12%

12

MUANDAMO WA MWEZI

SEHEMU YA KUMI NA MBILI

KUANDAMA KWA MWEZI KATIKA SEHEMU MOJA KUNATOSHELEZA KUANDAMA KWAKE DUNIA NZIMA

MNASEMA

12. Kuandama Kwa Mwezi Katika Sehemu Moja Kunatosheleza Kuandama Kwake Dunia Nzima Katika maelezo yaliyopita tumeeleza kwamba Hadiyth zote za Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) zilizotaja amri hii ya kufunga na kufungua ni Sahihi na ni zenye kukubalika mbele ya Wanavyuoni wala hazina khitilafu yoyote juu ya usahihi wake. Hadiyth zote hizo zimetaja amri hii ya hukumu ya kufunga na kufungua kwa ujumla - yaani ni jambo linalotekelezeka kwa watu wote katika siku moja. Wala agizo hilo halihusishi nchi fulani pasi na nchi nyengine. Ni agizo la ujumla 'aam.

Pia ni wazi kwamba agizo hilo la Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) halikutaja suala la kuwepo kwa matlai wala masafa gani, wala chengine chochote. Wala hakuna katika maelezo sahihi ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambayo yanakubalika na Wanavyuoni yaliyotaja kwamba 'kila nchi ifunge na ifungue kwa miandamo yao!' Kama ilivyoelezwa kwamba hoja inayotegemewa na baadhi ya Wanavyuoni wachache juu ya mas-ala haya ni kisa cha masimulizi ya Kuraib, masimulizi ambayo hayana ufafanuzi wa kina kama walivyoeleza hayo baadhi ya Wanavyuoni wengine na kuonyesha kuwa yana utatanishi (ihtimaalati). Jambo ambalo linaifanya hoja yake kuwa dhaifu. Kama yalivyoelezwa hayo na Wanazuoni wa fani ya "Usulul-Fiqhi."

JAWABU

Inaonesha tunaendelea kukariri yayo kwa yayo katika kila sura. Kudai kwamba Hadithi zote ni agizo la ujumla 'aam, ni kweli hilo ni agizo la ujumla lakini je ujumla huo uko mahala gani katika Hadithi hizo. Ujumla upo katika wenye kuamrishwa kwamba "Fngeni kwa kuuona". Kwa hivyo, ujumla unaopatikana ni kuwa watu wote wafunge kwa kuuona. Tumesema kwamba Lamu iliomo katika neno (Liru-uyatihi) inaitwa Harfu Jarri li-tta'alil. Yaani ni harufu yenye kulitia neno kasra na kuonesha sababu ya maneno yaliotangulia au sababu ya hukumu iliotajwa. Kwa hivyo, maana ya haya ni kuwa kuuona mwezi iwe ndio sababu ya kufunga au kwa lugha nyengine sababu ya kufunga iwe ni kuuona mwezi. Hii ndio maana ya maneno:"Fungeni kwa kuuona:" hakuna hapa kinachoonesha mas-ala ya kufunga kwa muandamo mmoja wala zaid i ya mmoja. Yaani ujumla hauambatani na sehemu bali unaambatana na walioamrishwa kwamba watu wote wafunge kwa kuuona: sio watu wote wafunge sawa. Ujumla huo ni sawa na ujumla uliomo katika Aya:"Simamisha sala kwa kutenguka jua" , na ujumla uliomo katika Hadithi isemayo:Usiku ukitokeza kutoka hapa na mchana ukaondoka kutokea hapa na jua likatua, basi aliyefunga ameshafungua (au na-afungue). Wala haina maana kuwa watu wa nchi moja wasali kwa kutenguka jua nchi nyengine, na wala haina maana kwamba usiku wa nchi moja ukiingia watu wa nchi nyengi wafuturu. Bali ujumla uliomo katika Aya ni kuwa watu wote wasali kwa kutenguka jua; na ujmla ulio katika Hadithi ni kuwa watu wote wafuturu kwa kuingia usiku: hakuna ndani ya maandiko haya mas-ala ya ujmla wa sehemu: ni ujumla wa wanaomrishwa.

