WITO KWA WAISLAMU KUUENDEA UKWELI (SEHEMU YA PILI)

WITO KWA WAISLAMU KUUENDEA UKWELI (SEHEMU YA PILI)
MAKALA NO. 2: MTUME MUHAMMAD ALIMTEUA IMAM ALI KUWA KHALIFA BAADA YAKE
BISMIHI TA'ALA
"NA KATIKA HAYA IMEKUJIA HAKI NA MAUIDHA NA UKUMBUSHO KWA WALE WANAOAMINI." (SURATUL HUD 11:120)
Katika makala yetu Na. 1 tumeonyesha waziwazi kabisa kuwa Mitume wote waliopita pamoja na mawasii, warithi na makhalifa wao wote waliteuliwa na Allah (s.w.t) tu, na mamlaka haya ya kumchagua Mtume au Khalifa hakupewa mtu yeyote katika Ummah.
Kama ilivyokuwa kwa mitume wote waliotangulia Mtume Muhammad (s.a.w.w.) pia kwa amri ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) alimteua Imam Ali bin Abitalib (a.s) kuwa Wasii na Imam na Khalifa wa Ummah wa Kiislamu baada yake. Alhamdullilah, sisi Shia Ithna Ashariyah tunatii amri hii ya Allah (s.w.t) kama amri iliyo juu yetu na tunaamini kwa dhati kuwa Imam Ali bin Abitalib (a.s) ni Khalifa wa kwanza wa Ummah wa Kiislamu.
Katika hii makala na. 2, tutaonyesha baadhi ya ushahidi kutoka katika Qur'an tukufu, Sunnah na Hadithi za Mtume Muhammad (s.a.w.w.)na kutoka katika Historia ya Uislamu, ushahidi ambao utathibitisha bila kuacha chembe ya shaka kuwa Mtume Muhammad (s.a.w.w.) hakumteua yeyote isipokuwa Ali bin Abitalib kuwa wasiy baada yake.
Waislamu wengi na maulamaa wakubwa wa Ahlul Sunnah Wal Jama'ah baada ya kuujua ukweli huu walibadili na kuwa wafuasi wa madhehebu ya Kiislamu ya Shia Ithna Ashariya na sasa wanaamini kwa dhati kabisa kuwa Imam Ali bin Abitalib ni Khalifa wa kwanza wa Waislamu baada ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.). Maelfu ya Waislamu kila mwaka wanaikubali (wanaifuata) njia ya haki, njia iliyonyooka baada ya kufanya utafiti na baadhi yao wameandika pia vitabu juu ya utafiti wao. Baadhi ya mifano ya Wanazuoni wa Kisunni walioingia katika madhehebu ya Shia Ithna Ashariya na wakaandika vitabu juu ya utafiti wao ni :
a) Sheikh Muhammad Samawi Tijani wa Tunisia ambaye baada ya kuwa Shia, aliandika vitabu kama vile: "Hatimaye Nimeongoka", "Shia ni Wafuasi Halisi wa Sunna ya Mtume", "Waulize Wale Wanaojua", "Kuwa Pamoja na Wakweli", n.k.
b) Sheikh Muhammad Mar'iy Al-Amin Al-Antaaqi wa Uturuki ambaye aliandika kitabu chenye kurasa 520 chenye jina "Kwa nini nilichagua madhehebu ya Shia - Madhehebu ya Ahlul-Bait (a.s)?"
c) Molwi Sheikh Hafidh Ali Muhammad Fathuddin Al-Hanafi aliyeandika kitabu "Fulkun Najaat Fil Imamah Wa-Salah" (Safina ya wokovu katika Uimamu na Sala). Kitabu hiki chenye kurasa 328 kinathibitisha Uimamu wa Ali bin Abitalib na jinsi Mtume (s.a.w.w.) alivyokuwa akisali.
d) Profesa Harun Abdallah wa Nigeria ambaye ana Shahada ya juu katika Uhandisi wa Madini (Mining engineering), alifanya utafiti wa kina na aliridhika kuwa madhehebu ya Shia Ithna Ashariya ni ya kweli. Aliandika kitabu juu ya utafiti wake "The Missing Link" ambacho kina kurasa 387.
