ADHANA: SHERIA NA VIPENGELE VYAKE KWA MUJIBU WA KITABU NA SUNNA (SEHEMU YA TANO)

ADHANA: SHERIA NA VIPENGELE VYAKE KWA MUJIBU WA KITABU NA SUNNA (SEHEMU YA TANO)
MANENO YAWANAVYUONI KUHUSIANA NA: KUHIMIZA SALA NI BORA KULIKO USINGIZI
Upande wa swahaba na tabiina wapo wanaoona kuwa jambo hilo ni bidaa wala Mtume hakuliamrisha, na kuwa lilizuka baada ya Mtume. Yafuatayo ni maelezo yao:
1. Ibnu Jariri anasema: .Amr bin Hafsa alinipa habari kuwa Saad muadhini ndiye mtu wa kwanza aliyesema:
الصلاة خيرمن النوم
(Sala ni bora kuliko usingizi), ilikuwa wakati wa utawala wa Umar hivyo Umar akasema: Ni bidaa, kisha akamuacha na wala Bilal hakumuadhinia Umar.
2. Pia amepokea toka kwake kuwa: Alinipa habari Hasan Muslim kuwa kuna mtu alimuuliza Twausi: Ni lini ilianza: Arabic text (Sala ni bora kuliko usingizi)? Akajibu: .Haikutamkwa hii wakati wa Mtume lakini Bilal aliisikia zama za Abu Bakr baada ya kifo cha Mtume (s.a.w.w.) ilikuwa ikitamkwa na mtu asiye muadhini, hivyo akaichukua toka kwake, kisha akaadhini kwa kipengele hicho, lakini toka wakati huo Abu Bakr hakuishi sana zikawa zimeingia zama za Umar. Akasema Umar: Tungemkataza Bilal kuhusu hili alilolizusha, utadhani kalisahau ameendelea kuwaadhinia watu kwa hili mpaka leo1.
3. Amepokea Abdur-Razaqi toka kwa Uyynati toka kwa Laythu toka kwa Mujahidu kuwa amasema: .Nilikuwa na Ibnu Umar akasikia mtu akihimiza (tathuwibi). Akasema: .Hebu twende zetu tutoke kwa mtu huyu wa bidaa2.
Kwa riwaya ya Abu Daud ndani ya Sunan yake, dhahiri ni kuwa mtu huyo alihimiza katika Sala ya adhuhuri na Sala ya Alasiri na si Sala ya Asubuhi3
4. Yaliyopokewa toka kwa Abu Hanifa kama ilivyo ndani ya Jamiul- Masanidi toka kwa Hamadi toka kwa Ibrahimu amesema: Nilimuuliza kuhusu tamko la himizo (tathuwibi) akasema: Hilo ni katika mambo yaliyozushwa na watu, nalo ni jambo zuri kati ya mambo waliyoyazusha. Kisha akaongeza kuwa: wao tamko hilo lilikuwa baada ya muadhini kumaliza adhana yake husema: Arabic text (Sala ni bora kuliko usingizi) . mara mbili.
Amesema: Riwaya hii ameitoa Imam Muhammad bin Al-Hasan (As- Shaybani) ndani ya kitabu chake Al-athar. Wao wawili wamepokea toka kwa Abu Hanifa. Kisha Muhammad akasema: Nayo ni kauli ya Abu Hanifa na ndio tunayoifuata4.
Riwaya hii inaonyesha kuwa kipengele hiki kilikuwa kinawekwa baada ya kumaliza adhana hizo ni zama za mtukufu Mtume au makhalifa na wala hakikuwa ni sehemu ya adhana bali muadhini alikitamka yeye mwenyewe kwa ajili ya kuamsha watu toka usingizin, kisha baadaye kikaingizwa ndani ya adhana.
