,
“Naam mimi ni matumaini yangu kuwa nifike huko penye chemchemi hiyo ya maisha na niweze kunywa maji hayo”
Basi kwa masikitiko makubwa sana wote wakasema
“Iwe vile atakavyo Mfalme wetu !”
Inasemekana kuwa Mtume Khidhr a.s. alikuwa pamoja naye. Mfalme aliwauliza Ma’ulamaa swali kuwa,
“Hebu niambieni katika wanyama wote ni mnyama gani huona vizuri zaidi kuliko wengine ?”
Wao walimjibu kuwa,
“Farasi jike akiwa bikira”
Hivyo Mfalme huyo alitayarisha jeshi la watu wenye akili na busara kuliko wengine elfu sita pamoja na Mafarasi jike bikira elfu sita na alimteua Mtume Khidhr a.s. awe ndio kiongozi wa msafara huo. Wakati anaondoka kwenda zake kuanza safari yake hiyo alitayarisha jeshi jingine la elfu sita aliowaacha hapo nyuma na kuwaambia wamsubiri kwa muda wa miaka kumi na mbili na lau kama hakurudi katika muda huo basi wao wanaweza kurudi nchini kwao. Wakati wanaingia katika kiza hicho Mtume Khidhr a.s. alimwuliza lau kama mtu atapotea katika kiza hicho watamtafutaje ?
Basi kwa hayo Bwana Dhulqarnain alitoa Almasi moja iliyokuwa ya rangi nyekundu akampa Mtume Khidhr a.s. na kumwambia lau itatokea hivyo basi hii almasi nyekundu kama utaitupa ardhini basi itatoa sauti na itatoa mwanga mkubwa na hivyo wale wote watakaoisikia sauti hiyo waelekee kwenye sauti hiyo, na wao wakaendelea na safari zao huku Mtume Khidhr a.s. akiwa mbele na Bwana Dhulqarnain akimfuata.
Wakaendelea na safari yao na ikafika siku moja katika kiza kali kabisa Bwana Dhulqarnain akaona maji na akawaambia maaskari wake wasubiri pale pale ila yeye tu ndiye atakayeendelea mbele na akateremka kutoka farasi wake (Mtume Khidhr a.s.) na akaenda kwa miguu hadi pale penye maji akatupa ile almasi yake nyekundu na alishangazwa sana kuona ni kwa nini haikutokea sauti wala mwanga.
Wakati hiyo almasi ilipofika kwenye kina cha chini ya maji ikagonga ardhi hapo ndio ikatokezea sauti na mwanga na Mtume Khidhr a.s. alipoangalia maji aliona ni meupe kuliko hata maziwa na yalikuwa matamu kuliko hata asali basi yeye akayanywa hayo maji akaoga na akaichukua tena hiyo almasi yake na kuwatupia wenzake waliokuwa amekuja naye na ilipogonga chini kwa kutokana na sauti na mwanga wenzake aliokuwa ameambatana nao wakaja na Bwana Dhulqarnain alikuwa yupo nyuma yao na kuja kuangalia wakaona chemchemi ya maisha haipo wala haionekani dalili yoyote kama ilikuwepo hapo.
Kwa muda wa usiku na mchana arobaini wao wakaendelea na safari yao katika kiza kali hicho na mwishoni wakakuta kuna mwanga unaonekana mbele. Mwanga huo ambao inasemekana ulikuwa ni mwanga kwa kudura za Allah swt na wakakuta kuna jumba moja zuri kabisa, Mfalme aliwaamuru majeshi wake wote wakae hapo wasubiri hapo na yeye peke yake alielekea na kuingia ndani ya jumba hilo na humo kulikuwa na susu moja na ambalo lilikuwa na ndege mmoja mdogo wa rangi nyeusi na kwa kumwona yeye, ndege huyo akauliza,
“Je wewe ni nani ?”
Kwa kusikia swali hilo kutoka kwa ndege huyo Bwana Dhulqarnain akajibu,
“Mimi ni Dhulqarnain.”
Kwa kusikia hayo ndege huyo mdogo akasema,
“Wewe ni Mfalme mkubwa sana, kwa nini umeacha nchi yako adhimu na umekuja kufanya nini hapa ? Je nchi hiyo kubwa kabisa haikutoshi wewe ?”