Wapendwa wasomaji, tuna uhakika kwamba baada ya kusoma makala haya na makala yatakayofuatia, mkiwa bila upendeleo akilini na ugumu wa kubadilika kutokana na mazoea na uzoefu wa nyuma, mtaukubali ukweli, na kuamini kuwa wafuasi wa madhehebu ya Ahlulbait ya Kishia wako katika njia iliyonyooka, wale ambao Mtume (s.a.w.w.) aliwatabiri: "Umma wangu baada yangu utagawanyika katika makundi 73 na wote watakuwa watu wa motoni isipokuwa kundi moja". (Al-Mustadrak ya Hakimu, Juzuu 1, Uk. 128; Sunan Abi Dawood, Juz. 4, Uk. 198; Sunan Ibn Maajah, Juz. 2, uk. 1321).
Wapendwa wasomaji, tunawaita katika njia iliyonyooka madhehebu ya Shia Ithna Ashariya, madhehebu ya Ahlul Bayt (a.s) na jiokoeni kutoka katika moto wa Jahanamu. Tafadhali jisikie huru kuja kututembelea na kuomba ushahidi na vitabu zaidi vya rejea. Waislamu walio wengi wanafuata madhehebu ya mashehe wao na babu zao kibubusa bila kuwa na ushahidi wowote, kama ilivyo kwa wasio Waislamu wanavyofuata dini za babu zao kibubusa. Qur'an Tukufu imewalaumu watu wa aina hii ambao hawafanyi utafiti ili kutafuta ukweli:
"Na wanapoambiwa Fuateni aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu, husema: Bali tutafuata yale tuliyowakuta nayo baba zetu. Je, hata kama baba zao walikuwa hawafahamu chochote wala hawakuongoka?" (Baqara 2:170).
UTHIBITISHO / USHAHIDI KWAMBA IMAM ALI NI KHALIFA WA KWANZA
Ni ukweli unaoeleweka wazi duniani kote kwamba kama unataka kumshawishi mtu kuuendea ukweli wa imani yako, na ikiwa mtu mwenyewe hakubaliani na imani yako, inabidi utumie mantiki na vitabu vyake yeye mwenyewe anavyovikubali. Kwa mfano kama unataka kumshawishi Mkristo juu ya Utume wa Nabii Muhammad (s.a.w.w.) inabidi umshawishi kwa kutumia ushahidi ulio katika kitabu chake anachokiamini: Biblia Takatifu.
Halikadhalika tutatoa ushahidi kuthibitisha kuwa Mtume Muhammad (s.a.w.w.) alimteua Imam Ali (a.s) kwa amri ya Allah (s.w.t) kuwa wasii wake, kutoka katika Qur'an Tukufu na vitabu vya Tafsiir, vitabu vya Siirah, vitabu vya Tarikh (Historia), na vitabu vya Hadithi vilivyoandikwa na Maulamaa wa Kisunni wao wenyewe.
USHAHIDI NA. 1 : HADITHUL INDHAAR AU DA'WAT DHUL ASHIRAH
Katika miaka ya mwanzo ya kutangaza Uislamu, aya hii iliposhuka: "Wa Andhir Ashiiratakal Aqrabiin" - "Na waonye jamaa zako wa karibu" (As-Shu'araa 26:214), Mtume Muhammad (s.a.w.w.) alimwita Imam Ali (a.s) na akasema: "Ewe Ali, Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameniamrisha kuwaita jamaa (ndugu) zangu wa karibu, hivyo niitie watoto wa Abdulmuttalib na tuandalie chakula kutokana na nyama ya kondoo na maziwa".
Imam Ali (a.s) anasimulia kuwa: "Niliwaita kama nilivyoamrishwa na Mtume na walihudhuria takriban watu 40 ikiwa ni pamoja na ami zake Mtume : Abutalib, Hamza, Abbas na Abulahab. Walipokusanyika, Mtume aliwaletea chakula. Ingawa chakula kilikuwa kichache, kiliwatosha kabisa wote waliokuwepo na bado chakula kingine kikabaki.
Baada ya chakula, Mtume alipotaka kuzungumza, Abulahab aliingilia kati na kusema: "Huyu mwenzenu (Muhammad (s.a.w.w.)amewaroga", hivyo watu wakasambaa bila kumsikiliza Mtume. Mtume aliniita tena na kusema: "Ewe Ali, huyu mtu ameingilia kati na kuzungumza kabla sijazungumza, hivyo waite tena kesho na utuandalie chakula kama leo".
