6%

3

MUANDAMO WA MWEZI

SEHEMU YA TATU

IKHTILAFU SIO UPINZANI

MNASEMA

"3. Ikhtilafu Sio Upinzani Tunapenda kumfahamisha ndugu Juma kwamba mara nyingi inaweza kutokezea katika jambo moja watu kutofautiana lakini hawapingani. Ni vyema kuelewa kwamba upinzani umo katika Siasa za kilimwengu na mambo mengine sio katika masuala ya Dini. Katika Dini hutokea Ikhtilafu. Masahaba (Radhiya Allaahu 'Anhum) pia walikuwa wakikhitilafiana katika baadhi ya mambo, lakini hawakuwa wakipingana. Kila mmoja aliweza kushika mwendo wake bila kugombana na mwenzake. Ama pale ulipotokea upinzani kwa bahati mbaya - jambo hilo liliwapelekea kugombana au kupigana vita, kwani jambo hilo ni katika amali za Kishetani. Lakini mara walipotanabahi juu ya udhaifu huo waliomba toba kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na kutakana misamaha baina yao Na huo bila shaka ndio mwendo wa watu wema.

Kwa bahati nzuri semina na makongano yote yaliyofanyika ndani na nje ya Zanzibar hapajatokea kuitwa 'pinzani' wala neno 'upinzani' halijatumika hata mara moja. Bali semina zote zilizowahi kufanyika zimekuwa zikisisitiza maneno ya 'umoja' na 'kuelimishana' wala sio 'kupingana.'

Neno 'upinzani' haliko katika midomo ya Wanavyuoni. Tanasikitika sana kuwa Ndugu yetu Juma Muhammad Rashid amelitumia neno ambalo si zuri la 'upinzani' na kulikariri katika kitabu chake zaidi ya mara 33. Kwa kweli hizo si kauli za wenye busara na hikma, bali ni kama alivyozoea kuzitumia. Kwa mfano pale alipokuwa akimlalamikia Shaykh Naaswir Bachuu, alisema: (Tazama pia katika uk. 109-110 uone upinzani alioutoa hapo halafu linganisha upinzani huo na upinzani alioutoa kabla ya hapo, utaona jinsi gani mwanamume alivyokuwa bingwa wa kubadilika! Na hili si jengine bali ni lile Waswahili wanalolisema: "Mfa maji hukamata maji.")

Tunamshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwamba kwa upande wa hapa kwetu Tanzania watu wanaruhusiwa kufunga na kufungua kwa mujibu wa misimamo yao (yote miwili) bila ya kugombana. Swala za 'Iyd kwa upande wa watu wanaofuata mwezi unapoonekana popote duniani wamekuwa wakiswali misikitini na viwanjani bila ya bughudha yoyote. Bali hata katika familia moja yenye misimamo hiyo tofauti, watu hawagombani. Huko ndiko kukhitilafiana sio kupingana".

JAWABU

Nakubaliana na nyinyi sana kwamba ikhtilafu si ugomvi. Lakini nyinyi wenyewe mutakumbuka kwamba munasisitiza kufata wanavyuoni. Wanavyuoni wa Kiislamu wanapozungumzia rai tafauti hutumia maneno haya: "Na ikapingwa kauli hii". Au:"Upinzani wa mwanzo ni kadha wa kadha..". Au: Na wakasema wale watupingao au waliotafauti na sisi. Au "Wakavutana". Au "Wamesukumana". Hizi ndio lugha za wanavyuoni na mimi nimechukua kutoka kwao. Nao kwa lugha hizo huwa hawakusudi kwamba kulikuwa na ugonvi, bali wanakusudia kwa kumekuwa ikhtilafu. Kwa hivyo, mimi sijakusudia upinzani kwa maana ya ugonvi, bali naku sudia kutokuafiki rai au kauli Fulani, na hilo ni jambo linalosemwa na wajuzi.

SEHEMU YA NNE

JUMA AMPINGA AL-IMAMU AL-SHAUKANI

MNASEMA 4.

