33%

DALILI ZA KIAMA

KIMEANDIKWA NA: HARUN YAHYA

KIMEFASIRIWA NA: SHUAYBU HUSEIN KIFEA

Dalili za Kiyama Katika kipindi chote cha historia ya ulimwengu Wanaadamu wameuelewa ukubwa wa milima na upana wake, na ukubwa wa mbingu kutokana na njia zao mbali mbali za uchunguzi ijapokuwa wamekuwa na fikra potofu kuwa maumbile haya yatadumu milele. Imani hii ndio iliyozaa falsafa za kishirikina na za kilahidi za Ugiriki na dini za Sumeria za Misri ya kale. Qur'an inatuambia kuwa wale wanaoamini hivi wapo katika hatia kubwa. Miongoni mwa vitu ambavyo Mwenyezi Mungu amevibainisha katika Qur'an ni kuwa Ulimwengu umeumbwa na kwamba utakuwa na mwisho wake. Ulimwengu, kama walivyo binadamu na viumbe vingine hai, utatoweka.

Dunia hii iliyopangiliwa vizuri ambayo imefanya kazi bila kasoro kwa mabilioni ya miaka, ni kazi yake Mola ambaye ameumba kila kitu, siku moja kwa amri yake itakoma kufanya kazi. Wakati huo tayari Mwenyezi Mungu amekwisha upanga. Wakati huo ambapo ulimwengu na kila kiumbe tokea vile visivyoonekana kwa macho hadi binadamu pamoja na Nyota na Magalaksi yatasita kufanya kazi, unaitwa "Saa" katika Qur'an. "Saa" hii haina maana kuwa muda wowote bali ni neno mahususi lililotumika katika Qur'an kuelezea wakati ambao dunia itakuwa imefika mwisho wake.

Pamoja na maelezo ya mwisho wa dunia, Qur'an ina maelezo ya kina ya namna tukio zima litakavyotokea; "Mbingu zitakapopasuka," "Bahari zitakapowashwa moto," "Milima itakapoendeshwa (angani kama vumbi)" "Jua litakapo kunjwa kunjwa". Kihoro na khofu ambayo watu watakuwa nayo katika tukio hili la kutisha imeelezwa kwa kina katika Qur'an. Aya zinasisitiza kuwa hakutakuwa na pa kukimbilia wala pa kujificha. Tunachoweza kukisema hapa ni kuwa Ulimwengu utakuwa katika janga kubwa ambalo halijawahi kutokea hapo kabla.

Aya nyingi za Qur'an zinabainisha kuwa suala la mwisho wa dunia limegusa hisia za watu wengi katika kila kipindi cha historia. Katika aya kadhaa inaelezwa kuwa watu walimuuliza Mtume (s.a.w) juu ya lini utakuwa mwisho wa dunia;

Wanakuuliza juu ya Saa hiyo (yaani Kiama) kutokea kwake kutakuwa lini? (7:187) ,

Wanakuuliza Kiama kutokea kwake kutakuwa lini? (79:42)

Mwenyezi Mungu akamuamrisha Mtume kulijibu swali hilo hivi; Ilimu yake iko kwa Mola wangu tu. Hakuna wa kuhidhirisha wakati wake ila yeye tu (7:187).

Hii maana yake ni kuwa Allah pekee ndiye aijuaye tarehe ya siku hiyo. Kutokana na aya hii tunaelewa kuwa elimu juu ya lini utafika wakati huo imefichwa kwa wanadamu. Lazima kuna sababu maalumu kwanini Mwenyezi Mungu ameifanya siku hii kuwa siri. La muhimu ni watu kujihadhari nayo; Ambao wanamuogopa Mola wao hata wanapokuwa Faraghani, na pia hukiogopa kiama (21:49). Kwahiyo watu wachunge mamlaka ya Mwenyezi Mungu na wautafakari ukubwa wake. Kabla ya siku hiyo ya machungu na majonzi haijawatokea kwa ghafla, watu waelewe kuwa mbali na Mwenyezi Mungu hakuna mahala pa kukimbilia. Kama siku ya mwisho ingejulikana watu walioishi huko nyuma pengine wasingelazimika kuufikiria kwa makini mwisho wa dunia, wasingejali matukio ya mwisho yaliyotajwa katika Qur'an.