Kwa kusikia hayo yeye akashtuka ! Na hapo ndege akaendelea kusema kuwa,
“Usishtuke isipokuwa naomba kila nikuulizacho unijibu”,
Hapo Bwana Dhulqarnain akamwambia,
“Naam endelea kuuliza utakacho kuuliza !!!
Hapo ndege akauliza,
“Je katika nchi yako watu wako wanapenda sana kuimba na kusikiliza nyimbo na muziki?”
Kwa hayo Bwana Dhulqarnain akajibu,
“Naam !”
Kwa kusikiliza hayo ndege huyo aliaza kutetemeka sana na susu lile likajaa kama sehemu mbili hivi ! Kwa kuona haya Bwana Dhulqarnain aliona maajabu makubwa sana, baada ya hapo ndege huyo aliendelea kuuliza,
“Je watu wa nchi yako wanapendelea kutoa ushahidi uongo ?”
Bwana Dhulqarnain akajibu,
“Naam !!”
Kwa kusikia hayo tena ndege huyo akaanza kutetemeka na susu hilo likajaa !
Kwa kuona hayo Bwana Dhulqarnain alishangazwa mno !
Ndege huyo akamwambia Bwana Dhulqarnain usishtushwe wala kuona maajabu !
Ndege aliendelea kuuliliza kumwambia Bwana Dhulqarnain naomba uniambie,
“Je watu wako wameacha kusema Lailaha Illallah, kalimah tukufu ?”
Bwana Dhulqarnain akajibu:
“Hapana”
Kwa kusikia hayo ndege huyu akapungua kwa sehemu mbili na tena akauliza swali,
“Je watu wako wameacha kusali ?”
Kwa hayo Bwana Dhulqarnain akamjibu,
“Laa watu hawajacha kufanya ibada wala kusali.”
Na kwa majibu hayo ndege huyo akapungua tena akawa mdogo akapungua na akaendelea kuuliza,
“Je watu wa nchi wameacha Ghusl-i-Jannaba ?
Na Bwana Dhulqarnain akajibu,
“Hapana wanafanya ghusl-i-Janaba!”
Kwa swali hilo ndege huyo akarudi katika hali aliyokuwa nayo hapo mwanzoni basi Bwana Dhulqarnain aliona ngazi moja iko mbele yake pale akaenda akapanda ngazi na akaona kuna kibanda kimoja ambamo kulikuwa na kijana mmoja mzuri sana huku akiwa ameinua kichwa chake anaangalia angani. Kijana huyo akamwuliza Bwana Dhulqarnain,
“Je wewe ni nani ?”
Bwana Dhulqarnain akajibu,
“Mimi ni Mfalme !”
Kijana huyo akamwambia,
“Je imekuwaje wewe umeacha nchi kubwa sana na ukaja mpaka huku, je ulicho nacho hakikutoshi ?”
Bwana Dhulqarnain akamwambia,
“Ni kwa nini wewe unaangalia mbinguni na huku umeweka mikono juu ya midomo yako?”
Kijana huyo akamwambia,
“Mimi nasubiri amri ya Allah swt ya kupiga mbiu siku ya Qiyama.”
Hapo Malaika huyo akachukua kijiwe kimoja akampa Bwana Dhulqarnain na kumwambia alichukue jiwe hilo pamoja naye kwani jiwe hilo lina njaa, likibakia na njaa nawe utabakia na njaa na litakapo shiba basi na tumbo lako litashiba, baada ya hapo Bwana Dhulqarnain alirudia kwa watu wake akawauliza watu ninaomba munielezee kitendawili hiki cha jiwe, nani anajua ?