Ndugu Juma Anampinga Al- Imam Shawkani Jambo jengine la kusikitisha ni kuwa ndugu Juma haonyeshi kuwaheshimu Wanavyuoni au kuwapa hadhi zao wanazostahiki. Wanavyuoni wana heshima zao hata pale wanapokosea. Ni vyema kuelewa kwamba Al Imam Shawkani alikuwa ni miongoni mwa Wanavyuoni wakubwa kama ilivyoelezwa kwenye historia yake fupi katika kitabu cha "Kuandama Kwa Mwezi" cha Shaykh Naaswir Bachuu Uk 35. Al Imam Shawkani aliandika vitabu vingi vya kukubalika pamoja na Tafsiri yake ya Qur-aan Tukufu inayojulikana kwa jina la "Fathul Qadir."

JAWABU

Al-Imamu Al-Shawkani - bali hata aliye chini ya yeye sana kwa elimu - ninamuheshimu sana. Na katika kitabu changu nimemnukuu kwa kumpa laqabu anayostahiki. Sehemu nyingi nimemwita Imamu. Huku ni kukikiri kuwa ni mtu wa maarifa mapana kwani Imamu hawi mtu yeyote bali ni yule aliyekusanya zana nyingi za elimu. Labda sehemu moja tu nilimwita Sheikh, nayo pia ni laqabu ya heshima. Sasa vipi munasema kwamba simpi heshima yake. Tukumbuke kwamba kumuheshimu mwanachuoni, si maana yake kwamba tusimpinge au kujadili maneno yake. Kufanya hivyo si kumuheshimu bali ni kumtakasa, nalo ni kosa. Pili: kwani nyinyi wale Maimamu wakubwa munaowapinga katika suala hili la muandamo wa mwezi huwa ndio mumewavunjia heshima yao?

MNASEMA

Ndugu Juma katika kujikweza kama kwamba yeye ana elimu kubwa zaidi na kwamba anakubalika zaidi kuliko Al Imam Shawkani, anathubutu kusema: ((Huo ndio upinzani wa pili wa Al-imamu Al-shaukaniy, lakini kama unavyoona jawabu yetu ya kwanza inajibu baadhi ya nukta zilizomo katika upinzani huu.)) [ uk : 111]". Kisha akamfananisha Al Imam Shawkani na watu wa kawaida (yaani labda ni mtu wa mitaani asiyekuwa na elimu) kwa kusema: ((Maneno haya ya Al-imamu Al-shaukaniy - kama yalivyo maneno ya watu wengi wa kawaida.))

JAWABU

Haya! Ubaya uko wapi hapa? Sasa nyinyi ndio munamuheshimu au munamtakasa. Kwani nani kasema kuwa mwenye elimu hajibiwi katika kutafuta haki? Ikiwa Ibn Abbaas kapingwa na watu ambao hawamuoni hata vumbi lake, itakujakuwa Al-Imamu Al-Shawkani. Kwani Sheikh Bachoo yeye katika hicho kitabu chake si anawapinga wanavyuoni wote waliotangulia Afrika Mashariki, au tuseme na yeye anajikweza na kujifanya ana elimu?! Kwa kweli haya ni maneno ya aliyefilisika: asiye na hoja.

Ama kauli yenu: "Kisha akamfananisha Al Imam Shawkani na watu wa kawaida (yaani labda ni mtu wa mitaani asiyekuwa na elimu)" hayana maana, kwani nimesema: ((Maneno haya ya Al-imamu Al-shaukaniy - kama yalivyo maneno ya watu wengi wa kawaida.)). Sasa sijui ni mtu gani wa mitaani aliye na daraja ya uimamu! Enyi walimwengu! Hebu fahamuni munayoyasoma. Mimi nafananisha kauli na kauli: si mtu na mtu. Al-Shawkani nimempa hadhi yake ya uimamu, lakini alichokisema hakikubaliki kwani hakina dalili za kisharia. Au munataka tuchukue tu kwa sababu msemaji ni fulani bila ya kutazama kilichosemwa?