Ispokuwa lazima ieleweke kuwa kuna aya nyingi zinazoelezea Saa hiyo na pale tunapozisoma tunakutana na ukweli madhubuti. Qur'an haitaji muda maalumu wa tukio hilo, bali inaelezea matukio ambayo yatatokea kabla yake. Aya hii inaelezea dalili kadhaa za saa hiyo;

Kwani wanangoja jingine ila Kiama kiwajie kwa ghafla? Basi alama zake (hicho Kiama) zimekwisha kuja. Kutawafaa nini kukumbuka wakati kitakapowajia? (47:18)

Kutokana na aya hii tunajifunza kuwa Qur'an inaelezea dalili zinazoonesha kufika kwa siku ya mwisho. Ili kuzielewa dalili hizi lazima tuzitafakari aya hizi. Vinginevyo kama aya inavyosema tafakuri yetu haitakuwa na maana pale Kiama kitakapotekea kwa ghafla. Baadhi ya hadithi za Mtume (s.a.w.w) ambazo zimetufikia zinazungumzia dalili za Kiama. Katika hadithi hizi za Mtume (s.a.w.w) , kuna dalili za Kiama na maelezo ya kina kuhusu kipindi kinachokaribia kuhusu muda wa kukaribia Kiama, kipindi hiki ambacho dalili za Kiama zitatokea kinaitwa "Siku za Mwisho"

Suala la siku za mwisho na dalili za kiama, limevuta hisia za wengi katika kipindi chote cha historia ya Uislamu. Ndio maudhui makuu ya vitabu vingi vya wanazuoni na watafiti wa Kiislamu. Tunapoyakusanya pamoja maelezo yote haya, ndipo tutakapofikia hitimisho muhimu. Aya za Qur'an na hadithi za Mtume (s.a.w.w) zinaoneshakuwa kipindi cha siku za mwisho kimegawanyika katika awamu mbili:

Awamu ya kwanza: ni pale ambapo mitihani ya kiroho na mali itausibu Ulimwengu.

Awamu ya pili: inaitwa zama bora, ni wakati ambapo mafundisho ya kimaadili ya Qur'an yatatawala na kuleta ustawi bora wa mwanadamu. Zama hizi zitakapofika mwisho wake na dunia itakapoingia katika kipindi ambacho jamii zitaporomoka, Kiama kitakuwa kimefika.

Shabaha ya mfululizo huu wa mafundisho ya Qur'n ni kuzitazama dalili za Kiama kupitia aya za Qur'an na hadithi za Mtume (s.a.w.w) na kubainisha kuwa dalili hizi zimekwishaanza kujitokeza katika wakati huu tulionao.

Ule ukweli kwamba kujitokeza kwa dalili hizi kulikwisha elezwa karne 14 zilizopita umzidishie Muumini Imani kwa Allah na unyenyekevu kwake. Kitabu hiki kimetayarishwa kwa kuzingatia ahadi ya Mola wetu;

Sema sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu, karibuni hivi atakuonesheni ishara zake na mtazifahamu (27:93)

Nukta yenye umuhimu makhsusi ambayo kwayo tunataka kumkumbusha msomaji ni kuwa Allah ndiye ajuaye ukweli juu ya kila kitu. Kama ilivyo katika mambo mengine yote, tuna chokijua sisi kuhusu mwisho wa dunia ni kile tu ambacho Allah amekibainisha kwetu.

1

DALILI ZA KIAMA

SAA INAKARIBIA

Watu wengi angalau hujuwa jambo fulani kuhusu siku ya mwisho na karibu kila mmoja amesikia jambo hili au lile kuhusu kishindo cha saa hiyo. Hata hivyo wengi wanaonekana kuwa na mwenendo ule ule juu ya suaala hili kama walivyo katika masuala mengine yenye uzito mkubwa. Kwamba hawataki kulizungumzia au hata kulifikira jambo hili.

