NABII SALEH A.S

BSMILAHI AR-RAHMANI AR-RAHIIMI

NABII SALEH A.S

Thamuud ni kabila mashuhuri la Kiarabu lililokuwa likiishi Hajjar, na Hajjar ipo kati ya Hijaaz na Tabuuk. Na Mtume wetu S.A.W alipita katika magofu yaliyobakia ya mji wa Thamuud wakati ule walipokuwa wakienda kwenye vita vya mwisho vya Tabuuk. Akawaomba Waislamu wasiuingie mji huo ila iwe kwao ni ibra (fundisho) yaliyowafika kina Thamuud; na bora wauepuke. Hivyo Waislamu wakauepuka kuuingia mji huo.

Na kabila la Thamuud lilikuwepo zamani baada ya kabila la Adi ambao wametajwa sana katika Qur-aani Tukufu. Na zile khabari za kina Adi na Thamuud zilikuwa maarufu hapo zamani. Mwenyezi Mungu S.W.T. alimtuma kwa kabila la Thamuud ndugu yao Saleh bin `Abiyd awalinganie ili wamwamini Mungu mmoja; lakini haukuwazidishia wito wake ila kuasi na upotofu juu ya upotofu. Kama alivyosema Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Suratil A`araaf aya ya 73, "

وَإِلَى ثَمُودَ أَخَاهُمْ صَالِحًا قَالَ يَاقَوْمِ اعْبُدُوا اللَّهَ مَا لَكُمْ مِنْ إِلَهٍ غَيْرُهُ…

Maana yake, "Na kwa Thamud tulimpeleka ndugu yao, Saleh. Akasema: "Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna Mungu ila Yeye.." Siku moja walipokuwa wamekusanyika katika mikutano yao akawaijia Nabii Saleh akirudishia kuwaambiya wito wake. Kama alivyosema Mwenyezi Mungu S.W.T. kwa kauli ya Nabii Saleh A.S. katika Surat Sh-shua`raa tokeya aya ya 142 mpaka 144, "

إِذْ قَالَ لَهُمْ أَخُوهُمْ صَالِحٌ أَلا تَتَّقُونَ * إِنِّي لَكُمْ رَسُولٌ أَمِينٌ * فَاتَّقُوا اللَّهَ وَأَطِيعُونِ

Maana yake, "(Wakumbushe) alipowaambia ndugu yao, (Nabii) Saleh: "Jee! Hamumchi Mungu? Bila shaka mimi kwenu ni Mtume mwaminifu. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nitiini." Wale watu wake wakaulizana wakasema: Jee! Mungu gani anayemmaanisha?" Kwani wao walikuwa na miungu mingi. Nabii Saleh A.S. akawajibu, kama ilivyokuja katika Surat Huud aya 61, "

…اعْبُدُوا اللَّهَ مَا لَكُمْ مِنْ إِلَهٍ غَيْرُهُ هُوَ أَنشَأَكُمْ مِنْ الأَرْضِ وَاسْتَعْمَرَكُمْ فِيهَا فَاسْتَغْفِرُوهُ ثُمَّ تُوبُوا إِلَيْهِ إِنَّ رَبِّي قَرِيبٌ مُجِيبٌ

Maana yake, "…Muabuduni Mwenyezi Mungu; nyinyi hamna Mungu ila Yeye. Yeye Ndiye aliyekuumbeni katika ardhi, na akakuwekeni humo. Basi muombeni msamaha (kwa makosa yenu yaliyopita), kisha mtubu Kwake. Hakika Mola wangu yupo karibu (na waja Wake), anapokea (maombi yao)." Wale watu wake wakamuudhi sana Nabii Saleh wakamtaka awaachilie mbali waendelee kuabudu yale masanamu yao waliorithi kutoka kwa baba zao, katika nyumba zao ambazo wamezichonga majabalini; wametulia kimya hawasikii hata sauti ya upepo wakati unapovuma wala mvua wakati inaponyesha.

