MAMBO MUHIMU KWA ATAFUTAYE ELIMU

 

MAMBO MUHIMU KWA ATAFUTAYE ELIMU

" Mtu anayepaswa kutafuta elimu ni lazima, hatua ya kwanza kabisa, apitie utakaso wa kiroho, aingize taqwa (uchaji Mungu) ndani ya roho yake, aondoshe nia mabaya na malengo ya kidunia, na kujipima mara kwa mara kuangalia iwapo elimu yake anaitafuta kwa ajili malengo ya kidunia. Mtu ni lazima akumbuke kwamba kumcha Mungu ni sifa maalum ya 'alim (mwanachuoni) na yeyote asiye kuwa na ucha Mungu huyo yuko nje ya daraja za wenye elimu, hata akiwa amehifadhi vitu vingi moyoni au awe anavutia anapozungumza.

" Katika kila hatua ya kutafuta elimu, ni lazima ufikiri kwa undani sana kuhusu lengo lako la msingi la kutafuta elimu. Jiulize: kwa nini natafuta elimu? Je ni kwa ajili ya kupata kazi nzuri, au kushindana na mwenzio au na kikundi, au kupata tuzo, shahada au nafasi kubwa katika jamii? Ikiwa unatafuta elimu ya juu, je waitafuta kwa ajili tu ya kuandika vitabu, nakala, au kutoa hotuba ili usifiwe kuwa ni mwanamume au mwanamke msomi?
Au kwa sababu ya kumridhisha Mungu na kuwatumikia waja wake?

" Elimu uipatayo ni lazima ikuongoze uwe mwema zaidi, ufanye vitendo vya uaminifu na ikufanye umpende na kumcha Mungu zaidi wakati ukiendelea. Elimu isiyomuongoza mtu kufanya mambo mema, hiyo si elimu ya kweli. Elimu inayoishia kwenye maneno tu na haina vitendo vyenye kuwatumikia viumbe wa Mwenyezi Mungu hiyo ni elimu duni sana na itatoweka na wakati.

" Chunguza tabia yako wakati ukitafuta elimu. Je elimu yakufanya uwe mnyenyekevu zaidi na mvumilivu kwa marafiki zake na wenzio? Au itakufanya uwe jeuri, mwenye kibri na mbishi? Je inafanya iwe ni vigumu kwako kukubali ukweli na kukubali kibri chako kwenye kadamnasi ya watu? Je inakufanya uwaonee wivu wale wenye elimu zaidi yako? Kumbuka kwamba ubinafsi unaondoshwa na kufutwa kwenye elimu ya kweli, miongoni mwa alama za maadili ya elimu ya kweli nikutokuwa na ubinafsi, ujuba, kujipenda na kibri.

" Unapokuwa ukitafuta elimu, basi daima muamini Mungu, mheshimu mwalimu wako na usione haya kujifunza hata kutoka kwa mdogo wako. Durusi na zingatia chochote ulichokisoma. Kila siku muombe Mwenyezi Mungu akusaidie na huruma zake akupe fikra njema, na akulinde kutokana na kuitumia elimu unayoipata kwa ajili ya mambo ya kidunia na malengo ya kibinafsi.

Hitimisho:
" Imam Ali (a.s.) amesema: "Mtu anayejitolea kwenda kutafuta elimu ni kama anayepigana katika njia ya Mwenyezi Mungu." [Al-Majlisi, Bihar al Anwar, Juz. 1, Uk. 179]
...Na mcheni Mwenyezi Mungu, naye Atawafundisha...
(Qur'an, 2: 282) Mtume mtukufu (s.a.w.w.) wa Uislamu amesema: "Kutafuta elimu ni wajibu kwa kila Muislamu, mwanamume au mwanamke." [Al-Majlisi Bihar al-Anwar, Juz. 1. Uk. 177]

Thamani ya roho …
Kutafuta Elimu
Kulingana na mafunzo ya kiislamu, kutafuta elimu ni moja katika matendo ya ibada yamuongozayo mtu kwenye njia ya Peponi. Hata hivyo, lengo la kutafuta elimu ni muhimu zaidi kuliko hata elimu yenyewe. Kutafuta elimu ya kweli kwa lengo la kidini, kwa ajili ya kumridhisha Mwenyezi Mungu na kuwahudumia viumbe wake, humpeleka mtu Peponi akiwa pamoja na mitume na mawalii. Lakini kutafuta elimu kwa madhumuni ya kibinafsi, au mazoea tu, au kwa malengo ya kidunia humpeleka mtu kwenye ujinga, madhambi kwa viumbe, na hatimaye kuingia Motoni.