Wanajitahidi kwa kila hali kujighafilisha na khofu watakayo ipata siku ya mwisho. Hawajali ukumbusho wa siku ya mwisho uliomo katika kitabu juu ya msiba wa kuhuzunisha. Wanaepuka kuutafakari ukweli kuwa siku hiyo hapana shaka itafika. Hawataki kuwasikiliza watu wanaoizungumzia siku hii nzito au kusoma maandiko juu siku hiyo.

Hizi ni baadhi ya hila ambazo watu wamezidumisha ili kuepuka kuifikiria hatari ya siku ya mwisho. Wengi hawaamini kwa dhati kuwa saa hiyo inakuja. Tumepewa mfano wa watu hawa katika aya moja ya suratil-al-Kahf inayomzungumzia tajiri aliyemiliki bustani; ambaye alikitilia shaka Kiama;

Wala sidhani kuwa Kiama kitatokea. Na kama (kitatokea hicho Kiama) nikarudishwa kwa Mola wangu, bila shaka nitakuta kikao chema kuliko hiki (alichonipa Ulimwenguni) (18:36)

Aya hiyo inabainisha taasubi ya mtu anayemuamini Allah lakini anayekwepa kufikiria hakika ya siku ya mwisho na anatoa madai yanayopingana na aya za Qur'an. Aya nyingine inaelezea wasi wasi na mashaka yaliyowajaa makafiri kuhusiana na siku ya mwisho;

Na wale waliokufuru wataambiwa je! Hazikuwa aya zangu zikisomwa kwenu, nanyi mkajivuna na mkawa watu waovu? Na inaposemwa hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni kweli na Kiama hakina shaka mlikuwa mkisema; hatujuwi Kiama ndio nini; hatudhani ila dhana tu wala hatuna yakini. (45:31-32).

Watu wengine ndio kabisa wanakana kuwa Kiama kipo. Wale wenye dhana hii wanatajwa hivi katika Qur'an:

Bali wanakadhibisha Kiama na tumewaandalia wanaokadhibisha Kiama Moto mkali kabisa. (Moto huo utakapowaona tokea mbali kabisa watasikia hasira yake na ngurumo yake). (25:11).

Chanzo kinachoweza kutuongoza katika njia sahihi na kutubainishia ukweli ni Qur'an. Tunapoangalia yale inayoyaelezea, tunabaini ukweli ulio dhahiri. Wale wanaojidanya kuhusu siku ya mwisho wanafanya dhambi kubwa sana, kwani Allah anabainisha katika Qur'an kuwa hakuna shaka yoyote siku ya mwisho ikaribu:

Na kwamba Kiama kitakuja, hapana shaka ndani yake;

Na kwa hakika Mwenyezi Mungu atawafufua walio makaburini (22:7) Na hatukuziumba Mbingu na Ardhi na vilivyomo ndani yake ispokuwa kwa haki. Na bila shaka Kiama kitafika (15:85)

Kwa yakini Kiama kitakuja, nacho hakina shaka lakini watu wengi hawaamini (40:59).

Yawezekana kuna watu wanaodhani ujumbe wa Quraan kuhusiana na siku ya mwisho ulifunuliwa zaidi ya miaka 1400 iliyopita na kwamba hiki ni kipindi kirefu kulinganisha na muda wa maisha ya binadamu. Lakini hapa ni suala la mwisho wa dunia, jua, nyota na kwa kifupi ulimwengu mzima. Tunapo chukulia kuwa ulimwengu una umri wa mabilioni ya miaka, karne kumi na nne ni kipindi kifupi sana cha wakati. Mwanazuoni mkubwa wa kiislamu wa zama hizi, Bediuzzaman Said Nursi alilijibu swali hilo namna hii :