Wanafanya mambo mabaya wala hakuna wakuwakataza. Wakamlaumu sana Nabii Saleh mara ya kwanza juu ya lile jambo alilokuja nalo wakasema: Sisi tulikuwa tukikutumainia utashika pahala pakubwa kama ni ndugu zako; sasa tena ulipopata elimu na fahamu umeutoa wapi huo wito wa kiajabu wa kutukataza kuabudu waliowaabudu baba zetu? Nasi pia tunashaka na wito wako." Kama ilivyokuja katika Surat Huud aya 62, "

قَالُوا يَاصَالِحُ قَدْ كُنتَ فِينَا مَرْجُوًّا قَبْلَ هَذَا أَتَنْهَانَا أَنْ نَعْبُدَ مَا يَعْبُدُ آبَاؤُنَا وَإِنَّنَا لَفِي شَكٍّ مِمَّا تَدْعُونَا إِلَيْهِ مُرِيبٍ

Maana yake, "Wakasema: "Ewe Saleh! Bila shaka kabla ya haya ulikuwa unatarajiwa kheri kwetu. (Sasa umeharibika). Jee, unatukataza kuabudu walioawaabudu babu zetu? Na hakika sisi tuna shaka na wasiwasi (katika nyoyo zetu) kwa haya unayotuitia."

Lakini yote hayo hayakumfanya Nabii Saleh kusimamisha wito wake, bali aliendelea nao ijapokuwa watu wake walimuomba awaachilie mbali waendelee na ile ibada yao ya kuabudu masanamu yao. Kama alivyosema Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Surat Huud aya ya 63, "

قَالَ يَاقَوْمِ أَرَأَيْتُمْ إِنْ كُنتُ عَلَى بَيِّنَةٍ مِنْ رَبِّي وَآتَانِي مِنْهُ رَحْمَةً فَمَنْ يَنصُرُنِي مِنْ اللَّهِ إِنْ عَصَيْتُهُ فَمَا تَزِيدُونَنِي غَيْرَ تَخْسِيرٍ

Maana yake, "Akasema: "Enyi watu wangu! Mnaonaje, ikiwa ninazo dalili zilizo wazi zitokazo kwa Mola wangu (za kunionesha ukweli wa haya), Naye amenipa Rehema kutoka Kwake, basi ni nani atakayeninusuru kwa Mwenyezi Mungu nikimuasi? Basi hamtanizidishia (kwa hayo mnayonitakia) ila khasara tu."

Nabii Saleh A.S. akasema kuwaambiya: Mnaniomba mimi nimuasi Mwenyezi Mungu! Jee, hamjui kwamba nikifanya hivyo nitaadhibiwa? Kwa hali hiyo sitasimamisha wito wangu kwenu, wala msifikiri kwamba mimi ninafanya hivyo ninatamaa ya mali yenu; sivyo hivyo. Huu wito wangu kwenu ni wahyi ambao ni amri iliyotoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kama alivyosema Mwenyezi Mungu S.W.T. kwa kauli ya Nabii Saleh katika Surat Sh-shua`araa aya ya 145, "

وَمَا أَسْأَلُكُمْ عَلَيْهِ مِنْ أَجْرٍ إِنْ أَجْرِي إِلاَّ عَلَى رَبِّ الْعَالَمِينَ

Maana yake, "Wala sikutakini ujira juu yake. Ujira wangu hauko ila kwa (Mwenyezi Mungu) Mola wa walimwengu wote." Wale watu wake wakamjibu: Ewe Saleh! Tuache unayotuitia kwani sisi tumestarehe kwa yale tuliyoyarithi kutoka kwa baba zetu; kutokana na ibada na nyumba zisizotikiswa na upepo na tunamiliki mabustani na mifereji. Na hayo ni mabustani yenye chemchemi ya kupendeza kabisa kwa watazamao. Tunafurahia tunayopata katika mabustani hayo; na sisi hatuna haja na wito wako. Nabii Saleh A.S. akawajibu akasema: Hiyo ni dhana mbaya kwani mkimuasi Mola wenu atawaangamiza nyinyi pamoja na starehe zenu za duniani. Kama alivyosema Mwenyezi Mungu S.W.T. kwa kauli ya Nabii Saleh katika Surat Sh-shua`araa aya ya 146 hadi ya 150, "

