Nabii Issa (A.S) katika Quran.


NABII ISSA (A.S) KATIKA QUR"ANI

Na hakika tulimpa Musa Kitabu na tukafuatisha baada yake Mitume wengine. Na tukampa Isa (Yesu), mwana wa Mariamu, hoja zilizo waziwazi, na tukamtia nguvu kwa Roho Takatifu. Basi kila walipo kufikieni Mitume kwa yale ambayo hayapendwi na nafsi zenu, mlijivuna; wengine mkawakanusha, na wengine mkawauwa. 2:87

Semeni nyinyi: Tumemuamini Mwenyezi Mungu na yale tuliyo teremshiwa sisi, na yaliyo teremshwa kwa Ibrahim na Ismail na Is-hak na Yaakub na wajukuu zake, na waliyo pewa Musa na Isa (Yesu), na pia waliyo pewa Manabii wengine kutoka kwa Mola wao Mlezi; hatutafautishi baina ya yeyote katika hao, na sisi tumesilimu kwake. 2:136

MITUME hao tumewatukuza baadhi yao juu ya wengineo. Katika wao wapo ambao Mwenyezi Mungu alisema nao, na wengine akawapandisha vyeo. Na tukampa Isa (Yesu) mwana wa Mariyam hoja zilizo wazi, na tukamtia nguvu kwa Roho Takatifu. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu alipenda wasingeli pigana walio kuwa baada yao baada ya kuwajia hoja zilizo wazi. Lakini walikhitalifiana. Basi wapo kati yao walio amini, na wengine kati yao walio kufuru. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu alipenda wasingeli pigana. Lakini Mwenyezi Mungu hutenda atakavyo. 2:253

Na pale Malaika walipo sema: Ewe Maryamu! Hakika Mwenyezi Mungu anakubashiria (mwana) kwa neno litokalo kwake. Jina lake ni Masihi Isa (Yesu) mwana wa Maryamu, mwenye hishima katika dunia na Akhera, na miongoni mwa walio karibishwa (kwa Mwenyezi Mungu).3:45

Isa (Yesu) alipo hisi kuwa kati yao pana ukafiri alisema: Nani wasaidizi wangu kwa Mwenyezi Mungu? Wanafunzi wake wakasema: Sisi ni wasaidizi wa Mwenyezi Mungu. Tumemuamini Mwenyezi Mungu, na shuhudia kwamba sisi hakika ni Waislamu. 3:52

Hakika mfano wa Isa (Yesu) kwa Mwenyezi Mungu ni kama mfano wa Adam; alimuumba kwa udongo kisha akamwambia: Kuwa! Basi akawa. 3:59

Sema: Tumemuamini Mwenyezi Mungu, na tuliyo teremshiwa sisi, na aliyo teremshiwa Ibrahim, na Ismail, na Is-haak na Yaakub na wajukuu zao, na aliyo pewa Musa na Isa (Yesu) na Manabii wengine kutoka kwa Mola wao Mlezi. Hatubagui baina yao hata mmoja, na sisi ni wenye kusilimu kwake. 3:84

Na kwa kusema kwao: Sisi tumemuuwa Masihi Isa (Yesu), mwana wa Maryamu, Mtume wa Mwenyezi Mungu - nao hawakumuuwa wala hawakumsalibu, bali walifananishiwa tu. Na hakika walio khitalifiana katika haya wamo katika shaka nayo. Wao hawana ujuzi nayo wowote, ila ni kufuata dhana tu. Wala hawakumuuwa kwa yakini. 4:157

Bali Mwenyezi Mungu alim- tukuza kwake, na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima. 4:158
Hakika Sisi tumekuletea wahyi wewe kama tulivyo wapelekea wahyi Nuhu na Manabii walio kuwa baada yake. Na tulimpelekea wahyi Ibrahim na Ismail na Is-haka na Yaakub na wajukuu zake, na Isa (Yesu) na Ayub na Yunus na Harun na Suleiman, na Daud tukampa Zaburi. 4:163

Na Mitume tulio kwisha kukuhadithia kabla yake, na Mitume wengine hatukukuhadithia. Na Mwenyezi Mungu alinena na Musa kwa maneno. 4:164
Mitume hao ni wabashiri na waonyaji, ili watu wasiwe na hoja juu ya Mwenyezi Mungu baada ya kuletewa Mitume. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima. 4:165