Ama kauli yenu: "Pia ni wazi kwamba agizo hilo la Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) halikutaja suala la kuwepo kwa matlai wala masafa gani, wala chengine chochote" pia haikujengeka katika misingi ya kielimu. Wanavyuoni inapotajwa hukumu huwa wanaitafuta illa (sababu) ya hukumu hio. Ikiwa sababu imetajwa kwa uwazi, basi ni hivyo: hio ndio maslak njia yake; ikiwa haikutajwa basi huwa wanaitafuta kwa njia tafauti Masalik 'illa njia za kutafuta sababu. Kisha wakiipata ndio huifanyia Qiasi baina yake na baina ya kitu ambacho hukumu yake ha ikutajwa. Kwa hivyo, baada ya kuzikusanya sifa zote zenye kufaa kuwa sababu ya kwanini Mtume(s.a.w.w) akaamuru hivyo, tunapata sababu mbili kama nilivyoeleza katika kitabu, kwamba:

Moja ni kuwa: iwe hivyo ndivyo walivyoamrishwa na Mtume(s.a.w.w) kutokuuchukua mwezi wa Sham, kwa sababu huko ni Sham. Kwa hivyo, Sham iwe ndio illa (sababu) ya kutokuuzingatia muandamo. Hii inamaanisha kwamba lau Kuraib alikuwa anatoka Misri au Pemba wangeukubali muandamo huo. Illa (sababu) hii ni dhaifu, haifai kuifanya kuwa ndio illa (sababu) ya hukumu hio ya Mtume(s.a.w.w) iliomo katika Hadithi ya Kuraib na Ibn Abbas. Kwani:

a) Ni (It is an intrasitive cause as opposed to a transitive one). Yaani ni sababu ambayo hai vuuki mahala pake, nayo inapingwa na sababu nyengine yenye kuvuuka mahala pake.

b) Ni "Kulifanya jina kuwa ndio sababu." Na inavyotakiwa sifa iwe ndio sababu: sio jina. Naam! Jina linaweza wakati mwengine kufanywa illa (sababu) ikiwa lina maana ya sifa. Katika jina "Sham" maana hii haipo. Pili ni kuwa: iwe Mtume(s.a.w.w) kawaamrisha hivyo kwa sababu Sham ni mbali. Illa (sababu) hii, ni sahihi na imekamilisha masharti ya utoaji wa illa (sababu).

Kwa hivyo, natija ni kuwa Mtume(s.a.w.w) kawaamrisha hivyo kwa sababu Sham ni mbali, sio kwa Sababu kule ni Sham. Tafauti za matlai, kwa sababu ya umbali au kwa sababu za kijografia, ni katika mambo yanayothibiti kwa njia ya Qias. Na Qias, nijuavyo, kwa Sunni, Ibadhi na Jumhur kwa ujumla ni dalili katika dalili za Kisharia. Kwa hivyo, kusema: "Pia ni wazi kwamba agizo hilo la Mtume(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) halikutaja suala la kuwepo kwa matlai wala masafa gani, wala chengine chochote" hakukujengeka katika misingi ya elimu, kwani elimu haiangalii nassun (andiko) tu; bali inaangalia andiko na Qias pia. Ama kauli yenu: "Wala hakuna katika maelezo sahihi ya Mtume(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambayo yanakubalika na Wanavyuoni yaliyotaja kwamba 'kila nchi ifunge na ifungue kwa miandamo yao" si kauli sahihi. Kwani ikiwa munataka Hadithi iseme "Jamani kila nchi na muandamo wao" basi riwaya yenye lafdhi hii haipo. Ama riwaya yenye maana hii ipo nayo ni riwaya ya Kuraib na Ibn Abbaas, nayo ni Hadithun Marf'u'u kwa mujibu wa lafdhi yake.

Pili ni kuwa kama vile ambavyo hakuna Hadithi ambayo lafdhi yake inasema: "Jamani kila nchi na muandamo wao" pia hakuna Hadithi yenye kusema "Jamani fungeni kwa muandamo mmoja". Kwa hivyo, suala hili linarejeshwa katika dalili zake nyengine kwa mujibu wa fani zinavyoeleza. Na tumeona kwamba Ibn Abbaas kaukataa muandamo wa Sham na akasema "Hivi ndivyo alivyotufunza Mtume(s.a.w.w) ". Kwa hivyo, mafunzo ya Mtume(s.a.w.w) , ni kutokuuzingatia mwezi wa mbali.