MNASEMA

Ndugu Juma katika kumuandama Al Imam Shawkani anaendelea kusema: ((Penye andiko huwa hapana ijtihadi;)) kama kwamba Al Imam Shawkani alikuwa hajui Qur-aan wala Hadiyth. Au kama kwamba Al Imam Shawkani anampinga Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

Jawabu Inaonekana nyinyi muko mashariki na elimu iko magharibi! Tafadhali fungeni safari muifate. Kauli ya Imamu yeyote awaye inarejeshwa katika dalili za kisharia. Maimamu wanakosea pia na mifano iko mingi. Na kutajia mifano mitatu tu:

1) Al-Imamu Al-Nawawi kunukuu Hadithi ifatayo:

"Tulikuwa tunasafiri pamoja na Mtume(s.a.w.w) , miongoni mwetu wako waliofunga na wako waliokula, na wako waliotimiza (rakaa za Sala) na wako waliopunguza. Basi aliyefunga hakumtia kasoro asiyefunga; wala asiyefunga (hakumtia kasoro) aliyefunga; wala aliyepunguza (rakaa katika Sala) (hakumtia kasoro) aliyetimiza; wala aliyetimiza (hakumtia kasoro) aliyepunguza." Hadithi hii kainukuu Al-imamu Al-nawawi katika Sharhu Sahihi Muslim na akainasibisha na Sahaba Abi Said Al-khudriy katika masimulizi ya Muslim katika Sahih yake. Wakati Hadithi hii haimo katika Sahihu Muslim. Hadithi ya Abi Said Al-khudriy alioiashiria Al-imamu Al-nawawi - katika mlango huo huo - ni Hadithi na. 95/2612, nayo inasema: "Tulikuwa tunasafiri pamoja na Mtume(s.a.w.w) katika mwezi wa Ramadhani. Hakumtia aibu aliyefunga kutokana na aliyekula, wala aliyekula kwa sababu ya kula kwake."

Na mfano wa Hadithi hii ni Hadithi na. 93/2610 na 96 /26134 na Hadithi nyengine tatu zinazofata mpaka mwisho wa mlango huo, wala hakuna maneno yanayosema: "Wala (hakumtia aibu) aliyepunguza (rakaa katika Sala) juu ya aliyetimiza; wala aliyetimiza juu ya aliyepunguza:" maneno haya hayamo katika Hadithi hio ya Muslim, bali kilichomo ni mas-ala ya kufunga na kutokufunga tu kwa msafiri katika mwezi wa Ramadhani. Na kwa sababu hii ndio maana Al-Shaukaniy akampinga Al-imamu Al-nawawi kwa maelezo yake hayo. Je tuseme Al-Imamu Al-Shawkani naye kafanya kosa kumpinga Al-Imamu Al-Nawawi, au kafanya wajibu wake wa kudhihirisha haki. Na je Al-Imamu Al-Nawawi kawa ndio si mwanachuoni tena kwa sababu hapa kakosea?! Fahamu ziko wapi?!!!!!!!!

Ibn Hisham: Ibn Hisham Al-Ansari ni bingwa mkubwa wa lugha. Katika kitabu chake Qatru Al-Nada anasema kwamba miongoni mwa sharti za kufanya kazi masdar ni kuwa baina yake na mtendwa wake pasiwe na kitu kilichokaa katikati. Anasema (Sharti) ya saba ni kuwa (ili masdar ifanye kazi) basi isiwe yenye kupambanuliwa kutokana na mtendwa wake. Na kwa hivyo, (w atu wa Nahau) wakairejesha kauli ya aliyesema kwamba (neno yawma katika Aya: Yawma tubla Al-Sarair ni mtendwa wa neno "Raj'ihi", kwani baina yao pamekuwa na upambanuzi kwa kuwekwa khabar.