5. As-Shaukani kanukuu toka kwenye Al-Bahri Al-Zakhari kuwa: Alikizua Omar. Mwanae akasema: .Hii ni bidaa. Imepokewa toka kwa Ali (a.s.) kuwa baada ya kusikia tamko hilo (tathuwibi) alisema: .Msizidishe ndani ya adhana kitu ambacho hakimo.. Kisha baada ya kutaja hadithi ya Abu Mahdhurat na Bilal akasema: .Tunasema ikiwa ni kwa sababu ya kukanushwa na Ali (as) na mwana wa Omar na Twausi basi tumekubali. Hivyo timeamrishwa kwa ajili ya kuhisisha hali na wala si kama sheria, hiyo ni ili tuoanishe kati ya riwaya hizo5.
6. Al-Amiru Al-Yamaniy As-Swinaiy (Aliyefariki mwaka 182) amesema: .Nilisema: Kutokana na haya ni kuwa kipengele hiki
الصلاة خيرمن النوم
(Sala ni bora kuliko usingizi) si miongoni mwa matamshi ya adhana iliyowekwa na sheria kwa ajili ya kuwaita watu waelekee kwenye Sala huku ikionyesha kuwa wakati wa Sala umeingia. Bali kipengele hiki ni kati ya matamshi ambayo yalianzishwa ili kumuamsha yule aliyelala, hivyo matamshi hayo ni sawa na ile tasbihi ya mwisho ambayo hivi sasa watu wameizoea hasa badala ya adhana ya kwanza.
Kisha akasema: Basi ukishalijua hili utakuwa mwepesi kwako mjadala uliyozoeleka kati ya wanazuoni kuhusiana na matamshi hayo, Je yenyewe ni sehemu ya matamshi ya adhana au siyo. Na je ni bidaa au siyo 6
7. Ibnu Qaddama amenukuu toka kwa Is.haqa kuwa baada ya kunukuu riwaya ya Abi Mahdhurat alisema: Hili ni jambo walilolizua watu.
Abu Isa amesema: .Hiki ndio kipengele cha kuhimiza (tathuwibi) kilichochukiwa na wanazuoni, na ndicho kilichomsababisha mwana wa Umar atoke msikitini alipokisikia 7.
8. Kwa sababu riwaya nyingi zilizotoka kwa Maimam wa Ahlul-Bait zinathibitisha kuwa ni bidaa. Amepokea Sheikh Tusiy kwa njia sahihi toka kwa Muawiya bin Wahabi alisema kuwa: Nilimuuliza Aba Abdullah kuhusu tamko la kuhimiza ambalo huwa kati ya adhana na iqama akasema: Hatulijui 8
9. Jambo lililodhihiri kwangu baada ya kudurusu riwaya zinazozungumzia adhana ni kuwa: Familia mbili zilifuatilia kwa undani yale yaliyopokewa toka kwa babu yao Abdallah bin Zaid na Abi Mahdhurat, hivyo zikafanya makusudi kueneza yale yaliyonasibishwa kwa babu yao kwa sababu yanaonyesha fadhila kwa familia, kwani laiti ingekuwa si hivyo basi jambo hili la sheria ya adhana kuletwa kwa ndoto, na kuongezwa kipengele cha kuhimiza katika adhana ya Sala ya Asubuhi lisingeenea kwa mapana ya namna hii. Kwa ajili hiyo huenda mtu angeweza kuyatilia shaka yale yaliyonukuliwa toka kwa babu yao.
Tayari umeshajua kuwepo kwa wapokezi ambao wanaonasibishwa na familia hizi mbili katika njia ya upokezi wa riwaya hizi.
