KISA CHA MFALME TAALUWT

BSMILAHI AR-RAHMANI AR-RAHIIMI

KISA CHA MFALME TAALUWT

Kisa cha mfalme Taawlut kimetolewa ndani ya Qurani Tukufu. Kisa hiki kilitokea baada ya kifo cha Nabii Musa A.S., wakubwa wa Ki-Bani Israil waliomba waletewe mfalme, hivyo kwa rehma za Mwenyezi Mungu S.W.T. alimletea wahyi Mtume Wake wa zama zile aliyeitwa Shamuweli A.S. kwamba awaambie watu wake kuwa Mola wao amewachagulia Taaluwt awe ndiye mfalme wao. Na huyu Taaluwt alikuwa ni mmoja katika askari wao na hakutokana na ukoo wa kifalme.

Lakini hata hivyo Mabani Israil hawakuridhika na shauri hilo lililotoka kwa Mola wao bali walimlalamikia Mtume wao wakasema: "Vipi atatutawala na hali yeye hakutokana na sisi, na sisi tuna haki zaidi yake, na juu ya hivyo yeye ni mtu fakiri?" Lakini Mtume wao aliwajibu akasema: "Mwenyezi Mungu S.W.T. Ndiye Aliyemchagua Taaluwt si mimi na akamzidishia elimu na nguvu."

Na kufafanua zaidi yaani mfalme huhitajia kuwa na elimu ya kivita na nguvu ya kimwili ili kupambana na maadui, na kuwa na ustahamilivu wa hali ya juu. Mtume wao akaendelea kuwajibu: "Mwenyezi Mungu humpa ufalme yule mtu amtakae na anayemuona anafaa si hovyo tu." Na Mtume wao akawaambia kwamba: "Alama ya kumjua Taaluwt amechaguliwa kuwa mfalme wenu ni Mwenyezi Mungu kukurejesheeni sanduku ambalo lilichukuliwa zamani kutoka kwenu, na ndani yake mna kitulizo cha nyoyo."

Ibn Abbaas R.A.A. kasema: "Walikuja Malaika wamebeba sanduku baina ya mbingu na ardhi mpaka wakaliweka kwa mfalme Taaluwt na hali watu wote waliohudhuria pale wanashuhudia kwa macho yao." Ssuddiyy kasema: "Sanduku lilipoletwa katika nyumba ya Taaluwt wakamwamini Mtume wao na wakamtii Taaluwt." Hapo mfalme Taaluwt akaliunda jeshi lake kubwa ambalo idadi yao ilikuwa askari 80,000.

Baada ya kwisha kuliunda hilo jeshi wakaanza safari yao tokea Baitul Muqaddas, na wakati huo hali ya hewa ilikuwa ni joto kali sana. Kwa hiyo kikawashika kiu kikali wakaomba maji. Mfalme wao akawatangazia kuwa: "Mola wenu atakufanyieni mtihani wa kutii na kuasi kwa kunywa maji katika mto Shariy`a baina ya Falastina na Jordan ambao unajulikana hivi sasa kwa jina la "Mto Jordan." Atakayekunywa maji yake basi hatakuwa pamoja nami.

Na asiyekunywa atakuwa pamoja nami. Isipokuwa atakayekunywa kwa kujaza kitanga cha mkono wake tu hapana kitu." Ssuddiyy kasema: "Katika jeshi lake la askari 80,000 walikunywa askari 76,000 na wale ambao walibakia hawakunywa ni askari 4,000 tu." Mara tu walipouvuka ule mto yeye pamoja na wale walioamini, basi wale wenye imani dhaifu nyoyoni mwao walipomuoana Jaaluwt na askari wake wakakata tamaa wakasema: "Leo hii hatumwezi Jaaluwt na askari wake." Kwani wakati huo Jaaluwt alikuwa na askari 10,000.

