20
19. Hitimisho Kuna milango katika kitabu alichoandika ndugu Juma ambayo hatukupenda kuizungumza, kwani ukichunguza utakuta maneno yake yote yamejengeka katika dhana mbili. Moja ni ile kauli aipendayo kuikariri kwamba (Penye andiko huwa hakuna ijtihadi:) Bila shaka andiko alilokusudia ni ile kauli ya Ibnu 'Abbas (Radhiya Allaahu 'Anhu) alipokataa mwezi wa Sham kwa kusema: (La! Hivi ndivyo alivyotuamuru Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)?.) Kwa upande wetu tumejaribu kuilezea kifani kauli hii na tumeonesha kwa kutumia ushahidi mbali mbali juu ya udhaifu unaopatikana katika kuitegemea kauli hiyo katika mas-ala haya.
Ni fani gani mulioitumia kubainisha Hadithi hio? Pili ni kosa kusema kuwa hio ni kauli ikiwa munakusudia kuwa ni ijtihad tu; hio si kauli kwa maana ya ijtihad bali ni Hadithi. Nakukumbusheni maneno yenu muliposema: "Isipokuwa Sahaba akisema: "Tumeamrishwa kadha" au "Tumekatazwa kadha." Jambo hilo hupewa hukumu ya "Rafii" yaani hio inazingatiwa kuwa ni Hadithi ya Mtume(s.a.w.w) . Kwa bahati mbaya, maneno yenu haya - ambayo ni sahihi kwani ndivyo ilivyo katika elimu ya Hadithi - ni kinyume na matendo yenu. Tazama kwamba hamuiti hio kuwa ni Hadithi bali munasema "Kisa" au "Kauli"; wakati muitakayo nyinyi ndio munaita "Hadithi". Hii inaashiria kwamba hamuutaki ukweli bali munataka kulazimisha rai hata kama ni kinyume na fani za elimu.
Dhana ya pili ya ndugu Juma imejengeka katika msingi dhaifu wala haina nafasi katika uwanja wa fani (kitaalamu) nao ni kule kusukuma kwake juu ya elimu ya Jiografia. Umeonekana udhaifu wake hasa pale alipokuwa akijaribu kuelezea tofauti iliyopo baina ya nchi na nchi katika suala zima la kutofautiana kwa masaa na kuingia kwa usiku na mchana kwa baadhi ya nchi. Kwa upande wa suala hilo pia tumeshalieleza na kulitolea mifano mbali mbali.
Udhaifu munao nyinyi, kwa kudai kwenu kwamba inawezekana kwa ulimwengu mzima kufunga sawa sawa na kwamba wote wanakutana katika usiku na mchana, ilhali kuna sehemu nyingi ambazo zimepishana kwa masaa mengi: huku usiku kule mchana; jua likitua kule huku ni asubuhi. Sasa vipi watafunga sawa sawa na kukutana kwa usiku na mchana. Nyinyi hamuoni haya munavyosukuma kwa kunukuu kanuni za kiusuli halafu hata kuzifasiri hamujui licha ya kuzitumia?! Kanuni nyengine munazinukuu kutolea hoja nazo ni dhidi yenu, yote hayo nyinyi hamuyajui na munasukuma na wenyewe mumeridhia!
Mwisho tunachukua fursa hii kumuonya ndugu Juma kuwa amuogope Mwenyezi Mungu hususan katika mas-ala ya kielimu. Akumbuke kuwa Mwenyezi Mungu Ameonya juu ya mtu kusema jambo au kufanya asilolijua. Aelewe kwamba ataulizwa juu ya hilo Lingekuwa jambo la busara kama ndugu Juma angalikubali kuuliza na kufanya utafiti zaidi juu ya mas-ala haya kama agizo la Mwenyezi Mungu linavyotutaka.
Wala usifuate (ukipita ukiyasema au kuyafanya) usiyo na ilimu (ujuzi) nayo. Hakika masikio na macho na moyo, hivyo vyote vitaulizwa. (17: 36)
Jawabu
Hii ni nasaha nzuri kwa ndugu kumpa nduguye. Nami nakupeni nasaha yangu kwa udhati: si kwa kukejeli. Tafadhali chukueni vitabu vya fani hususan usulu-fiqhi, usulul-hadith, balagha, nahau na sarfu. chukueni vitabu hivyo, nendeni kwa mtu kama Sheikh Aliyani akusaideni. Au kwa wale walio Pemba nawende kwa mtu kama Sheikh Kabi. Hawa wataweza kukusaidieni kwani wana uwezo mzuri. Vyenginevyo mutakuwa siku zote munasukuma mukinukuu kitu ambacho kukifasiri hamujui wala hamujui mahala pa kukiweka.
Muogopeni Mwenyezi Mungu hususan katika mas-ala ya kielimu. Kumbukeni kuwa Mwenyezi Mungu Ameonya juu ya mtu kusema jambo au kufanya asilolijua. Aeleweni kwamba mutaulizwa juu ya hilo Lingekuwa jambo la busara kama ndugu zetu mungelikubali kuuliza kwani Allah anasema:
﴿ وَلَا تَقْفُ مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ ۚ إِنَّ السَّمْعَ وَالْبَصَرَ وَالْفُؤَادَ كُلُّ أُولَـٰئِكَ كَانَ عَنْهُ
مَسْئُولًا﴾
Wala usifuate (ukipita ukiyasema au kuyafanya) usiyo na ilimu (ujuzi) nayo. Hakika masikio na macho na moyo, hivyo vyote vitaulizwa. (17: 36)