Saa (ya kufika kiyama) imekaribia (54 :1) kwamba siku ya mwisho iko karibu. Hata kama ni baada ya miaka elfu moja au miaka mingi zaidi ya hii bado hili halivurugi ukaribu wake. Kwa sababu siku ya mwisho ni saa iliyopangwa kwa ajili ya ulimwengu, na katika uwiano wa maisha ya ulimwengu, miaka elfu moja au elfu mbili ni sawa na dakika moja au mbili katika mwaka. Kwa hiyo siku ya mwisho sio tu ni saa iliyopanga kwa ajili ya binadamu kwamba ionekane iko mbali sana.

Kuhubiriwa kwa mafundisho ya Qur'an ulimwenguni Katika Quran, tunakuta maneno yanayorudiwarudiwa; suna ya Allah yaani kawaida au dasturi [Sunnat Lllahi]: huu ni msemo wenye maana ya njia au sheria ya MwenyeziMungu. Kwa mujibu wa Quraan,sheria hizi hazibadiliki daima. Aya inasema: Hii ni kawaida ya mwenyezimungu iliyokuwa kwa wale waliopita zamani; walahutapata mabadiliko katika kawaida ya mwenyezimungu. (33:62)

Kanuni mojawapo ya mwenyezimungu isio badilika nikuwa, kabla ya mangamizi,kwanza jamii hupelekewa muonyaji[mjumbe].ukweli huu unabainishwa kwa maneno haya: Walahatukuangamiza mji wowote ila ulikuwa na waonyaji wa kuwakumbusha wala hatukuwa madhalim,tukawawngamiza pasina kuwapelekea waonyaji] (26:208-209). Katika historia yote, Mwenyezi Mungu ametuma muonyaji au mkumbushaji kakika kila jamii iliyokengeuka, akiwalingania kufuata njia sahihi. Sasa wale walio endelea nauovu wao ndio walio angamizwa baada ya kutimiza ule muda waliopangiwa na wakawa fundisho kwa vizazi vilivyo fuata. Tunapo iangalia kanuni hii ya mwenyezi Mungu siri nyingi muhimu zina bainika kwetu Siku ya mwisho ni msiba wa mwisho utakao ukumba ulimwengu. Quraan ni kitabu cha mwisho cha mwenyezi Mungu kilichoshushwa kuwanasihi walimwengu. Muongozo wa Qur'an utabakia hadi mwisho wa dunia. Moja ya aya zake inasema-

Hayakuwa haya ila nimawaidha kwa watu wote (6:90). Wale wanaodhani kuwa Qur'an inazungumzia wakati au mahali fulani wanakosea sana kwasababu Qur'an ni wito wa jumla kwa walimwengu wote. Tokea wakati wa Mtume (s.a.w.w) ujumbe wa Qur'an ulikwishaenea duniani kote. Kutokana na maendeleo ya makubwa ya Teknolojia ya zama zetu,Qur'an yaweza kusambazwa kwa wanadamu wote. Hivi leo, sayansi, elimu, mawasiliano na usafilishaji vinafikia hatua ya mwisho ya maendeleo yao hasa hasa tekinolojia ya kompiuta na mtandao wa Internent, watu katika sehemu mbalimbali wanaweza kubadilishana taarifa papo kwa hapo.

Mapinduzi ya sayansi na tekinolojia yameunganisha mataifa yote ya dunia nzima maneno kama utandawazi (Globolization) yameongezwa katika msamiati. Kwa kifupi vikwazo vyote vinavyo kwaza umoja wa walimwengu vinaondoshwa kirahisi tu. Kwakuzingatia ukweli huu ni rahisi kusema kuwa katika zama zetu hizi za mawasiliano ya papo kwa hapo, Mwenyezi Mungu ameweka aina zote za maendeleo ya tekinolojia kwa manufaa yetu ni jukumu la Waislamu kutumia vema tekinolojia hizi kwa ajili ya dawa katika maisha yote ili watu wayapate mafundisho ya Qur'an.