Hapo wale watu waliokuwa na akili na maarifa na busara wa hali juu waliokuwa wameambatana nao waliagiza mizani moja na wakachukua jiwe lile ambalo Bwana Dhulqarnain alilopewa na yule Malaika wakaliweka katika sahani moja na sahani ya pili wakaweka jiwe lingine kuangalia kama litakuwa sawa katika uzani lakini wakaona kuwa jiwe lile alilopewa Bwana Dhulqarnain na Malaika likawa ni zito, wenyewe wakaendelea kuongezea mawe mengine katika sahani ile ya pili na mpaka sahani ya pili ikajaa bado lile jiwe likawa ni zito kuliko mawe rundo yaliyowekwa katika sahani ya pili. Kwa kuona uhakika huo hao wote walimwambia Bwana Dhulqarnain kuwa sisi tumeshindwa kitendawili hiki cha jiwe hili ulilopewa na Malaika !
Hapo Mtume Khidhr a.s. akamwambia Dhulqarnain,
“Ewe Mfalme kitendawili hiki cha jiwe hili hawa watu hawataweza kukuambia lakini mimi ninajua jibu lake.”
Kwa kusikia hayo Bwana Dhulqarnain moyo wake ulitulia na akamwomba Mtume Khidhr a.s. amtatulie kitendawili hicho. Mtume Khidhr a.s. aliliweka jiwe katika sahani moja ya mzani na katika sahani ya upande wa pili aliweka kijiwe kimoja cha udongo na mara wakaona wote kuwa jiwe hilo likawa ni zito na hawakuweza kujizuia kusema,
“Tunajua kuwa Mtume Khidhr a.s. si mchawi na hivyo tuna yakini kuwa yeye si mchawi lakini hatuelewi siri ya jambo hili.”
Kwa kuyasikia hayo Bwana Dhulqarnain akamwambia Mtume Khidhr a.s. awaelezee siri hiyo watu hao ambao wana shauku ya kujua ! Hapo Mtume Khidhr a.s. akasema,
“Ewe Mfalme! Utukufu wa Allah swt sisi hatuwezi kujifanya wajuaji mbele Yake kwani yeye anawajaribu waja wake kwa njia mbalimbali mfano anamjaribu ‘Alim kwa ‘Alim (mwenye ilimu anajaribiwa kwa mwenye ilimu), ilimu inajibiwa kwa ilimu, aliyesoma anajaribiwa kwa aliye mjahili, na aliye jahili anajaribiwa kwa aliye soma na hawa wote ndivyo wanavyo jaribiwa, na mimi na wewe pia tunajaribiwa kwa pamoja”
Na kusikia hayo Dhulqarnain akasema,
“Ewe Mtume Khidhr a.s.! Rehema za Allah swt zikushukie wewe lakini naomba utuambie basi kuhusu kitendawili hiki cha jiwe hili.”
Kwa hayo Mtume Khidhr a.s. alianza kumjibu akasema,
“Ewe Mfalme Malaika huyo amekupa jiwe hili ambalo lina matamanio yasiyo toshelezwa kwani umejionea mwenyewe kuwa kila ulivyokuwa ukiendeleza kuongeza jiwe upande wa pili wa sahani ilikuwa haitoshi mkaendelea kuongezea na maelfu ya majiwe mkaweka lakini bado jiwe hilo halikutosheka lilikuwa linataka mawe zaidi na zaidi. Lakini pale nilipoweka mie kirundo kidogo cha udongo basi kikavunja uroho wake wa kutamani mawe mengine” 2
Mtume Khidhr a.s. akamwambia,
“Ewe Mfalme na hali yako wewe ni sawa na jiwe hili kwani Allah swt amekujaalia nchi kubwa sana lakini bado hauna subira na bado uko katika harakati za kujiongezea zaidi ! Kwa hakika hapa ulipo wewe leo ni mahala ambapo hakuna binaadamu wala majini yeyote walio kwisha kufika hapa je nchi uliyo nayo wewe haikukutosha ?”
Binaadamu hali yake ni hivi hivi hadi pale atakapofikishwa kaburini ndipo atakapokuwa ameyaacha hayo.
Kwa kusikia hayo Bwana Dhulqarnain aliangua kilio na akakiri kuwa kile ukisemacho wewe Mtume Khidhr a.s. ni mambo ya kweli na yaliyo ya haki tupu nami kamwe sitataka kujiongezea zaidi ya yale niliyonayo na aligeuka na kuelekea Dhulmat na katika vikanyagio vya mafarasi kulikuwa kukija sauti kama kuna changarawe, kwa hayo wale aliokuwa ameambatana nao katika msafara huo wakamwuliza,
“Je ni nini hayo ?”
