BIBI FATIMAH ZAHARA (A.S) 5

HISTORIA YA MASUMIN (A.S)

MA'ASUMAH WA PILI

BIBI FATIMAH ZAHARA (A.S)

Sehemu ya Tano

FATIMAH ZAHARA NDANI YA HADITH za Mtume (s.a.w.w).

16. FATIMAH ZAHARA (a.s) NA ADAM (a.s)

Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.w) anasema: Mwenyezi Mungu alipomuumba Adamu Baba wa watu na kumpulizia roho yake na kupata uhai, Adam aligeukia kuliani mwa Ar-shi mara akaona nuru tano za watu wamesujudu na wengine wamerukuu. Adamu akasema: Ewe Mola wangu ulishaumba yeyote yule kwa udongo kabla yangu?

Mwenyezi Mungu akasema: Hapana.

Adamu (a.s) akasema: Na hawa watu watano ambao ninawaona wanakipambo changu na sura yangu ni akina nani? Mwenyezi Mungu akasema: Hawa watano ni katika watoto wako, kama si wao nisingekuumba wewe. Hawa watano nimewagawia majina katika majina yangu, na kama si wao nisingeumba pepo (mabustani mazuri kwa ajili ya watiifu) wala moto (Gereza lenye mateso na adhabu kali zenye kuumiza kwa ajili ya waasi) wala Ar-shi (ikulu iliyo katika milki ya Allah) wala Kursiyyu (kiti cha enzi) nisingeumba mbingu na Ardhi, wala Malaika watu na Majini.

Mwenyezi Mungu anasema: Mimi ndiye Mahmoud huyu hapa ni Muhammad, Mimi ndiye Al Alliyyu na huyu hapa ndiye Ally, Mimi ndiye Faatwir na huyu hapa ndiye Fatimah, Mimi ndiye Al Ihsanu na huyu ndiye Hassan, Mimi ndiye Al Muhsinu na huyu ndiye Hussein.

Mwenyezi Mungu anasema: Nimeapa kwa utukufu wangu hatokuja kwangu yeyote yule na chuki ya kumchukia mmoja wao chuki hiyo hata kama ni kidogo sana sawa na punje ya hardali isipokuwa mtu huyo nitamuweka katika Gereza la mateso (moto) na sitojali chochote katika matendo yake yaliyo ya utii.

Ewe Adam hawa ndiyo marafiki wangu katika viumbe wangu, kupitia hao ninaokoa na kupitia kwao naangamiza, kama una haja yoyote kwangu tawasali na hawa watano.

Mtukufu Mtume Muhammad saww anasema: Sisi (watano na kizazi chetu) ndiyo Jahazi lenye kuokoa atakaye fungamana nalo (ataongoka na) ataokoka na atakaye jiweka mbali nalo (atapotea na) kuangamia na yeyote atakaye kuwa na haja ya kutatuliwa na Mwenyezi Mungu ni aombe kupitia kwetu Ahlul Bayt.

17. FATIMAH ZAHARA (A.S) na JAHAZI LA NUHU  (A.S)

Mtukufu Mtume (s.a.w.w) anasema: Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:

وَحَمَلْنَاهُ عَلَىٰ ذَاتِ أَلْوَاحٍ وَدُسُرٍ .

Na tukamchukua kwenye ile (Jahazi iliyotengenezwa) kwa mbao na misumari. Qur-an: 54:13.

Mtukufu Mtume saww anasema: Mbao (Al wahu) ni mamiti yaliyo tengenezea Jahazi, misumari (Dusuri) ni Sisi (Ahlubaiti Rasulallah) ndiyo wenyewe, kwani Nuhu alitawasali kupitia kwetu Ahlul Bayt, alisema kabla ya kuanza safari: Ewe Mola wangu, Ewe msaada wangu kwa huruma zako na ukarimu wako nisaidie kwa kupitia hizi nafsi tano tukufu, Muhammad, Aliy, Hassan, Hussain na Fatimah ambao wao kwa ujumla ni watukufu wakarimu, ulimwengu uimarike kwa sababu yao, unisaidie kupitia majina yao wewe peke yako ndiye utaweza kuielekeza upande uliyo na Njia Iliyonyooka.

Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.w) anasema: Kama siyo sisi (Ahlubaiti) Jahazi lisingetembea na watu wake.

18. MALAIKA a.s wamsaidia KUFANYA KAZI Bibi FATIMAH ZAHARA a.s:

Kutoka kwa Ummu Ayman anasema: Siku moja nilienda kumtembelea kiongozi wangu Fatimah Zahara (a.s) nyumbani kwake, siku hiyo ilikuwa na joto kali la kiangazi nikaenda hadi mlangoni kwake, nikaona mlango umefungwa, nikaangalia kupitia mianya ya mlango, mara nikamuona Fatimah Zahara as amelala karibu na kihuri, na nikaona kihuri kikitwanga ngano chenyewe, na ile hali kikizunguka pasipo mkono wa kukizungusha, na bembea la mtoto likitikisika pembeni yake, na Hussein (a.s) amelala ndani ya bembea, nikaona mkono (ukivuta Tasbihi) ukimtakasa Mwenyezi Mungu na kuzihesabu Tasbihi karibu na mkono wa Fatimah Zahara (a.s).