10. Hakika kifungu cha kwanza na cha pili kinathibitisha kuwa yeye Allah ndiye Mungu wa ulimwengu wote na kisicho Yeye ni sawa na si rabi hakina utawala wowote mbele ya Allah. Kifungu cha tatu kinathibitisha kuwa Muhammad (s.a.w.w.) ni Mtume wa Allah ambaye alimtuma kufikisha ujumbe wake na kutekeleza wito wake. Hivyo mwisho wa kifungu hicho tangazo na wito wake unabadilika toka katika uthibitisho mpaka kwenye wito wa kuelekeza kwenye Sala ambayo ameifaradhisha Mwenyezi Mungu na ambayo mwanadamu huitumia kuwasiliana na Mwenyezi Mungu, na kupitia Sala hiyo unyenyekevu wa mwanadamu huchanganyikana na utukufu wa muumba. Kisha hutoa wito kuelekea kwenye ushindi na uokovu na amali bora ambayo ndio lengo la Sala. Na baada ya kumaliza wito wa ushindi na amali bora hurudia tena kutaja ukweli halisi wa milele ambao ulitamkwa wazi wazi mwanzo wa vifungu vya adhana, hivyo husema:
الله اكبر الله اكبر لااله الا الله لااله الا الله
Allah Mkubwa Allah Mkubwa. Hapana mola wa haki isipokuwa Allah. Hapana mola wa haki isipokuwa Allah.
Hii ndio hali halisi ya adhana na muundo wake huku yote mawili yakiwa katika mtiririko mmoja ambao umehitimishwa na sheria ya Mwenyezi Mungu kwa ufanisi. Huku ukielezea ukweli halisi wa milele na kumzuwia mwanadamu asijifunge katika minyororo ya dunia na udanganyifu wake. Hii ndio hali halisi anayoihisi kila anayesikia adhana na kila mwenye kufatilia vifungu vya adhana na maana yake. Lakini hapa kuna ukweli ambao mimi au mwingine hawezi kuuficha (Iwapo tu mtu huyo atajiepusha na mtazamo wake wa mwanzo au ubinafsi wa kimadhehebu) nao ni kuwa: Muadhini anapotoka katika kifungu cha wito wa kuelekea kwenye Sala na ushindi na amali bora (katika adhana ya asubuhi) kisha akaingia kwenye tangazo la kuwa:
الصلاة خيرمن النوم
Sala ni bora kuliko usingizi, hapo anakuwa katoka kwenye kilele cha fasaha na kwenda kwenye maneno yasiyo fasaha. Kwani anakuwa anatangaza jambo ambalo linafahamika hata kwa watoto wadogo, kwani anapigia kelele jambo ambalo linafa- hamika kwa wote isipokuwa yule asiyefahamu mambo ya kiakili. Kwa sababu kule kutangaza kuwa sala ni bora kuliko usingizi ni sawa na mtu anayesimama katika mkusanyiko wa watu na kutangaza eti mbili ni nusu ya nne.
Hili ndilo nililolihisi pindi nilipozuru Nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu mwaka 1375 A.H. huku nikisikia adhana toka haramu mbili takatifu. Bado akili na ubongo wangu unaamini kuwa kifungu hiki si miongoni mwa maneno ya Allah, bali kilipandikizwa kati ya vifungu vya adhana kwa sababu maalumu. Na hilo ndilo lililonifanya nichambue maudhui hii na kuandika ujumbe huu.
HITIMISHO
BIDAA BAADA YA BIDAA
Hakika historia ya adhana na iqama imejaa bidaa huku mikono ya waanzilishi wa bidaa imetumika kwa malengo ya mapendekezo ambayo hayakubaliki ndani ya sharia. Yafuatayo ni baadhi ya mambo yaliyozushwa (bidaa ) baada ya Mtume:
ADHANA YA PILI SIKU YA IJUMAA
Mwenendo wa Mtume zama zake na zama za mashekhe wawili (Abubakari na Umar) ni kuadhini pindi Imam anapopanda mimbari kwa ajili ya kutoa hotuba. Lakini baada ya watu kuongezeka zama za Khalifa wa tatu khalifa aliamrisha adhana ya pili, nayo ni adhana inayotolewa pindi unapoingia wakati wa adhana, nayo hufahamika kama adhana ya pili ya Khalifa.
Imepokewa toka kwa Shafii kuwa ni sunna siku ya ijumaa kuwa na adhana moja wakati wa kupanda mimbari10
Ikiwa adhana ni kati ya mambo yanayomuhusu Mwenyezi Mungu tu basi mwanadamu hana haki kisheria kuongeza au kupunguza chochote humo. Huku khalifa alikuwa na uwezo wa kutatua suala husika kwa njia nyingine, nayo ni njia ya kuwatangazia watu kwa njia ambazo kwa namna yoyote ile hazitoingiliana na sheria ya Kiislamu, wala haikupasa kumwamrisha muadhini atoe adhana nyingine ambayo haikuwepo kabla.