Akajibu kuwa,
“Yeyote yule atakaye chukua atajuta na yeyote yule hatakaye chukua pia atajuta !!!”
Wengi wao walichukua na pale walipotokezea nje ya kiza hicho wakaona kuwa hayo waliyoyazoa wakisikia sauti za changarawe kumbe si changarawe bali ni almasi, hivyo wale ambao hawakuchukua walianza kuonyesha majuto yao na wale waliokuwa wamechukua walianza kujiambia je ni kwa nini hawakuchukua zaidi ili wangenufaika zaidi ! Baadaye wakafika Darul Hukumah Humatul Jandal ambapo aliaga dunia.
Al Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. wakati anaelezea alisema kuwa Allah swt amteremshie rehema ndugu yangu Bwana Dhulqarnain kwani yeye hakuwa na kosa la binafsi bali alikuwa anategemea kufika pale alipokuwa akitarajia na kama wakati wa kwenda angeona almasi hizo ambazo zilikuwa zikisikika kama changarawe basi bila shaka angezoa kwa sababu wakati wa kwenda alikuwa na mapenzi ya dunia lakini wakati wa kurudi alikuwa hana matamanio na dunia hivyo hakuokota almasi yoyote na vile vile aliwaonya wale waliotaka kuokota. Vile vile Al Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. aliulizwa,
“Je Bwana Dhulqarnain alikuwa ni Mtume au ni Malaika ?”
Al Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. alijibu kuwa,
“Bwana Dhulqarnain hakuwa Mtume wala Malaika bali alikuwa ni mja mwema wa Allah swt .”
Imepatikana riwaya kutoka Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. kuwa Bwana Dhulqarnain alikuwa ni mja mwema wa Allah swt ambaye alikuwa akiwalingania watu kuja katika haki na ikatokea kwamba yeye alijeruhiwa kichwani na kwa kipindi fulani akawa Ghaib na baada ya kipindi fulani tena akatokezea mbele yao na tena akajeruhiwa kichwani mwake na baada ya hapo Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. akasema miongoni mwenu pia kuna Shakhsiyyah mmoja anayeitwa 'Ali ibn Abi Talib a.s. ambaye juu ya ardhi hii ni mtu ambaye ana uwezo wa hali ya juu kabisa na ambaye amejaaliwa utukufu na ambao utukufu huu utaendelea hadi kwa Al Imam Mahdi Sahibuz-Zamaan a.s. na kwa ajili yake ardhi zote zitatapika yale yote yaliyo kuwa ndani mwake na yeye ndio atakae kuwa akihukumu nyoyo za watu”.
Bwana Dhulqarnain akawa anawalingania watu katika haki na njia ya Allah swt na akawajengea Msikiti mmoja mzuri kabisa na tena alianza safari yake ya kutembelea dunia na njiani akamwona mzee mmoja ambaye alikuwa akifanya ‘ibada ya Allah swt , naye akamkaribia huyo mtu akamwambia,
“Je kwa nini ulipouona uso wangu huu wa kutisha wewe haukushtuka ?”
Mzee huyo akamwambia,
“Kwa hakika jeshi la Allah swt ni jeshi kubwa kabisa kuliko lako sasa itawezekanaje mimi ninamuomba Allah swt na lau kama nitaacha kulenga moyo wangu mawazo yangu na fikara zangu kwake yeye nikakugeukia wewe sasa nani atakaye nitimizia mimi maswala yangu ?”
Bwana Dhulqarnain akamwambia mzee huyo,
“Kama utakubali ninaomba nikushirikishe wewe katika ufalme wangu na uishi pamoja nasi !”
Mzee huyo akamwambia Bwana Dhulqarnain,
“Kama wewe utanipa dhamana ya mambo manne basi mimi niko tayari kukubali jambo hilo uliloniambia:
1. Neema, na Raha kamwe isiondoke,
2. Unipatie siha (afya) ambamo mimi kamwe nisiwe mgonjwa,
3. Unijalie ujana ambao uzee hautanikaribia kamwe,
4. Maisha yale ambayo mimi sitapata kifo !!! ”
Bwana Dhulqarnain akamwambia mzee huyo,
“Ewe mzee ! Vitu hivi vinne binaadamu hanavyo katika uwezo wake.”