Siku ya pili walipokuja, Mtume (s.a.w.w.) aliwaletea chakula na walikula wakashiba kama jana yake. Walipomaliza kula Mtume alisimama juu na kuwahutubia: "Enyi wana wa Abdulmuttalib, kwa hakika Mwenyezi Mungu amenituma kwa watu wote kwa ujumla na kwenu nyinyi niwaite katika Uislamu. Mwenyezi Mungu ameniamrisha kuwa ni waonye ndugu (jamaa) zangu wa karibu, hivyo ninawaita katika mambo mawili ambayo ni mepesi sana katika ulimi lakini ni mazito sana katika mizani (siku ya Kiyama). Mambo hayo ni Shahada ya Laa Ilaaha Illallah na kwamba mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Yeyote atakayezingatia (atakayeitikia) wito huu na kunisaidia atakuwa ndugu yangu, msaidizi (Waziri) wangu, Wasii wangu, Mrithi wangu na Khalifa baada yangu".
Hakuna aliyejibu isipokuwa mimi (Ali bin Abitalib) nilisimama na kusema: "Mimi Ewe Mtume wa Allah". Mtume aliniambia nikae chini na akarudia tena maneno yale. Hakuna aliyejibu isipokuwa mimi. "Mimi, Ewe Mtume wa Allah". Mtume aliniambia nikae chini na akarudia maneno yale mara ya tatu. Ilipokuwa hakuna aliyesimama isipokuwa mimi, Mtume aliweka mkono wake katika bega langu na kutangaza: "Huyu (Ali) Ni Ndugu Yangu, Wasii Wangu, Waziri (Msaidizi) Wangu, Mrithi Wangu Na Khalifa Baada Yangu Kwenu, Hivyo Msikilizeni Na Mtiini".
Wale waliohudhuria waliposikia maneno haya, walisimama juu wakicheka na kumwambia Abutalib: "(Mtume) amekuamrisha umsikilize na umtii mtoto uliyemzaa mwenyewe!"
Huu ni ushahidi na uthibitisho wa kwanza katika ushahidi mwingi uliopo, ambapo Imam Ali bin Abiitalib aliteuliwa kuwa wasiy na Khalifa baada ya Mtume. Hadithi hii inapatikana katika vitabu vifuatavyo vya Kisunni:
- Taarikh Tabari - Juz. 3, uk. 560.
- Sharh Nahjul Balagha cha Ibn Abil Hadiid, Juz. 3, uk. 263.
- Al-Kaamil cha Ibn Al-Athiir - Uk. 24.
- Taariikh Jawami cha Suyuti.
- Musnad cha Imam Ahmad bin Hambal; na vitabu vingine vingi vya Kissuni.
Kwa sababu hadithi hii ni ushahidi uliodhahiri juu ya Uimamu na Ukhalifa wa Imam Ali bin Abitalib, baadhi ya Maulamaa na waandishi wa vitabu wa Kisunni, wameanza kujaribu kuificha hadithi hii. Moja ya watu waliojaribu kuficha hadithi hii ni Muhammad Husayn Haykal wa Misri. Katika toleo la kwanza la kitabu chake "Hayaat Muhammad" (Maisha ya Muhammad (s.a.w.w.) iliitaja hadithi kwa urefu wake kama ilivyo Hadithi ya Indhaar, lakini aliiondoa katika toleo lake pili na la tatu la kitabu hicho hicho kimoja. Kwanini anaamua kuuficha ukweli na kujipendelea upande wake? Inashangaza. Qur'an tukufu inasema:
"Na msiufiche ukweli kwa uongo na wala msifiche ukweli na hali mnajua". (Baqara 2:42).
USHAHIDI / UTHIBITISHO NA. 2 - AYA YA WILAYAH
Ayatul Wilayah ni aya nyingine ya Qur'an inayothibitisha Ukhalifa wa Ali bin Abitalib (a.s) bila shaka yoyote. Aya hii ipo katika Suratul Maidah (5:55) ambayo inasema:
"Walii wenu ni Allah, Mtume wake na waumini wanaosimamisha sala na wanaotoa zakat ili hali ya kwamba wanarukuu". (5:55).