Na cha kushangaza zaidi ni kuwa hata wanazuoni wenyewe wametofautiana upande wa hukumu kuhusu adhana mbili za siku ya ijumaa, na ni ipi inayohusiana na uharamu wa kuuza uliyopo ndani ya Aya ya Mwenyezi Mungu:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا نُودِيَ لِلصَّلَاةِ مِنْ يَوْمِ الْجُمُعَةِ فَاسْعَوْا إِلَىٰ ذِكْرِ اللَّهِ وَذَرُوا الْبَيْعَ ۚ ذَٰلِكُمْ خَيْرٌ لَكُمْ إِنْ كُنْتُمْ تَعْلَمُونَ
Enyi mlioamini inaponadiwa kwa ajili ya Sala siku ya ijumaa, basi nendeni upesi kumtaja Mwenyezi Mungu na acheni biashara, hiyo ni bora kwenu ikiwa mnajua.. 62:9
2.Baada ya kipindi cha maswahaba kupita wanazuoni wa Kufa wa kihanafi walianzisha kipengele kipya cha kuhimizia (tathuwibi) nacho ni kuongeza:
حي علي الصلاة حي علي الفلاح
Njooni kwenye Sala, njooni kwenye ushindi mara mbili baada ya adhana na iqama katika adhana ya alfajiri. Na hiyo ilipendekezwa na wanazuoni wa zamani wa kihanafi iwe ni kwenye alfajiri tu, wakadai ni makuruhu nyakati nyingine, lakini wale wa sasa wakapendekeza iwe kwenye sala zote isipokuwa magharibi kwa ajili ya ufinyu wa wakati.
Na hilo ni baada ya watu kuanza kupuuzia mambo ya kidini wakasema: Kuhimiza kati ya adhana na iqama wakati wa sala kuwe kulingana na wanavyofahamu watu wenyewe wa mji husika, sawa iwe kwa kuunguruma au kusema: Sala sala au kwa namna nyingine
3.Abu Yusufu alizua jipya kwa kuruhusu tamko la kuhimiza kwa ajili ya kumtanabahisha kila anayesimamia mambo na masilahi ya Waislamu, kama vile Imam na kadhi na mfano wa hao, hivyo baada ya muadhini kumaliza adhana aseme: Amani iwe juu yako ewe kiongozi, njoo kwenye Sala njoo kwenye ushindi, kaswali Allah atakurehemu.
Katika hili wafuasi wa Shafi na baadhi ya wafuasi wa Maliki wameungana na Abu Yusufu. Pia wafuasi wa Hanbali wameungana naye kwa sharti tu iwapo Imam au mfano wake hakusikia adhana, lakini Muhammad bin Hasan amelikanusha kwa sababu watu wote ni sawa katika amri ya jamaa. Baadhi ya wafuasi wa Maliki wameungana naye katika hilo11.
KUONDOLEWA KWA KIPENGELE: NJOONI KWENYE AMALI BORA
Tumesema mwanzo kuwa bidaa katika adhana si kuingiza kipengele cha kuhimiza tu bali kuna mfano mwingine kama huo nao ni kuondolewa katika vipengele vya adhana na iqama kipengele cha:
حي علي خيرالعمل
Njooni kwenye amali bora, eti kwa lengo la kuzuwia tangazo hili ndani ya adhana lisiwe ni sababu ya kuzuwia watu kwenda kwenye jihadi. Kwa sababu iwapo watu watajua kuwa Sala ni amali bora basi watajihusisha tu na Sala na wataacha jihadi.
Mbele ya macho ya Mwenyezi Mungu hili ni kuichafua na kuigilia sheria ya Mwenyezi Mungu kwa falsafa ya kitoto. Kwani kwa hakika mwenye jukumu la kuweka sheria tangu mwanzo alifahamu tahadhari hiyo lakini pamoja na hayo yote aliingiza kipengele hicho katika adhana.