Ama kauli yenu: "Kama ilivyoelezwa kwamba hoja inayotegemewa na baadhi ya Wanavyuoni wachache juu ya mas-ala haya ni kisa cha masimulizi ya Kuraib, masimulizi ambayo hayana ufafanuzi wa kina kama walivyoeleza hayo baadhi ya Wanavyuoni wengine na kuonyesha kuwa yana utatanishi (ihtimaalati)" pia si kauli sahihi. Kwanza walioizingatia Hadithi ya Kuraib ndio Jumhur kama tunavyoshuhudia leo practically (kimatendo) kwamba asilimia kubwa ya Waislamu wa madhehebu mbali mbali duniani wanafata msimamo huu. Pili ni kuwa usahihi na udhaifu haupimwi kwa wingi na uchache hata kama ilikuwa munavyodai nyinyi ndio kweli kauli ya Jumhur; bali kipimo ni dalili za Kisharia. Ama kudai kuwa masimulizi ya Kuraib hayana ufafanuzi, sijui munataka ufafanuzi gani. Riwaya imeshaeleza kwa uwazi kwamba Ibn Abbaas kaukataa muandamo wa Sham na akasema kuwa hivyo ndivyo Mtume(s.a.w.w) alivyowaamuru, bado munasema kuwa haina ufafanuzi?! Ni wazi kwamba hamutaki wala sidhanii kuwa mumekuwa musiofahamu kiasi hicho hata ikawa hamuifahamu Hadithi hii.

Ama dai kwamba masimulizi hayo yana utatanishi (ihtimaalati), tumeshayajibu sana na sijui ni utatanishi (ihtimaalati) gani munaoukusudia. Ibn Al-Qayyim katika nakala mulizomnukuu kwa kughushi na Al-Suyuti katika nakala mulioibutua kipande wamesema: Kauli yake (Ibn Abbaas aliposema): 'Hivi ndivyo alivyotuamuru Mtume(s.a.w.w) ,' ina uwezekano kwamba makusudio kwayo ni kuwa yeye Mtume(s.a.w.w) katuamuru tusiikubali shahada ya mtu mmoja katika kufuturu, au katuamuru kwamba tutegemee uoni wa mji wetu: wala tusitegemee uoni wa wengine. Na hii maana ya pili ndipo inapomili tarjama (yaani heading) ya mtunzi (wa kitabu hiki), lakini maana ya mwanzo ina uwezekano (huu na ule) basi ushahidi wake hauendi sawa kwani uwezekano wa namna tafauti unaifisidi dalili, kana kwamba wameona kwamba chenye kufahamika akilini ni maana ya pili wakajenga dalili juu yake. Kwa hivyo, ihtimal wanayoikusudia wao ni kuwa inawezekana kuwa maana iliokusudiwa ni kutokuchukua ushahidi wa mtu mmoja katika kufuturu; na inawezekana ikawa maana iliokusudiwa ni kwamba tutegemee uoni wa mji wetu: wala tusitegemee uoni wa wengine. Kisha wakabainisha kwamba maana ya pili ndio sahihi na kwamba maana ya mwanzo ndio yenye ihtimal (utata kama munavyoita), kwa hivyo maana ya mwazo si sahihi.

Lakini tunasema kwamba bila shaka dai hilo kwamba riwaya hio ina uwezekano kwamba makusudio yake ni kuwa Mtume(s.a.w.w) katuamuru tusiikubali shahada ya mtu mmoja katika kufuturu, ndio maana ya maneno "Hivi ndivyo alivyotuamuru Mtume s.a.w." ni dai dhaifu kwani:

1) Ibn Abbaas aliukataa muandamo wa Ramadhani huko Sham; si muandamo wa mfunguo mosi. Kama riwaya yenyewe inavyosema: "Ukaniandamia mwezi wa Sham nami niko Sham", na muandamo wa Ramadhani hauhitaji mashahidi wawili, bali shahidi mmoja anatosha.