Maulamaa wote wa Tafsiir na Hadith, wa Kishia na Kisunni, wanakubali kwamba aya hii iliteremka kwa ajili ya Imam Ali bin Abitalib (a.s). Baadhi ya mifano ya wasimuliaji wa hadithi wa Kisunni ni kama ifuatayo:
a) Suyuti amesimulia katika tafsiir yake katika kitabu chake Tafsiir Durrul Manthur kwamba Ali bin Abitalib alitoa pete yake kama sadaka kwa masikini alipokuwa katika sala akirukuu; hivyo Allah akateremsha aya hii ya Wilayah. (5:55).
b) Mwanazuoni wa Kisuni Tabrani katika kitabu chake "Awsat" amesimulia kuwa: "Siku moja maskini mmoja alisimama pembeni ya Ali ambaye alikuwa katika sala akirukuu (Sunnah) na akaomba chochote, hivyo Ali akampa pete yake kutoka kidole chake alipokuwa katika Rukuu. Mtume (s.a.w.w.) alipokuja msikitini Imam Ali alimuarifu Mtume juu ya tukio hili na hapo hapo ikashuka aya ya Wilayah. (5:55).
Mtume alisoma aya hii kwa sabaha zake na akasema: "Man Kuntu Mawlahu Fa Alliyun Mawlahu. Allahumma Waali Man Waalaahu, Wa Aadi Man Aadaahu". Yaani: "Kwa yeyote ambaye mimi ni kiongozi wake, Ali ni kiongozi wake wa kumtawalia mambo yake. Ewe Mwenyezi Mungu, kuwa rafiki wa rafiki yake (na Ali) na kuwa adui wa yule anayeonyesha uadui kwa Ali".
c) Fakhruddin Raazi katika Tafsiir yake amesema kuwa Abudhar Al-Ghaffari alisimulia kuwa: Siku moja Mtume alimuomba Allah kwa kusema:
"Ewe Allah, ndugu yangu Nabii Musa alikuomba kwa kusema kipanue kifua changu, irahisishe kazi yangu na ondoa uzito katika kauli yangu, ili waelewe kile ninachokisema na nipatie Wazir (msaidizi) kutoka katika familia yangu, Haruun ndugu yangu, nizidishie nguvu kupitia kwake na mfanye awe mshirika wangu katika kazi yangu….". (Taha 20:25-32).
"Ewe Allah, mimi ni Muhammad, Mtume wako na mjumbe wako Mpendwa, hivyo ninakuomba ukipanue kifua changu, uirahisishe kazi yangu na unipe Wazir (msaidizi) kutoka katika familia yangu, Ali ndugu yangu na niongezee nguvu kupitia kwake ….".
Abudhar anaendelea kwa kusema : "Wallah, Mtume hakumaliza hata kumaliza dua yake, Jibriil akaja na kuteremsha aya ya Wilayah (5:55) ambapo Ali alitoa pete yake kama sadaka kwa masikini alipokuwa akirukuu".
Maulamaa wengine wa kisunni waliosimulia tukio hili ni : Al-Ganji Shafii katika Kifayat Al-Talib, Shablanji katika Noorul Absaar, Al-Waahidi katika Asbaabun Nuzul, Zamakhshari katika Tafsirul Kashshaf, Ibn Hajr Asqalani katika Al-Kafi Ash-Shafi, Abubakar Ahmed bin Ali Ar-Razi Al-Hanafi katika Ahkamul Qur'an, Al-Qurtubi Al-Undulusi katika Al-Jami' Li Ahkamil Qur'an, Shahabuddin Al-Aluusi katika Ruuhul Ma'aani, Sibt ibn Al-Jawzi katika Tadhkirah, na waandishi wengine wengi wa Kissuni.
Watafiti wa ukweli wanatakiwa warejee vitabu hivyo hapo juu ili waupate ukweli kuwa Ali bin Abitalib ni Walii, Imam, Khalifa na Wasii baada ya Mtume kama ilivyo katika aya hii ya Wilaya. (5:55).
Qur'an tukufu inaendelea katika aya inayofuata kwa kusema: "Na kwa wale walioukubali Uwalii wa Allah na Mtume wake na wale walioamini (Imam Ali bin Abitalib), basi kwa hakika kundi la Allah (Shia wa Imam Ali) ndio wenye kufaulu". (Maidah 5:56). Aya hii inafuatia baada tu ya aya ya Wilaya (5:55).
Kwa bahati mbaya, baadhi ya watu wanakana Uwalii na Ukhalifa wa Imam Ali bin Abitalib (a.s) mara tu baada ya Mtume (s.a.w.w). Juu yao Qur'an inasema : "Wanazitambua neema za Allah, kisha wanazikataa, na wengi wao hawana shukrani". (Nahl 16:83).