أَتُتْرَكُونَ فِي مَا هَاهُنَا آمِنِينَ * فِي جَنَّاتٍ وَعُيُونٍ * وَزُرُوعٍ وَنَخْلٍ طَلْعُهَا هَضِيمٌ * وَتَنْحِتُونَ مِنْ الْجِبَالِ بُيُوتًا فَارِهِينَ * فَاتَّقُوا اللَّهَ وَأَطِيعُونِ

Maana yake, "Jee, (mnafikiri kuwa) mtaachwa salama katika haya yaliyopo hapa (kwenu). Katika mabustani, na chemchemi? Na mimea na mitende yenye makole yaliyowiva (yanakaribia kukatika kwa kuzaa kwake sana). Na mnachonga milimani majumba mkistarehe tu. Basi mcheni Mwenyezi Mungu na nitiini mimi."

Lakini watu wake walikuwa ni watu wajeuri sana; wakamjibu Mtume wao wakasema: Vipi tutakufuata na wewe ni mtu mmoja tu unayetuita katika dini yako na sisi ni wengi? Na vipi Mwenyezi Mungu akakuchagua wewe tu? Wakajadiliana lile jambo lao wenyewe kwa wenyewe kisha wakasema: Ameteremshiwa yeye tu dini hii mpya bila sisi kuambiwa; ama huyu ni mtu muongo kabisa anayejiona. Pia wakamsingizia kuwa yeye ni mtu aliyerogwa. Wakaendelea kumjibu wakasema: Wewe si Malaika kutoka mbinguni hata ukawa Mtume; wala huna tofauti yoyote ile na sisi. Na ikiwa unataka tukuamini basi tuletee muujiza wa kutuonesha kwamba kweli wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Kama alivyosema Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Suratil Qamar aya ya 25, "

أَؤُلْقِيَ الذِّكْرُ عَلَيْهِ مِنْ بَيْنِنَا بَلْ هُوَ كَذَّابٌ أَشِرٌ

Maana yake, "Ni yeye tu aliyeteremshiwa huo ukumbusho (kuwa Mwenyezi Mungu ni mmoja) kati yetu sisi? Bali huyu ni muongo, (na) mwenye kiburi!" Pia kasema Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Surat Sh-shua`araa aya ya 153 na ya 154, "

قَالُوا إِنَّمَا أَنْتَ مِنْ الْمُسَحَّرِينَ * مَا أَنْتَ إِلا بَشَرٌ مِثْلُنَا فَأْتِ بِآيَةٍ إِنْ كُنْتَ مِنْ الصَّادِقِينَ

Maana yake, "Wakasema Hakika wewe ni miongoni mwa waliorogwa (wakakosa akili). Wewe si chochote ila ni mtu kama sisi. Basi lete muujiza ikiwa ni miongoni mwa wasemao kweli."

Nabii Saleh A.S. akawauliza: Muujiza gani mnaoutaka mletewe? Wakamjibu: Utoke pamoja nasi siku ya idi yetu umuombe Mungu wako nasi tuwaombe miungu yetu, ikiwa Mungu wako atakujibu tutakufuata na ikiwa miungu yetu itatujibu utufuate. Nabii Saleh akajibu: Nimekubali. Ilipofika ile siku ya idi yao wakatoka nje ya mji wao wakayaomba masanamu yao kuwa ombi lolote lile atakaloliomba Nabii Saleh asijibiwe, kisha akasema mkubwa wao: Ewe Saleh! Tutolee kutoka katika hili jiwe kubwa lililojitenga na jabali ngamia jike mwenye mimba pevu; aliyekaribia kuzaa. Basi ukifanya hivyo tutakuamini. Nabii Saleh akachukua ahadi kutoka kwao kuwa akifanya wanavyotaka wataamini. Wakakubali. Kisha akasali rakaa mbili akamuomba Mola wake awaletee muujiza walioutaka kaumu yake ili wapate kumuamini.