Hayo ni maneno ya Ibn Hisham pamoja na kundi la wanavyuoni. Sasa someni Aya hii:

Neno It'am ni masdar; na neno yatiman na miskinan ni watendwa wa Masdar hio. Hata Ibn Hisham mwenyewe alipoingia kueleza migawanyiko ya masdar 'aamil katoa mfano wa Aya hii hii. Haya je tumfate Ibn Hisham au tufate dalili za kielimu? Na je Ibn Hisha tayari kageuka kuwa mtu wa mitaani kwa sababu hapa kakosea? Kwa hivyo, wanavyuoni wanakosea, na wanapokosea na sisi pakitubainikia kwa dalili sahihi kuwa hili ni kosa huwa tunazinduana kuwa hili ni kosa, hata akiwa aliyelifanya ni nani, wala huko hukumpunguzii mwanachuoni kima chake, kwani hakuna asiyekosea. Na nadhani hivyo ndivyo Uislamu unavyotutaka.

Al-Hafidh Ibn Hajar: Kuna Hadithi inasema: "(Kasimulia Abu Said Al-Khudri) kwamba kikundi cha Masahaba wa Mtume (s.a.w.) walipita kwa kabila moja la Kiarabu, mtu mmoja kati yao akadonolewa (na ng'e), wakasema: 'Kuna mzinguaji kati yenu?' Mmoja wao akamzingua kwa Al-Hamdu. Basi akapewa kikundi cha ghanam (kondoo au mbuzi) akakataa kukichukua. Wakaja kwa Mtume(s.a.w.w) wakamtajia hayo, akasema: 'Aliyechukua kwa zinguo la batili (ndiye aliye chukua haramu), (ama wewe) kwa hakika umechukua kwa zinguo la haki. Chukueni na mie munipe sehemu yangu". Hadithi hii pia kaipokea Al-Bukhari kutoka kwa Abu Sa'id bin Al-Mu'allah na kutoka kwa Ibn Ibn Abbas kwa lafdhi tafauti kidogo.

Al-Hafidh Ibn Hajar kawakosoa waliosema kuwa Hadithi hii imesimuliwa kutoka kwa Abu Sa'id Al-Khudri. Anasema Ibn Hajar: "Al-Ghazali na Al-Fakhr Al-Razi wakifatiwa na Al-Baydhawi wamekinasibisha kisa hiki kwa Abu Sa'id Al-Khudri nalo ni kosa, bali yeye (mwenye kisa hiki) ni Abu Sa'id Al-Mu'alla". Tazama Fat-hu Al-Bari j. 9, uk. 5076, katika sherehe ya Hadithi na. 4474. Nami nasema: lakini maelezo hayo ya Ibn Hajar ya kuwakosoa Al-Ghazali, Al-Razi na Al-Baydhawi, bado ni maelezo ya kufirikiwa kwani kisa hiki kimesimuliwa pia na Muslim Hadithi na. 2201, na Abu Dawud Hadithi na. 3415 na wengine kutoka kwa Abu Sa'id Al-Khudri. Kwa hivyo, Al-Ghazali na wenziwe hawakukosea isipokuwa ikiwa Ibn Hajar anadai kuwa sanad hizo ni dhaifu na ya Al-Bukhari yenye kusema kuwa muhusika alikuwa ni Abu Sa'id Al-Mu'allah ndio sanad sahihi.

Utaona kwamba Ibn Hajar kawakosoa wanavyuoni wengine. Wakati pia na yeye kakosea katika kuwakosoa huko kwani walivyosema wao ndivyo ilivyo katika Sahihu Muslim. Sasa tusema wanavyuoni hawa wakubwa tayari wameshakuwa watu wa mitaani kwa kukosowana huku? Jamani! Sisi tumeambiwa tuwaheshimu Maulamaa: sio tuwatakase na kwamba hata mtu akikosea asiambiwe. Sasa kama kanuni inayokubalika kwa Umma mzima inasema: "Penye andiko huwa hapana ijtihadi", je Al-Imamu Al-Shawkani akenda kinyume na kanuni asirejeshwe kwa sababu yeye ni mwanachuoni mkubwa. Nakukumbusheni maneno yenu yaliomo kitabuni mwenu muliposema: "Kutegemea maneno, matupu ya mwanachuoni kama ni Khaas bila ya kuonyesha dalili zenye kukubalika kifani, huo utakuwa ni udhaifu". Haya mumeyasema nyinyi kuzipinga kauli za wanavyuo ni musiokubaliana nao. Sasa vipi munanilaumu kwa kitu mukitendacho?!

