SUALI KUHUSU FUNGA

BSMILAHI AR-RAHMANI AR-RAHIIMI

SUALI KUHUSU FUNGA

SWALI: Kwa mujibu wa aya ya 184 ya Suratul Baqara, mgonjwa amekatazwa kufunga. Maana ya ugonjwa au maumivu ni nini? Je, maumivu ya mguu, mkono na tumbo ndiyo yanayokusudiwa hapa au ni maumivu makali ambayo yanamdhoofisha mtu kama vile shinikizo la damu, kijisukari na vidonda vya tumbo? Shariffa Ismail Mnape, Tehran Iran. JAWABU: Funga imelazimishwa na kuwajibishwa kwa mtu aliye na afya na akili timamu pamoja na kuwa anapaswa kuwa amebaleghe. Pamoja na hayo, dini tikufu ya Kiislamu imewaondolea baadhi ya watu jukumu hilo muhimu kutokana na sababu kadhaa zikiwemo zilizotajwa na msikilizaji wetu, Bi Mnape, yaani ugonjwa au maumivu makubwa. Kwa hakika wagonjwa ambao wana matatizo ya kimwili pia wanajumuishwa katika kundi hilo. Kwa mfano mtu ambaye anahofia kwamba akifunga, maumivu yake yataongezeka au kukumbwa na magonjwa mengine, anaruhusiwa kutofunga. Ni wazi kuwa funga inaweza kuharamishwa kwa mtu kama huyo katika baadhi ya hali au wakati.

Katika upande wa pili magonjwa ambayo hayana uhusiano wowote na funga na wala hayaongezeki kutokana na funga hiyo hayapaswi kumfanya mtu asitekeleze ibada yake ya funga. Kwa hivyo mtu anayekabiliwa na maumivu kama hayo analazimika kufunga wakati wake unapowadia. Kuhusu ni maumivu yapi yanayomdhuru mtu wakati wa funga na ni yapi yasiyomdhuru, ni suala linalopaswa kubainishwa kwa mashauriano na daktari mtaalamu. Hata hivyo uamuzi wa mwisho kuhusiana na suala hilo ni wa mgonjwa mwenyewe. Umuhimu wa suala hili unatokana na ukweli kwamba kuna baadhi ya madaktari wasiozingatia wala kuyapa umuhimu masuala ya kidini na kwa hivyo ni rahisi kwao kupuuza funga na kumwambia mgonjwa asiyeathiriwa sana na funga kutofunga, wakati ni muhimu sana kwake kutekeleza jukumu na ibada hiyo muhimu ya kidini. Kwa hivyo, uamuzi wa mwisho kuhusiana na suala hilo unamhusu mgonjwa mwenyewe, ambaye hata akiwa na wasiwasi na hofi tu kwamba, maumivu makali aliyonayo yataongezeka pindi anapofunga, anaruhusiwa kutofunga katika hali hiyo na kusubiri hadi maumivu hayo yatakapopungua.

Maumivu kama hayo, ni kama yale yanayohusiana na magonjwa kama vile ya kijisukari, shinikizo la damu na maumivu makali ya figo. SWALI: Mtu aliyeshauriwa na daktari kumeza dawa katika vipindi vitatu tofauti vya siku, anapaswa kufunga kwa njia gani? Shariffa Ismail Mnape, Tehran, JK Iran JAWABU: Jibu la swali hili kwa hakika linahusiana na mtazamo wa daktari mwenyewe. Kama daktari huyo anaweza kumruhusu mgonjwa wake kutumia dawa hizo nyakati za usiku au kuakhirisha wakati wa kuzitumia, mgonjwa huyo anapaswa kufuata maelekezo ya daktari na kufunga kama kawaida. Lakini kama daktari atahisi kuwa mgonjwa hawezi kutumia dawa hizo nyakati za usiku kutokana na kuwa jambo hilo linaweza kuathiri mwenendo wa kupona kwake, mgonjwa huwa hana budi ila kutumia dawa hizo nyakati wa mchana na hivyo kutofunga. Funga hiyo inapaswa kuakhirishwa hadi wakati mwingine anapopata nafuu. Anapaswa kulipa siku ambazo hakufanikiwa kufunga ndani ya mwezi wa Ramadhani nje ya mwezi huo mtukufu.

SWALI: Msafiri halazimiki kufunga. Sasa watu kama vile madereva wanaosafiri kila siku kati ya miji mbalimbali wanapaswa kufanya nini katika hali kama hii? -Shariffa Ismail Mnape, Tehran, JK Iran. JAWABU: Wanazuoni wengi wanaamini kwamba watu ambao shughuli yao ni kusafiri kama vile madereva, wanapaswa kufunga na hakuna tatizo lolote kuhusiana na suala hilo.