Na hapo huyo mzee akamwambia Bwana Dhulqarnain,
“Wewe Dhulqarnain huna vitu hivi vinne, havipo katika uwezo wako lakini Allah swt ninaye muabudu mimi yeye anao uwezo na viko chini katika kudura yake, na wewe pia uko chini yake.”
Kwa kuyasikia haya Bwana Dhulqarnain akamwambia huyo mzee,
“Ewe mzee kwa kweli wewe uliyoyasema ni mambo ya ukweli na haki kabisa.”
Na akaendelea na safari yake, njiani wakati anaendelea na safari yake akakutana na ‘Alim na kufanya mazungumzo naye basi huyo Alim akamwuliza Bwana Dhulqarnain,
• “Naomba uniambie ni vitu gani hivyo viwili ambavyo daima vinakaa vikizunguka?
• Je ni vitu gani viwili ambavyo vipo katika ulimwenguni tangu ulipoanza ?
• Je ni vitu gani viwili ambavyo moja inaifuatia ya pili yake ?
• Je ni vitu gani viwili ambavyo ni maadui miongoni mwao ?
Yeye Bwana Dhulqarnain akajibu kuwa,
• Ni mwezi na jua.
• Kile kilichopo kwa milele ni ardhi na mbingu,
• kile ambacho moja kinafuatia kingine ni usiku na mchana na
• vile vilivyo na uadui baina yao ni kifo na maisha.”
Huyo Alim kwa kusikia majibu hayo alisema kwa hakika wewe ni mwenye ilimu na busara ya hali ya juu !
Bwana Dhulqarnain aliendelea na safari yake pamoja na jeshi lake na mara akamwona mzee mmoja mkongwe alikuwa akigeuza geuza mafuvu ya vichwa vya watu walio kufa miaka mingi iliyopita kama kwamba anatafuta kitu fulani katika nyuso za mafuvu hayo. Kwa kuona maajabu haya, Dhulqarnain alishangazwa ni kwa nini huyo mzee anageuza geuza mafuvu haya na akamwuliza,
“Je ni kwa nini wewe unageuza geuza mafuvu haya ?”
Basi mzee huyo mkongwe akamjibu Dhulqarnain,
“Mimi ninatafuta katika mafuvu haya ni nani alikuwa tajiri na nani alikuwa masikini, je ni nani alikuwa mfalme na ni nani alikuwa fakiri ?
Kwa kusikia haya Bwana Dhulqarnain akasema,
“Kwa hakika mambo haya ni mambo yenye nasiha kubwa kwangu mimi kwani baada ya kufa hakuna tofauti kati ya tajiri wala masikini kwa sababu wote wanakuwa hali moja !”
Bwana Dhulqarnain kutoka hapo aliendelea mbele na safari yake akakuta kuna kabila moja ambalo watu wake wote walikuwa wakiishi kwa pamoja kwa kushirikiana na kama ndugu moja na wakifanya ‘ibada ya Allah swt na walikuwa hawamtendei mtu yeyote ubaya wa aina yoyote ile na akaona jambo la kustaajabisha kuwa wao walikuwa wametengeneza makaburi mbele ya majumba yao. Kwa hayo Bwana Dhulqarnain hakujizuia na akawauliza watu hao,
“Je ni kwa nini mnatengeneza makaburi mbele ya majumba yenu ?”
Wao walimjibu,
“Sisi tunafanya hivi kwa sababu daima tuwe tukikumbuka mauti !”
Bwana Dhulqarnain akaendelea kuwauliza,
“Je ni kwa nini majumba yenu hayana milango?”
Wo wakajibu kuwa,
“Miongoni mwetu hakuna waovu wala wezi !”
Bwana Dhulqarnain akaendelea kuwauliza,
“Je kwa nini nyie hamna kiongozi ?”
Wao walimjibu
“Sisi hatutendeani dhuluma miongoni mwetu!”
Bwana Dhulqarnain akaendelea kuwauliza,
“Je kwa nini hamna mahakama ?”