Ingelikwa dharau lau nilisema kuwa Al-Shawkani hana akijuacho. Na mimi ni nani hata niseme kuwa Al-Shawkani hajui?! Mimi nadai kuwa hapa kakosea. Sasa nyinyi, ili iwe mumenijibu basi mubainishe kuwa: "Aa si kweli hakukokesea, na kanuni hio si kweli haipo". Hapo itakuwa mumenijibu. Lakin munaleta maneno ya mtu aliyefilisika na hoja munasema: "Kama kwamba Al Imam Shawkani alikuwa hajui Qur-aan wala Hadiyth. Au kama kwamba Al Imam Shawkani anampinga Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)". Kwani nyinyi hao munaowapinga munaitakidi kuwa hawajui Qur-ani na Hadithi au wanampinga Allaah na Mtume Wake(s.a.w.w) , au kwa sababu munahisi kuwa wamejitahidi na kukosea? Kwanini nyinyi mujiweke katika dhana safi na wenzenu muwaweke kwenye dhana mbovu?

Munasema Angalia katika kitabu chake Ndugu Juma kwenye uk 108 - 109 ameeleza misimamo ya Wanazuoni wawili mashuhuri; yaani Al Imam Badru Din na Shaykh Al Khalil ambao wamejaribu kuukosoa msimamo wa Al Imam Shawkan lakini kwa njia nzuri. Wote wawili wameonyesha kwamba ile ni Ijtihadi ya Al- Imam Shawkani katika kumfahamu Ibni ''Abbas katika kisa cha Kuraib wala hawakumfanya Al Imam Shawkani kama ni mpinzani. Ni vyema kuelewa pia kwamba wanaweza kutokea Wanavyuoni wengine wanaoweza kusema pia kwamba na hizo ni Ijtihadi za Al Imam Badru Din na Shaykh Al Khalil katika kumfahamu Al Imam Shawkani. Wala huwezi kusema kuwa Al Imam Shawakani alikuwa halifahamu andiko, Shaykh Al Khalil ndio amelifahamu andiko. Hizo zote ni Ijtihadi katika kukifahamu kisa cha Kuraib.

Jawabu Hapa hakuna sula la nani analifahamu andiko, suala ni kuwa mujibu wa Usulul Hadithi (elimu ya Hadithi), maneno ya Ibn Abbbaas yasemayo: "Hivi ndivyo alivyotuamuru Mtume(s.a.w.w) ," je yanazingatiwa kuwa ni Hadithi au si Hadithi? Hakuna hapa suala la kumfata Al-Imamu Al-Shawkani wala Al-Imamu Al-Khalili wala Imamu atayekuja: wote wanarejeshwa katika kanuni (pr iciples) zile zile na hakuna mwenye uwezo wa kuwa juu ya kanuni: kanuni ziko juu ya wote. Kwa hivyo, sisi tulipompinga Al-Imamu Al-Shawkani na kumuunga mkono Al-Imamu Badru Al-Din, si kwa sababu yule ni Al-Shawkani na huyu ni Al-Khalili au kwa sababu yule ni mtu wa madhehebu iliotafauti na yetu, bali ni kuwa huyu kasema kitu kilicho sawa na kanuni za Hadithi; yule kenda kinyume na kanuni. Pamoja na hayo, hatupingi ijtihadi ya Al-Imamu Al-Shawkani.

SEHEMU YA TANO

NDUGU JUMA ANATOA RAI BINAFSI

Munasema 5. Ndugu Juma Anatoa Rai Binafsi Katika kitabu chake alichokiandika, Ndugu Juma ameonyesha udhaifu wake wa kulazimisha kujaribu kujibu hoja za kitabu cha Shaykh Naaswir Bachuu. Maneno yake mengi yametawaliwa na ubinafsi. Hakupenda kuwa muadilifu katika kueleza hoja zake ingawa yeye mwenyewe anapokwama kihoja hujifanya kumgomba Shaykh Naaswir Bachuu huku akimwambia: (Kwa ufupi ni kuwa hii ni hoja ambayo haina faida yoyote ya kielimu, lakini tunaijadili kwa ajili ya watu wa mitaani tu).