Ukweli wa elimu
" Mtume Muhammad (s.a.w.w.) amesema: "Elimu si kitu kinachopatikana kwa kusoma sana, bali ni nuru ya Mwenyezi Mungu anayoiingiza ndani ya moyo wa mja wake apendaye kumuongoza." [Al-Majlisi, Bihar al Anwar, Juz. 67, Uk. 140]
" Matawi yote ya elimu, licha ya asili yake, yanaweza kugawanywa katika mafungu mawili: (1) Elimu ya Akhera, ambayo lengo lake kuu ni kufikia daraja ya juu ya kuwa karibu na Mwenyezi Mungu, kuwatumikia viumbe wa Mungu, na kupata malipo mema ya Akhera. (2) Elimu ya kidunia, ambayo lengo lake kuu ni kupata mambo ya kimaada, utajiri, cheo cha kijamii, na kujitosheleza kwa tamaa za kibinafsi. Kwa hivyo, ni nia ya kupata elimu ndiyo inayoangaliwa, aidha itakuwa ni ya kidunia au ni kwa ajili ya Akhera.
" Kila roho inayoendelea kujitakasa kutokana na mielekeo michafu na ubinafsi itapata motisha wa kimalaika. Hivyo basi elimu anayoipata mtu ni ya kweli, ni ya Mwenyezi Mungu, kwa sababu inamuongoza kufanya matendo mema na kumuelekeza kuwa karibu na Mwenyezi Mungu. Elimu hii ya kweli ni taa ya kiroho inayomuonyesha njia ya moja kwa moja kwa Mwenyezi Mungu na kwenye makazi ya baraka Zake.

" Roho inayotawaliwa na ubinafsi na mielekeo miovu hupata motisha wenye hulka za kishetani, na hivyo kumuongoza kwenye ujinga-mkanganyo (m.y. Mtu kuwa mjinga na kutojua kama yeye ni mjinga), na kwenye kifuniko chenye utata kinachoziba ukweli wa lengo la Mwenyezi Mungu la kuumba, dhati ya Mwenyezi Mungu, na maisha ya Akhera. Kwa hivyo, elimu yoyote inayopatikana moja kwa moja kwa malengo ya kidunia, ubinafsi, na matendo maovu, hatimaye ni yenye kupelekea motoni.
" Mtume Muhammad (s.a.w.w.) amesema "Hakika, elimu inakusanya mambo matatu: 'alama imara', 'wajibu adilifu', na 'sunnah thabiti'. Zaidi ya hayo ni ziada tu." [Al Kulayni, al Kafi, Juz. 1, "kitab fadhl ul 'ilm", "bab sifat al 'ilm wa fadhluh", Hadith #1] " Neno 'alama imara' linamaanisha elimu yenye maana kiakili, miongozo sahihi na mafuzo ya Mwenyezi Mungu. 'Wajibu adilifu' inamaanisha elimu ya maadili na utakaso wa kinafsi. 'Sunnah thabiti' maana yake ni elimu yenye mitazamo ya kimaada na inahusisha aina ya harakati za kimwili. Kuna wakati ambapo kutafuta elimu huwa ni 'wajibu adilifu' na wakati mwingine huwa ni 'sunnah thabiti'.

" Elimu za utabibu, anatomia (viungo vya mwanaadamu), elimu ya falaki, unajimu n.k. ikwa zitaangaliwa kama ni ishara na alama za Mwenyezi Mungu, au elimu zinazohusu historia na ustaarabu, zitakapoangaliwa kama ni njia ya kupata funzo na kuwa na hadhari na matukio, haya yote yatawekwa katika fungu la `alama imara', kwa sababu kwa njia ya hizo, elimu ya Mwenyezi Mungu au ya ufufuo hupatikana au huthibitishwa.