Al-Qushajiy (Mwana theiolojia wa kiashaira) amenukuu kauli ya Khalifa wa pili kwa kusema: .Khalifa wa pili alisema akiwa juu ya mimbari kuwa: Vitu vitatu vilikuwepo zama za Mtume na mimi navikataza na ninaviharamisha na nitatoa adhabu kwa atakayevitenda: Ndoa ya muda (muta.), Muta.atil-Hajji
حي علي خيرالعمل
na njooni kwenye amali bora.12
Mashia wote wamekubaliana kuwa hiki ni kifungu cha adhana na hivyo ndivyo walivyoanzia zama za Mtume mpaka leo, na hilo limekuwa ni alama yao. Wanahistoria wengi wamekuwa wakiwaita Mashia kwa jina la utani kuwa ni: Wasema حي علي خيرالعمل (njooni kwenye amali bora).
Abufarji amesema ndani ya kitabu Maqatilu Twalibina, mlango wa mauwaji ya Al-Husayni bin Ali bin Al-Hasan bin Al-Hasani bin Ali (a.s.) kuwa: Hakika yeye alitawala Madina ndipo Abdallah bin Al-Hasan Al- Aftusi akapanda kwenye mnara ambao upo kichwani kwa Mtume sehemu ya majeneza, akamwambia muadhini: Adhini kwa kutamka: حي علي خيرالعمل.Njooni kwenye amali bora. 13
Al-Halabiy amesema: Imenukuliwa toka kwa mwana wa Umar na toka kwa Zainul-Abidina Ali bin Husein (a.s.) kuwa wao wawili walikuwa ndani ya adhana zao wakisema baada ya .njooni kwenye ushindi.: .njooni kwenye amali bora.14
أُولَٰئِكَ الَّذِينَ هَدَى اللَّهُ ۖ فَبِهُدَاهُمُ اقْتَدِهْ
Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu amewaongoza, basi fuata muongozo wao.. (6:90)
•    1. Al-Imam Maliki: Al-Muwatwau: 78 namba 8 38.
•    2. . Al-Mutaqiy Al-Hindiy: Kanzul-Ummal: 8/357 namba 23252 na 23251. Na riwaya ya Abdul-Razaqi katika Al-Muswanaf: 1/474 namba1827 1828 na 1829.
•    3. Abdul-razaqiy Al-Swinaiy: Al-Muswanafu:1475 namba 1832. Pia imepokewa na Al-Mutaqiy Al-Hindiy ndani ya Kanzul-Ummal: 8/357 namba 23250
•    4. Abu Daudi: As-sunan:1/148 namba 538
•    5. Al-Khawazimiy: Jamiul-Masanidi:1/296
•    6. Al-Shaukaniy: Naylul-Awtwari: 2/38
•    7. Al-Swinaiy:Siubulul-Salami fi Sharhi bulughul-Marami:1/120
•    8. Ibnu qadamat Al-mughniy. 1/420
•    9. Al-wasailu:4/650 mlango wa 22 mlango wa adhana na Iqama Hadithi ya 1
•    10. .Al-Majimuu: 3/132
•    11. Al-mausuat Al-fiqihiyat: 2/361 neno adhana
•    12. Alaul-dini Al-Qushujiy (Alifariki mwaka 879 A.H. huko Qistwintwiniyya): Sharhul-Tajridi: Soma tafsiri yake katika kitabu chetu (Buhuthu fil-milali wal-Nihali Juzu ya 2. Chapa ya Beirut
•    13. Abul - faju Al-isfihaniy (284 - 357): Maqtalul- twalibina:297
•    14. Burhanil-Dini Al-Halabiy: As-Siyrat:2/305
MWISHO WA MSURURU WA MAKALA HIZI ZA: ADHANA SHERIA NA VIPENGELE VYAKE KWA MUJIBU WA KITABU NA SUNNA