USHAHIDI / UTHIBITISHO NA. 3 - HADITH AL-MANZILAH
Wanazuoni wote wa Kishia na Kisunni wanakubali juu ya usahihi wa hadithi hii. Mtume Muhammad (s.a.w.w.) alipokwenda katika vita vya Tabuk katika mwaka wa 9 Hijria, alimuacha Imam Ali kama Khalifa wake Madina. Tabuk (katika mpaka wa Syria) ilikuwa ni mbali sana na Mtume alipaswa kumuacha mtu thabiti na mwenye imani kubwa ili kuulinda mji mkuu wa Dola ya Kiislamu Madina, kutokana na uovu wa washirikina, na hususan wanafiki ambao walikuwa wanasubiri wapate nafasi japo ndogo ili walete mtafaruku Madina. Hivyo Mtume alimteua Imam Ali ili awe Khalifa wake katika kipindi hiki ambapo Mtume alikuwa safarini.
Wanafiki walianza kumchokoza Imam Ali kuwa hakwenda Jihad ili kuokoa maisha yake na kwamba alikuwa anaogopa kifo. Imam Ali hakufurahia maneno haya, hivyo alikwenda kwa Mtume kumuomba aende naye vitani (Jihad). Mtume alijibu kuwa haikuwa vizuri kwake yeye Mtume kuondoka bila kumteua Ali kama Khalifa wake, pale Madina.
Kisha alisema: "Amaa Tardhaa An Takuuna Minni Bi Manzilati Haaruna Min Musa, Illaa Annahu Laa Nabiyya Ba'dii" - "Je hauridhiki kwamba wewe kwangu una nafasi kama ile aliyokuwa Haruni kwa Musa, isipokuwa tu hakuna Mtume baada yangu?"
Hadithi hii inathibitisha waziwazi kuwa nafasi ya Ali ni sawa na ile ya Haruni. Sasa tujiulize ni ipi ilikuwa nafasi ya Haruni ? Hebu tuiangalie nafasi ya Haruni katika Qur'an Tukufu.
"Na nipatie Waziri kutoka katika familia yangu, Harun ndugu yangu, na niongezee nguvu kupitia kwake na mfanye awe mshirika katika kazi yangu". (Taha 20:29-32).
"----- Na Musa alisema kumwambia ndugu yake Haruun; Kuwa Khalifa wangu miongoni mwa watu wangu ---- ". (A'araf 7:141).
Aya hizo hapo juu zinathibitisha kuwa Harun alikuwa ni Ndugu, Waziri, Msaidizi, Khalifa na Mrithi wa Nabii Musa. Halikadhalika kwa mujibu wa Hadithi Al-Manzilah, Imam Ali ni Ndugu, Wazir, Msaidizi, Khalifa, na Mrithi wa Mtume Muhammad baada yake. Je, bado tu hamuielewi na kuitii amri ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.) enyi Waislamu!
Hadithi ya Manzilah imesimuliwa na mamia ya Wasimuliaji wa hadithi wa Kisunni, baadhi yao ni kama ifuatavyo:
- Sahih Bukhari, Baab Ghazwat Tabuk, Juz. 3, uk. 54.
- Sahih Bukhari, Baab Manaqib Ali Bin Abitalib, Juz. 2, uk. 185.
- Sahih Muslim, Baab Fazail Ali, Juz. 2, uk. 236.
- Musnad Ahmad bin Hambal, Juz. 1, uk. 98 na uk. 236.
- Hakim katika Al-Mustadrak, Juz. 3, uk.109.
- Suyuti katika Tarikhul Khulafa, uk. 65.
- Ibn Al-Kathir katika Usudul Ghaabah, Juz. 4, uk. 26.
- Ibn Hajr Al-Asqalani katika Isaabah, Juz. 2, uk. 507.
- An-Nasai katika Khasais, Uk. 7 na Uk. 15.
- Taariikh Ibn Asaakir, Juz. 4, Uk. 96 n.k.
Soma makala Na. 3 kwa ushahidi zaidi juu ya Ukhalifa wa Imam Ali bin Abitalib (a.s.). Qur'an Tukufu inasema:
"Na sema: Ukweli sasa umefika (umekuja), na uongo umeondoka, na daima uongo huwa ni wenye kuondoka". (Bani Israel 17:81).

ITAENDELEA KATIKA MAKALA IJAYO