Jawabu Hizo ni tuhuma zenu baada ya kushindwa kujibu hoja zangu. Sijui nani anayejilazimisha kujibu hoja na ambaye anakwama? Na hayo maneno: (Kwa ufupi ni kuwa hii ni hoja ambayo haina faida yoyote ya kielimu, lakini tunaijadili kwa ajili ya watu wa mitaani tu), niliyatoa baada kuwa nimeshajibu hoja au nilisema hivyo tu ikawa basi? Sasa asiyemuadilifu ni mimi au nyinyi ambao munataka kuonesha kitu tafauti na kilivyo. Mimi niliyasema hayo baada ya kuwa nimeshajibu, kisha ndio nikabainisha kwamba kielimu - yaani kwa watu wa mustawa wa elimu - suala hilo alililolileta Sheikh Nassor Bachoo halina maana lakini kulijadili kwangu ni kwa kuzingatia akili za watu wa mitaani. Nyinyi mumeyachukua maneno haya na kufanya kuwa ni ushahidi kuwa sikujibu bali nimekwama. Munadhani mutawadanganya watu na watu vitabu vyote wanavyo?!

MNASEMA

Ni kweli kwamba mlango wa Ijtihadi uko wazi, lakini si vyema katika wakati wetu huu mtu kutoa rai binafsi za kujikweza bila kunukuu hoja za Wanazuoni waliotangulia tena wanaokubalika. Katika kitabu cha Shaykh Naaswir Bachuu kuna hoja nyingi mno zilizotajwa kutoka kwenye vitabu vya Wanazuoni wakubwa ambao wameonyesha misimamo mbali mbali juu ya maudhui haya ya muandamo wa mwezi, lakini Ndugu Juma hakuijibu hata moja zaidi ya kumponda Al Imam Shawkani. Angalia misimamo ya Wanazuoni waliotajwa katika kitabu cha 'Kuandama Kwa Mwezi' cha Shaykh Naaswir Bachuu uk 5 - 11, 51 - 56, 59 - 74, 129 - 133. Pia angalia: 'Makubaliano Katika Mikutano Ya Wanavyuoni' yalivyoelezwa ambayo ndugu Juma ameyafumbia macho uk 134 - 155.

JAWABU

Kwanza mimi si mujtahid, kwa hivyo huo mlango uko wazi kwa mujtahidin. Ikiwa nyinyi wenzangu mumefikia daraja hio, basi musiwache kuupita mlango huo ili nasi tufaidike kwa ijtihada zenu. Lakini maandishi yenu yanaonesha kuwa hata daraja talabatul 'Ilmi hamujafikia. Pili ni kuwa aliyefikia daraja ya ijtihad halazimiki kunukuu maneno ya wanavyuoni wengine. Hata akinukuu basi hanukuu kwamba ndio dalili yake bali ni kuonesha kuwa wako waliosema kauli kadha. Kwa hivyo, kauli yenu: "Lakini si vyema katika wakati wetu huu mtu kutoa rai binafsi za kujikweza bila kunukuu hoja za Wanazuoni waliotangulia tena wanaokubalika" si kauli sahihi. Tatu: Hata mujtahid si kwamba ana haki ya kusema kitu kinyume na kanuni za lugha na usuli. Nakusudia kanuni walizokubaliana Umma mzima au zisizopingana na Qur-ani na Suna.

Nne: Katika mjadala huwa hapategemewi fulani kanena, bali panategemea dalili za Kisharia na maneno ya fulani hurudishwa katika dalili za kisharia. Na hicho ndicho nilichokifanya. Nakukumbusheni kauli yenu muliposema: "Kutegemea maneno, matupu ya mwanachuoni kama ni Khaas bila ya kuonyesha dalili zenye kukubalika kifani, huo utakuwa ni udhaifu". Na wanavyuoni nimewanukuu wengi. Lakini narudia tena kauli za wanavyuoni ni hoja pale walipokubaliana: si walipotafautiana. Wakitafautiana, basi huwa kauli zao si hoja, bali kila mmoja anaambiwa lete hoja ya Kisharia.