Lakini Mwenyezi Mungu anayashuhudia aliyo kuteremshia wewe. Ameyateremsha kwa kujua kwake - na Malaika pia wanashuhudia. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa shahidi.4:166
Hakika walio kufuru na wakazuilia Njia ya Mwenyezi Mungu, wamekwisha potelea mbali. 4:167
Hakika wale walio kufuru na wakadhulumu hawi Mwenyezi Mungu kuwasamehe wala kuwaongoa njia. (4:168)
Isipo kuwa njia ya Jahannamu. Humo watadumu milele. Na hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi. 4:169

Enyi Watu! Amekwisha kujieni Mtume huyu na haki itokayo kwa Mola wenu Mlezi. Basi aminini, ndiyo kheri yenu. Na mkikakanusha basi hakika viliomo mbinguni na duniani ni vya Mwenyezi Mungu tu. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Mwenye hikima. 4:170

Enyi Watu wa Kitabu! Msipite kiasi katika dini yenu, wala msimseme Mwenyezi Mungu ila kwa lilio kweli. Hakika Masihi Isa (Yesu) mwana wa Maryamu ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na neno lake tu alilo mpelekea Maryamu, na ni roho iliyo toka kwake. Basi Muaminini Mwenyezi Mungu na Mitume wake. Wala msiseme: Utatu. Komeni! Itakuwa kheri kwenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mungu mmoja tu. Ametukuka Yeye na kuwa na mwana. Ni vyake Yeye vyote viliomo katika mbingu na katika ardhi. Na Mwenyezi Mungu ni Mtegemewa wa kutosha. 4:171

Masihi hataona uvunjifu kuwa mtumwa wa Mwenyezi Mungu, wala Malaika walio karibishwa. Na watakao ona uvunjifu utumwa wa Mwenyezi Mungu na kufanya kiburi, basi atawakusanya wote kwake. 4:172
Na ama walio amini na wakatenda mema atawalipa ujira wao sawa sawa, na atawazidishia kwa fadhila yake. Na ama wale walio ona uvunjifu na wakafanya kiburi, basi atawaadhibu adhabu iliyo chungu. Wala hawatopata mlinzi wala wa kuwanusuru asiye kuwa Mwenyezi Mungu. 4:173
Enyi watu! Umekufikieni ushahidi kutoka kwa Mola wenu Mlezi. Na tumekuteremshieni Nuru iliyo wazi. 4:174
Ama wale walio muamini Mwenyezi Mungu, na wakashikamana naye, basi atawatia katika rehema yake na fadhila, na atawaongoa kwenye Njia Iliyo Nyooka. 4:175

Na tukawafuatishia hao Isa (Yesu) bin Maryamu kuyahakikisha yaliyo kuwa kabla yake katika Taurati, na tukampa Injili iliyomo ndani yake uwongofu, na nuru na inayo sadikisha yaliyo kuwa kabla yake katika Taurati, na uwongofu na mawaidha kwa wachamngu. 5:46
Na wahukumu Watu wa Injili kwa yale aliyo teremsha Mwenyezi Mungu ndani yake. Na wasio hukumu kwa yale aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu basi hao ndio wapotofu. 5:47
Na tumekuteremshia wewe (Muhamad), kwa haki, Kitabu hichi kinacho sadikisha yaliyo kuwa kabla yake katika Vitabu na kuyalinda. Basi hukumu baina yao kwa aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu, wala usifuate matamanio yao ukaacha Haki iliyo kujia. Kila mmoja katika nyinyi tumemwekea sharia yake na njia yake. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli taka ange kufanyeni nyote umma mmoja, lakini ni kukujaribuni kwa aliyo kupeni. Basi shindaneni kwa mambo ya kheri. Kwa Mwenyezi Mungu ndio marejeo yenu nyote, na atakuja kuwaambieni yale mliyo kuwa mkikhitalifiana. 5:48

Na wahukumu baina yao kwa aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu, wala usifuate matamanio yao. Nawe tahadhari nao wasije kukufitini ukaacha baadhi ya aliyo kuteremshia Mwenyezi Mungu. Na wakigeuka, basi jua kwamba hakika Mwenyezi Mungu anataka kuwasibu kwa baadhi ya dhambi zao. Na hakika wengi wa watu ni wapotofu. 5:49
Je, wao wanataka hukumu za Kijahiliya (kijinga)? Na nani aliye mwema zaidi katika kuhukumu kuliko Mwenyezi Mungu kwa watu wenye yakini? 5:50
Walilaaniwa walio kufuru miongoni mwa Wana wa Israili kwa ulimi wa Daud na wa Isa (Yesu) mwana wa Maryamu. Hayo ni kwa sababu waliasi na wakawa wanapindukia mipaka. 5:78