Wao wakajibu,
“Sisi hatugombani wala hatuna mtafaruku wa aina yoyote’
Bwana Dhulqarnain akaendelea kuwauliza,
“Je kwa nini hamna Mfalme yoyote ?”
Wo wakajibu kuwa,
“Hakuna yeyote miongoni mwetu aliye na matamanio zaidi na hivyo wote tuna matakwa yetu yaliyo sawa,”
Bwana Dhulqarnain akaendelea kuwauliza,
“Je ni kwa nini mna mali wote sawa sawa ?”
Wo wakajibu kuwa,
“Sisi tunafanya mgawano kwa uadilifu miongoni mwetu”
Bwana Dhulqarnain akaendelea kuwauliza,
“Kwa nini nyie hamgombani ?”
Wo wakajibu kuwa,
“Sisi tunaishi kwa mapenzi na udugu,”
Bwana Dhulqarnain akaendelea kuwauliza,
“Kwa nini nyie muna kauli na shauri moja ?”
Wo wakajibu kuwa,
“Kwa sababu sisi tumeisha changua njia moja wote kwa pamoja ! Sisi hatutakiani ubaya wowote miongoni mwetu wala hakuna mtu anaye msuta mwenzake,”
Bwana Dhulqarnain akaendelea kuwauliza,
“Kwa nini miongoni mwenu hakuna mauaji yoyote ?
Wakajibu,
“Kwa sababu sisi tunazidhibiti vyema nafsi zetu,”
Bwana Dhulqarnain akaendelea kuwauliza,
“Je ni kwa nini nyie hamghadhabikiani na hamuhamaki ?”
Wao wakajibu,
“Kwa sababu sisi tuna muelekeo wa kunyenyekeana na kupendana,”
Bwana Dhulqarnain akaendelea kuwauliza,
“Je ni kwa nini wakazi wa kabila lenu wana umri mrefu kuliko makabila mengine ?”
Wo wakajibu kuwa,
“Kwa sababu sisi tunatimiza haki miongoni mwetu na tumejiepusha mbali na dhuluma za kila aina.”
Bwana Dhulqarnain aliendelea kuuliza,
“Kwa nini hampatwi na balaa la njaa ?”
Wakajibu,
“Sisi daima huwa tunafanya toba kwa Allah swt ,”
Bwana Dhulqarnain akaendelea kuwauliza,
“Je kwa nini nyie hamna misiba au huzuni na majanga ?”
Wakajibu,
“Sisi huwa tunafanya subira kwa balaa tunapopatwa na huwa tunajipa moyo katika sura kama hizo ili tuweze kukabiliana nayo,”
Bwana Dhulqarnain akaendelea kuwauliza,
“Je kwa nini mali zenu haziharibiki au kuteketea ?”
Wakajibu,
“Sisi tuna imani kamili juu ya Allah swt peke yake kwa sababu tunajua kile kinacho fanyika kitakacho tusibu itakuwa ni maslahi anayo tutakia Allah swt mwenyewe na bila shaka ni mema tu kwa ajili yetu.”
Bwana Dhulqarnain akaendelea kuwauliza,
“Je mababu zenu pia walikuwa na utamaduni na desturi na tabia “kama za kwenu hizi ?
Wakajibu,
“Naam mababa na mababu zetu walikuwa daima wakiwahurumia sana masikini na walikuwa wakiwasaidia na kuwatimizia haja zao na yeyote yule aliye kuwa akiwakosea wao walikuwa wakiwasamehe na daima wakiwawia wema, wakiwa takia msamaha kwa uhalifu wote, walikuwa na uhusiano mwema pamoja na majamaa zao, na kamwe walikuwa hawafanyi hayana katika amana, na walikuwa wakitekeleza mema yote na ndiyo maana Allah swt amewawia kwa ukarimu.”