2) Pili katika riwaya mulioitolea hoja - nayo ni riwaya dhaifu: riwaya ya bedui - tunapata kwamba Mtume (s.a.w.) mwenyewe kauchukua muandamo wa mtu mmoja (bedui) katika mwezi wa mfungo.

MNASEMA

Kwa hivyo agizo hilo la kufunga na kufungua kwa pamoja litaendelea kuwa hivyo kwani hakuna riwaya sahihi isiyo na utata yenye kuvua ujumla huu. Tamko hili ni: "Tamko lisilo na mipaka maalum."

JAWABU

Riwaya sahihi isio na utata yenye kuuvua ujumla huo iko: ni riwaya ya Kuraib na Ibn Abbas. Na wala hakuna utata wowote ndani yake; utata munao nyinyi wenyewe.

MNASEMA

Ama jambo la kusema kila watu na mtenguko wao wa jua kwa hivyo wana wakati wao wa kuswali na kufunga (Swaum) ndio hivyo hivyo; ni vyema ieleweke hivyo ni vitu viwili tofauti. Swala imeambatana na mitenguko ya jua na Swaum imeambatana na kuandama kwa mwezi. Mas-ala ya nyakati za Swala yameshaelezwa na kufafanuliwa na Mwenyewe Mwenyezi Mungu katika Qur-aan na pia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amelibainisha kwa uwazi kabisa katika Hadiyth. Wala hakuna ikhtilafu yoyote mbele ya Wanazuoni juu ya jambo hilo. Ijmai ya Wanazuoni wamekubaliana kuwa kila sehemu, wala si kila nchi nzima inaweza kusali kwa wakati mmoja. Kwani mtenguko wa jua unaweza kutofautiana hata katika nchi moja. Angalia Dar es Salaam na Kigoma wanaswali na kufuturu tofauti, lakini wanafunga kwa mwandamo mmoja. Kila sehemu itaswali kwa wakati wake kwa kutegemea mtenguko wake wa jua. Mwenyezi Mungu Amebainisha hayo katika Surat Bani Israil (17: 78) kama ifuatavyo:"Simamisha Swala jua linapopinduka (likaenda magharibi) mpaka giza la usiku". Kwa upande wa Swaum hapakupatikana ufafanuzi wa kina ambao unakubali ka mbele ya "Jamhur" ya Wanazuoni. Hakuna hoja isiyokuwa na utata katika jambo la kuanza kufunga na kufungua kwa kutegemea kila nchi au kila eneo moja peke yake. Kwa mantiki hiyo ndio maana "Jamhur" ya Wanavyuoni wetu wakaonelea ni bora kutegemea Sunnah, yaani Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) zilizo wazi ambazo zinaashiria umoja katika kufunga kwa pamoja. Kukamata andiko sahihi ni bora kuliko kung'ang'ania jambo lisilofahamika ambalo lina utatanishi.

"Kutumia madondoo kama Qur-aan au Sunnah ni bora zaidi kuliko kuiwacha (au kuipuuza na kuzingatia dalili zenye utata)".

JAWABU

Kuwepo kwa andiko na ijmaa ya nyakati tafauti za Sala na kutokuwepo kwa andiko la wazi juu ya wapi hadi wapi tufunge, ndiko kuliko juzisha kufanya Qias hicho cha sala na funga. Qias sharti yake ni kuwepo kwa msingi nacho ni kitu ambaho hukumu yake imetajwa; tawi nacho ni kitu ambacho hukumu yake haikutajwa; hukumu nayo ni moja katika hukumu tano za kifiq-hi; na illa jami'a (sababu yenye kuvijumuisha) vitu viwili hivyo na - kwa hapa - ni ukweli kwamba:

1) Jua ni kipimo cha wakati.

2) Jua ni sababu ya kuwajibikiwa na ibada.

3) Mwezi ni kipimo cha nyakati.

4) Mwezi ni sababu ya kuwajibikiwa na ibada.