Haukuchukua muda mrefu mara lile jiwe kubwa likaanza kutikisika halafu Mwenyezi Mungu S.W.T. akawatolea ngamia jike ambaye alikuwa na umbo kubwa sana. Wakaona jambo lile ni kubwa sana na dalili ya wazi kabisa na uwezo mkubwa wa ajabu; basi wengi katika kaumu yake walimwamini Nabii Saleh. Kama alivyosema Mwenyezi Mungu S.W.T. kwa kauli ya Nabii Saleh katika Surat Huud aya ya 63, "

وَيَا قَوْمِ هَذِهِ نَاقَةُ اللَّهِ لَكُمْ آيَةً فَذَرُوهَا تَأْكُلْ فِي أَرْضِ اللَّهِ وَلا تَمَسُّوهَا بِسُوءٍ فَيَأْخُذَكُمْ عَذَابٌ قَرِيبٌ

Maana yake, "Enyi watu wangu! Huyu ngamia wa Mwenyezi Mungu ni muujiza kwenu (mlioutaka mletewe ili kuonesha ukweli wa Utume wangu). Basi mwacheni ale katika ardhi ya Mwenyezi Mungu; wala msimguse kwa ubaya, isije ikakuangamizeni adhabu iliyo karibu."

Lakini baadhi yao pia wakaendelea kukufuru na kumkanusha Nabii Saleh wakati ngamia alipozaa mbele yao kama walivyoomba wenyewe. Baada ya kutokea mambo yote hayo waliyoyataka, Nabii Saleh akawatangazia akasema: Huyu hapa ngamia jike ambaye ndiye muujiza mlioutaka, hivyo lazima mumgawie sehemu yake ya maji ya kisima; iwe siku yenu moja ya kuteka maji kisimani na siku moja ya ngamia ya kunywa maji yote ya kisima, na badala yake mumkamue ngamia ili awape maziwa ya kuwatosheleza siku nzima. Wale walioamini waliiheshimu ile amri ya Mtume wao na wakajua kwamba kuweko kwa yule ngamia ni dalili wazi ya imani yao.

Lakini wale waliokufuru wakachukulia kwamba kuweko kwa yule ngamia ni dalili wazi ya uwongo wao na kufuru yao na ukaidi wao. Na wakaona kwamba jinsi wakati unavyopita ndivyo watu wengi watakavyoamini. Na jambo hili litawafanya wapoteze ukubwa wao na vyeo vyao kwa watu. Na sababu nyingine wakati ngamia akienda machungani wanyama wao walikuwa wakimkimbia kwa kumuogopa kwa jinsi umbile lake lilivyokuwa kubwa. Na jambo hili liliwadhuru, na hayo yote hayakuwa ila ni majaribio na mtihani kutoka kwa Mola wao kwa ajili ya kupimwa imani yao. Kwa hivyo, wakafanya njama ya kutaka kumuuwa yule ngamia jike.

Inasemekana mwanamke mzee aliyekuwa kafiri aliyejulikana kwa jina la "Ummu Ghanam," alikuwa ni adui mkubwa kabisa wa Nabii Saleh. Na huyu mwanamke mzee alikuwa na wasichana wazuri sana na mwenye mali.

Hivyo akamshurutishia Qaddaar bin Saalif ikiwa kama atamuuwa yule ngamia basi amchague msichana yeyote yule mzuri katika mabinti zake anayemtaka kisha amchukue. Na mwanamke mwingine aliyeitwa Saduwf aliyekuwa tajiri na mzuri akajionesha nafsi yake kwa mwanaume aliyeitwa Masda`a bin Mahraj ikiwa anamtaka basi sharti kwanza amuuwe yule ngamia; Masda`a akakubali.

Akaondoka Qaddaar na Masda`a ikiwa pamoja na watu wengine saba wakawa jumla watu tisa. Kama alivyowaita Mwenyezi Mungu S.W.T. kuwa watu tisa hao walikuwa wakifisidi katika mji huo. Kwa hivyo hawa watu tisa wakakusanyika pamoja wakaondoka kwenda zao kutaka kumuua yule ngamia wa Mwenyezi Mungu. Kama alivyosema Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Suratin Naml aya ya 48, "

وَكَانَ فِي الْمَدِينَةِ تِسْعَةُ رَهْطٍ يُفْسِدُونَ فِي الأرْضِ وَلا يُصْلِحُونَ

Maana yake, "Na walikuwamo mjini watu tisa wakifanya ufisadi katika nchi (hiyo) wala hawafanyi (jambo lolote) la maslaha (ila kuharibu tu).

MWISHO