Lakini wale wenye elimu wakawatia moyo kwamba miadi ya Mola wao ni haki, na nusura haiji ila kutoka kwa Mwenyezi Mungu tu na si kutokana na idadi ya askari wala silaha. Ndiyo maana wakasema: "Makundi mangapi madogo ya Waislamu yameshinda makundi makubwa ya kikafiri kwa idhini ya Mola Mtukufu, na Yeye yupo pamoja na wale wenye kusubiri." Kisa hiki cha mfalme Taaluwt kimetolewa katika Suratil Baqarah tokea aya ya 246 mpaka 251, "

أَلَمْ تَرَ إِلَى الْمَلإِ مِنْ بَنِي إِسْرَائِيلَ مِنْ بَعْدِ مُوسَى إِذْ قَالُوا لِنَبِيٍّ لَهُمْ ابْعَثْ لَنَا مَلِكًا نُقَاتِلْ فِي سَبِيلِ اللَّهِ قَالَ هَلْ عَسَيْتُمْ إِنْ كُتِبَ عَلَيْكُمْ الْقِتَالُ أَلاَّ تُقَاتِلُوا قَالُوا وَمَا لَنَا أَلاَّ نُقَاتِلَ فِي سَبِيلِ اللَّهِ وَقَدْ أُخْرِجْنَا مِنْ دِيَارِنَا وَأَبْنَائِنَا فَلَمَّا كُتِبَ عَلَيْهِمْ الْقِتَالُ تَوَلَّوْا إِلاَّ قَلِيلاً مِنْهُمْ وَاللَّهُ عَلِيمٌ بِالظَّالِمِينَ * قَالُوا أَنَّى يَكُونُ لَهُ الْمُلْكُ عَلَيْنَا وَنَحْنُ أَحَقُّ بِالْمُلْكِ مِنْهُ وَلَمْ يُؤْتَ سَعَةً مِنْ الْمَالِ قَالَ إِنَّ اللَّهَ اصْطَفَاهُ عَلَيْكُمْ وَزَادَهُ بَسْطَةً فِي الْعِلْمِ وَالْجِسْمِ وَاللَّهُ يُؤْتِي مُلْكَهُ مَنْ يَشَاءُ وَاللَّهُ وَاسِعٌ عَلِيمٌ * وَقَالَ لَهُمْ نَبِيُّهُمْ إِنَّ آيَةَ مُلْكِهِ أَنْ يَأْتِيَكُمْ التَّابُوتُ فِيهِ سَكِينَةٌ مِنْ رَبِّكُمْ وَبَقِيَّةٌ مِمَّا تَرَكَ آلُ مُوسَى وَآلُ هَارُونَ تَحْمِلُهُ الْمَلاَئِكَةُ إِنَّ فِي ذَلِكَ لآيَةً لَكُمْ إِنْ كُنتُمْ مُؤْمِنِينَ * فَلَمَّا فَصَلَ طَالُوتُ بِالْجُنُودِ قَالَ إِنَّ اللَّهَ مُبْتَلِيكُمْ بِنَهَرٍ فَمَنْ شَرِبَ مِنْهُ فَلَيْسَ مِنِّي وَمَنْ لَمْ يَطْعَمْهُ فَإِنَّهُ مِنِّي إِلاَّ مَنْ اغْتَرَفَ غُرْفَةً بِيَدِهِ فَشَرِبُوا مِنْهُ إِلاَّ قَلِيلاً مِنْهُمْ فَلَمَّا جَاوَزَهُ هُوَ وَالَّذِينَ آمَنُوا مَعَهُ قَالُوا لاَ طَاقَةَ لَنَا الْيَوْمَ بِجَالُوتَ وَجُنُودِهِ قَالَ الَّذِينَ يَظُنُّونَ أَنَّهُمْ مُلَاقُو اللَّهِ كَمْ مِنْ فِئَةٍ قَلِيلَةٍ غَلَبَتْ فِئَةً كَثِيرَةً بِإِذْنِ اللَّهِ وَاللَّهُ مَعَ الصَّابِرِينَ * وَلَمَّا بَرَزُوا لِجَالُوتَ وَجُنُودِهِ قَالُوا رَبَّنَا أَفْرِغْ عَلَيْنَا صَبْرًا وَثَبِّتْ أَقْدَامَنَا وَانْصُرْنَا عَلَى الْقَوْمِ الْكَافِرِينَ * فَهَزَمُوهُمْ بِإِذْنِ اللَّهِ وَقَتَلَ دَاوُودُ جَالُوتَ وَآتَاهُ اللَّهُ الْمُلْكَ وَالْحِكْمَةَ وَعَلَّمَهُ مِمَّا يَشَاءُ وَلَوْلاَ دَفْعُ اللَّهِ النَّاسَ بَعْضَهُمْ بِبَعْضٍ لَفَسَدَتْ الأَرْضُ وَلَكِنَّ اللَّهَ ذُو فَضْلٍ عَلَى الْعَالَمِينَ