Walikuwa hawakatazani maovu waliyo kuwa wakiyafanya. Hakika ni maovu yalioje mambo waliyo kuwa wakiyafanya! 5:79
Na pale Mwenyezi Mungu atapo sema: Ewe Isa (Yesu) bin Maryamu! Kumbuka neema yangu juu yako, na juu ya mama yako, nilipo kutia nguvu kwa Roho Takatifu, ukazungumza na watu katika utoto na utuuzimani. Na nilivyo kufunza kuandika na hikima na Taurati na Injili. Na ulipo tengeneza udongo sura ya ndege, kwa idhini yangu, kisha ukapuliza ikawa ndege kwa idhini yangu; na ulipo waponesha vipofu na wakoma kwa idhini yangu; na ulipo wafufua wafu kwa idhini yangu; na nilipo kukinga na Wana wa Israili ulipo wajia na hoja zilizo wazi, na wakasema walio kufuru miongoni mwao: Haya si lolote ila ni uchawi mtupu! 5:110

Na nilipo wafunulia Wanafunzi kwamba waniamini Mimi na Mtume wangu, wakasema: Tumeamini na shuhudia kuwa sisi ni Waislamu. 5:111
Wanafunzi walipo sema: Ewe Isa (Yesu) bin Maryamu! Je, Mola wako Mlezi anaweza kututeremshia chakula kutoka mbinguni? Akasema: Mcheni Mwenyezi Mungu ikiwa nyinyi ni Waumini. 5:112
Wakasema: Tunataka kukila chakula hicho, na nyoyo zetu zitue, na tujue kwamba umetuambia kweli, na tuwe miongoni mwa wanao shuhudia.5:113

Akasema Isa (Yesu) bin Maryamu: Ewe Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wetu! Tuteremshia chakula kutoka mbinguni ili kiwe Sikukuu kwa ajili ya wa mwanzo wetu na wa mwisho wetu, na kiwe ni Ishara itokayo kwako. Basi turuzuku, kwani Wewe ndiye mbora wa wanao ruzuku. 5:114
Mwenyezi Mungu akasema: Hakika Mimi nitakuteremshieni hicho. Lakini yeyote katika nyinyi atakaye kanya baadae, basi hakika Mimi nitampa adhabu nisiyopata kumpa yeyote katika walimwengu. 5:115
Na pale Mwenyezi Mungu atakapo sema: Ewe Isa (Yesu) bin Maryamu! Ati wewe uliwaambia watu: Nifanyeni mimi na mama yangu kuwa ni miungu badala ya Mwenyezi Mungu? (Na Isa (Yesu)) atasema: Subhanaka, Wewe umetakasika! Hainifalii mimi kusema ambayo si haki yangu. Ikiwa nilisema basi bila ya shaka umekwisha yajua. Wewe unayajua yaliyo ndani ya nafsi yangu, lakini mimi siyajui yaliyo katika nafsi yako. Hakika Wewe ndiye Mjuzi mkubwa wa yaliyo fichikana. 5:116

Sikuwaambia lolote ila uliyo niamrisha, nayo ni: Muabuduni Mwenyezi Mungu, Mola wangu Mlezi na Mola wenu Mlezi. Na mimi nilikuwa shahidi juu yao nilipo kuwa nao. Na ulipo nifisha ukawa Wewe ndiye Muangalizi juu yao. Na Wewe ni shahidi juu ya kila kitu. 5:117
Ukiwaadhibu basi hao ni waja wako. Na ukiwasamehe basi Wewe ndiye Mwenye nguvu na Mwenye hikima. 5:118
Mwenyezi Mungu atasema: Hii ndiyo Siku ambayo wasemao kweli utawafaa ukweli wao. Wao watapata Bustani zipitazo mito kati yake. Humo watadumu milele. Mwenyezi Mungu amewawia radhi, nao wawe radhi naye. Huku ndiko kufuzu kukubwa. 5:119
Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi na vilivyomo. Naye ni Muweza wa kila kitu. 5:120

Na Zakaria na Yahya na Isa (Yesu) na Ilyas. Wote walikuwa miongoni mwa watu wema. 6:85
(Mtoto) akasema: Hakika mimi ni mtumwa wa Mwenyezi Mungu. Amenipa Kitabu, na amenifanya Nabii. 19:30
Na amenijaalia ni mwenye kubarikiwa popote pale niwapo. Na ameniusia Sala na Zaka maadamu ni hai. 19:31
Na nimtendee wema mama yangu. Wala hakunifanya niwe jeuri, mwovu. 19:32