Faida ya kutafuta elimu ya kweli
" Mtume Muhammad (s.a.w.w.) amesema: "Anayefuata njia ya kutafuta elimu, Mwenyezi Mungu humsahilishia ya kwenda Peponi. Na Malaika huwakunjulia mbawa zao watafutao elimu kwa kuridhika nao. Kila kiumbe aliyeko mbinguni na duniani humtakia msamaha atafutaye elimu, hata samaki baharini. Ubora wa mwanachuoni (alim) kwa mcha Mungu (abid) ni kama ubora wa mwezi kamili unapong'aa usiku juu ya nyota zingine. Wanavyuoni ni warithi wa mitume, kwani mitume hawakuacha urithi wa mali bali wa elimu. Kwa hivyo anayejishughulisha nayo hupata faida nyingi." [Al Kulayni, al Kafi, Juz. 1, "kitab fadhl ul-'ilm", Hadith #1]

Sifa za kimaadili za elimu ya kweli
" Elimu inapotafutwa kwa nia ya Mwenyezi Mungu, huifanya shakhsiya ya mtu kuwa ya kidini. Mtu kama huyo ana sifa zenye motisha wa Allah, na tabia, maneno na vitendo vyake huonyesha hayo. " Imam Ali (a.s.) alikuwa akisema: 'Ewe mtafutaji elimu, elimu ina fadhla nyingi. (Ikiwa utaifikiria kuwa ni kama mwanaadamu) kichwa chake ni unyenyekevu, jicho lake ni kutokuwa na wivu, sikio lake ni kuelewa, ulimi wake ni ukweli, kumbukumbu yake ni kutafiti, moyo wake ni nia nzuri, utambuzi wake ni maarifa (ma`rifah) ya vitu na mambo, mkono wake ni huruma, mguu wake ni kuwatembelea wanavyuoni, azimio lake ni uaminifu, busara yake ni ucha mungu, makazi yake ni uokovu, kupanda kwake ni uaminifu, silaha yake ni ulaini wa mazungumzo, upanga wake ni kuridhika (ridha), jeshi lake ni kujadiliana na wanavyuoni, utajiri wake ni mwenendo mwema, akiba yake ni kutofanya madhambi, mahitaji yake ni safari ya mema, maji yake ya kunywa ni upole, mwongozo wake ni wa Mwenyezi Mungu, na marafikizake ni kuwapenda wateule." [Al Kulayni, al-Kafi, kitab fadhl al-'ilm, bab al nawadir, Hadith # 3]

" Mtume Muhammad (s.a.w.w.) aliulizwa: "Elimu ni nini?" Akajibu: "Ni kunyamaa kimya". Akaulizwa: "Kisha?" Akajibu: "Kusikiliza kwa makini." Akaulizwa tena: "Kisha?" Akajibu: "Kukumbuka." Akaulizwa: "Kisha?" Akajibu: "Kuifanyia kazi (uliyoisoma)." Akaulizwwa tena: "Kisha?" Akajibu: "Kueneza." [Al-Majlisi, Bihar al-Anwar, Juz. 2, Uk. 28] " Imam Ali (a.s.) alikuwa akisema: "Kuna alama tatu za mwanachuoni: "Elimu, Subira na kuwa kimya". [Ibid, Juz. 2, Uk. 59] Imekatazwa kutafuta elimu kwa… Kulingana na mafunzo ya Ahlul Bayt (a.s.) wa Mtume (s.a.w.w.), imekatazwa kutafuta elimu kwa ajili ya mambo ya kidunia na malengo ya ubinafsi. " Imam Ali (a.s.) amesema: "Usitafute elimu kwa malengo manne: (1) Kutukuzwa mbele ya watu wa elimu (2) Kushindana na asiye na elimu (3) Kujionyesha kwenye kadamnasi ya watu (4) Kuwavutia watu kwa minajli ya kupata ukubwa." [Al-Majlisi, Bihar al-Anwar, Juz. 2, Uk. 31]

MWISHO