Vile vile inapatikana katika historia ya kuwa Bwana Dhulqarnain yeye alikuwa ni mtu kutokea Alexandria, na alikuwa ni mtoto mmoja tu wa wazazi wake, alikuwa na tabia njema na alikuwa akiongea na watu kwa tabia nzuri na alikuwa mnyenyekevu na alikuwa daima akiwalingania watu katika haki kiasi kwamba watu walijishughulisha mno katika ibada za Allah swt , na kwa hakika yeye aliwajengea kaumu hiyo Msikiti mmoja mkubwa uliokuwa wa kisasa katika zama hizo, na baada ya hapo ndipo yeye alipotoka kwenda kuzunguka dunia ambapo watu walimsisitiza kuwa asiende popote na Kaumu yake walikuwa wamejitolea tayari kumtumikia kwani kwa sababu yake ukoo mzima ulikuwa una raha na amani na kwamba mama yake pia alikuwa ni mzee hivyo alimhitaji Dhulqarnain akiwa kama ni mtoto mmoja tu, yeye aliwaambia
“Maneno yenu ni kweli lakini hali yangu ni sawa na mtu ambaye ameng’olewa macho yake na moyo wake na masikio yake hayapo katika uwezo wake na kwamba kuna anaye mkimbiza mbele yake sasa mtu kama huyu masikini atafanyaje?”
“Basi hali yangu ni sawa hali ya mtu kama huyo kwani uwezo fulani uwezo fulani unao nivuta mimi basi mimi ndivyo ninavyo vutika kwenda huko na ninawausieni mje msikitini humu kufanya ‘ibada, mfanye utiifu na daima muwe mkimpa moyo mama yangu na mumfikishieni habari njema daima ili apate kuishi kwa raha.”
Na baada ya hayo yeye akaondoka katika safari yake hiyo.
KUWAZUIA YAJUJ NA MAJUJ
Ili kuwaokoa kaumu hiyo wasishambuliwe na kuingiliwa Yajuj na Majuj, Bwana Dhulqarnain aliwajengea ukuta kaumu hiyo kama vile ilivyoelezwa katika habari iliyopita. Hawa Yajuj na Majuj walikuwa ni viumbe vilivyokuwa vinaonekana kama binaadamu vifupi
Allah swt anasema katika Quran, Sura Al-Kahf, 18, Ayah 83 - 98.
“Wanakuuliza khabari za Dhul-Qarnain, Waambie: Nitakusimulieni baadhi ya hadith yake.
Sisi tulimtilia nguvu katika ardhi na tukampa njia za kila kitu
Hata alipo fika machwea-jua aliliona linatua katika chemchem yenye matope mausi. Na hapo akawakuta watu. Tukasema: Ewe Dhul-Qarnaini ! Ama uwaadhibu au watwae kwa wema.
Akasema: Ama aliye dhulumu basi tutamuadhibu, na kisha atarudishwa kwa Allah swt wake Mlezi amuadhibu adhabu isiyo juulikana.
Na ama aliye amini na akatenda mema basi atapata malipo mazuri. Nasi tutamwambia lilio jepesi katika amri yetu.
Kisha akaifuata njia.
Hata alipofika katikati ya milima miwili,alikuta nyuma yake watu ambao waliweza kwa shida kufahamu neno (wanaloambiwa).
Wakasema:“Ewe Dhulqarnain! Hakika Yajuj na Majuj wanafanya uharibifu katika ardhi.Basi je,tukupe ujira ili utie baina yetu na baina yao kizuizi?”
Akasema:“Yale ambayo Allah swt wangu amenimakinishia ni bora (kuliko ujira wenu.Nitakufanyieni bure);Lakini nisaidieni kwa nguvu zenu. Nitaweka baina yenu na baina yao kizuizi chenye imara.”
Nileteeni vipande vya chuma.” Hata alipoijaza nafasi iliyo katikati ya milima miwili,alisema:“Pulizeni”mpaka alipokifanya (kile chuma) kuwa moto,alisema “Nileteeni shaba iliyoyayuka niimwage juu yake.”
Hivyo (Yajuj na Majuj) hawakuweza kuukwea wala hawakuweza kuutoboa.
Akasema:“Hili ni rehema itokayo kwa Allah swt wangu.Na itakapofika ahadi ya Allah swt wangu ya kufika Qayama),atauvunjavunja.Na ahadi ya Allah swt wangu ni kweli tu.”