5) Jua likitenguka sehemu moja: haiwi sababu ya watu wa sehemu nyengine yenye matalai tafauti kuwajibikiwa na sala.

6) Kwa hivyo, na kuonekana kwa mwezi katika sehemu ya mbali kusiwe ni sababu ya watu wan chi ya mbali kuwajibikiwa na ibada ya funga.

Ama kauli yenu: "Kwani mtenguko wa jua unaweza kutofautiana hata katika nchi moja. Angalia Dar es Salaam na Kigoma wanaswali na kufuturu tofauti, lakini wanafunga kwa mwandamo mmoja". Haya ndio niliokwambieni kuwa ni mas-ala ya ijtihad, au yanayojuzu kufanyiwa ijtihad. Yaani wapi hadi wapi tufunge sawa, hilo halikubainishwa na riwaya yoyote; lakini ukweli kwamba muandamo wa mbali usiwe hoja kwa walio mbali; hili limebainishwa na riwaya ya Ibn Abbaas na Kuraib. Kwa hivyo, ikiwa watu wa Kigoma wamefata ijtihad fulani ya wanavyuoni juu ya mas-ala ya masafa gani, hili kwa ujumla linakubalika. Lisilokubalika ni kufunga dunia nzima kwa muandamo mmoja. Na hili ndilo ninalotafautiana na nyinyi. Ama ukweli kuwa mbona basi tunafuturi tafauti na watu wa Kigoma; hili halijuzu ijtihadi kwa sababu ya kuwepo andiko la wazi kwamba wasifuturu hadi jua lituwe. Kwa ufupi ni kuwa, masafa gani tufunge sawa; hapa ijtihad inajuzu kwa sababu ya kukosekana andiko lenye kuhadidi masafa; masafa gani tufuturu sawa, hili halijuzu ijtihad kwa sababu ya kuwepo andiko lenye kubainisha suala hili.

Ama kusema kwenu: "Kwa upande wa Swaum hapakupatikana ufafanuzi wa kina ambao unakubalika mbele ya "Jamhur" ya Wanazuoni. Hakuna hoja isiyokuwa na utata katika jambo la kuanza kufunga na kufungua kwa kutegemea kila nchi au kila eneo moja peke yake. Kwa mantiki hiyo ndio maana "Jamhur" ya Wanavyuoni wetu wakaonelea ni bora kutegemea Sunnah, yaani Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) zilizo wazi ambazo zinaashiria umoja katika kufunga kwa pamoja". Ninasema: kutopatikana ufafanuzi wa kina ndiko kunakohalalisha kufanya Qias, kwani lau palikuwa na andiko, basi Qias kisingelijuzu kama walivyosema: kwenye andiko hakuna Qias. Lakini sijakufahamuni muliposema : Kwa manti ki hiyo ndio maana "Jamhur" ya Wanavyuoni wetu wakaonelea ni bora kutegemea Sunnah, yaani Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) zilizo wazi ambazo zinaashiria umoja katika kufunga kwa pamoja". Ni Jumhur ya wanavyuoni wenu gani?

Pili : ni kuwa na Hadithi ya Kuraib pia ni sunna ya Mtume(s.a.w.w) iliowazi.

Tatu : ni kuwa na Hadithi mulioitegemea nyinyi pia haiko wazi kwani inasema"Fungeni kwa kuuona" . Kweli Hadithi hii ko wazi katika kubainisha kwamba kufunga hakutakiwi ila baada ya kuuona mwezi; lakini haiko wazi katika kubainisha je tufunge kwa muandamo mmoja au kila watu wawe na muandamo wao. Ufafanuzi huu, unapatikana katika Hadithi ya Kuraib ambayo hamuitaki: munaipiga chenga!!!

Ama kauli yenu: "Kukamata andiko sahihi ni b ora kuliko kung'ang'ania jambo lisilofahamika ambalo lina utatanishi". Nimeshakufahamisheni kwamba Hadithi ya Kuraib pia infahamika na haina utatanishi, na kwamba Hadithi: "Fungeni kwa kuuona" ndio ambayo inafaa au inaelekea kuambiwa kuwa ina utata, kwani haikufafanua je tufunge kwa muandamo mmoja au miandamo tafauti.