Na amani iko juu yangu siku niliyo zaliwa, na siku nitakayo kufa, na siku nitakayo fufuliwa kuwa hai. 19:33
Huyo ndiye Isa (Yesu) mwana wa Maryamu. Ndiyo kauli ya haki ambayo wanaifanyia shaka. 5:34
Haiwi kwa Mwenyezi Mungu kuwa na mwana, Subhanahu, Yeye ametakasika! Anapo lihukumia jambo basi huliambia tu: Kuwa! Likawa. 19:35
Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mola wangu Mlezi, na Mola wenu Mlezi. Basi muabuduni Yeye. Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka. 19:36
Lakini makundi yakakhitalifiana wao kwa wao. Basi ole wao hao walio kufuru kwa kuhudhuria Siku iliyo kuu! 19:37

Watasikia na wataona vizuri vilioje Siku watakayo tufikia! Lakini madhaalimu sasa wamo katika upotofu ulio dhaahiri. 19:38
Na waonye siku ya majuto itapo katwa amri. Nao wamo katika ghafla, wala hawaamini. 19:39
Na tulipo chukua ahadi kwa Manabii na kwako wewe, na Nuhu na Ibrahim na Isa (Yesu) mwana wa Mariamu, na tulichukua kwao ahadi ngumu, 33:7
Ili (Mwenyezi Mungu) awaulize wakweli juu ya ukweli wao. Na amewaandalia makafiri adhabu chungu. 33:8
Amekuamrisheni Dini ile ile aliyo muusia Nuhu na tuliyo kufunulia wewe, na tuliyo wausia Ibrahim na Musa na Isa (Yesu), kwamba shikeni Dini wala msifarikiane kwayo. Ni magumu kwa washirikina hayo unayo waitia. Mwenyezi Mungu humteua kwake amtakaye, na humwongoa kwake aelekeaye. 42:13

Na hawakufarikiana ila baada ya kuwajia ilimu kwa sababu ya husuda iliyo kuwa baina yao. Na lau kuwa haikwisha tangulia kauli kutoka kwa Mola wako Mlezi ya kuakhirisha mpaka muda maalumu, basi bila ya shaka palingeli hukumiwa baina yao. Na hakika walio rithishwa Kitabu baada yao wanakitilia shaka inayo wahangaisha. 42:14 Basi kwa haya waite! Nawe simama sawa sawa kama ulivyo amrishwa, wala usiyafuate matamanio yao. Na sema: Naamini aliyo teremsha Mwenyezi Mungu katika Vitabu. Na nimeamrishwa nifanye uadilifu baina yenu. Mwenyezi Mungu ni Mola wetu Mlezi, na Mola wenu Mlezi. Sisi tuna jukumu kwa vitendo vyetu, na nyinyi mna jukumu kwa vitendo vyenu. Hapana kuhojiana baina yetu na nyinyi. Na Mwenyezi Mungu atatukusanya pamoja, na marejeo ni kwake. 42:15

Hakuwa yeye (Isa (Yesu)) ila ni Mtumwa tuliye mneemesha na tukamfanya ni mfano kwa Wana wa Israili. 43:59
Na alipo kuja Isa (Yesu) na dalili zilizo wazi, alisema: Nimekujieni na hikima, na ili nikuelezeni baadhi ya yale mliyo khitalifiana. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na mnit'ii mimi. 43:63
Kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mola wangu Mlezi, na ni Mola wenu Mlezi. Basi Muabuduni Yeye tu. Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka. 43:64

Lakini makundi kwa makundi yao yalikhitalifiana wao kwa wao. Ole wao walio dhulumu kwa adhabu ya siku chungu. 43:65
Je! Nini wanangojea ila Saa iwajie kwa ghafla na wala wao hawatambui? 43:66
Siku hiyo marafiki watakuwa ni maadui, wao kwa wao, isipo kuwa wachamngu. 43:67
Enyi waja wangu! Hamtakuwa na khofu siku hiyo, wala hamtahuzunika. 43:68
Ambao waliziamini Ishara zangu na walikuwa Waislamu. 43:69

Ingieni Peponi, nyinyi na wake zenu; mtafurahishwa humo. 43:70
Watakuwa wanapitishiwa sahani za dhahabu na vikombe; na vitakuwamo ambavyo nafsi zinavipenda na macho yanavifurahia, na nyinyi mtakaa humo milele. 43:71
Na hiyo ni Pepo mliyo rithishwa kwa hayo mliyo kuwa mkiyafanya. 43:72
Mnayo humo matunda mengi mtakayo yala. 43:73
Kwa hakika wakosefu watakaa katika adhabu ya Jahannamu. 43:74
Hawatapumzishwa nayo na humo watakata tamaa. 43:75
Wala Sisi hatukuwadhulumu, bali wao ndio walio kuwa madhaalimu. 43:76