Nikashangaa hayo yote niliyoyaona nikamwacha Fatimah nikaondoka hadi kwa kiongozi wangu Mtume wa Mwenyezi Mungu nikamsalimia, na nikamwambia: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Hakika mimi nimeona maajabu sijawahi kuona mfano wake kamwe.

Mtukufu Mtume (s.a.w.w) akaniambia umeona nini Ewe Ummu Ayman?

Nikasema hakika mimi nilitaka kwenda kwa kiongozi wangu Fatimah Zahara (a.s) nikakuta mlango umefungwa, mara mimi nikaona kihuri kinatwanga ngano na kujizungusha pasipo mkono wa kukizungusha na nikaona bembea la Hussein as likijitikisa pasipo mkono wa kulitikisa na nikaona mkono unahesabu Tasbihi Ukimtakasa Mwenyezi Mungu Mtukufu karibu na mkono wa Fatimah Zahara (a.s) na sioni mwenye mkono huo!

Yakanishangaza sana haya niliyoyaona ewe kiongozi wangu!.

Mtukufu Mtume (s.a.w.w) akasema: Ewe Ummu Ayman! Jua hakika Fatimah Zahara as alikuwa na saumu na alikuwa kachoka kwa njaa, ni muda mrefu tangu alipoamka, Mwenyezi Mungu akamtia usingizi akalala, utakatifu ni wa Mwenyezi Mungu asiyelala. Mwenyezi Mungu akatuma wakili Malaika amfanyie chakula cha familia yake, Mwenyezi Mungu akatuma Malaika mwingine wa kutikisa bembea la mtoto wake Hussein (a.s) asije akamsumbua katika usingizi wake. Mwenyezi Mungu akatuma Malaika mwingine, amtakase Mwenyezi Mungu Mtukufu karibu na mkono wa Fatimah Zahara as ili malipo ya Tasbihi aendelee kuyapata yeye. Hakika kwa Fatimah haifai kupumzika kumtaja Mwenyezi Mungu. Akilala Mwenyezi Mungu anafanya malipo ya Tasbihi ya yule Malaika kwa ajili ya Fatimah (a.s).

Ummu Ayman akasema: Niambie ni nani aliyekuwa akitwanga na nani aliyekuwa anatikisa bembea la Hussein as na kumbembeleza na nani aliyekuwa akifanya Tasbihi?

Mtukufu Mtume (s.a.w.w) akatabasam hali ya kucheka na akasema: Mtwangaji alikuwa Jibrilu (a.s), mbembelezaji wa Hussain (a.s) ni Mikael (a.s) na mfanya Tasbihi ni Israfil (a.s)

Hadith hizi zinapatikana pande zote ahlisuna na Shi'ah

19. UTUKUFU WA FATIMAH ZAHARA AS.

FATIMAH Zahara as anajukumu kubwa katika kujenga na kuipa nguvu misingi ya dini ya kiislam na kuimarisha nguzo zake, ambapo anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika hadithi Quds: "Na Lau kama si Fatimah nisingewaumba nyinyi (Mtume Muhammad saww na wasii wake Ally bin Abi Twalib as)", hivyo Fatimah Zahara ni zawadi ya Mwenyezi Mungu na tuzo la uchamungu kwa Mtukufu Mtume saww pale Mwenyezi Mungu Aliposema:

إِنَّا أَعْطَيْنَاكَ الْكَوْثَرَ .

Hakika tumekupa Kheir nyingi sana. Quran: 108 :1

NA neema nyingi, naye ndio siri ya uimamu na kitovu cha Kuumbwa Maimamu Maasumu as ambapo yeye ndio ameupa uhai, nuru na amesimamisha dini ya haki kupitia kwa watoto wake na misimamo yake ya kihistoria.. Hadi leo hii unaona Uislamu umehifadhika kwa fadhila za kupatikana kwake na kwa kuwepo Imamu Mahdi (a.s) yeye ni baraka katika baraka za Fatimah (a.s).

Kuna hadithi nyingi sana mutawatiri zinazoelezea nafasi ya Fatimah Zahara (a.s) na zimepokewa na pande mbili ahlisuna na Shi'ah katika vitabu vyao mbali mbali. Na kama ambavyo kutukuza cheo chake Fatimah Zahara (a.s) ni kutukuza hadhi ya unabii na dini ambayo ameiteremsha Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Fuatana nami sehemu ya Sita Hisoria ya Maasumah Fatimah bint Muhammad (s.a.w.w)

Rejea: Shawahidu Tanzil Jz 1 UK 414

Najahul Haq UK 190

Tafsir Burhan cha Baharan Jz 3 UK 170

Nurul Abswar, Tafsir Tha'alabi katika tafsir ya Aya ya 54 suratul Furqan.

Yanabiul Mawaddah Jz 1 UK 118. Na UK 10-11 na babul Awal UK 14.

Tadhkiratul Khawas cha Ibn Jawz UK 46

Kashiful Ghumah Jz 2 UK 48

Dalailun Nubuwah Jz 2 UK 148.