Ama kanuni isemayo: "Kutumia madondoo kama Qur-aan au Sunnah ni bora zaidi kuliko kuiwacha (au kuipuuza na kuzingatia dalili zenye utata)". Kanu ni hii ni ushahidi wetu dhidi yenu, lakini kama munavyojionea wenyewe nyinyi hizi fani hamuzijui: munasukuma tu. Maana ya kanuni hii ni kuwa ikiwa neno - kwa mfano - halifasiriki katika uhakika wake, basi hupewa hukumu ya majazi: lakini sio kuwa liachwe. Na kwa ufupi ni kuwa andiko lolote likiwa linaweza kutendewa kazi basi haliwachwi: huwa linatendewa kazi. Na kwa maana hii, yanaingia maandiko mawili ambayo dhahir yake ni kuwa yana mgongano. Maandiko hayo huwa hayawachwi yote wala haliachwi moja madamu yanaweza kutendewa kati yote, bali kila moja hupewa maana linoyostahiki. Kwa hivyo, sisi ndio tulioitumia kanuni hii: sio nyinyi, kwani sisi tumezitendea kazi Hadithi zote mbili: Hadithi "Fungeni kwa kuuona", na Hadithi "Hivi ndivyo alivyotuamuru Mtume(s.a.w.w) " katika masimulizi ya Kuraib. Kusu Hadithi "Fungeni kwa kuuona", tumesema kwamba maana ni kuwa watu wote ni lazima wafunge kwa kuuona mwezi, yaani kuonekana kwa mwezi ndio kuwe sababu ya mfungo; na Hadithi ya Kuraib na Ibn Abbaas tumesema inatoa ubainifu wa kwamba muandamo wa mwezi wa mbali si hoja kwa waliombali. Kwa hivyo, kanuni hio hamukuielewa na mungeielewa musingelipata tabu katika kuzifasiri Hadithi mbili hizo.

MNASEMA

Ama suala la kuingia alfajiri na kujizuilia kula na kunywa katika hukmu ya kuanza kufunga au kuanza kufuturu wakati wa kuzama kwa jua, mambo hayo hayana mjadala au khitilafu kama hizo kwani Mwenyewe Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ameshayafafanua katika Qur-an Tukufu kama ifuatavyo:"Na kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa Alfajiri katika weusi wa usiku. Kisha timizeni Swaum mpaka usiku" . (2: 187) Jambo hilo la k utokuwepo khitilafu yoyote katika mas-ala haya, inamaanisha kwamba kila sehemu itajizuilia kula na kunywa kutokana na kuingia alfajiri yake na kila sehemu itafuturu baada ya kuzama jua kwa upande wake.

JAWABU

Haya! Iko wapi hio hoja katika Aya hii?!"Na kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa Alfajiri katika weusi wa usiku. Kisha timizeni Swaum mpaka usiku" . Je hapa wanaombiwa ni watu wan chi moja au wan chi zote? Nadhani jawabu iko wazi kwamba ni watu wan chi zote. Sasa je usiku ukiingia nchi moja na watu wan chi nyengie nao wafuturu? Kama si hivyo, basi vipi Hadithi "Fungeni kwa kuuona" iwe ni dalili ya kufunga sawa duniani kote; lakini Aya"Na kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa Alfajiri katika weusi wa usiku. Kisha timizeni Swaum mpaka usiku". isiwe hoja kwamba tufuturu sawa ilhali ujumla ulioko huku ndio ulioko kule? Kwa kweli, ndugu zetu humujui mukisemacho, na Aya hii ni hoja dhidi yene: si hoja yenu.