Nao watapiga kelele waseme: Ewe Malik! Na atufishe Mola wako Mlezi! Naye aseme: Hakika nyinyi mtakaa humo humo! 43:77
Kwa yakini tulikuleteeni Haki, lakini wengi katika nyinyi mlikuwa mnaichukia Haki. 43:78
Au waliweza kupitisha amri yao? Bali ni Sisi ndio tunao pitisha. 43:79
Au wanadhani kwamba hatusikii siri zao na minong'ono yao? Wapi! Na wajumbe wetu wapo karibu nao, wanayaandika. 43:80
Sema: Ingeli kuwa Rahmani (mungu) ana mwana, basi mimi ningeli kuwa wa kwanza kumuabudu.43:81
Ametakasika Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, Mola Mlezi wa A'rshi, na hayo wanayo msifia. 43:82

Basi waache wapige porojo wakicheza mpaka wakutwe na hiyo siku yao waliyo ahidiwa. 43:83
Na Yeye ndiye Mungu mbinguni, na ndiye Mungu katika ardhi. Naye ndiye Mwenye hikima, Mwenye ujuzi. 43:84
Na ametukuka Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi na viliomo ndani yake. Na uko kwake ujuzi wa Saa ya Kiyama, na kwake Yeye mtarudishwa. 43:85
Wala hao mnao waomba badala yake Yeye hawana uweza wa kumwombea mtu, isipo kuwa anaye shuhudia kwa haki, na wao wanajua.43:86

Na ukiwauliza ni nani aliye waumba? Bila ya shaka watasema: Mwenyezi Mungu! Basi ni wapi wanako geuziwa? 43:87
Na usemi wake (Mtume) ni: Ewe Mola wangu Mlezi! Hakika hawa ni watu wasio amini. 43:88
Basi wasamehe, na uwambie maneno ya salama. Watakuja jua. 43:89
Tena tukafuatisha nyuma yao Mitume wengine, na tukamfuatisha Isa (Yesu) bin Mariamu, na tukampa Injili. Na tukajaalia katika nyoyo za walio mfuata upole na rehema. Na umonaki (utawa wa mapadri) wameuzua wao. Sisi hatukuwaandikia hayo, ila kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu. Lakini hawakuufuata inavyo takiwa kuufuata. Basi wale walio amini katika wao tuliwapa ujira wao. Na wengi wao ni wapotovu. 57:27

Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na muaminini Mtume wake, atakupeni sehemu mbili katika rehema yake, na atakujaalieni muwe na nuru ya kwenda nayo. Na atakusameheni. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. 57:28
Ili watu wa Kitabu wajue kwamba wao hawana uweza wowote juu ya fadhila za Mwenyezi Mungu. Na fadhila zote zimo mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Humpa amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye fadhila kuu. 57:29
Na Isa (Yesu) bin Mariamu alipo sema: Enyi Wana wa Israili! Hakika mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu, ninaye thibitisha yaliyo kuwa kabla yangu katika Taurati, na mwenye kubashiria kuja Mtume atakaye kuja baada yangu; jina lake ni Ahmad! Lakini alipo waletea hoja zilizo wazi, walisema: Huu ni uchawi ulio dhaahiri! 61:6

Na ni nani mwenye kudhulumu zaidi kuliko yule anaye mzulia Mwenyezi Mungu uwongo, naye anaitwa kwenye Uislamu? Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu madhaalimu. 61:7

Wanataka kuizima nuru ya Mwenyezi Mungu kwa vinywa vyao. Na Mwenyezi Mungu atakamilisha nuru yake ijapo kuwa makafiri watachukia. 61:8

Yeye ndiye aliye mtuma Mtume wake kwa uwongofu na Dini ya haki ili ipate kuzishinda dini zote, ijapo kuwa washirikina watachukia. 61:9

Enyi mlio amini! Kuweni wasaidizi wa Mwenyezi Mungu, kama alivyo sema Isa (Yesu) bin Mariamu kuwaambia wanafunzi wake: Nani wasaidizi wangu kwa Mwenyezi Mungu? Wakasema wanafunzi: Sisi ni wasaidizi wa Mwenyezi Mungu! Basi taifa moja la Wana wa Israili liliamini, na taifa jingine lilikufuru. Basi tukawaunga mkono walio amini dhidi ya maadui zao, wakawa wenye kushinda. 61:14

MWISHO