SWALI: Huko kwetu Tanzania kuna sala iitwayo Taraweheh ambayo ni mashuhuri sana na husaliwa baada ya sala la Ishaa katika mwezi huu mtukufu. Tokea nije nchini Iran sijawahi kushuhudia au hata kusikia watu wakiizungumzia sala hii hapa nchini. Jambo hilo limenipelekea nijiulize swali hili kuwa, je, ni kwa nini sala hii haizingatiwi na jamii ya Wairani? Je, ibada hii si ya Waislamu wote? Shariffa Ismail Mnape, Tehran JK Iran. JAWABU: Kama unavyojua Bi Mnape, kuna ibada nyingi sana za sunna ambazo zinapaswa kutekelzwa na Waislamu na hasa katika mwezi mtukufu wa Ramadhani. Sala na ibada kama hizo ambazo si za wajibu zina baraka nyingi na humpelekea mja kusamehewa na kupata maghfira kutoka kwa Muumba wake. Sala zote za sunna zinapaswa kuwa zimethibitishwa na Bwana Mtume (SAW). Kutokana na kuwa sala hii ya Taraweheh haijaashiriwa popote katika vitabu vya Kishia kuwa ilikuwa ni mojawapo ya sala za sunna za Mtume, au kuwa alishauri sala hii isaliwe na Waislamu kama sala ya nafila au mustahab, sala hii haifahamiki sana kati ya jamii ya Wairani.

SWALI: Ni kwa nini Beitul Muqaddas imegawanywa katika sehemu mbili za Mashariki na Magharibi? -Philip K. Chepkwony, Eldoret, Kenya.

JAWABU: Kabla ya kujibu swali hili ni vyema tuashirie hapa kwamba Beitul Muqaddas nzima ni mojawapo ya sehemu za ardhi ya Wapalestina ilitotekwa na kukaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel mwaka 1948 kufuatia kutangazwa rasmi kuundwa kwa utawala huo mwezi Mei 1948. Kufuatia kutekwa kwa ardhi za Wapalestina na utawala huo wa kigaidi majeshi ya nchi za Kiarabu yalichukua uamuzi wa kupambana kijeshi na utawala huo na kufanikiwa kuzikomboa baadhi ya ardhi hizo mwanzoni mwa vita hivyo. Miongoni mwa ardhi hizo zilizokombolewa ni pamoja na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, Ukanda wa Gaza na Beitul Muqaddas ya Mashariki. Kwa hivyo utawala wa Kizayuni wa Israel uliendelea kuikalia Beitul Muqadds ya Magharibi na ya Mashariki kupewa Jordan ambayo ilipewa jukumu la kuwarejeshea Wapelstina sehemu hiyo ya Beitul Muqaddas mara tu baada ya kujulikana mustakbali wa Wapalestina. Tokea mwaka 1948 hadi 1967, Israel ilifanya mabadiliko makubwa katika muundo wa kijografia, kijamii na kisiasa wa Beitul Muqaddas Magharibi. Iliharibu nembo na alama zote za Wapalestina katika eneo hilo ikiwa ni pamoja na kuharibu namna ya ujenzi wa nyumba, mabarabara na majina yake, kuwafukuza Wapalestina katika eneo hilo na kuzihamishia huko wizara zote za utawala huo ghasibu yakiwemo makao makuu ya Waziri Mkuu.

Baada ya muda mfupi, muundo wa eneo hilo lote la Magharibi uligeuka na kuwa wa Kizayuni na Kiyahudi. Hata bbada ya hatua hiyo ilikuwa wazi kwamba utawala ghasibu wa Israel ilikuwa na nia ya kuiteka sehemu ya Waarabu ya Beitul Muqaddas. Kwa hivyo mwaka 1967, kufuatia vita mashuhuri vya siku sita kati ya Waarabu na utawala huo wa Kizayuni, jeshi la utawala huo lilivamia na kuiteka sehemu hiyo ya Beitul Muqaddas Mashariki na kuiunganisha na ardhi nyinginezo zilizotekwa za Wapalestina na kutajwa kuwa ni Israel. Kama mnavyojua nyote wapenzi wasikilizaji, sehemu ya Beitul Muqaddas Mashariki ni eneo maalum na takatifu kwa wafuasi wa dini nyingi zote za Mwenyezi Mungu na hasa Waislamu. Katika eneo hilo kuna msikiti wa al-Aqsa ambacho ni Kibla cha kwanza cha Waislamu. Katika eneo hilohilo kuna ukuta wa Nudba au Buraq ambapo Mtume Mtukufu (SAW) alipaa kwenda mbinguni katika usiku wa Miiraaj. Katika eneo hilo pia kuna makanisa ambapo Nabii Isah (AS) alikuwa akipewa mafunzo na Nabii Zakaria na pia kuteremshiwa chakula kutoka mbinguni. Pamoja na kupita miaka 36 ya kutekwa sehemu hiyo ya Beitul Muqaddas Mashariki, lakini hadi sasa utawala ghasibu wa Israel haujafanikiwa kumiliki wala kulidhibiti eneo hilo. Huenda suala hilo linatokana na idadi kubwa ya Wapalestina wanaoishi katika eneo hilo na pia maeneo mengi matakatifu yanayopatikana katika eneo hilo. Kwa hivyo katika kipindi chote hiki cha miaka 36 utawala ghasibu wa Israel umekuwa ukifanya jitihada za kubadilisha taratibu sura halisi ya eneo hilo na kuifanya ionekane kuwa ni ya kizayuni. Kujengwa kwa vitongoji 40 vya Mayahudi katika eneo hilo la Beitul Muqaddas Mashariki na kuhamishia humo zaidi ya Wazayuni laki 1.6 kutoka pembe zote za dunia ni miongoni mwa jitihada hizo.