Ama kauli yenu kwamba: "Suala la kuingia alfajiri na kujizuilia kula na kunywa katika hukmu ya kuanza kufunga au kuanza kufuturu wakati wa ku zama kwa jua, mambo hayo hayana mjadala au khitilafu". Mwiso wa kunukuu. Nami nasema: Eleweni kwamba kwa kutokuwepo khilafu hizo, ndio imewezekana kufanya Qias sahihi kisichopingika kwa wenye kujua taratibu za Qias, kwani ikiwa Aya inasema:"Na kuleni na kunyweni" na hii ni amri ya ujumla kwa watu wote, na pamoja na hayo wanaokula si wote bali ni baadhi tu ambao usiku umeingia kwao; basi na Hadithi "Fungeni kwa kuuona" haijawa dalili ya kuwa watu wote wafate muandamo mmoja. Ukiniambia "Kule kuna dalili kwamba waliokusudiwa ni wale ambao usiku umeigia kwao". Nitakujibu kwamba na huku kuna dalili kwamba wanaomrishwa katika Hadithi"Fungeni kwa kuuona" ni wale ambao mwezi kwao umeandama. Kule dalili ni ijma'a; huku dalili ni Hadithi ya Ibn Abbaas ya kuukataa muandamo wa mbali na kusema: "Hivi ndivyo alivyotuamuru Mtume(s.a.w.w) ".

MNASEMA

Ama ile hoja inayotolewa na baadhi ya ndugu zetu kama Juma isemayo: "Mbona watu wa nchi fulani wakifuturu nyinyi hamfuturu nao?" Au "Wakifuturu watu wa Saudia na nyinyi mufuturu basi." Bahati nzuri kwa upande wetu tumeshajibu mara nyingi katika makala haya kwamba jambo hili haliingizwi katika mjadala kama huu kwani jambo hilo halizungumzwi hata katika nchi moja yenye kufuata muandamano mmoja. Tumetoa maelezo kwamba katika Tanzania, Mji wa Dar-es-salaam hauwezi kufuturu sawa na mji wa Kigoma kwani kuna tofauti ya zaidi ya dakika 40. Jua linazama au kuchomoza dakika 40 kabla ya Kigoma. Kwa hivyo, Dar es Salaam wanaanza kufuturu mwanzo wakati bado jua halijatua Kigoma. Al-Marhuum Shaykh Abdulla Al-Farsy alipokua akiifasiri Aya ya Quran isemayo:"Kisha timizeni Swaum mpaka usiku" . Aliitolea maelezo yafuatayo: "Na ilipoambiwa:"Fungeni Swaum mpaka usiku" . Muradi ni magharibi - jua likishakuc hwa tu, ndio usiku wenyewe uliokusudiwa, kama alivyobainisha hivi Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), na akahimiza watu wafungue jua tu likishakuchwa, na wakawie kula daku"

JAWABU

Kwanza ni lazima tufahamiane ni kwa sababu gani pakatolewa hoja hio. Hoja hio imetolewa kujibu dai kwamba Hadithi "Fungeni kwa kuuona" ni Aam (ya ujumla). Na kwa hivyo, inawahusu Waislamu wote wan chi zote. Hapo ndio na sisi tukajibu kwamba na Aya isemayo: (Simamisha sala kwa kutenguka jua), pia ni ya jumla: haiwahusu watu wa nchi fulani pasi na nyengine. Na Hadithi"Usiku ukitokeza kutoka hapa na mchana ukaondoka kutokea hapa na jua likatua, basi aliyefunga ameshafungua (au na-afungue)" pia ni ya jumla. Sasa je ujumla huu unamaanisha kuwa watu wa Maka au nchi nyengine wakifuturu, watu wote wafuturu pamoja nao? Sisi hapa tunajibu hoja ya kuwepo kwa ujmla katika maandiko haya, kwamba ujumla tu haojatoa jawabu madamu kuna maandiko mengine ambayo nayo ni lazima yazingatiwe ili tuwe tumeyatendea kazi maandiko yote na kufikia maana sahihi.

Sasa ukweli kwamba "Jua linazama au kuchomoza dakika 40 kabla ya Kigoma. Kwa hivyo, Dar es Salaam wanaanza kufuturu mwanzo wakati bado jua halijatua Kigoma" hakujahalalisha kufunga kwa muandamo mmoja duniani madamu kuna andiko sahihi la Hadithi lililoonesha hivyo. Bali hali kama hizi zitabaki kama ni uwanja wa i jtihadi. Ama pale kwenye andiko, ni lazima andiko litendewe kazi.