KUANGAMIZWA KWA KAUMU YA NABII SHU`AIB A.S

KUANGAMIZWA KWA KAUMU YA NABII SHU`AIB A.S

Watu wa kaumu ya Shu`aib wakamsingizia kuwa ati Mtume wao karogwa. Na wakamwambia: "Ungelikuwa kweli ni Mtume basi ungetuijia kwa umbo la Kimalaika au mwenye sifa tofauti na mwanadamu. Kwa hiyo tunakudhania wewe ni muongo." Kama alivyosema Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Surat Sh-shua`raa aya ya 185 na ya 186,

{قَالُوا إِنَّمَا أَنْتَ مِنْ الْمُسَحَّرِينَ * وَمَا أَنْتَ إِلاَّ بَشَرٌ مِثْلُنَا وَإِنْ نَظُنُّكَ لَمِنْ الْكَاذِبِينَ}

Maana yake, "Wakasema: "Hakika wewe ni miongoni mwa waliorogwa. Na wewe si chochote ila ni mtu tu kama sisi, na kwa yakini tunakuona wewe ni katika waongo." Wakazidi kumwambia: "Ikiwa wewe ni Mtume wa kweli basi tuangushie vipande vya mbingu." Kama alivyosema Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Surat Sh-shua`raa aya ya 187, "

{ فَأَسْقِطْ عَلَيْنَا كِسَفًا مِنْ السَّمَاءِ إِنْ كُنْتَ مِنْ الصَّادِقِينَ }

Maana yake, "Hebu tuangushie vipande vya mbingu ikiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli." Nabii Shu`aib akawajibu majibu ya mtu muumini mkweli wa imani kama ilivyokuja katika Surat Sh-shua`raa aya ya 188, "

{…رَبِّي أَعْلَمُ بِمَا تَعْمَلُونَ }

Maana yake, "…Mola wangu anajua zaidi mnayoyatenda." Wakaja wakubwa waliotakabari wa kaumu yake kwa Mtume Shu`aib wakimtishia na kumwahidi kwamba watamtoa katika mji wao yeye pamoja na wale waliomwamini. Kama alivyotusimulia Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Suratil A`araaf aya ya 88, "

{قَالَ الْمَلأُ الَّذِينَ اسْتَكْبَرُوا مِنْ قَوْمِهِ لَنُخْرِجَنَّكَ يَاشُعَيْبُ وَالَّذِينَ آمَنُوا مَعَكَ مِنْ قَرْيَتِنَا أَوْ لَتَعُودُنَّ فِي مِلَّتِنَا…}

Maana yake, "Wakuu waliotakabari katika kaumu yake wakasema: "Ewe Shu`aib! Tutakutoa wewe pamoja na wale waliokuamini katika mji wetu, au mrejee katika mila yetu…" Nabii Shu`aib akawajibu kama alivyosema Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Suratil A`araaf aya ya 88, "

…أَوَلَوْ كُنَّا كَارِهِينَ

Maana yake, "…Ingawa (sisi) tunaichukia (hiyo mila yenu)?" Nabii Shu`aib akawajibu jibu la mwisho kabisa. Kama ilivyokuja katika Suratil A`araaf aya ya 89, "

قَدْ افْتَرَيْنَا عَلَى اللَّهِ كَذِبًا إِنْ عُدْنَا فِي مِلَّتِكُمْ بَعْدَ إِذْ نَجَّانَا اللَّهُ مِنْهَا وَمَا يَكُونُ لَنَا أَنْ نَعُودَ فِيهَا إِلاَّ أَنْ يَشَاءَ اللَّهُ رَبُّنَا وَسِعَ رَبُّنَا كُلَّ شَيْءٍ عِلْمًا عَلَى اللَّهِ تَوَكَّلْنَا رَبَّنَا} {افْتَحْ بَيْنَنَا وَبَيْنَ قَوْمِنَا بِالْحَقِّ وَأَنْتَ خَيْرُ الْفَاتِحِينَ

Maana yake, "Bila shaka itakuwa tumemzulia uwongo Mwenyezi Mungu tukirudi katika mila yenu baada ya kwishakutuokoa nayo Mwenyezi Mungu. Wala haiwi kwetu sisi kuirejea mila hiyo, ila akitaka Mwenyezi Mungu Mola wetu. Ujuzi wa Mola wetu umeenea katika kila kitu. Kwa Mwenyezi Mungu tunategemea. Ewe Mola wetu! Tuhukumie baina yetu na kaumu yetu kwa haki, Nawe Ndiye Mbora wa wanao hukumu." Ikawa tena hakuna faida ya kuwaita katika imani ikabaki mvutano ima Nabii Shu`aib na wafuasi wake warejee katika mila ya kikafiri, au watoke katika nyumba zao na nchi yao na mali yao kwa dhulma na uadui. Lakini Mola wao aliwanusuru kutokana na makafiri, ikawashika adhabu ya siku ya kivuli. Mwenyezi Mungu S.W.T. aliufunga upepo likazidi joto kupita kiasi, na akalifumba jua kwa siku saba mfululizo ikawa kivuli, na likaja joto kali zaidi. Baadhi yao walikufa kwa sababu ya joto kali; na wengineo waliobaki wakafa kwa mtetemeko wa ardhi. Kama ilivyokuja katika Surat Sh-shua`raa aya ya 189, "

{فَكَذَّبُوهُ فَأَخَذَهُمْ عَذَابُ يَوْمِ الظُّلَّةِ إِنَّهُ كَانَ عَذَابَ يَوْمٍ عَظِيمٍ}

Maana yake, "Basi walimkanusha, na ikawashika adhabu ya siku ya kivuli. Hakika hiyo ilikuwa adhabu ya siku kubwa." Na pia Mwenyezi Mungu S.W.T. kasema katika Suratil A`araaf aya ya 91, "

{فَأَخَذَتْهُمْ الرَّجْفَةُ فَأَصْبَحُوا فِي دَارِهِمْ جَاثِمِينَ}

Maana yake, "Basi tetemeko la ardhi likawatoa roho zao, na wakaamkia majumbani mwao wamejifudikiza, wamekwishakufa." Akawa Nabii Shu`aib hana lawama kwani yeye aliwafikishia kwao ujumbe wa Mola wake lakini wao wenyewe hawakumsikiliza maneno yake. Na mwisho wa wakaidi ni kuangamia. Hivyo Nabii Shu`aib alipoona adhabu iliyowashukia na kuangamizwa kaumu yake, aliwaachilia mbali na akajivua nafsi yake asiwe mkosa pamoja nao akasema kama ilivyokuja katika Suratil A`araaf aya ya 93, "

{… يَا قَوْمِ لَقَدْ أَبْلَغْتُكُمْ رِسَالاتِ رَبِّي وَنَصَحْتُ لَكُمْ فَكَيْفَ آسَى عَلَى قَوْمٍ كَافِرِينَ}

Maana yake, "…Enyi kaumu yangu! Nimekufikishieni ujumbe wa Mola wangu, na nimekunasihini; basi vipi nihuzunike juu ya watu makafiri?"

MWISHO