Maana yake, "Hukuwaona watukufu katika Wana wa Israili baada ya Musa, walipomwambia Nabii wao: "Tuwekee mfalme ili tupigane katika Njia ya Mwenyezi Mungu?" Akasema: "Jee, haielekei ikiwa mtaandikiwa vita kuwa msipigane?" Wakasema: "Itakuwaje tusipigane katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na hali tumetolewa majumbani kwetu na watoto wetu?" Lakini walipoandikiwa kupigana waligeuka, isipokuwa wachache miongoni mwao.

Na Mwenyezi Mungu anawajua madhalimu. Na huyo Mtume wao akawaambia: "Mwenyezi Mungu amekuchagulieni Taaluwt kuwa mfalme." Wakasema: "Vipi atakuwa na ufalme juu yetu, na hali sisi tumestahiki zaidi kupata ufalme kuliko yeye, naye hakupewa wasaa wa mali?" Akasema: "Mwenyezi Mungu amemchagua juu yenu na amemzidishia wasaa wa elimu na kiwiliwili. Na Mwenyezi Mungu humpa ufalme Wake amtakaye.

Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa (na) Mwenye kujua." Na Nabii wao akawaambia: "Alama ya ufalme wake ni kukujieni lile sanduku ambalo mna ndani yake kituliza nyoyo zenu, kitokacho kwa Mola wenu, na mna masazo ya yale waliyoyaacha watu wa Musa na watu wa Harun; wakilichukua Malaika (kukuleteeni yaani limo katika hafadhi yao japo limechukuliwa juu ya gari). Bila shaka katika hayo mna dalili kwenu (ya ufalme wake juu yenu) ikiwa nyinyi mnaamini. Basi Taaluwt alipoondoka na majeshi, alisema: "Mwenyezi Mungu atakufanyieni mtihani kwa mto (mtakaokutana nao njiani huko mnakokwenda).

Basi atakayekunywa humo si pamoja nami, na asiyekunywa atakuwa pamoja nami; ila atakayeteka kwa kiasi cha kujaza kitanga cha mkono wake (akanywa hayo tu, huyo hana makosa)." Lakini walikunywa humo isipokuwa wachache tu miongoni mwao. Basi alipovuka yeye na (wakavuka) wale walioamini pamoja naye, walisema: "Leo hatumwezi Jaaluwt na majeshi yake."

Wakasema wale wenye yakini ya kukutana na Mola wao: "Makundi mangapi madogo yameshinda makundi makubwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu." Na Mwenyezi Mungu yu pamoja na wafanyao subira. Na walipotoka kupambana na Jaaluwt (mfalme wa hao maadui) na majeshi yake, walema hao wa Taaluwt: "Mola wetu! Tumiminie subira, na uithibitishe miguu yetu, na utusaidie juu ya watu hawa makafiri."

Basi (hao watu wa Taaluwt) wakawaendesha mbio (hao maadui zao) kwa idhini ya Mwenyezi Mungu; na Daudi akamwua Jaaluwt, na Mwenyezi Mungu akampa (huyu Daudi) ufalme na hekima. Na akamfundisha aliyoyapenda. Na kama Mwenyezi Mungu asingalizuia watu, baadhi yao kwa wengine, kwa yakini ardhi ingaliharibika. Lakini Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila (kubwa) juu ya walimwengu wote.

MWISHO