MAUMBILE YA YAJUJ NA MAJUJ
Yajuj na Majuj walikuwa ni viumbe vyenye miguu minne na wakifanana na wanaadamu kisura na wao walikuwa ni wafupi mno mbele ya watu wa zama hizo. Na watoto wao walikuwa wakizaliwa kama watoto wa wanaadamu na walikuwa hawakui zaidi ya shubiri tano na sura zao zilikuwa aina moja na walikuwa wazururaji. Kwa kuwa ngozi zao zilikuwa ngumu kama zile za ngamia, hivyo hawakuathirika kwa baridi wala joto. Walikuwa na makucha makubwa na meno makali na masikio yao yalikuwa marefu kiasi kwamba walikuwa wakitandika moja na kujifunika kwa la pili. Walikuwa wakiingiliana kama wanyama na chakula chao kikubwa kilikuwa ni samaki kwa sababu kulikuwa kukinyesha mvua za samaki, na kama kulikuwa na kasoro ya samaki basi walikuwa wakishambulia miji na kuchafua na kuvuruga kila kitu kiasi kwamba watu walipokuwa wakizisikia sauti zao, walikuwa wakikimbia na kuacha makazi yao kwa sababu ilikuwa ni vigumu mno kuwakabili kwani walipokuwa wakiingia mijini basi miji yote ilikuwa ikijaa wao tu. Idadi yao ilikuwa kubwa mno kiasi kwamba hakuna mtu mwingine ajuaye isipokuwa Allah swt . Wao walikuwa hawafi hadi wamezaa watoto zaidi ya elfu moja.
Katika vitabu tunapata habari zaidi kuwa Yajuj na Majuj ni makabila mawili yaliyokuwa makubwa kutokana na kizazi cha Yafus, mwana wa Mtume Nuh a.s. Na katika Agano la Kale, Majuj anaelezwa kuwa ni Chifu wa Mashech na Tunal. Kwa sasa Moscow ndio mto unaosimama mji huo,uitwao Moscow, mji mkuu wa Urusi; Tabul ni mto huko Urusi ambapo kuna mji Tobolsk.
Katika historia tunapata kujua kuwa Bwana Dhulqarnain alikuwa ni mtoto wa mama mdogo wa Mtume Khidhr a.s. na utawala wake ulienea 3457 baada ya Mtume Adam a.s. kuja humu duniani, na katika mwaka 3460 aliujenga ukuta huo kwa ajili ya kuwazuia Yajuj na Majuj, na katika 3470 alikutana na Mtume Ibahim a.s., na kwa muda wa miaka 40 alikuwa akizunguka duniani na hatimaye katika umri wa miaka 500 yaani 3497 tangu Mtume Adam a.s. aje humu duniani yeye alifariki akaaga dunia na amezikwa katika Makka Al Mukarramah.
•    1. Vitabu vikuu vitukufu vya Allah swt ni vinne.
1. Tawrat - Kilicho teremshwa kwa Mtume Musa a.s
2. Zaburi – Kilicho teremshwa kwa Mtume Daud a.s.
3. Ijili - Iliyoteremshwa kwa Mtume Issa a.s.
4. Qur'an Tukufu – Iliyoteremshwa kwa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w.
Mitume mingi hawakupata vitabu hivi vitukufu lakini walikuwa wanapata vitabu vinavyoitwa Sahifa.
•    2. Hapa jambo la busara tunalo ambiwa ni kwamba mfano wa jiwe hilo ni sisi binaadamu ambao kamwe hatutosheki kwa kidogo wala haturidhiki kwa kingi wala hatukinai kwa kingi hadi hapo mauti itakapo fika ndipo matumaini yetu matamanio yetu yatakapokwisha. Tunaona kuwa leo mtu anataka kujilimbikizia mali na utajiri kwa kiasi alicho nacho hatosheki bali anataka kutafuta zaidi na zaidi kwa njia yoyote ile iwe halali iwe haramu yeye mradi ajilimbikizie utajiri. Na Qur'an Tukufu anakumbusha kuwa tutakapofika kabirini ndipo hapo tutakaposhtuka kuona kuwa sasa ndio tumezinduka kutoka usingizini mwetu.

MWISHO