Sasa mimi hata nikinukuu wanavyuoni wa dunia nzima, ikiwa sikutoa ushahidi unaokubalika kielimu ni kazi bure. Ama Al-Imamu Al-Shaukani yeye tumeyajadili maneno yake kiurefu kwa vile Sheikh Bachoo na wengine wameonekana kuyategemea zaidi maneno yake. Na pia Al-Shawkani ndiye aliyeijadili Hadithi husika kwa urefu kulikoni wengine. Ama madai yenu muliposema: "Kumponda Al Imam Shawkani". Mimi nakanusha kwa nguvu dai hilo, mimi sijamponda bali sikukubaliana naye kwa vile nimeona hoja alizotoa ni kinyume na kanuni za Hadithi na Usuliil Fiq-hi. Sasa ili nanyi muwe mumenisomesha basi onesheni kuwa hoja zake ni sawa kwa mujibu wa kanuni za Hadithi na Usulil-Fiq-hi.

MUNASEMA

Angalia Ndugu Juma alivyokuwa akijenga baadhi ya hoja zake binafsi (za umimi) pale aliposema: (Nasi tunasema kwamba Aya ndio, lakini hoja yake katika Aya hio ni hoja dhaifu sana .) [uk. 71] ((Isipokuwa upinzani ambao - mimi kwa upande wangu - nauona kuwa una muelekeo juu ya tafsiri hii tulioitoa hapa,)) [uk. 62] Ziko wapi hapa hoja za Wanavyuoni wanaokubalika zaidi ya kudai: (Mimi kwa upande wangu nauona) au: (Ninasema bila shaka)

JAWABU

Na nyinyi munasema: "Sisi tunamjibu hivi.." wala hakuna mwanachuoni aliyejibu hivyo mulivyojibu nyinyi, ni rai zenu binafsi tu. Kwa hivyo, na nyinyi muna ubinafsi. Aidhan Sheikh Bachoo anasema: "Ni kweli kwamba msimamo wa upande wetu". Mimi sioni tafauti ya maneno "Sisi" au "Nasi" na maneno "Upande wetu" zote ni dhamiri (pronouns) za ubinafsi. Kwa hivyo, kosa hili nimejifunza kutoka kwenu. Ama kauli yangu (Isipokuwa upinzani ambao - mimi kwa upande wangu - nauona kuwa una muelekeo juu ya tafsiri hii tulioitoa hapa)". Ninasema:

1) Kama hilo nimelisema kwa mtazamo wangu, mulitaka niwadanganye watu niwambie hivi ndivyo walivyosema wanavyuoni. Mimi sighushi kama munavyofanya mimi: langu nasema kuwa hili ni langu; na la wanavyuoni nasema kuwa hili kalinena fulani.

2) Pili ni kuwa mulitakiwa munukuu kile nilichokisema kisha mukijibu kama mulikusudia kutafuta ukweli. Lakini hamukufanya hivyo, na badala yake munatafuta kitu ambacho munadhania kuwa hiki kitamtia aibu Juma ndio munataja. Sasa nikisema ninavyoona mimi, kitu gani kilichokuwa haramu hapa ni hii kauli au ni yale nilioyasema. Kama ni hii kauli, basi uharamuu wanaufanya wanavyuoni wote wa Umma, kwani kwenye rai zao binafsi husema: Au yaani ninavyoona mimi. Kama uharamu uko katika yale nilioyasema, tafadhali yanukuuni kisha muyajadili na kubainisha kosa liko wapi.

3) Tatu ni kuwa narudia tena kwamba kitabu cha mjadala huwa hakitegemei kauli za wanavyuoni, bali huwa kinajadili mambo kwa mujibu wa misingi yake ya kilugha na kiusuli na hivi ndivyo nilivyofanya. Sasa kama nyinyi munadai kuwa nimekosea kwa mujibu wa fani hizi, tafadhali nukuuni maneno yangu na muonesha kosa liko wapi.