Pamoja na kutekelezwa njama hizo zote za Wazyuni, kukiwemo kuuchoma moto msikiti wa al-Aqsa, jambo la kuvutia hapa ni kuwa, bado eneo hilo la Mashariki lina utambulisho wake wote wa Kiarabu na Kitaifa. Kuibuka kwa mapambano ya Intifadha tarehe 26 Septemba 2000 ni mfano wa wazi kuhusiana na ukweli huu kwamba pamoja na njama zote ambazo zimekuwa zikifanywa na Wazyuni kwa lengo la kubadilisha sura ya Beitul Muqaddas Mashariki, lakini bado Quds Tukufu itaendelea kuwa eneo na mji mkuu wa taifa la Palestina. SWALI: Kuna tofauti baina ya ukoloni, ubeberu na udhibiti?- Ustadh Muhsin Chalinze, Dar es Salaam, Tanzania JAWABU:Pamoja na kuwa maneno haya yaliyotajwa na msikilizaji wetu huyu hayana tofauti kubwa, lakini hata hivyo hutumika kubainisha vipindi au mbinu zinazotumiwa na wakoloni katika kufikia malengo yao katika nchi mbalimbali za dunia Neno ambalo ni mashuhuri zaidi katika ya maneno hayo matatu ni ukoloni ambalo ni kongwe zaidi kuliko maneno mengine mawili yaliyotajwa. Kimsingi maana ya neno ukoloni au Colonization kwa Kimombo ni kuhajiri kundi kutoka sehemu au nchi moja hadi nyingine kwa lengo la kutafuta makao huko. Lakini inavyoeleweka ni kuwa neno hilo limetumika katika historia ya ukoloni kumaanisha udhibiti na wa kisiasa na kijeshi wa nchi zenye nguvu dhidi ya nchi nyinginezo ambazo dhaifu. Aina hiyo ya udhibiti ilienea sana katika kipindi cha katikati ya karne ya 17 hadi mwishoni mwa karne ya 18.

Lakini neno ukoloni lilipata maana mpya katika karne ya 19 na 20 ambao ukoloni huo ulitajwa kuwa ni ukoloni-mambo leo kutokana na kubadilika kwa sura ya ukoloni wa zamani. Ukoloni-mambo leo ulitumika kumaanisha harakati mpya iliyofanywa na madola makubwa kwa lengo la kutafuta malighafi ya kutumiwa na nchi hizo kutoka katika nchi zilizokuwa zimekoloniwa. Siasa hizo za wakoloni zilipelekea kubadilika kwa mfumo wa kisiasa na kubuniwa serikali vibaraka kwa malengo ya kudhamini maslahi ya wakoloni katika nchi zilizokuwa zimekoloniwa. Jambo hilo liliyapa fursa nzuri madola makubwa kwa ajili ya kupora maliasilizi za nchi dhaifu na hasa barani Afrika, ambapo athari mbaya za suala hilo zingali zinaonekana hadi leo. Pamoja na kupewa uhuru nchi hizo lakini bado zinalazimika kufungamana na kutii amri za wakoloni wao wa zamani ambao walitumia mbinu hatari za kuzifanya nchi hizo ziwe tegemezi hata baada ya kupewa uhuru wa kidhahiri.

Madola makubwa yalitumia mbinu za kiuchumi na kisiasa kuzibana nchi dhaifu zilizokuwa zimekoloniwa. Mbinu hizo za ukoloni katika sura ya masuala ya uchumi na viwanda unajulikana kama Neo-Colonialism au Ukoloni-Mambo Leo. Hali hiyo imezipelekea nchi dhaifu kuendelea kubaki katika hali ya umasikini na kutoendelea kiuchumi na kiufundi. Ibara au neno hilo lilianza kutumiwa sana kufuatia kikao cha Nchi Zisozofungamana na Upande Wowote cha Bandung nchini Indonesia mwaka 1965. Katika kikao hicho Sukarno, Rais wa wakati huo wa Indonesia alilaani vikali siasa hizo za madola makubwa za kuzibana nchi dhaifu kupitia masuala ya uchumi na utamaduni Katika hali ya hivi sasa pia, madola hayo na hasa Marekani yanajaribu kuzitishwa nchi nyinginezo za dunia fikra zake kwa lengo la kuzidhibiti kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni nchi hizo.

MWISHO